Mama Kanisa anawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutangaza, kutetea na kushuhudia: ukweli, utakatifu, ukuu na changamoto za maisha ya ndoa na familia. Mama Kanisa anawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutangaza, kutetea na kushuhudia: ukweli, utakatifu, ukuu na changamoto za maisha ya ndoa na familia. 

Utakatifu, Ukuu, Ukweli, Uzuri na Changamoto za Ndoa na Familia!

Siku ya Ndoa Duniani ilianzishwa kunako mwaka 1983, tukio linalopania kuhamasisha tunu msingi za maisha ya ndo na familia, ili kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na changamoto za maisha ya ndoa na familia. Kumbe, Sikukuu ya Wapendanao iwe ni fursa ya kutafakari amana na utajiri wa maisha ya ndoa na familia na wala si sikukuu ya kujiachia na kuzama katika uovu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia, kwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kanisa linatambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani; ni mahali pa kujifunzia fadhila mbali mbali za Kikristo, kiutu na kijamii! Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, tangu tarehe 7 hadi 14 Februari 2021 limeadhimisha Juma la Ndoa na kilele chake ni katika maadhimisho ya Siku ya Wapendanao Duniani, maarufu kama “Valentine Day”.

Maadhimisho ya Mwaka 2021 yamenogeshwa na kauli mbiu: “Kuwa, Kushikilia na Kuheshimu Ndoa”. Tema hii imechaguliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani ili kuwahamasisha wanandoa kupyaisha kila siku ahadi zao za ndoa, kama njia ya kujenga na kudumisha familia kama Kanisa dogo la nyumbani. Siku ya Ndoa Duniani ilianzishwa kunako mwaka 1983, tukio linalopania kuhamasisha tunu msingi za maisha ya ndo na familia, ili kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na changamoto za maisha ya ndoa na familia. Kumbe, Sikukuu ya Wapendanao iwe ni fursa ya kutafakari amana na utajiri wa maisha ya ndoa na familia na wala si sikukuu ya kujiachia na kuzama katika uovu! Waamini wasimame imara kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Waishi kwa uaminifu na upendo viapo vyao vya ndoa; kwa kupendana, kuheshimiana, kuvumiliana na kusaidiana: wakati wa shida na raha. Mama Kanisa anawahamasisha wanandoa kuhakikisha kwamba, wanatumia muda mrefu zaidi pale inapowezekana wakiwa kwenye familia zao.

Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kuimarisha misingi ya ndoa na familia mintarafu mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu sanjari na mafundisho tanzu ya Kanisa. Waamini nchini Marekani, wamepata nafasi ya kumtafakari Mtakatifu Yosefu, mfano bora wa kuigwa kama Baba wa familia na mwenye upendo wa dhati, wakati huu Kanisa linapoadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Yosefu. Itakumbukwa kwamba, Mwaka huu ulitangazwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu”. Ulizinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2020 na unatarajiwa kufungwa tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu kuwa ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi.

Katika hali ya unyenyekevu Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa haki, akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, familia nyingi zinakabiliana na magumu hasa katika mchakato wa kumwilisha upendo wa Mungu katika maisha ya ndoa na familia. Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza wanandoa na familia kujikita katika sala, kwani familia inayosali, itaweza kudumu na kukabiliana na changamoto za maisha kwa pamoja, bila ya kuteteleka, kwani sala ni uti wa mgongo wa maisha ya ndoa na familia. Familia zijenge na kudumisha ari na moyo wa maisha ya Kisakramenti na Ibada: kwa kusali Rozari Takatifu mara kwa mara; kwa kusoma na kutafakari Neno la Mungu kwa pamoja kama Familia inayowajibikiana bila kusahau kuhudhuria mikutano ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo!

Familia iwe ni mahali ambapo wanafamilia na majirani wanaonjeshana tone la upendo na msamaha. Hapa ni mahali pa kukumbatia na kuenzi Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Familia iwe ni chemchemi ya upendo na ukarimu kwa watu wanaoteseka kutokana na majanga mbali mbali ya maisha kama vile wakimbizi, wahamiaji na wote waliokumbwa na maafa asilia sehemu mbali mbali za dunia. Familia iwe ni mahali pa kulinda, kuendeleza na kurithisha tunu bora za maisha ya ndoa na familia, kwa kutambua kwamba, ndoa ni muungano thabiti kati ya Bwana na Bibi na wala si jambo la mpito! Huu ndio uelewa kadiri ya mpango wa uumbaji na ukombozi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya binadamu na kwamba, ndoa ni kielelezo cha upendo wa juu kabisa kwa Kristo na Kanisa lake!

Kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 5 tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, hapo tarehe 19 Machi 2021 ametangaza kwamba, itakuwa ni siku ya kuzindua Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani itakayoadhimishwa mjini Roma tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Baba Mtakatifu anatarajia kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika matukio yote haya! Hii ni changamoto na mwaliko kwa watu wote wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya upendo ndani ya familia. Wosia huu wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, ni matunda ya mwanga wa Neno la Mungu unaozingatia ukweli na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo.

Wosia unatoa mwelekeo wa Kristo Yesu katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuzijengea familia uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia anasema Baba Mtakatifu Francisko ni muda muafaka kwa familia ya Mungu kurejea tena na kufanya tafakari ya kina kuhusu Wosia huu ambao unakazia: Upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka kuwa ni chemchemi na asili ya maisha. Baba Mtakatifu anatoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, mintarafu utume wa maisha ya ndoa na familia. Anawahimiza wazazi na walezi kuimarisha elimu, malezi na makuzi ya watoto wao, ili waweze kuwajibika kikamilifu katika maisha yao. Ni wajibu wa Kanisa kuwasindikiza, kung’amua na kuwasaidia wanafamilia wanaolegalega katika maisha na wito wao wa ndoa na familia. Tafakari hii ifanywe kwa msaada wa nyenzo mbalimbali za shughuli za kichungaji kwa kusikiliza na kuyafanyia kazi mapendekezo yanayotolewa na watu wa Mungu.

Mkazo utolewe kwenye maandalizi ya wana ndoa watarajiwa, elimu kuhusu maana na mahusiano ya kimaumbele miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” usaidie kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano kati ya familia na Kanisa, kwa kuwashirikisha zaidi wanandoa katika maisha na utume wa Kanisa. Malezi na katekesi ya kina, itolewe kwa mihimili yote ya Uinjilishaji, ili kukabiliana barabara na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazoendelea kuibuliwa katika maisha ya ndoa na familia. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, familia kama Kanisa dogo la nyumbani linaimarishwa zaidi, kwa kutambua dhamana na utume wake usiokuwa na mbadala!   Ni wakati wa kukuza na kuhamasisha wito wa kimisionari ndani ya familia, kwa kuwajengea wazazi na walezi uwezo wa kufundisha na kuwarithisha watoto wao: imani na tunu msingi za Kiinjili; kwa kuwaandaa kikamilifu tangu awali kushiriki na kujisadaka katika maisha ya ndoa na familia, bila kusahau wito wa Daraja Takatifu. Kumbukizi ya ndoa iwe ni fursa ya kupyaisha tena katekesi na maagano ya ndoa, ili kuweza kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.

Siku ya Ndoa Duniani
15 February 2021, 16:17