Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 5 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Nguvu ya Kristo Yesu katika kuwaondolea watu dhambi na kuwaponya magonjwa na udhaifu wao wa kimwili. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 5 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Nguvu ya Kristo Yesu katika kuwaondolea watu dhambi na kuwaponya magonjwa na udhaifu wao wa kimwili. 

Tafakari Jumapili 5 Mwaka B: Yesu Ni Mganga wa Roho Na Mwili!

Mababa wa Kanisa waliona kuwa uponyaji wa Yesu ambayo Injili zinayatoa ni ishara ya uponyaji wa wakristo kutoka maisha ya dhambi, dhambi ambayo ni ugonjwa unaoweza kupelekea mauti ya mtu kiroho na kimwili. Kristo aliyeamua kuukomboa ulimwengu kwa njia ya mateso amekuja kuifunua sura ya ukombozi ya mateso kwa wote wanaounganisha mateso yao na mateso ya Kristo.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya 5 ya mwaka B wa Kanisa. Ufafanuzi wa Masomo ya Misa kwa ufupi: Somo la Kwanza (Ayu 7:1-4, 6-7). Somo la kwanza linatoka kitabu cha Ayubu. Mkasa wa Ayubu unafahamika vizuri kwa wengi. Yeye alikuwa ni mtu tajiri na alikuwa pia ni mcha Mungu. Alipata majaribu makubwa sana ambapo kwanza watoto wake wote walifariki, pili mali zake zote zilitoweka na tatu mwili wake ulishambuliwa na magonjwa mazito. Pamoja na hayo yote, Biblia inaonesha kuwa Ayubu hakumwasi Mungu. Naye Mungu akamjalia upya yote aliyokuwa ameyapoteza. Ni kitabu chenye mafundisho mengi kuhusu fumbo la maisha ya mwanadamu hasa juu ya mwitikio wa mwanadamu mbele ya mateso. Katika kifungu kidogo tunachokisoma leo katika somo la kwanza, Ayubu anazungumza na rafiki zake waliokuja kumtazama na anawaelezea namna anavyoteseka.

Ayubu anasema zipo nyakati na kazi ngumu ambazo mwanadamu anazipitia lakini zote hizo zina wakati wa kupumzika na wakati wa kupata ujira wa ugumu wa kazi. Yeye lakini anaona ni mtu aliyeandikiwa kuteseka bila kupumzika. Na tena anaendelea kusema wakati wa usiku huwa ni wakati wa mtu kupumzika kutokana na uchovu wa kazi za kutwa nzima. Yeye lakini mateso aliyonayo hayapumziki hata unapoingia usiku. Tena usiku huwa ni mrefu zaidi kwake.  Ayubu anaona maisha yamekwisha mshinda na hawezi tena kuyatawala. Anaona maisha ni kama upepo; hawezi kuyashika na tena yanapita mbio. Maneno anayotamka Ayubu katika somo la leo ni maneno yanayowakilisha hali ya ubinadamu tangu enzi na enzi. Hali ya ubinadamu unaoteseka kwa adha mbalimbali za maisha, adha ambazo kwa kiasi fulani zinaonekana kumpokonya mwanadamu uwezo wa kuyatawala maisha yake. Ni maneno yanayoonesha mipaka ya maisha ya mwanadamu.

Somo la Pili (1Kor 9:16-19, 22-23): Katika somo la pili, Paulo anaeleza ari yake ya kitume: ari iliyomsukuma kuzunguka huku na huku akiihubiri Injili. Mtume Paulo anafahamika pia kama mtume wa mataifa. Maana yake ni kwamba ni yeye ambaye kati ya mitume wote amekuwa mstari wa mbele kuipeleka Injili nje ya mipaka ya uyahudi. Ndiye aliyeyaendea mataifa na ndiye alisisitiza sana fundisho kuwa watu wa mataifa nao ni warithi wa matunda ya ukombozi ya Kristo. Anachokieleza katika somo hili la leo ni msukumo binafsi aliokuwa amejiwekea. Huo ulikuwa ndio kama kauli mbiu yake: “Ole wangu nisipoihubiri Injili”. Ni kauli mbiu ambayo nadhani kila mmoja wetu angeichukua na kuiweka katika mazingira yake. Mwalimu aseme “ole wangu nisipofundisha wanafunzi”, Hakimu aseme “ole wangu nisipotoa hukumu ya haki”, Dereva aseme “ole wangu nisipoendesha kwa usalama” na kadhalika na kadhalika.  Tunachokiona katika somo hili ni kuwa Mtume Paulo ameuchukua wajibu wake wa kitume na kuupa nafasi ya kwanza kabisa katika maisha yake. Kwa ajili ya utume, anakuwa tayari kuachilia hata yale ambayo kwake ni haki ya msingi na anafanya hata yale ambayo huenda katika hali ya kawaida asingeyafanya. Ameishi katika hali zote za maisha ili awapate walio katika hali hizo za maisha kwa ajili ya Kristo. Yote hayo ameyafanya ili kuhakikisha kuwa injili inawafikia wote katika hali zao zote walizonazo.

Injili (Mk 1:29-39): Katika somo la Injili, Yesu anadhihirisha ujio wa ufalme wa Mungu kwa kuhubiri na kuponya wagonjwa. Historia ya maisha ya mwanadamu ambayo tangu mwanzo ilionekana kuelemewa na magonjwa pamoja na mateso mbalimbali, inapata kwa njia ya Kristo sura mpya. Magonjwa na mateso hayawi tena ukomo katika fumbo la maisha bali yanakuwa ni ufunguo wa ukamilifu wa maisha yenyewe. Injili hii ya leo inamuonesha Yesu akianza kwanza kumponya mama mkwe wa Petro. Kutoka katika kitanda chake cha ugonjwa, Yesu anamgusa kwa mkono wake wa uponyaji, anamwinua na mara hiyo hiyo anapona. Kutoka kwa mtu huyo mmoja, Yesu anaenda sasa kuponya umati. Kama tunavyosoma katika Injili hii, walimletea Yesu wagonjwa wote wa eneo hilo. Ni ajabu kidogo kuona kuwa Injili haisemi aliwaponya wote. Inasema tu aliwaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali. Inawezekana ni namna tu ya uandishi wa Mwinjili Marko na inawezekana pia kuwa Mwinjili Marko anataka kuonesha kuwa si wagonjwa wote walioponywa kwa sababu moja au nyingine anazozijua Yesu mwenyewe. Tunachokiona kwa hakika ni kuwa Yesu ameonesha nguvu yake ya uponyaji.

Mababa wa Kanisa, yaani waliokuwa viongozi wa Kanisa la Mwanzo baada ya Mitume, walipokuwa wakisoma miujiza ya Yesu ya uponyaji, mafundisho yao yalijikita zaidi katika uponyaji wa kiroho.  Waliona kuwa maelezo ya uponyaji wa Yesu ambayo Injili zinayatoa ni ishara ya uponyaji wa wakristo kutoka maisha ya dhambi, dhambi ambayo ni ugonjwa unaoweza kupelekea mauti ya mtu kiroho na kimwili. Pamoja na mafundisho hayo ya mababa wa Kanisa, ni muhimu kusisitiza pia mwono mpana wa mafundisho ya Kanisa kuhusu fumbo la mateso ya kimwili katika maisha ya mwanadamu. Yeye Kristo aliyeamua kuukomboa ulimwengu kwa njia ya mateso amekuja kuifunua sura ya ukombozi ya mateso kwa wote wanaounganisha mateso yao na mateso ya Kristo.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kupata ufafanuzi wa masomo ya dominika ya leo, masomo ambayo yamegusa kwa namna ya pekee fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu. Ninakualika sasa katika tafakari yake fupi.  Hata hivyo, ninapenda tu kuyaleta kama yalivyo, mafundisho ya Mtakatifu Gregori Mkuu, papa, kumhusu Ayubu. Ni mafundisho ambayo ninaona yanatoa muhtasari mzuri kabisa kuhusu fumbo la mateso ambalo tunapenda kulitafakari kwa dominika hii. “Mtu huyu Ayubu, aliyejaliwa fadhila nyingi sana, hakufahamika na yeyote kuwa yupo hivo, isipokuwa na Mungu tu. Bila mateso yake angebaki hivyo hivyo na hakuna ambaye angemfahamu. Kwa hakika, hata kabla ya mateso yake, Ayubu aliziishi fadhila zake za wema, ustahimilivu na imani kwa Mungu. Lakini ni pale tu yalipoibuka mateso katika maisha yake ndio manukato ya fadhila zake hizo yalipoanza kusambaa. Yeye ambaye katika maisha tulivu na yasiyo na misukosuko hazina yake hii kubwa ilikuwa imejificha, ni katika mateso ndipo ikafunuliwa. 

Ni kama tu chupa ya marashi yenye harufu nzuri, inapokuwa imefungwa na imewekwa katika utulivu, hakuna anayesikia harufu nzuri ya manukato yake. Ila pale inapofunguliwa na kutikiswa tikiswa, hapo manukato yake husikika. Tena ni kama ubani wenye harufu nzuri, usioweza kujulikana bila kuwekwa katika kaa la moto. Na pale unapounguzwa ndipo harufu yake hupaa. Vivyo hivyo basi na fadhila za watakatifu wa Mungu zinazofanywa kung’aa wakati wa mateso na misukosuko yao.” Mungu mwenyewe na atutie nguvu, atuimarishe wakati wa mateso na atujalie ukombozi wa kiroho na kimwili kwa njia ya Kristo aliyekuja kuchukua mateso yetu na kutukomboa kwa njia ya mateso.

Liturujia j5
05 February 2021, 16:25