Jimbo Katoliki la Morogoro katika maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2021 limezindua Katekisimu Ndogo, chombo cha uinjilishaji mpya! Jimbo Katoliki la Morogoro katika maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2021 limezindua Katekisimu Ndogo, chombo cha uinjilishaji mpya! 

Jimbo Katoliki Morogoro Lazindua Katekisimu Ndogo: Chombo Makini

Katekisimu Ndogo inatoa mwongozo wa mafundisho ya Katekesi kwa watoto wa mafundisho ya Ekaristi Takatifu na Kipaimara, ambayo pia itakuwa chachu ya kuamsha moyo wa Sala na Ibada ndani ya familia. Katekisimu inazingatia kikamilifu hitaji la watoto, waamini, na watu wa ndoa ambayo ina maswali na majibu, nukuu za Biblia ili kupata urahisi wa ufafanuzi na mvuto kwa watoto.

Na Angela Kibwana, - Morogoro, Tanzania.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni amana, urithi na utajiri wa imani; matunda ya Mafundisho ya kina kutoka kwa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hiki ni chombo mahususi chombo cha kusaidia mchakato wa ukuaji na ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, chachu ya utakatifu wa maisha yenye mvuto na mashiko katika azma nzima ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Katekisimu ambayo ni muhtasari wa Imani ya Kanisa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya nyakati. Ni muhtasari wa adhimisho la Fumbo la Pasaka katika Sakramenti za Kanisa, Sakramenti za Kristo, Sakramenti za wokovu, imani na uzima wa milele. Lengo la maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa. Katekisimu ni muhtasari wa dira na mwongozo wa Maisha ya Kikristo na Adili unaofumbatwa katika Amri kumi za Mungu zinazopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha: kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani, kama mhutasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Katekisimu ni muhtasari wa Maisha ya Sala kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale na Sala kuu ya Baba Yetu kama ilivyofundishwa na Kristo Yesu kwa kubeba mafundisho mazito katika maisha na utume wake. Hii ni kazi iliyovaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II kama chombo muhimu sana cha maisha na utume wa Kanisa katika kukabiliana na changamoto mamboleo.

Monsinyo Lazarus Msimbe SDS, Msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki Morogoro amesema Katekisimu mpya inatoa mwongozo wa mafundisho ya Katekesi kwa watoto wa mafundisho ya Ekaristi Takatifu na Kipaimara, ambayo pia itakuwa chachu ya kuamsha moyo wa Sala na Ibada ndani ya familia, kama Kanisa dogo la nyumbani. Katekisimu hii inazingatia kikamilifu hitaji la watoto, waamini, na watu wa ndoa ambayo ina maswali na majibu, nukuu za Biblia ili kupata urahisi wa ufafanuzi, pamoja na picha ili kuwasaidia watoto kuelewa haraka wanapotazama picha zilizomo katika kitabu hicho. Aidha, Katekisimu hii imewekewa maelekezo yaliofupishwa katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki ambayo itasaidia waamini kujiimarisha kiroho mintarafu mafundisho ya: Imani, Sakramenti, Maisha Adili na Maisha ya Sala licha ya kuonekana ni ndogo kwa mtazamo, lakini thamani yake ni kubwa zaidi, itakayosaidia waamini wanapokuwa katika ibada za jumuiya ndogondogo za Kikristo. “Katekesimu hii imewekwa kwa mtindo wa maswali na majibu mafupi, pamoja na nyimbo kuwasaidia wakatekumeni, wanandoa na familia zetu, tupo hapa duniani ili kumjua Mungu, kumpenda na kumtumikia ili kufika mbinguni” amesema Monsinyo Lazarus Msimbe.

Ni katika muktadha huu, Padre Ponsiani Seluhinga, Mkurugenzi wa Katekesi na Idara ya Kichungaji Jimbo Katoliki Morogoro, Tanzania amezitaka familia kutumia Katekesimu Ndogo ya Jimbo Katoliki Morogoro iliyoboreshwa na kuzinduliwa Mwezi Mei, 2021 ili kujinufaisha kiroho wao pamoja na kuwasaidia watoto wao kuishi kadiri ya imani ya Kanisa. Monsinyo Lazarus Msimbe Msimamizi wa Kitume Jimboni humo amefanya uzinduzi huo katika adhimisho la Misa Takatifu iliyofanyika katika Parokia ya Roho Mtakatifu Kiwanja cha Ndege Jimboni humo, iliyokwenda sanjari na shangwera wakati wa Sherehe ya Pentekoste Kijimbo iliyofanyika parokiani hapo. Padre Ponsian Seluhinga amemshukuru Monsinyo Msimbe kwa utayari wake kukubali mchakato wa kurekebisha Katekesimu ndogo ya zamani kwa kusoma alama za nyakati na kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Mchakato huo ulianza mwaka 2020 baada ya kuona Katekisimu Ndogo ya zamani toleo la pili ya jimbo iliyochapishwa kunako mwaka 1995, kukosa maelezo ya kina na kukosa mtitiriko mzuri kuhusiana na masuala ya kiimani, lengo ikiwa ni kumsaidia msomaji aweze kuelewa kilichoelezwa katika Katekisimu Ndogo na kupata ufafanuzi katika Biblia Takatifu.

“Ni jambo la kumshukuru Mungu baada ya mchakato huu kukamilika imepata ruksa maalum kutoka kwa msimamizi wetu, tunashukuru kwamba ameweza kutusaidia kukichapisha Kitabu hiki, sasa kimeweza kutoka tunawaalika waamini kununua kwa ajili ya manufaa ili kujua nini wanachopaswa kukiishi katika kukuza imani” amesema. Wakati huo huo, kwa upande wa watoto wanaofanya mafundisho ya dini na waliopo shule za msingi na sekondari, Katekisimu mpya toleo la tatu itawasaidia kujisomea wao wenyewe nyumbani kwa sababu ina lugha nyepesi, itajibu maswali mbalimbali yanayonekana ni changamoto kwao hasa maswali magumu wanayoyasikia mitaani kutoka kwa vijana wenzao wa madhehebu mengine; itawaimarisha vizuri kushikilia misimamo ya imani yao na kuwa tayari kuitolea ushuhuda makini katika maisha. Katekisimu hii ni msaada mkubwa kwa familia mbalimbali ambazo ndio walezi na Makatekista wa kwanza katika familia yaani baba na mama. Kwa hiyo wazazi wanapokuwa na kitabu hicho wajitahidi kuwasaidia watoto wao ili nao pia kama wazazi iwasaidie waweze kubadilika na kuishi kadiri ya Mafundisho yanayotolewa na Kanisa Katoliki katika: Imani, Sakramenti, Maisha Adili na Maisha ya Sala. “Niwaombe kila Katekesta Jimboni Morogoro naomba wajitahidi kupata nakala waweze kusaidia watoto katika utume wa mafundisho ya dini, lakini pia hata sisi mapadre tujitahidi kupata nakala ili iweze kutusaidia na baada ya uzinduzi huu itaanza kutumika rasmi” amesema Padre Seluhinga. 

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Makatekista Jimbo la Morogoro [UMAMORO] Katekista Augustino Madenge ambaye ni mwalimu wa Makatekista Chuo cha Katekesi Mzumbe Jimboni Morogoro, amepongeza jitihada za uongozi wa jimbo kuwasaidia Makatekista kupata zana ya kuweza kuipeleka Injili kwa watoto kwa sababu, watoto wakijengwa vizuri kiimani kwa msingi mzuri imani itaendelea na Kanisa litaendelea kuku ana kupanuka zaidi. Ni matumaini yake ni kwamba Katekesimu hiyo ambayo ni muhtasari wa mafundisho na maadili ya kanisa katoliki italeta mwelekeo mzuri wa imani ya Kanisa Katoliki, kwa sababu itawawezesha watoto wadogo ambao bado wapo shuleni kujengewa uthubutu wa kuelewa mafundisho ya dini kwa ushirikiano wa Makatekista na wazazi katika ngazi ya familia “kutoka kwa katekisimu hii kumewafurahisha sana Makatekista ambao siku zote ndio wanaoitumia kwa ajili ya kufundishia watoto na waamini kwa ujumla, tulikuwa na pengo kubwa lakini sasa tunafuraha kupata katekesimu hii, tunashukuru sana kupata wazo hili kutoka idara ya katekesi jimbo na msimamizi kutekeleza wazo hili ambalo lina kichwa cha Bwana” amesema Katekesta Madenge

Naye Mkurugenzi wa Utoto Mtakatifu Jimboni Morogoro [PMS] Padre Melkiades Mogela amesema kuwa kuzinduliwa kwa katekesimu mpya ya jimbo iwe ni fursa kwa wazazi, na walezi kuitangaza injili kwa watoto wao, kama mhimili wa kwanza wa kukuza Injili kuanzia katika ngazi ya familia kwa kukaa na kusali pamoja na watoto wao ili kuifahamu imani yao, hasa kuwafafanulia maswali na majibu yaliomo katika kitabu hicho. Katekisimu mpya ilioboreshwa ni toleo la tatu ambayo imeanza kutumika mara baada ya uzinduzi wake ikiwa imeboreshwa kwa kufuatilia mtiririko uliopo katika katekesimu kubwa, ambapo katekesimu ya pili ilitoka mwaka 1995, hivyo waamini wa majimbo mbalimbali wanaalikwa kuinunua ili kuendelea kujiimarishwa katika maisha ya kiroho.

Jimbo Morogoro

 

 

30 May 2021, 16:13