Mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa yanayotekeleza dhamana na utume wake nchini Iraq katika tamko lao, wanakazia umuhimu wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu katika huduma kwa maskini. Mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa yanayotekeleza dhamana na utume wake nchini Iraq katika tamko lao, wanakazia umuhimu wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu katika huduma kwa maskini. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Mshikamano Kidugu

Mashirika ya kitaifa na kimataifa yanayotekeleza dhamana na utume wake nchini Iraq katika tamko lao yanasema, yanayo furaha kubwa kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, ili kuwafariji ndugu zake. Iraq imetumbukia katika: vita, ukosefu wa amani kutokana na mashambulizi na vitendo vya kigaidi ambavyo vimevuruga umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Hija hii inafumbata mambo makuu matatu: Ukaribu wa Baba Mtakatifu kwa Wakristo nchini Iraq, kuhamasisha ujenzi wa Iraq mpya katika haki na usawa na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kudumisha udugu wa kibinadamu. Mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa yanayotekeleza dhamana na utume wake nchini Iraq katika tamko lao yanasema, yanayo furaha kubwa kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo ya kidugu. Iraq katika miaka ya hivi karibuni imejikuta ikitumbukia katika vita, ukosefu wa amani na usalama kutokana na mashambulizi na vitendo vya kigaidi; mambo ambayo yamevuruga kabisa umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Kuna idadi kubwa sana ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi ya kudumu.

Kuna watu wengi ambao wameathirika sana kutokana na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, kiasi cha watu wengi kutumbukizwa katika umaskini wa hali na kipato! Serikali ya Iraq haina nguvu za kiuchumi za kuweka kutekeleza changamoto zote hizi kwa ufanisi mkubwa. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unatambua na kuthamini mchango wa dini mbalimbali katika kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu inatambua na kuthamini umoja na upendo wa kidugu kati ya waamini wa dini mbalimbali duniani. Hii ni changamoto ya kupendana na kushikamana kwa ajili ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mashirika haya yanataka kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, amani, maridhiano na upatanisho wa Kitaifa, ili kukuza haki, wajibu na kudumisha usalama wa raia na mali zao. Ni wakati wa kuendelea kujielekeza katika huduma kwa maskini na wahitaji zaidi kwa kukataa katu katu kishawishi cha wongofu wa shuruti. Lengo ni mshikamano katika huduma.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija yake ya Kitume nchini Iraq ili kuonesha uwepo wake wa karibu kwa Wakatoliki pamoja na Wakristo wote katika ujumla wao. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, Wakristo katika ujumla wao wamateseka sana. Wengi wao wamepoteza maisha na wengine kulazimika kuikimbia nchi yao, ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Ni katika muktadha huu, Iraq inahitaji uwepo wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili, aweze kuwatia shime katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu hata katika hali na mazingira magumu kama haya. Pili, Hija hii ya Kitume inalenga kuragibisha mchakato wa ujenzi wa wa Iraq mpya. Baba Mtakatifu anataka kuwahamasisha watu wa Mungu nchini Iraq kusimama kidete dhidi ya rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma. Wawe tayari kupinga mifumo yote ya ubaguzi, ili kila mwananchi aweze kuwajibika barabara katika ujenzi wa nchi yake; kwa kuwa na haki na nyajibu sawa. Tatu, hija hii inapania pamoja na mambo mengine, kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, umoja, ushirikiano na maelewano ya kidugu. Baba Mtakatifu analenga kuwahamasisha Waislam na Wakristo kuimarisha udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Tamko 2021

 

 

04 March 2021, 15:11