Patriaki Bartholomeo wa kwanza katika katekesi makini kuhusu Kipindi cha Kwaresima anakazia umuhimu sala, toba, wongofu wa ndani na upendo kwa Mungu na jirani ili kuondokana na ubinafsi. Patriaki Bartholomeo wa kwanza katika katekesi makini kuhusu Kipindi cha Kwaresima anakazia umuhimu sala, toba, wongofu wa ndani na upendo kwa Mungu na jirani ili kuondokana na ubinafsi. 

Patriaki Bartolomeo wa Kwanza: Katekesi Makini ya Kwaresima!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza: Kwaresima ya Mwaka 2021 ni Karantini ya pekee. Siku 40 zinazomwezesha mwamini kuingia katika undani wa maisha yake, tayari kufanya toba na wongofu wa ndani, kwa kujikita na kuambata mambo msingi ya maisha. Kipindi cha Siku 40 ni wakati wa kufunga, tayari kujiondoa katika mambo yale yanayomzamisha mwamini katika malimwengu. Yaani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwaresima ni Kipindi cha toba na wongofu wa ndani; ni muda wa sala inayomwilishwa katika matendo; kielelezo makini cha imani tendaji. Ni muda wa kuondokana na uchoyo, ubinafsi, tabia ya mtu kutaka kujitafuta binafsi na ulaji wa kupindukia. Hiki ni kipindi cha huduma ya upendo kwa Mungu na jirani, ili hatimaye, kumwachia Mwenyezi Mungu aweze kufanya maskani miongoni mwa waja wake. Katika toba, wongofu wa ndani na sala, Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake mwanga unaoyaangazia maisha ya ndani, ili kuwa na maamuzi makini, tayari kutekeleza dhamana na utume kwa uwajibikaji bora zaidi. Ni wakati wa sala binafsi na zile za kijumuiya ili sala hizi ziwe ni chemchemi ya faraja, ujasiri, sadaka, msamaha na upatanisho. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol, tarehe 15 Machi 2021 amezindua Kipindi cha Kwaresima kwa katekesi makini inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa Fumbo la Msalaba yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu na kwa kadiri ya Kalenda yao ya Liturujia, wataadhimisha Pasaka ya Bwana Mei Mosi, 2021. Hiki ni kipindi cha Siku 40 za: Sala, Toba na Wongofu wa ndani.

Ni wakati wa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Kwa namna ya pekee, Kwaresima ni mwaliko kwa kila mwamini kubeba vyema Msalaba wa maisha yake na kumfuasa Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu. Msalaba ni hukumu na ahadi ya ulimwengu. Mtakatifu Paulo katika Waraka wake wa Pili kwa Wakorintho 4: 8- 9 anasema: “Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi”. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol anatumia sehemu hii ya Maandiko Matakatifu kufanya rejea mintarafu janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kumekuwepo na athari kubwa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Kuna watu wengi wanaendelea kupoteza maisha. Kuna mamilioni ya watu ambao wanaishi kwenye karantini.

Kwaresima ya Mwaka 2021 ni Karantini ya aina yake! Yaani ni Siku 40 zinazomwezesha mwamini kuingia katika undani wa maisha yake, tayari kufanya toba na wongofu wa ndani, kwa kujikita na kuambata mambo msingi ya maisha. Kipindi cha Siku 40 ni wakati wa kufunga, tayari kujiondoa katika mambo yale yanayomzamisha mwamini katika malimwengu. Ni wakati wa kufanya mchakato wa dhati ili kuratibu maana ya maisha pamoja na mahusiano yao na malimwengu. Ni muda muafaka wa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo, kama kielelezo cha imani tendaji. Kufunga kuwe na chapa ya Ufufuko wa Kristo Yesu, yaani mfungo umwezeshe mwamini kuendelea kuwa ni chombo cha furaha na ujenzi wa urafiki na udugu wa kibinadamu, ili kuwafungulia waamini neema ya kuwa tena ni wana wa Mungu. Neema na baraka ya Kipindi cha Kwaresima inaboresha sana sadaka ya upendo na majitoleo kwa Mungu na jirani. Neema hii ni msaada mkubwa katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Uchafuzi na uharibifu wa mazingira unajenga uadui kati ya binadamu na mazingira.

Jicho la Mwenyezi Mungu lililosheheni huruma na upendo lilimwokoa Zakayo na Mathayo waliokuwa watumwa wa fedha; lilimwokoa mwanamke mzinzi aliyekuwa amehukumiwa adhabu ya kifo kwa kupigwa mawe na Magdalena aliyekita furaha yake kwa kiumbe. Ni jicho la huruma lililomfanya Mtume Petro aangue kilio baada ya usaliti. Ni huruma na msamaha wa dhambi uliomhakikishia Paradiso, mwizi aliyetubu. Kristo Yesu ni ufunuo wa sura inayoonekana ya Baba asiyeonekana; sura ya Mungu anayejifunua kwa uweza, lakini zaidi kwa njia ya msamaha na huruma! Kipindi cha Kwaresima kimetundikwa katika huruma, msamaha na upendo wa Mungu kwa binadamu. Huruma ya Mungu inakita mizizi yake katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu!

Kipindi cha Kwaresima ni mwaliko mahususi kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo; kwa kumwilisha Amri Kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani. Ni kwa njia hii, Wakristo wanaweza kuwa ni “chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” Mt. 5:13-14. Kwaresima ni kipindi cha kuondokana na uchoyo pamoja na ubinafsi, ambao hauna tija wala mashiko kwa maisha ya kiroho. Kwaresima iwasaidie waamini kutubu na kumwongokea Mungu tayari kupyaisha maisha yao yanayofumbatwa katika msamaha, manga’amuzi ya maisha ya kiroho na kiutu; ushiriki mkamilifu wa Ekaristi Takatifu; kwa kuonesha ukarimu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol anahitimisha katekesi yake kwa mwaliko kwa waamini kufunga na kusali, ili kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu ili uweze kuwaokoa na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Patriaki Kwaresima
16 March 2021, 16:30