Tume ya Uchaguzi Uganda imemtangaza Rais Yoweri Kaguta Museveni mwenye umri wa miaka 76 kuwa Mshindi wa Ucahguzi Mkuu wa Rais na Wabunge Uliofanyika tarehe 14 Januari 2021. Tume ya Uchaguzi Uganda imemtangaza Rais Yoweri Kaguta Museveni mwenye umri wa miaka 76 kuwa Mshindi wa Ucahguzi Mkuu wa Rais na Wabunge Uliofanyika tarehe 14 Januari 2021. 

Uchaguzi Mkuu Uganda: Rais Museveni Kashinda kwa 58.64%

Rais mteule Museveni amepata kura 5,851,037 sawa na asilimia 58.64 % ya kura zote halali zilizopigwa. Mpinzani mkuu aliyemnyima usingizi Rais Museveni wakati wa kampeni zake ni msanii Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, ambaye amejinyakulia nafasi ya pili katika uchaguzi huu, kwa kupata kura 3,475,398 sawa na asilimia 34.83 % ya kura zote halali zilizopigwa! Amani tu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tume ya Uchaguzi nchini Uganda (EC) imemtangaza Yoweri Kaguta Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge uliofanyika nchini Uganda, Alhamisi tarehe 14 Januari 2021. Rais mteule Museveni amepata kura 5,851,037 sawa na asilimia 58.64 % ya kura zote halali zilizopigwa. Mpinzani mkuu aliyemnyima usingizi Rais Museveni wakati wa kampeni zake ni msanii Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, ambaye amejinyakulia nafasi ya pili katika uchaguzi huu, kwa kupata kura 3,475,398 sawa na asilimia 34.83 % ya kura zote halali zilizopigwa! Rais mteule Yoweri Kaguta Museveni mwenye umri wa miaka 76 aliingia madarakani kunako mwaka 1986 na hivyo kuwa ni kati ya Marais kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki waliodumu madarakani kwa muda mrefu zaidi. Wakati huo huo, Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anampongeza Rais mteule Yoweri Kaguta Museveni kwa Tume ya Uchaguzi nchini Uganda kumtangaza kuwa Rais. Tanzania itaendeleza urafiki na udugu wao kwa maslahi mapana ya wananchi wa nchi hizi mbili. Rais Magufuli anawapongeza Waganda kwa kukamilisha mchakato wa uchaguzi mkuu na anawataka kuendelea kudumisha amani na upendo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda katika barua yake ya kichungaji ya mwaka 2021 kuhusu Uchaguzi Mkuu iliyotiwa mkwaju na Askofu Joseph Antony Zziwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Kiyinda-Mityana inajikita zaidi katika Mafundisho Jamii ya Kanisa mintarafu masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi na kwamba, Kanisa lina wajibu na dhamana ya kutangaza na kushuhudia Injili hadi miisho ya dunia. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakita msingi wake katika: Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni wajibu wa watu wa Mungu nchini Uganda kuendeleza umoja wa kitaifa na mshikamano wa kidugu; kama sehemu ya ujenzi wa demokrasia na jamii ya watu wa Mungu nchini Uganda. Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda katika masuala ya Kisiasa linakazia umuhimu wa kulinda amani na kudumisha haki msingi za binadamu kama kielelezo cha ukomavu wa kisiasa.

Wananchi watambue haki na wajibu wao katika mchakato mzima wa kukuza demokrasia nchini Uganda. Umoja, mshikamano na maridhiano ya Kitaifa ni mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee, kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema; sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi mkuu nchini Uganda. Rushwa na ufisadi ni hatari kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Uganda. Vitisho ni dhana ambayo imepitwa na wakati. Wananchi wa Uganda wanapaswa kutambua kwamba, bado gonjwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 lipo na wanapaswa kuchukua tahadhari kwa kufuata ushauri wa madaktari na wafanyakazi katika sekta ya afya. Maaskofu wanatambua mchango mkubwa wa vijana wa kizazi kipya katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Uganda, kumbe, wanapaswa kuwa na nidhamu bora na uwajibikaji unaosukumwa na dhamiri nyofu kamwe wasikubali kutumiwa na wanasiasa kwa ajili ya mafao yao binafsi.

Haki, amani, usalama, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Uganda ni mambo yanayopaswa kuvaliwa njuga. Vyombo vya ulinzi na usalama viendelee kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kufuata utawala wa sheria. Watu wajenge uzalendo kwa nchi yao, kwa kuheshimu na kuthamini tunu msingi za maisha ya wananchi wa Uganda. Waandishi wa habari watekeleze majukumu yao kwa unyenyekevu, wakitafuta ili hatimaye watangaze ukweli na kamwe wasikubali kutumiwa na wanasiasa kwa ajili ya masilahi yao binafsi. Familia ya Mungu nchini Uganda baada ya mchakato mzima wa uchaguzi na hatimaye matokeo kutangazwa rasmi sasa ni wakati wa kujikita katika majadiliano na upatanisho ili kujenga umoja na mshikamano wa udugu kitaifa.

Uchaguzi Mkuu Uganda

 

17 January 2021, 14:55