Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu nchini Ghana wanalaani mauaji ya kijana mdogo wa umri wa miaka kumi aliyeuawa na vijana wenzake. Baraza la Maaskofu nchini Ghana wanalaani mauaji ya kijana mdogo wa umri wa miaka kumi aliyeuawa na vijana wenzake. 

Ghana:Mauaji kwa sababu ya kishirikina ni hatari kwa usalama wa kitaifa!

Baraza la Maaskofu nchini Ghana wanalaani mauaji ya kijana mdogo wa umri wa miaka kumi aliyeuawa na vijana wenzake,kwa nia ya kutumia sehemu za mwili wake katika mazoezi ya kishirikina ili wawe matajiri.“Kitendo cha kutisha cha vijana hawa kinapaswa kutumika kama kichocheo cha kugundua kwamba labda tumepoteza dira yetu kama watu,mtu binafsi na kama taifa zima”,maaskofu wamesema.

Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Lazima tuwalinde vijana wetu kutokana na mambo fulani. Kwa hivyo sehemu ya kile ambacho vyombo vya habari vinapendekeza vinapaswa kukaguliwa kwa vijana, hasa mazoea yanayodaiwa kupata pesa rahisi na haraka. Amesema hayo Askofu Mkuu Philip Naameh Tamale, Rais wa Baraza la Maaskofu nchini Ghana (GCBC), katika taarifa juu ya mauaji ya kimila, mara baada ya polisi kuwakamata vijana wawili, mmoja mwenye umeri wa 16 na mwingine 18, kwa mashtaka ya kumuua kikatili kijana mdogo Ishmael Mensah Abdallah, mwenye umri wa miaka 10 tu, kwa nia ya kutumia sehemu za mwili wake kwa mazoezi ya kishirikina. Tukio hili lilitokea siku ya Jumamosi Takatifu tarehe 3 Aprili 2021

Tukio hili la kusikitisha na la kutisha, lililotokea katika kitongoji cha Kasoa katika Mkoa wa Kati, linatupatia changamoto sisi kama watu na kama taifa, na linahitaji hatua za haraka kuzuia tukio kama hili jingine kwa siku zijazo lisitokee amesema Askofu Mkuu Naameh. “Kitendo cha kutisha cha vijana hawa kinapaswa kutumika kama kichocheo cha kugundua kwamba labda tumepoteza dira yetu kama watu, mtu binafsi na kama taifa zima.

Askofu mkuu Naameh amefafanua zoezi hili la waganga wa kienyeji ni tishio kwa usalama wa kitaifa. Katika taarifa yake, Rais wa Baraza la Maaskofu (GCBC) ameshutumu vyombo vya habari vya ndani kwa vipindi vya utangazaji ambavyo watu wanaodaiwa kuwa wachawi hufundisha mazoezi  ya kichawi na ahadi ya kuwafanya watu kuwa matajiri kwa muda mfupi tu. Hii inamaanisha kuwa hatujachukua tahadhari za kutosha kutathmini kile tunachowalisha akili za vijana wetu hadi kufikia hatua kwamba wanafikiria uwezekano wa kumuua mtu kwa utajiri sio mbaya.”

Askofu Mkuu Naameh kwa niaba ya Maaskofu wote wa Ghana anaomba “wadau wote, hasa wasimamizi wa nafasi yetu ya vyombo vya habari, kukandamiza shughuli za wadanganyifu hawa  ambao kupitia vituo vyao vya kutoa sauti wanaendelea kueneza uovu na udanganyifu wa pesa rahisi kutoka kwa watangazaji na majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Maaskofu wanalaani tabia ya kupendelea utajiri, unaodhihirishwa katika kuabudu hata matajiri bila kuwa na shaka la chanzo cha utajiri wao, wakilinganisha michango na uongozi mzuri na imani kwamba pesa lazima itolewe kwa ndoana au kwa hila na ili kuweza kupanga njia mpya ya  kuelekea maadili halisi, kama vile ya kufanya kazi kwa bidii na uaminifu ndani ya jamii.  Aidha maaskofu hao wamemkabidhi roho ya kijana Ishmael Mensah Abdallah kwa huruma ya Mungu na kuwaombea faraja wazazi na familia nzima na Bwana awaongoze vijana katika ulimwengu huu wa kisasa, amehitimisha ujumbe huo.

16 April 2021, 14:44