Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Yosefu kwa tafakari ya kina mintarafu makundi mbalimbali mintarafu karama na maisha ya Mtakatifu Yosefu mtu wa haki. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Yosefu kwa tafakari ya kina mintarafu makundi mbalimbali mintarafu karama na maisha ya Mtakatifu Yosefu mtu wa haki. 

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Mwaka wa Mt. Yosefu!

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Tanzania linawaalika watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika ufunguzi wa maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu ambao umeanza kuadhimishwa rasmi tarehe 8 Desemba 2020 na utahitimishwa tarehe 8 Desemba 2021. Mwaka huu upambwe kwa semina, makongamano, hija, warsha, mafungo na matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwaka wa Mtakatifu Yosefu ulizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na unatarajiwa kufungwa hapo tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu. Anasema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa.

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika waraka wake kwa watu wa Mungu nchini Tanzania anawaalika kushiriki kikamilifu katika ufunguzi wa maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu ambao umeanza kuadhimishwa rasmi tarehe 8 Desemba 2020 na utahitimishwa tarehe 8 Desemba 2021. Ufunguzi huu ni kwa majimbo yote Katoliki nchini Tanzania. Mwaka huu upambwe kwa semina, makongamano, hija, warsha, mafungo na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Chama cha Umoja wa Wanaume Wakatoliki Tanzania, UWAKA sasa kitambuliwe kama Chama cha Mtakatifu Yosefu. Maadhimisho ya Ibada mbalimbali yanogeshwe pia kwa nyimbo za Mtakatifu Yosefu. Kila mwezi kuwepo na shughuli maalum itakayohusisha makundi yakioanisha na fadhila za Mtakatifu Yosefu. Mwezi Machi 2021 ni Mwezi wa Mtakatifu Yosefu na Familia. Kumbe, mwezi huu, watu wa Mungu nchini Tanzania wanapaswa kutafakari na kumwilisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Mwezi Aprili 2021 ni wakati wa waamini kutafakari kuhusu wito wa Upadre. Mwezi Mei ni nafasi ya kumtafakari Mtakatifu Yosefu na wafanyakazi. Mwezi Juni, familia ya watu wa Mungu nchini Tanzania itamtafakari Mtakatifu Yosefu na vijana. Julai ni Mwezi wa kumwangalia Mtakatifu Yosefu na viongozi wa kijamii. Mwezi Agosti waamini watamtafakari Mtakatifu Yosefu na walimu wa dini shuleni kwa kuangalia umuhimu wa dini katika kuwafunda vijana wa kizazi kipya tunu msingi za maisha ya imani, fadhila na utu wema! Mwezi Septemba ni fursa makini kwa watanzania kumtafakari Mtakatifu Yosefu kwa kuzama zaidi katika vyama vya kitume katika mchakato mzima wa ushuhuda na kuyatakatifuza malimwengu. Mwezi Oktoba, itakuwa ni fursa kwa watawa kutafakari maisha yao ya wakfu mintarafu mwanga wa maisha ya Mtakatifu Yosefu.

Mwezi Novemba, ambao kimsingi Mama Kanisa ameutenga kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea waamini marehemu itakuwa ni nafasi ya kumtafakari Mtakatifu Yosefu Mwombezi wa wagonjwa na wale wote waliokufani. Ni fursa pia ya kujiombea kifo chema. Mwezi Desemba, Familia ya Mungu nchini Tanzania itamtafakari Mtakatifu Yosefu mlinzi na msimamizi wa watoto. Huu ni wakati muafaka wa kufanya katekesi kuhusu dhamana na wajibu wa wazazi na walezi kwa watoto wao hasa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Wazazi na walezi wafundishe kwa mifano bora ya maisha yao! Huu ndio mpango mkakati elekezi katika maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu kama ulivyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Tanzania
17 March 2021, 16:30