Tafuta

Jumapili ya Huruma ya Mungu: Umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho na Maana ya Saa Kuu ya Huruma ya Mungu katika maisha ya mwamini! Jumapili ya Huruma ya Mungu: Umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho na Maana ya Saa Kuu ya Huruma ya Mungu katika maisha ya mwamini! 

Jumapili ya Huruma ya Mungu: Upatanisho na Sala Kuu ya Huruma

Padre Wojciech anafafanua kwa kina na mapana kuhusu Saa ya Huruma Kuu; Umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, ili kulipyaisha Kanisa la Kristo kwa chachu ya utakatifu wa maisha. Umuhimu wa ushiriki wa Ibada ya Misa Takatifu kwa uchaji, Sakramenti ya Upatanisho, Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu, sala sanjari na kudumisha Ibada ya Njia ya Msalaba katika maisha!

Na Padre Wojciech Adam Kościelniak, - Kiabakari, Musoma, Tanzania.

Kituo cha Hija Kitaifa cha Huruma ya Mungu, Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma ni shule ya sala, toba na wongofu wa ndani kwa waamini ndani na nje ya Tanzania. Kama sehemu ya maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu Padre Wojciech Adam Kościelniak, Muasisi wa Kituo cha Hija Kitaifa cha Huruma ya Mungu, Kiabakari anafafanua kwa kina na mapana kuhusu Saa ya Huruma Kuu; Umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, ili kulipyaisha Kanisa la Kristo kwa chachu ya utakatifu wa maisha. Waamini wajitahidi kushiriki Ibada ya Misa Takatifu kwa uchaji na ibada; wakimbilie daima huruma ya Mungu kwa Sakramenti ya Upatanisho; wajenge utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu na maisha ya sala sanjari na kudumisha Ibada ya Njia ya Msalaba katika uhalisia wa maisha yao. Jumapili ya Huruma ya Mungu ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000. Mtakatifu Maria Faustina Kowalska ni kati ya watakatifu waliotangaza, wakashuhudia na hatimaye, kueneza Ibada ya huruma ya Mungu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, huruma ya Mungu ni kinga na kimbilio la maskini na wadhambi. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu katika maisha yao, ili waweze kupata msamaha na maondoleo ya dhambi. Huruma ya Mungu inazidi uelewa, maarifa na ufahamu wa akili ya binadamu.

Katika mafunuo yake kwa Mtakatifu Sista Faustina, Bwana wetu Yesu Kristo alimwomba asali na kutafakari kuhusu Mateso yake kila alasiri saa tisa kamili saa itukumbushayo Kifo cha Bwana Msalabani. “Saa tisa kamili omba Huruma yangu, hasa kwa ajili ya wakosefu; na walau kwa muda mfupi tu jizamishe kwenye Mateso yangu, hasa pale nilipoachwa peke yangu bustanini katika saa ya masikitiko makuu, nikatoka jasho la Damu... Hii ni saa ya Huruma Kuu... Katika saa hii sitakataa ombi lolote litakaloombwa na roho yoyote kwa ajili ya Mateso yangu.” (1320). “Kila mara usikiapo saa tisa inagonga, jizamishe kabisa katika Huruma yangu; uiabudu na kuitukuza; usifu uweza wake mkuu kwa ajili ya dunia nzima, na hasa kwa ajili ya wakosefu; kwa kuwa katika saa hiyo Huruma ilifunguliwa wazi kwa ajili ya kila roho. Katika saa hii unaweza kujipatia kila kitu, kwa ajili yako na wengine waombao; ilikuwa ndiyo saa ya neema kwa dunia nzima-Huruma iliishinda Haki (...) Jitahidi kusali Njia ya Msalaba katika saa hii upatapo nafasi; na iwapo hutaweza, walau ingia kanisani kwa muda mfupi, uabudu Sakramenti Takatifu, ambamo mna Moyo wangu uliojaa Huruma; na basi, iwapo utashindwa kuingia kanisani, walau jizamishe katika sala, hata kwa dakika chache, popote pale utakapokuwa.” (1572).

Kutokana na maelezo haya ni dhahiri kwamba Bwana wetu anataka tuzamishe mawazo na mioyo yetu katika Mateso yake; tuyatafakari kila ifikapo saa tisa alasiri, bila kujali uzito wa shughuli tulizo nazo. Ataka tuombe Huruma yake. Katika Kitabu cha Mwanzo (Mwa 18:16-32), Abrahamu alimwomba Mungu apunguze masharti ya Huruma yake kwa watu wa Sodoma na Gomora. Hapa, Yesu mwenyewe anatupunguzia masharti kwa sababu ya majukumu mbalimbali tuliyo nayo maishani na anatuomba tusali walau kidogo tu tukiomba Huruma yake, ili aweze kutumwagia sote Huruma yake. Labda sote hatuwezi kusali Njia ya Msalaba au kumuabudu Yesu katika Ekaristi Takatifu, lakini tunaweza kunyamazisha akili na mawazo yetu kwa muda mfupi, tukamfikiria alivyoachwa mwenyewe bustanini Gethsemane akiteseka. Tunaweza kusali sala fupi walau ya mshale kama: "Ee Yesu, unihurumie!" au "Ee Yesu, kwa ajili ya Mateso yako makali, utuhurumie sisi na dunia nzima!" Ingawaje hii yaweza kuonekana ni tafakari fupi sana, lakini inatuleta ana kwa ana na Msalaba wa Yesu; na kama Mtakatifu Papa Yohane Paulo II alivyoandika kwenye barua yake ya TAJIRI WA HURUMA: "Ufunuo wa Upendo wenye Huruma hutimilika katika Msalaba” (8). Anaendelea kuandika kuwa Mungu anatualika "kumwonea huruma Mwanaye wa pekee Msulibiwa” (8). Hivyo, tafakari yetu itufikishe katika hali ya upendo ambao "siyo tu tendo la mshikamano na Mwana-wa-mtu Mteseka, bali pia ni namna fulani ya 'huruma' ambayo kila mmoja wetu anamwonesha Mwana wa Baba wa milele’ (8).

Napenda nitoe tahadhari kuhusu upotoshaji unaofanywa na baadhi ya waamini ambao wanafundisha kwamba Rozari ya Huruma (Divine Mercy chaplet) inatakiwa kusaliwa saa tisa katika Saa ya Huruma ya Mungu peke yake na kwamba Saa ya Huruma ya Mungu maana yake ni kusali tu Rozari ya Huruma saa tisa alasiri. Dhana hii si ya kweli. Hakuna sehemu hata moja katika Shajara ya Mtakatifu Sista Faustina ambapo Yesu anamwagiza Sista Faustina - na kupitia kwake anatuagiza sote - asali Rozari ya Huruma Saa ya Huruma Kuu kwa Ulimwengu Mzima. Alisema yafuatayo, nanunkuu tena: “Kila mara usikiapo saa tisa inagonga, jizamishe kabisa katika Huruma yangu; uiabudu na kuitukuza; usifu uweza wake mkuu kwa ajili ya dunia nzima, na hasa kwa ajili ya wakosefu; kwa kuwa katika saa hiyo Huruma ilifunguliwa wazi kwa ajili ya kila roho. Katika saa hii unaweza kujipatia kila kitu, kwa ajili yako na wengine waombao; ilikuwa ndiyo saa ya neema kwa dunia nzima-Huruma iliishinda Haki (...) Jitahidi kusali Njia ya Msalaba katika saa hii upatapo nafasi; na iwapo hutaweza, walau ingia Kanisani kwa muda mfupi, uabudu Sakramenti Takatifu ya Ekaristi, ambamo mna Moyo wangu uliojaa Huruma; na basi, iwapo utashindwa kuingia Kanisani, walau jizamishe katika sala, hata kwa dakika chache, popote pale utakapokuwa.” (1572).

Hivyo, unaweza kusali Rozari ya Huruma wakati wowote na saa yoyote na si saa 9 alasiri tu kama wanavyopotosha wengine. Unaweza kusali pia saa tisa lakini Saa ya Huruma ya Mungu lengo lake na mantiki yake ni pana na kubwa zaidi kuliko kusali Rozari ya Huruma peke yake. Bila kutafakari Mateso ya Bwana katika Saa ya Huruma ya Mungu tutakuwa hatujatimiza lengo lake hata kama tutasali Rozari kumi za Huruma ya Mungu. Nawaombeni sana na nawatahadharisha sana - tufuate kwa uaminifu kauli na mafundisho ya Yesu mwenyewe kupitia kwa Mtakatifu Sista Faustina. Tafsiri nyingine ni upotoshaji wa waamini. Tuepuke tabia za namna hii. Na wanaofundisha hivyo mwanyooshe na kuwasaidia waelewe usahihi wa mafundisho ya Kanisa!

Ibada ya Upatanisho: “Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; ikiwa ashona, kile kipya kilichotiwa huliharibu lile vazi kuukuu, na pale palipotatuka huzidi. Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya katika viriba vipya.” (Mk 2:21-22). Somo hili la Injili ya Mtakatifu Marko tunalifahamu fika. Katika Somo hili Yesu anatuonya tusishone kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu wala kutia divai mpya katika viriba vikukuu. Matokeo ya tendo hili yanajulikana. Katika lugha asilia ya Injili hii - lugha ya Kigiriki - neno lililotafsiriwa kwa kiswahili kwa msamiati huu - “pale palipotatuka huzidi” - ni neno “mpasuko”. Neno hili tunafahamu linamaanisha nini katika ulimwengu tunamoishi. Ni mpasuko, ni utengano. Tunapoadhimisha Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo 18-25 Januari kila mwaka, ndipo tunapogundua kinagaubaga jinsi Kanisa moja la Kristo lilivyotatuka kwa mipasuko na michaniko mingi midogo midogo na mikubwa. Kanisa ni moja na linaundwa na Wakristo waliogawanyika, waliotawanyika, waliotengana, waliochanika na kupasuka katika imani zao, madhehebu yao, safari zao za kwenda mbinguni. Mipasuko na michaniko ni ishara ya ukuukuu wa kitu fulani. Kwa kawaida vitu vya zamani ni vidhaifu na vinachanika na kupasuka kwa upesi. Gari la zamani linaharibika mara kwa mara, nyumba ya zamani huwa inapasuka hapa na pale, nguo zetu za zamani zinachanika na kutatuka kiurahisi.

Uchakavu wa Kanisa na mipasuko yake haitokani na umri mkubwa wa Kanisa letu la karne ishirini sasa. Bali zaidi, uchakavu wa Kanisa unatokana na ukweli kwamba Kanisa ni jumuiya ya waamini ambao - bila kujali umri wao wala tarehe za kuzaliwa za kila mmoja wao - wanambeba na kumtunza ndani mwao ‘mtu wa zamani’, mtu wa dhambi. Mgawanyiko, utengano na mipasuko ndani ya Kanisa la Kristo vinaanzia kwenye nafsi ya kila mmoja wetu na kuenea katika mahusiano yetu, mahusiano ya jumuiya za waamini na madhehebu. Lakini kila mmoja wetu aliitwa na Yesu tuingie Kanisani, tuwe Kanisa, yaani tuvue utu wa kale kwa kudhamiria kabisa na si kimchezomchezo na kufufuka kwa utu mpya ndani yake Yesu Kristo Mfufuka, tuzaliwe upya katika Kristo - Adamu mpya - kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Somo la Injili hii ya Mtakatifu Marko linatuita kwa upyaisho huo kamili wa nafsi zetu na maisha yetu, kwa Pasaka yetu kamili katika Pasaka ya Bwana - yaani kuacha kabisa yaliyopita, kumzika mtu wa zamani ndani mwetu kwa sas ana kwa daima, mtu wa dhambi na kufufuka kwa maisha mapya kabisa ya Mashauri ya Kiinjili. Maisha ya -‘ndiyo, ndiyo; hapana, hapana!’.

Kinyume cha hatua hii ya mabadiliko kamili ya kipasaka - wengi tunafanya mabadiliko “feki”, mabadiliko robo, mabadiliko ya juu juu tu. Hapo Mkristo Mbatizwa kwa makusudi mazima anambakiza mtu wa zamani, mtu wa dhambi ndani yake, anaendelea kuishi maisha ya zamani na huenda kutoka katika Injili ya Kristo anachagua sehemu 2-3 zinazomfaa kwa mfumo wa maisha ya “Ukristo feki”, Ukristo jina tu; anachagua na kukubali huenda maneno machache tu ya Yesu yanayomfaa katika Ukristo huo feki na anashona maneno haya ya Bwana kama viraka katika vazi kuukuu la mtazamo wake wa utu wa zamani. Kanisa linaendelea kuwa na mitatuko, michaniko na mipasuko mingi kwa sababu hiyo, linazeeshwa na kudhoofishwa kwa utu wa zamani uliotiwa viraka vichache vya Injili katika nafsi na maisha ya waamini wake. Mitatuko, michaniko, mipasuko ya kila mmoja wetu inalifanya Kanisa kuwa vilevile, limegawanyika na kutawanyika, limetatuka, kuchanika na kupasuka.

Tufanyeje? Inawezekana kweli kubadilisha hali hii? Somo letu la Injili linatuonya tusijaribu kufunika mipasuko ya Kanisa kwa viraka vilivyotolewa kutoka mahali pengine. Haitoshi kuimba nyimbo za Kanisa la Mashariki kama ishara ya sala ya pamoja wakati wa Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo. Haitoshi kusali katika juma hilo - ili wanafunzi wa Yesu hatimaye wawe wamoja. Haitoshi kuwaalika wachungaji wa madhehebu mengine katika ibada za Juma hilo. Na baada ya ibada hizo kila mchungaji na kila mkristo anarudi kwenye dhehebu lake akiendelea kuamini kwamba Kanisa lake ni bora zaidi na la kweli na mengine ni feki. Na tunaendelea kuishi vivyo hivyo tulivyozoea na michaniko na mitatuko na mipasuko inabaki pale pale. Miaka inapita na kuta za uadui, mashaka, wasiwasi, woga, kutopendana na kutofahamiana zinaendelea kuimarika na kututenganisha. Tunahitaji toba na wongofu wa ndani, mabadiliko ya kweli ndani yake Kristo Mfufuka, kila mmoja wetu. Upyaisho mkamilifu wa maisha yetu; tunahitaji kumzika kabisa kwa milele yote yule mtu wa zamani, yule mpagani, anayetutawala ndani mwetu kwa kutumia mizizi ya dhambi, tamaa ya macho, tamaa ya mwili na majivuno - katika mawazo, maneno, maamuzi na mitazamo yetu. Umoja wa Kanisa ni tunda la toba, wongofu wa ndani na wa kudumu wa kila mmoja wetu, kila familia, kila jumuiya, kila shirika na nyumba ya kitawa, kila JNNK, kila Parokia. Kumvua na kumzika mtu wa kale na kumvaa Kristo kikamilifu katika upya wa maisha ya kikristo.

Katika hija yetu tukiwa hapa kwa Baba wa Huruma tujihoji kwa ujasiri wa kikristo katika ukweli wote, katika Mwanga wa Roho Mtakatifu, hali yangu ikoje, hali yetu ikoje kiukweliukweli? Yesu anatuambia - iweni wenye huruma kama Baba! Kauli hii inadai wongofu wetu kamili. Mabadiliko katika fikra na nyanja zote. Kama Baba! Pamoja na hali halisi ya Kanisa letu linalozeeshwa kwa michaniko na mipasuko yetu na maisha ya kujaribu kuchanganya upagani wetu na Ukristo wetu, ni jambo linalotia moyo na nguvu kabisa kumwona Yesu ndani ya Kanisa lake. Pamoja na matatizo yote tuliyo nayo sisi sote ni Sakramenti ya Yesu. Ni jambo linalotia moyo na nguvu kumwona Yesu katika Maandiko Matakatifu, katika Ekaristi Takatifu. Lakini Mungu anatamani sana tumgundue Yesu, tutambue uwepo wake ndani ya kila mmoja wetu. Ukweli huu, hadhi hii ya kuwa mtoto wa Mungu, mwana wa Mungu imefunikwa mara nyingi kwa dhambi zangu, ujinga wangu, hata uelewa wangu wa dini uliopotoka.

Mungu Baba daima anakusudia kunisaidia kuondoa kila kitu kinachomfunika Mwanaye ndani mwangu na kuponya mipasuko, michaniko na majeraha yanayoletwa na mkanganyiko wangu wa kushindwa kumfuata Kristo kwa moyo usiogawanyika. Kazi hii si mastahili yangu hata kidogo, wala si haki yangu iwe hivyo. Ukweli huu ni hali halisi aliyofikiria Mungu mwanzoni kabisa mwa uumbaji wa ulimwengu aliponifikiria kwanza. Mungu aliona sura ya Mwanaye ndani mwangu. Kila mmoja wetu anabeba ndani mwake ufanano huo, kwa sababu tuliumbwa kwa sura na mfano wake. Ukweli huu uliandikwa na Yohane Mwinjili mwanzoni kabisa kwa Injili yake - Yn 1:1-5.9-13: “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza (…) Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.”

Mwenzangu, ulipata ujumbe huu sawasawa? “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.’ Wewe na mimi na sisi sote na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana vilifanyika kwa Neno, "Logos", Nafsi ya Pili ya Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo. Tulifanywa kwa sura na mfano wake. Katika maisha yetu tunakazana kwa msaada wa Yule Mwovu kufuta kabisa ufanano wetu na Yesu, kufunika na kuzika sura ya Mwana wa Mungu kwa vifusi vya dhambi zetu na uovu wa kila aina. Kazi ya Baba wa Huruma ni kufukua Sura ya Mwanaye ndani mwetu. Kazi na wajibu wangu ni kushirikiana na Mungu katika lengo hili. Hii ndiyo kazi ya wongofu wetu na ukombozi wetu. Baba Mtakatifu Francisko alisema kwamba katika kazi ya Ukombozi, Mungu hapachiki viraka katika nafsi zetu. Kufikiri kwamba dhambi zangu zinaleta mitatuko katika roho yangu na kwa njia ya Ukombozi Bwana anatia viraka palipotatuka - ni kosa. Ukweli ni kwamba, Yesu anapotukomboa, anatuumba upya. Kila mara tunapoenda kuungama anatuumba upya. Na kila mara anatuumba vizuri zaidi. Usiku wa Pasaka tuliimba kwamba kazi ya uumbaji ilikuwa nzuri mno, lakini kazi ya ukombozi ilikuwa nzuri mno zaidi. Baada ya Ibada ya Upatanisho wakati wa Sherehe hii ya Huruma ya Mungu tutaondoka hapa tukiwa bora zaidi kuliko wakati ule Bwana alipotuwaza kwanza katika kazi ya uumbaji.

Kumbe, wewe ni Mtoto wa Mungu. Umepewa hadhi ambayo haifutiki. Hakuna nguvu na mamlaka duniani na mbinguni inayoweza kukunyang’anya hadhi hiyo. Kwa dhambi zetu tunaifunika hadhi hiyo, tunaificha, tunaizika, lakini Baba wa Huruma daima anaondoa mapazia hayo ya dhambi kwa huruma yake na kutuonyesha daima, tazama, jinsi ulivyo kweli katika hulka yako. Kila mmoja wetu ni sura ya Mwana wa Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo. Ndiyo maana ibada ya kwanza ya Maadhimisho ya Sherehe ya Huruma ya Mungu ni ibada hii ya Upatanisho ya pamoja na ibada ya mwisho ya Mkesha Mtakatifu itakayotuandaa moja kwa moja kwa Misa Kuu ya Sherehe ya Huruma ya Mungu ni Ibada ya Kudhihirisha Uso wa Huruma katika nafsi zetu na maisha yetu. Hapo tutakuwa tuemkamilisha kazi ya uumbaji mpya wa nafsi zetu ndani ya Sherehe hii ya pekee ya Huruma ya Mungu. Ukweli huu na hadhi hii ni jambo ambalo unapaswa kulipokea kwa imani, maana neema hii kubwa haituondolei uhuru wa kuamua na sisi bado tunaweza kutenda dhambi. Neema ya kuhesabiwa haki mbele ya Mungu kwa njia ya Ukombozi wa Bwana wetu Yesu Kristo haituondolei uwezo wa kutenda dhambi! Hii ndiyo Injili anayoihubiri Mtakatifu Paulo. Nasi tuifuate kwa uaminifu. Amina.

11 April 2021, 08:06