Tafakari ya Neno la Mungu: Sherehe ya Pasaka ya Bwana: Kiini cha imani ya Kanisa kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na Mkombozi wa ulimwengu. Tafakari ya Neno la Mungu: Sherehe ya Pasaka ya Bwana: Kiini cha imani ya Kanisa kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na Mkombozi wa ulimwengu. 

Sherehe ya Pasaka ya Bwana: Ufufuko wa Yesu Kiini cha Imani

Pasaka ni siku ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, ni siku ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti ambao sisi nasi kwa ubatizo tunakufa kuhusu dhambi na kufufuka pamoja na Kristo. Ni shangwe kuu kwani Bwana wetu Yesu Kristo amefufuka kweli kweli. Utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele (Lk.24:34; Ufu.1:6). Ufufuko wa Yesu ni kiini cha imani ya Kanisa kwa Yesu Kristo!Pasaka!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Pasaka. Pasaka ni siku ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, ni siku ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti ambao sisi nasi kwa ubatizo tunakufa kuhusu dhambi na kufufuka pamoja na Kristo. Ndiyo maana katika wimbo wa mwanzo tunaimba; “Nimefufuka na ningali pamoja nawe; umeniwekea mkono wako, maarifa hayo ni ya ajabu, alaluya (Zab.139:18, 5-6). Ni shangwe kuu kwani Bwana amefufuka kweli kweli. Utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele (Lk.24:34; Ufu.1:6). Pasaka ni “sherehe ya sherehe zote.” Sherehe hii tunaiadhimisha kwa majuma saba. Majuma haya saba Mama Kanisa anayaita “kipindi cha pasaka”. Hitimisho lake ni Sherehe ya Pentekoste. Tukumbuke kuwa kila jumapili ya mwaka ni Pasaka ya Bwana, kwani Kanisa huadhimisha kifo na ufufuko wake. Hii ni kuonyesha kuwa Imani na matumaini yetu yote, msingi wake ni ufufuko wa Yesu Kristo. Ndiyo maana mtume Paulo anasema; “Kama Kristo hakufufuka kutoka wafu, basi imani yetu ni bure (Rej. 1Cor 15:14-19). Kwa ufufuko wa Yesu, njia ya kwenda mbinguni kwa Baba imefunguliwa kama anavyosali Padre katika sala ya mwanzo; “Ee Mungu, umetufungulia leo mlango wa milele kwa njia ya Mwanao wa pekee aliyeshinda mauti. Tunakuomba utujalie sisi tunaoadhimisha kufufuka kwake Bwana wetu, tufufuke katika nuru yako kwa kufanywa wapya na Roho wako.” Hivyo ni siku ya furaha. Ni siku ya shangwe kama wimbo wa katikati unavyoimba; “Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, tuishangilie na kuifurahia” (Zab 118:24).

Somo la kwanza la Matendo ya Mitume (Mdo.10:34; 37-43), ni hotuba ya Mtume Petro akiwa nyumbani kwa Kornelio Kapteni/Jemedari wa jeshi la Kirumi aliyekaa katika mji wa Kaisaria. Kornelio alikuwa mwadilifu na mkarimu kwa maskini. Alipata maono akiagizwa atume wajumbe waende katika mji wa Yafa alikokuwako Petro akisali, ili aje kuwahubiria habari za Kristo mfufuka. Mungu alimwarifu Petro kwa njia ya  ndoto kuwafuata wajumbe wa Kornelio na kwenda nao nyumbani kwake. Mtume Petro anatii licha ya kuwa ilikuwa ni kinyume na sheria ya kiyahudi ya kuingia katika nyumba za wapagani na kula pamoja nao. Mtume Petro alipoingia nyumbani kwake, Kornelio alimkaribisha kwa heshima na kumwambia; tupo hapa kusikiliza ujumbe ambao Mungu amekupa kwa ajili yetu (Mdo 10:33). Mtume Petro akawaeleza habari za kuja kwake Yesu Kristo duniani; jinsi alivyohubiri katika nchi ya Palestina na kutenda mema na miujiza mbalimbali, akiponya watu magonjwa yao ya kimwili na kiroho.

Lakini alihukumiwa kifo cha msalaba pasipo na hatia (Mdo 10:39), na siku tatu baadaye Mungu alimfufua kutoka wafu (Mdo 10:40). Mtume Petro akasisitiza; “Sisi ni mashahidi wa tukio hili; tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kutoka wafu”. “Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.” Ujumbe huu ndio msingi wa yote ambayo Kanisa linahubiri hata leo. Ufufuko wa Yesu ni nguzo kuu ya imani yetu (1Cor 15:14). Sherehe ya pasaka ina maana tu kwa wale wanaofanywa wapya katika maisha ya kiroho kwa kufanya toba ya kweli na kuziacha njia zao za dhambi. Kumbe kwa ambaye katika kipindi cha kwaresima alifunga vyema, akasali vizuri, akatenda matendo ya huruma, akalisoma na kulitafakari Neno la Mungu na kumwongokea, Pasaka kwake ni siku ya furaha ni siku ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti.

Katika somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai, mtume Paulo anatueleza wazi matunda ya kufufuka na huku kufanywa upya kuwa; tumerudishwa katika maisha ya kweli katika Kristo (Kol 3:1). Tunashiriki uzima ule ule ambao Yesu mwenyewe anaoishi na amefufuka hafi tena. Hii inaonyesha jinsi gani sikukuu ya pasaka ilivyo na maana kubwa tunapofikiria juu ya maajabu ambayo Yesu ametutendea! Lakini kufufuka huku katika maisha mapya katika Kristo kusipofanyika ndani ya mioyo yetu, furaha yetu ya pasaka ni bure. Katika Ubatizo tulikufa na kufufuka na Kristo; tukaahidi kumfuata daima katika maisha ya taabu na raha. Yatupasa kuishi kadiri ya ahadi hiyo tukiacha mabaya na kutenda mema. Mtume Paulo anawaambia Wakolosai; “Mawazo yenu yalenge mambo ya mbinguni, siyo mambo ya duniani” (Kol 3:2). Ujumbe huu unatuhusu sisi sote tuliokwisha kubatizwa. Hii haimaanishi kuwa tuupuuze ukweli wa maisha. La hasha kama watu wengine, tunapaswa kuchapa kazi na kujibidisha katika kuleta maendeleo katika maisha yetu kwani Paulo anasema “asiyefanya kazi na asile”. Lakini yote yanapaswa kulenga katika sifa na utukufu wa Mungu. Ni kwa maneno na matendo yetu tunaushuhudia ufufuko wa Yesu Kristo.

Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 20:1-9), inasimuliwa ukweli mkuu wa imani yetu kwamba Kristo amefufuka. Ushahidi ni wazi: Kaburi li tupu, vitambaa alivyolalia vimezongwazongwa, na baadaye akajionyesha kwa wafuasi wake. Injili inatueleza kuwa; Maria Magdalena alikwenda kaburini mapema asubuhi siku ya jumapili, kungali bado giza na kukuta kaburi li wazi. Alirudi mbio kuwapasha habari mtume Petro na Yohane anayetajwa kama “mwanafunzi yule mwingine ambaye Yesu alimpenda”. Petro na Yohane walishika njia kwa mbio kuelekea kaburini. Nao waliona kaburi li wazi, wakaingia, wakaviona vitambaa vya sanda vimelala na ile leso iliyokuwako kichwani pake yake ikiwa imezongwazongwa mbali mahali pa peke yake. Yohane alipoona na alimini. Hivi leo ni siku ya furaha kubwa tunapoadhimisha kiini cha imani yetu. Tunaalikwa kufurahia ufufuko wa Yesu na ufufuko wetu pia pamoja na Kristo.

Tukumbuke kuwa hakuwezi kuwa na furaha ya kweli ya Pasaka kwa walioshindwa kufufuka, kutoka katika dhambi na kuingia katika maisha mapya ya kipasaka katika Kristo. Ndiyo maana katika sala ya kuombea dhabihu Padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali; “Ee Bwana, tunakutolea sadaka kwa furaha ya sikukuu ya Pasaka, Kanisa lako linazaliwa upya na kulishwa kwa sadaka hizi.” Nao utangulizi unashuhudia kuwa ni “shangwe kubwa zaidi; kwa kuwa Kristo ametolewa sadaka awe Pasaka yetu. Yeye ndiye Mwana kondoo wa kweli aliyeondoa dhambi za dunia, alishinda mauti yetu kwa kufa kwake, akaturudishia uzima wetu kwa kufufuka kwake. Na kwa sababu hiyo, watu wote wanaitukuza Sherehe ya Pasaka kwa furaha kubwa po pote duniani. Nao Malaika wote wa mbinguni wanaimba wimbo wa kukutuza, wakisema bila, mwisho.” Mitume walishuhudia ufufuko wa Yesu mahali popote walipokwenda. Nasi pia tuushuhudie ufufuko wa Yesu na ufufuko wetu; kwa njia ya maisha yetu mema ya Kikristo.

Pasaka ya Bwana

 

03 April 2021, 16:29