Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya V ya Kipindi cha Pasaka Mwaka B wa Kanisa. Kristo Yesu ni Mzabibu wa kweli: Muhimu kujenga umoja na mafungamano ili kuzaa matunda ya toba, wongofu na utakatifu wa maisha. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya V ya Kipindi cha Pasaka Mwaka B wa Kanisa. Kristo Yesu ni Mzabibu wa kweli: Muhimu kujenga umoja na mafungamano ili kuzaa matunda ya toba, wongofu na utakatifu wa maisha. 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 5 ya Pasaka: Mshikamano na Yesu

Neno la Mungu linatualika tuujenge muunganiko na Mungu wetu aliye Mtakatifu katika Kristo Yesu, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu ili tuweze kuzaa matunda mema na kustahilishwa kuingia katika ufalme wa mbinguni. Ili tuweze kufanikiwa katika kutenda matendo mema kwa kuishi kwa upendo, sharti ni moja, kuunganika na Kristo aliye kama mzabibu nasi tukiwa kama matawi.

Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya neno la Mungu dominika ya tano ya Pasaka mwaka B. Neno la Mungu dominika hii linatualika tuujenge muunganiko na Mungu wetu aliye Mtakatifu katika Kristo Yesu, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu ili tuweze kuzaa matunda mema na kustahilishwa kuingia katika ufalme wa mbinguni. Ili tuweze kufanikiwa katika kutenda matendo mema kwa kuishi kwa upendo, sharti ni moja, kuunganika na Kristo aliye kama mzabibu nasi tukiwa kama matawi. Somo la kwanza la matendo ya mitume (Mdo 9:26–31), linasimulia maisha ya Mtakatifu Paulo mara baada ya kuongoka kwake. Sauli ambaye alikuwa mtesi wa Kanisa, alipoongoka na kuanza kuhubiri neno la Mungu, haikuwa rahisi kwa mitume wa Yesu kumwamini haraka. Ushuhuda wa Barnaba wa kuongoka kwake ndio uliowafanya mitume waamini kuwa kweli Sauli ameongoka nao wakampokea.

Mtume Barnaba ni mfano wa kuigwa. Kama Barnaba nasi tunapaswa kushuhudia kuongoka kwa wale ambao mbele ya macho ya Kanisa na jamii wanaonekana kuwa waovu kuwa sasa wamemwongokea Mungu na kuwa watu wapya. Paulo pia ni ishara wazi ya wongofu katika Kristo. Neema ya Mungu ni kubwa zaidi ya dhambi. Hakuna dhambi kubwa inayoweza kushida neema na huruma ya Mungu kwa mwongofu. Mungu anamsamehe kila anayetubu na kukiri makosa yake na anaweza kumchagua mtu yeyote anayemtaka yeye awe chombo cha kueneza habari njema ya wokovu hata kama mwanzoni alikuwa ni mdhambi. Hii ni habari njema, hatuna sababu ya kukata tamaa kwa sababu ya ukubwa wa dhambi zetu na hatuna sababu ya kubaki katika hali ya dhambi bali tufungue mioyo yetu, tumruhusu Kristo mfufuka aingie ili neema yake ifanye kazi ndani mwetu.

Mtume Paulo baada ya kupokelewa na mitume alihubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina lake Yesu, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani. Nao waliposhindwa kujibizana naye wakajaribu kumwua naye akakimbilia Kaisaria, akaenda mpaka Tarso akimhubiri Kristo. Paulo aliyatoa maisha yake yote, akawa tayari kuvumilia taabu zote (1Kor 4:9–13; 2Kor 6:4–10; 11:23–27) ili kumtangaza Kristo na kwake hakuna chochote kilichoweza kumtenganisha na upendo wa Kristo (Rum 8:35–39). Paulo aliipokea na kuitegemea neema ya Mungu ndiyo maana anasema; “Ni kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo, na neema ya Mungu haikuwa bure” (1Kor 15:10; 2Kor 3:5; 2Kor 4:7). Tumwombe Mungu kama alivyomteua mtume Paulo ili nasi tuwe ni vyombo viteule vya kueneza Habari Njema. Atujalie neema ya kueneza huruma na upendo wake katika familia, jumuiya, Kanisa na jamii kwa ujumla. Paulo alipodhulumiwa kwa sababu ya Injili, habari njema ya wokovu, hakukata tamaa na kurudi nyuma bali alisonga mbele akiitumainia neema ya Mungu. Nasi tuwe na ujasiri na tusione aibu wala kukata tamaa katika kuishuhudia Imani yetu kwa Yesu Kristo mfufuka.

Katika somo la pili la Waraka wa Kwanza wa Yohane kwa Watu Wote (1Yoh 3:18–24), Mtume Yohane anasisitiza mapendo ya kweli yaonekane zaidi katika kutenda mema; na kwani ni katika kutenda mema tunapata furaha na amani ya kweli katika maisha yetu. Tena tukitaka kuishi katika umoja na Mungu, yatupasa kumwamini Kristo na kumpenda jirani. Mtume Yohane anaposisitiza mapendo kwa jirani, anasisitiza mapendo yasiyo na unafiki wala hila. Ni mapendo yasiyo na masharti, kama anavyosema; “Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli. Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake.” Kisha akasisitiza; “Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri. Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye, naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa. Matunda ya kuzishika amri za Mungu na kuishi kwa upendo ni kwamba; “lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake.”

Mwinjili Yohane katika Injili ya leo (Yoh 15:1–8), kwa kutumia mfano wa mzabibu na matawi, anatueleza kwa kina kabisa uhusiano wetu na Yesu Kristo, Bwana na mwokozi wa maisha yetu. Mfano huu wa mzabibu na matawi yake unatuonyesha umoja uliopo kati ya Yesu na sisi wakristo-wafuasi wake. Kwa kujiunga na Yesu tu tutaweza kuzaa matunda ya mapendo na kutenda matendo mema. Kwa nguvu yetu wenyewe hatuwezi kitu. Yesu mwenyewe anaweka wazi ukweli huu akisema; “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wangu.”

Tuombe neema ili haya maneno ya Kristo yakae ndani mwetu na kweli yatusaidie kutenda matendo ya Kikristo. Tukae ndani ya Baba na mwana ili tuzae matunda mema ya wokovu.  Tuweni vyombo vya kuleta amani na upendo kati yetu. Tumwombe Mungu aziguse familia zetu, aguse miito yetu, aguse akili zetu ili zimwelekee yeye tu. Tumwombe baraka katika kazi za mikono yetu, kazi za akili zetu na atupe afya njema, ili tuweze kudumu katika kumtumikia yeye katika ndugu zetu. Tumwombe Bwana atupe moyo wa utayari ili tuendelee kuwa ni vyombo bora vya uinjlishaji kuanzia katika maisha yetu binafsi, familia, jumuiya na Kanisa kwa ujumla ili tuweze kustahilishwa kuurithi uzima wa milele ambao Padre kwa niaba yetu jamii ya wamiini anauomba katika sala ya koleta akisema; “Ee Mungu, umetuletea ukombozi na kutufanya watoto wako. Tunakuomba utusikilize kwa wema sisi wanao, ili katika kumwamini Kristo tupate uhuru wa kweli na urithi wa milele.” Na katika sala baada ya Komunio anahitimisha akisali; “Ee Bwana, tunakuomba uwe na sisi taifa lako. Na kama ulivyotujalia mafumbo haya ya mbinguni, utufikishe kwenye uzima, utuondoe katika maisha ya zamani na kutuweka katika maisha mapya.”

Jumapili 5 ya Pasaka
30 April 2021, 07:24