Tafakari ya Neno la Mungu, Maadhimisho ya Juma Kuu: Jumapili ya Matawi, mwanzo wa maadhimisho ya sikukuu muhimu za historia ya Ukombozi. Tafakari ya Neno la Mungu, Maadhimisho ya Juma Kuu: Jumapili ya Matawi, mwanzo wa maadhimisho ya sikukuu muhimu za historia ya Ukombozi. 

Juma Kuu: Jumapili ya Matawi: Fumbo la Mateso na Kifo cha Yesu

Ni dominika ya furaha kwa sababu tunakumbuka siku ile Yesu alipoingia Yerusalemu kwa shangwe. Hii ni ishara ya nje ya kumuungama Kristo Yesu aliyeteseka, akafa na kufufuka kwa ajili yetu sisi. Pili, Kanisa linaweka mbele yetu mateso makali aliyoyapata Kristo na kutueleza mapato yake, ushindi dhidi ya dhambi na mauti, ushidni unaodhihirishwa na utukufu wa ufufuko wake kwa wafu!

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya matawi. Ni Dominika ya furaha na ni Domenika ya huzuni au mateso. Ni Dominika ya furaha kwa sababu katika sehemu ya kwanza ya ibada ya Dominika hii, tunakumbuka siku ile Yesu alipoingia Yerusalemu kwa shangwe akiwa amepanda mwanapunda kama ishara ya mfalme wa amani na utakatifu wake. Watu walimlaki kwa shangwe wakiwa na matawi ya mitende, huku wakiimba nyimbo za furaha (Zek 9:9; Mt. 21:5; Yoh 12:14). Sisi tunapofanya haya maandamano sio kwamba tunaiga ama kurudia mambo ya kihistoria yaliyopita, bali ni ishara tu ya nje ya kumwungama Kristo aliyeteseka, akafa na kufufuka kwa ajili yetu sisi kuwa ni mfalme wa maisha yetu. Sehemu ya pili ya ibada ya Dominika hii ni kumbukumbu ya historia ya mateso na kifo cha Yesu Kristo. Katika sehemu hii ya pili Kanisa linaweka mbele yetu mateso makali aliyoyapata Kristo na kutueleza mapato yake, ushindi dhidi ya dhambi na mauti, ushidni unaodhihirishwa na utukufu wa ufufuko wake kama anavyosali Padre kwa niaba ya jamii ya waamini katika sala ya mwanzo-koleta akisema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, ulitaka Mwokozi wetu atwae mwili na kuteswa msalabani ili wanadamu wapate kufuata mfano wa unyenyekevu wake. Utujalie kwa wema wako tuweze kuwa na uvumilivu kama yeye, na kustahili kushi mateso ya Yesu Kristo ambayo tunaweza kuyafahamu vizuri tu, tukiyatazama pamoja na ufufuko wake. Kwa hiyo liturjia ya adhimisho hili imejaa mwanga wa pasaka ikitudhihirishia kuwa Kristo si mshindwa bali ni mshinda.

Katika somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya: Tunatafakari utabiri wa Mtumishi wa Mungu aliye mwaminifu katika kazi yake, ambaye haogopi magumu wala mateso. Mtumishi huyu ndiye Yesu aliyevumilia mateso makali ili atukomboe kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Kwa uaminifu wake, Mungu alimpa uwezo ili aweze kuwafundisha na kuwapa matumaini wanyofu, wanyonge, maskini na waliovunjika moyo. Kwa usikivu wake, Mungu alimwamsha asubuhi baada ya asubuhi, alizibua sikio lake apate kusikia Neno lake, alimpa nguvu na uvumilivu dhidi ya watesi wake. Mtumishi huyu, hakuficha uso wake asipate fedheha na kutemewa mate, hakukata tamaa bali aliwatolea watesi wake mgongo wake walipoamua kumchapa mijeledi, walipoamua kumng’oa ndevu mashavuni mwake, hakuficha uso wake. Kwa mateso haya sisi tumekombolewa. Katika somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi tunaona na kuonja matunda ya utii, unyenyekevu na uvumilivu wa Yesu Kristo, mtumishi mwaminifu wa Mungu. Dhambi na mauti viliingia katika historia ya mwanadamu kwa kosa la kukosa utii kwa Mungu. Kwa utii wa Kristo, dhambi na mauti vimeangamizwa. Kwa kutotii kwa Adamu na Eva tulitengwa na Mungu, kwa kutii kwake Kristo tumeunganishwa na Mungu. Nasi tunaalikwa kutii. Tutii amri za Mungu na za Kanisa. Tutii mafundisho ya Kanisa, tuwatii na kuwasikiliza wazazi na viongozi wa Kanisa kwani; asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Tukubali kutii kuwa sisi kwa asili tu binadamu, lakini tusiung’ang’anie kwa nguvu ubinadamu wetu bali tuuachilie, tujitwalie hali ya kimungu ili tukaishi milele yote mbinguni kwa Mungu Baba.

Injili kama ilivyoandikwa na Marko inasimulia Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo ndiyo kiini cha sehemu ya pili ya maadhimisho ya Dominika hii ya matawi. Yesu anakamatwa akiwa bustanini Gethsemane akisali, naye bila ubishi anaanza safari ya ukombozi kuelekea Golgota kusulubiwa. Safari yenye mateso makali, anabebeshwa msalaba mzito, anafanyiwa dhihaka, anapigwa mijeledi, anavuliwa nguo, anatemewa mate, anatukanwa, anasulubishwa msalabani na hatimaye anakufa kwa sababu ya dhambi zetu na kuonekana kuwa mtu aliyelaaniwa na Mungu (Kum. 21:22-23). Ni mateso makali mno na kifo cha aibu mno. Lakini kwa kifo chake kilivyokuwa cha pekee, dunia ilitetemeka, jua lilififia, kukawa giza juu ya nchi, pazia la hekalu likapasuka mara mbili, walioshuhudia walisadiki uaguzi wa manabii na kusema hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu. Naye alipochomwa ubavu kwa mkuki, vilitoka damu na maji, ndizo chemichemi za Sakramenti za Kanisa. Hii inatuonesha kuwa hakuna utukufu pasipo mateso, hakuna Pasaka bila Ijumaa kuu. Mateso na mahangaiko ya maisha ni mwangwi tu wa mateso ya Kristo kwa ajili ya dhambi zetu.

Ndiyo maana Kanisa linahimiza kuvumilia mateso tuyapatayo katika kuikiri na kuishuhudia imani yetu kwani yanatushahilisha kuingia katika ufalme wa mbinguni kama tukiyapokea kwa imani na bila manung`uniko. Lakini tutambue kuwa majukumu yanayotukabili katika maisha ya kila siku sio mateso bali ni wajibu wetu. Pia, mateso yatokanayo na dhambi zetu wenyewe, hayatuletei wokovu bali yatatupeleka kwenye moto wa milele, tusipoyakiri, kuyaungama na kuyaacha kwani yanazidi kumtesa Kristo. Katika simulizi la mateso ya Yesu, umati wa watu walipiga makelele wakisema: Asulubishwe! Asulubishwe! Nasi kwa mawazo, maneno na matendo yetu maovu na kwa dhambi zetu tunatoa mlio na makelele hayo hayo: Msulubishe! Msulubishe! Petro alijaribu kupambana na nguvu za giza kwa upanga. Kristo alipambana na kumshinda shetani si kwa mapanga na vitisho bali kwa uvumilivu wake, kwa unyenyekevu wake, kwa upole wake na kwa utii wake kwa Mungu Baba. Je, sisi hatuna fikra kama za Petro za kupambana na nguvu za shetani na Ibilisi kwa ubanga wa giza, maseng’enyo, malumbano, mapigano, visasi na fitina? Je, hatusemi kila siku katika makundi ya watu; Msulubishe! Msulubishe! Mwondoshe! Mwondoshe! Tukumbuke kuwa hatupaswi kumpigania Kristo kwa upanga bali kwa ushuhuda wa maneno na matendo mema.

Mtume Petro alimkana Yesu mara tatu akisema mimi si mfuasi wa mtu huyu, akasisitiza mimi simjui mtu huyu. Sisi nasi tunafanya jambo hilo hilo kila tunapoionea aibu Injili, tunaporudi nyuma kiimani na kukosa matumaini kwa Kristo kwa sababu ya matatizo na magonjwa na hivyo kuamua kutafuta suluhu katika dhambi. Jogoo amekwisha wika mara ya tatu, tunaalikwa kujirudi, tujiweke chini ya msalaba, kwani hatuna tumaini lingine, japo kwao wanaopotea msalaba ni kikwazo na upuuzi, kwetu sisi ni nguvu ya Mungu, alama na bendera ya ushindi, kama tukiutazama kwa imani na moyo wa toba. Hata tunaposikia; Hatumjui mtu huyu! Mwondoshe! Mwondoshe! Msulubishe! Msulubishe! Tusikate tamaa, au kukwazika na kurudi nyuma, bali kama mtumishi wa Mungu, tusonge mbele tukimtumainia Mungu, bila kuogopa kupigwa mijeledi, kutemewa mate, kung’olewa ndevu mashavuni, kuvikwa taji la miiba, kuvuliwa nguo, kupigwa kwa mwanzi wala kusulubiwa kwa ajili ya kumshuhudia Kristo, Mkombozi wa maisha yetu. Katika hili juma kuu tunalolianza, tuombe neema ya kuwa wasikivu na watii, tukisali pamoja na mtumishi wa Mungu kwa unyenyekevu tukisema; “Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, huniamsha sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao”. Tukubali kufundishwa na kuelekezwa. Tuwe watii. Tujipatanishe na Mungu ndipo tutakapokuwa na sababu ya kufurahia siku ya Pasaka na tunuie kutorudi nyuma tena mpaka tutakapomaliza safari ya maisha yetu hapa duniani, tukafurahi milele yote katika Pasaka ya Mbinguni.

Jumapili Matawi
24 March 2021, 14:47