Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, muda muafaka wa: sala, toba na wongofu wa ndani unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, muda muafaka wa: sala, toba na wongofu wa ndani unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. 

Jumatano ya Majivu: Kwaresima: Muhimu: Sala, Toba na Matendo!

Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini za kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni kipindi kinachotualika kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo, kwa kufunga na kutenda matendo ya huruma, kama vile kuwasaidia wahitaji hasa maskini, kuwatembelea wagonjwa, wafungwa na wazee. Ni safari ya toba na wongofu!

Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, siku ya jumatano ya majivu tunapoanza kipidi cha Kwaresima katika mwaka B. Jumatano ya Majivu ni siku rasmi na ya kwanza katika kipindi cha Kwaresima, kipindi cha toba, kipindi cha kujipatanisha na Mungu, kipindi cha kujipanisha na Kanisa, kipindi cha kujipatanisha na ndugu katika familia, ni kipindi cha kujipatanisha na marafiki na kujipatanisha mtu na nafsi yake. Kwaresima ni nini? Ni kipindi cha siku arobaini za kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni kipindi kinachotualika kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo, kwa kufunga na kutenda matendo ya huruma, kama vile kuwasaidia wahitaji hasa maskini, kuwatembelea wagonjwa na hata wafungwa. Ni safari ambayo kilele chake ni adhimisho la fumbo la ukombozi wetu yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo tunaloliadhimisha katika juma kuu, kuanzia Alhamisi kuu, Ijumaa kuu na Jumamosi kuu, kilele chake ni dominika ya Pasaka.

Kusali, kujitoa sadaka kwa ukarimu kwa ajili ya wahitaji na kufunga, ndizo nguzo kuu tatu za kipindi cha Kwaresima, kipindi cha toba na wongofu wa ndani. Siku hii ya kwanza ya kipindi hiki cha Kwaresima huitwa Jumatano ya Majivu kutokana na tendo la kupakwa majivu katika paji la uso na wakati huo mhudumu wa tendo hili takatifu la kiroho akisema; Mwanadamu kumbuka, u mavumbi wewe na mavumbini utarudi. Jina hili la Jumatano ya Majivu, lilianza kutumika rasmi mwaka 1099 na Papa Urbani II, mwanzoni iliitwa “Mwanzo wa Mfungo”. Majivu yanayotumika siku hii ya Jumatano ya Majivu ni ya matawi ya mitende yaliyotumika Jumapili ya Matawi ya mwaka uliopita ambayo yanaashiria ushindi dhidi ya kifo na mauti kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa nini majivu? Majivu ni alama au ishara tu ya nje inayoashiria toba ya ndani ya mioyo yetu kama ilivyo rangi ya kijivu ambayo ni rangi ya toba na matumaini. Kupakwa majibu ni ishara ya toba yetu ya ndani ya nafsi zetu tunayoifanya ambayo inatutakasa na kutusafisha na uovu wote, kama Majivu yanavyotumika kusafisha vyombo.

Kumbe kupakwa majivu kwa maana nyingine ni kusema kuwa tu wachafu, tu wadhambi tunahitaji kusafishwa, tunahitaji kutakaswa katika Sakramenti ya Upatanisho. Majivu ni mbolea na mbolea hutumika kukuza mimea na kuifanya izae matunda mema, mengi na bora. Toba ya kweli tunayoifanya ndani mwetu ikiashiriwa na alama ya majivu hutusaidia kukua na kuzaa matunda mema ya kiroho. Majivu haya yanapakwa kwenye paji la uso, kama vile siku ya ubatizo tulipopakwa mafuta ya Krisma takatifu, tukaondolewa dhambi ya asili na adhabu zake zote, kwa ishara ya Msalaba, alama ya ushindi tuliyokombolewa nayo. Kumbe, majivu yanatukumbusha kufanya toba na kuungama dhambi tulizotenda baada ya ubatizo. Kupakwa majivu katika paji la uso ni kukiri hadharani bila kujificha kuwa tu wadhambi na tunahitaji huruma ya Mungu Baba, tunahitaji msamaha, tunahitaji kutakaswa na kufanywa upya watoto wa Mungu na wa kanisa.

Asili ya kujipaka majivu kama alama ya toba: Tendo hili la kiroho la kupakwa majivu katika paji la uso ni ishara ya toba ya kweli, ishara ambayo imekuwa ikitumika kwa maelfu ya miaka iliyopita hata kabla ya kuja Kristo. Katika ulimwengu wa wayahudi majivu yalikuwa ni alama ya huzuni, masumbuko, uchungu au uduni (Ayubu 2:8, 30:19; Zab 102:10). Baadaye utamaduni huu wa kupakwa majivu ulitumiwa na wakristo wa kwanza kama alama ya toba. Mwaka 600 hivi, Gregori Mkuu aliifanya siku ya Jumatano ya majivu kuwa siku ya kwanza ya Kwaresima na kufanya kipindi hiki cha toba kuwa ni cha siku arobaini. Miaka ya 800 hivi, baadhi ya makanisa yaliadhimisha Ibada ya Jumatano ya Majivu kwa ajili ya wadhambi waliokubuhu katika dhambi na waliojulikana. Sasa pale walipoamua kufanya toba ndio walipakwa majivu. Hivi wakati huu si wote walipakwa majivu ila tu wale waliokuwa wadhambi waliojulikana wazi, kama vile makahaba, wauaji na waasi. Kuanzia karne ya 11, Kanisa kwa kutambua kuwa mbele za Mungu hakuna asiye na dhambi, liliamuru tendo hili liwe kwa waamini wote likiambatana na kufunga, kusali, kutoa sadaka, na kufanya matendo ya huruma.

Kama Mwenyezi Mungu alivyowaita watu wake kufanya toba nyakati za Nabii Yoeli katika somo la kwanza, nasi anatuita tumrudie kwa mioyo yetu yote, kwa kufunga na kwa kulia na kwa kuomboleza. Tunaalikwa tuirarue mioyo yetu, na siyo mavazi yetu. Mwaliko na mwito ni kwa watu wote, kama anavyosema Nabii Yoeli; kusanyikeni kusanyiko kuu; kusanyikeni watu, litakaseni kusanyiko, kusanyikeni wazee, kusanyeni watoto na hao wanyonyao maziwa (Yoe 2:15). Naye Mtume Paulo, katika somo la pili la Waraka wake wa pili kwa Wakorintho, anatusihi tukubali kupatanishwa na Mungu kwa njia ya Kristo, yeye asiyejua dhambi alifanywa kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye (2Kor 5:21). Katika Injili Yesu anatuonya tusiwe wanafiki, tusifanye matendo mema ili tuonekane machoni pa watu wengine, kwani kwa kufanya hivyo tunakuwa tumepokea thawabu yetu kwa njia ya watu wanaotutazama, kutustaajabia, na kutusifia.

Kumbe, matendo yetu mema yasilenge kujionesha kwa watu wengine, bali yawe ni mawasiliano binafsi kati yetu na Mungu yaani kujenga muungano na Mungu wetu aliyemtakatifu kwa sala, sadaka na kufunga tukitembea wakati wote na Kristo, kuanzia asubuhi tunapoamka hadi tunapoelekea kulala, wakati wa usiku. Matumaini ya mafungo yetu hayana budi kujengeka katika njaa na kiu ya muungano na Mungu wetu mtakatifu. Muungano huu unawezekana tukiwafungulia mlango wenzetu hasa wahitaji na kuwapatia yale tutakayojinyima. Ni katika mfungo ndipo tunaweza kuiga mfano wa Msamaria mwema, anayejitolea kumsaidia mhitaji bila kuangalia tofauti zao kama anavyosisitiza Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Mfungo unaoambatana na huduma kwa wahitaji ni njia ya kushinda tofauti zetu na vishawishi vinavyoambatana na tofauti hizo. Kwa hiyo, tunaalikwa katika kila hali tuliyonayo tushiriki mfungo huu wa Kwaresima kwa malengo ya kuhuisha maisha yetu ya kiroho na kujiweka karibu zaidi na Mungu.

Hatua za kuchukua ili tuweze kufanya vema mapinduzi ya kiroho, toba na kubadilika. Tukubali kwamba sisi ni wadhambi. Tusipokubali kuwa tu wadhambi hatutaona hitaji la kufanya toba na wongofu wa ndani. Ndiyo maana Kwaresima lazima ianze kwa tendo la kupakwa majivu hadharani ili kukubali na kukiri hadharani kuwa tu wadhambi na tunahitaji kufanya toba. Sala, kufunga na matendo ya huruma ni mambo matatu ambayo tunahimizwa kuyafanya katika kipindi hiki cha Kwaresima. Yesu anatuangalisha kuwa, ili tuweze kufaidika kutokana na sala, matendo yetu ya huruma, na kufunga kwetu, tuondokane na unafiki. Mnafiki ndiye mdhambi pekee ambaye Yesu aliimkemea hadharani bila kusita; huu ndio ufarisayo. Tusianze kipindi hiki cha Kwaresima kwa mazoea. Tukiingie kipindi hiki kama vile ni cha kwanza na cha mwisho katika maisha yetu. Tuitumie Kwaresima hii kana kwamba hakuna tena Kwaresima nyingine. Kwa hakika hakuna hata mmoja mwenye uhakika wa kuiona Kwaresma nyingine. Mtume Paulo anatukumbusha kwamba kipindi cha Kwaresima ndio wakati uliokubalika, siku ya wokovu ndiyo sasa. Tusisubiri wakati mwingine. Tukitumie vema kipindi hiki. Nawatakieni nyote mwanzo mwema wa kipindi cha Kwaresima.

Jumatano ya Majivu
17 February 2021, 15:21