Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 2 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Dhana ya wito katika maisha na utume wa Kanisa: Mambo msingi: Mfuasi wa Kristo, Shuhuda na Mtangazaji wa Habari Njema. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 2 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Dhana ya wito katika maisha na utume wa Kanisa: Mambo msingi: Mfuasi wa Kristo, Shuhuda na Mtangazaji wa Habari Njema. 

Jumapili 2 Mwaka B: Wito: Mfuasi, Shuhuda na Mtangazaji wa Neno!

Dhana ya wito katika Maisha ya mkristo ni dhana pana na inagusa maisha yake mazima. Katika upana wake huo, dominika hii inatualika tuuangalie na kuutafakari wito wetu wakristo katika maeneo matatu: kuwa mfuasi, kuwa shuhuda wa Kristo na kuwa yule ambaye anawapeleka watu kwa Kristo au kwa maneno mengine kuwa yule ambaye anawafanya watu wavutiwe na Kristo.

Na Padre William, Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Dominika ya 2 ya Mwaka B wa Kanisa inaleta kwetu tafakari kuhusu wito. Dhana ya wito katika Maisha ya mkristo ni dhana pana na inagusa maisha yake mazima.  Katika upana wake huo, dominika hii inatualika tuuangalie na kuutafakari wito wetu wakristo katika maeneo matatu: kuwa mfuasi wa Kristo, kuwa shuhuda wa Kristo na kuwa yule ambaye anawapeleka watu kwa Kristo au kwa maneno mengine kuwa yule ambaye anawafanya watu wavutiwe na Kristo. Masomo ya Misa kwa ufupi: Somo la Kwanza (1Sam 3:3b-10, 19). Somo la kwanza linaelezea wito wa Samweli. Tangu akiwa mtoto mdogo, mama yake alimpeleka hekaluni akakae na kuhudumia huko. Na alifanya hivyo kama alama ya shukrani kwa Mungu kwa sababu mama huyo alikuwa mgumba. Alimpata mtoto huyo baada ya muda mrefu wa kufunga na kusali. Hii inaweza kueleza pia kwa nini alimwita Samweli. Samweli kwa kiebrania (kutoka Shem -Jina na El – Mungu) humaanisha Jina la Mungu, inawezekana mama yake Samweli alilitaja mara nyingi sana Jina la Mungu akisali kuomba kupata mtoto.

Akiwa hekaluni, usiku, anasikia sauti ikimwita. Na yeye bila kujua ni nani anamwita akaenda kwa Eli, aliyekuwa kuhani. Eli anapogundua kuwa ni Mungu anamwita Samweli, basi anamfundisha namna ya kuitikia. Hii huenda isiwe tu ni kujua maneno ya kusema pale Mungu anapokuita bali inakwenda mbali zaidi. Inajumuisha namna ya kujiweka tayari kuupokea wito na hasa zaidi namna ya kujibidiisha kuuishi wito ambao Mungu anakuitia. Maneno hayo “Nena Bwana kwa kuwa mtumishi wako anasikia” yanakuwa ni kiashirio cha utayari wote kabisa wa kuupokea wito. Tuyaangalie kidogo na mazingira ambamo Samueli ameitwa ili kuona wito anaoitiwa ni wito wa namna gani. Samweli anaitwa katika kipindi ambacho tunaweza kusema ukuhani ulikuwa umelala. Eli alikuwa mzee na hakuweza kuwakanya wanae waliokuwa wakiukufuru ukuhani. Tena yeye kama kuhani na mwangalizi wa matakatifu alipaswa kulala hekaluni lakini hakufanya hivyo akimwachia mtoto Samweli wajibu huo. Kumbe Mungu anapomwita Samweli anamaanisha kuusitisha ukuhani wa Eli na kuleta sura mpya ya matumaini, si tu katika uhuhani bali katika taifa zima la Israeli. Naye Samweli akakua na hakuliacha neno la Mungu lidondoke chini.

Somo la Pili (1Kor 6:13c-15°, 17-20): Katika somo la pili, Mtume Paulo anakemea vikali mmomonyoko wa maadili ulokuwa umewakumba wakristo wa Korintho. Kwa ukali kabisa anawaonya wakristo dhidi ya zinaa. Anawakumbusha kuwa mwili wa mkristo ni kiungo cha Kristo na ni hekalu la Roho Mtakatifu. Mazingira ya Paulo kutoa maonyo haya kile ambacho tunakiona katika aya moja inayotangulia somo hili. Kilichokuwa nyuma ni kwamba wakristo wa Korinto walikuwa na dhana potofu kuhusu ile hali ya kuwa “huru ndani ya Kristo”. Walipoyasikia mafundisho kuwa anayempokea Kristo anakuwa mtu huru na anatawaliwa na Roho Mtakatifu na basi wakaona kuwa anayetawaliwa na Roho anaweza kufanya chochote mwili unachomtuma. Yanayotokea katika mwili hayahusiani kwa lolote na Roho. Hapo Paulo akawaambia: vitu vyote ni halali, ndiyo. Lakini si vyote vifaavyo (1Kor 6:12).

Mtume Paulo anapowaambia kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo anarekea katika teolojia yake pana kabisa kuhusu mwili. Katika barua zake, anapoutaja mwili huwa anarejea kimoja kati ya vitu hivi viwili. Cha kwanza ni mwili kama ubinadamu dhaifu na ulio daima na maelekeo ya dhambi na cha kitu cha pili anauzungumzia mwili kama ubinadamu katika ile hali yake ya kuhusiana – kujenga mahusiano kati ya mwanadamu na mwanadamu lakini pia kati ya mwanadamu na Mungu. Sasa neno (la Kiyunani) analolitumia katika somo la leo kumaanisha mwili ni lile linalouzungumzia mwili mintarafu mahusiano kati ya mwanadamu na mwanadamu ambayo pia inahusu mahusiano kati ya mwanadamu na Mungu. Kumbe, katika mantiki hii, Paulo anapowaasa Wakorinto waikimbie zinaa na ya kuwa zinaa ni dhambi ambayo mtu anaitenda juu ya mwili wake mwenyewe anamaanisha kuwa inaharibu uwezo wa mwanadamu kuingia katika mahusiano yanayofaa kati yake na mwanadamu mwenzake lakini pia kati yake na Mungu. Ule uhusiano wa mkristo kama kiungo katika mwili wa Kristo na mkristo kama hekalu la Roho Mtakatifu unavunjika. Ndiyo maana basi anamalizia kwa kusema “mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi mtukuzeni Mungu katika miili yenu”.

Injili (Yn 1:35-42): Somo la Injili ya dominika hii ya pili yam waka B wa Kanisa inagusia dhana ya wito, dhana ambayo tumeona imetawala katika somo la kwanza kuhusu wito wa Samweli. Hapa mwinjili Yohane anaeleza namna wito wa wanafunzi wa kwanza wa Yesu ulivyokuwa. Tunachokiona ni kwamba wito huu umekuwa kwa hatua mbalimbali. Ilianza hatua ya ushuhuda ambao Yohane Mbatizaji anautoa kwa Yesu – “Tazama, Mwanakondoo wa Mungu”, Hatua iliyofuata ikawa hawa ambao walikuwa ni wanafunzi wa Yohane Mbatizaji wakaupokea ushuhuda huo kama mwaliko wa kumfuata Yesu, wakamfuata. Ikafuata hatua ya mahojiano kati yao na Yesu. Yesu akawauliza mnatafuta nini? Na wao wakajibu kwa swali “mwalimu unakaa wapi”? Tunaweza kuyaona mahojiano haya mafupi kama muhtasari tu unaobeba dhana nzima ya mang’amuzi katika wito. Wanafunzi wanapenda kujua Yesu anakaa wapi. Na hapa si kujua tu bali ni kufika na kukaa naye. Kwa maneno mengine wanapenda kuingia katika undani wa maisha ya Yesu na kimsingi kuwa na mahusiano ya kudumu na yeye.

Hiki anakisisitiza sana Mwinjili Yohane kwa sababu katika injili nyingine tunaona kuwa Yesu anapowaita Mitume haanzi moja kwa moja kukaa nao. Wanaondoka kwenda kuendelea na shughuli zao na baadaye ndipo wanaitwa tena na hapo ndipo wanaanza utume wao. Kwa Yohane ni tofauti. Pale pale wanapopokea wito hapo hapo wanabaki hadi mwisho. Na mwinjili anaposema walibaki hadi saa 10 tunalazimika kuitafsiri saa hii si kadiri muda katika siku bali kadiri ya nambari 10 ya Kiyahudi ikimaanisha ukamilifu au mang’amuzi. Hapo tunaona kuwa wanafunzi walikaa na Yesu katika ukamilifu ama walikaa naye hadi kufikia mang’amuzi sahihi ya wito wato. Hatua ya mwisho anayoionesha mwinjili Yohane ni kama ile ya kwanza. Wao walipata ushuhuda wa Yohana Mbatizaji, sasa na wao wakaenda kutoa ushuhuda kwa wenzao kiasi cha kumleta kwa Yesu Simoni ambaye Yesu akampa jina Petro.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tafakari tuliyoifanya katika masomo imetuingiza katika dhamira ya wito kama ambavyo Kanisa linatualika tuitafakari katika dominika hii. Nasi tunapenda katika siku ya leo kuutafakari wito kama ufuasi, ushuhuda na “udalali” wa Kristo. Masomo ya leo yametuonesha kuwa kuwa mfuasi ni kukaa na yule unayetaka kumfuata. Ndivyo alivyofanya Samweli – kwanza kukaa na El ni kama mfuasi wake na hasa zaidi kukaa Hekaluni palipokuwa ni makao ya Mungu duniani ili kuonesha ufuasi wake. Katika Injili wafuasi wa kwanza wa Yesu nao wamefanya kitu hicho hicho. Wameonesha ufuasi wao kwa kuomba kukaa na Yesu. Wito, ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News ni ushuhuda. Ni sawa na kuwa balozi, yaani yule anayemtambulisha Kristo na yule anayemwakilisha Kristo. Anayeitwa na anayepokea wito anaitwa kuwa mwakilishi wa Kristo katika mazingira anayoishi na kufanyia kazi.

Ushuhuda mkubwa kabisa ambao tumeuona katika masomo ya leo ni ule wa Yohana Mbatizaji. Yeye amemshuhudia Kristo kama ndiye mwanakondoo wa Mungu. Yohane aliyekuwa na utume wa kumtayarishia Kristo njia kwa kufundisha toba na maondoleo ya dhambi, anamkiri Kristo kuwa ndiye yule mwanakondoo aliyechinjwa zamani za Musa kule Misri na damu yake ikapakwa katika milango ya waisraeli ili kuashiria ukombozi wao kutoka utumwa wa Farao. Na kwamba ukombozi anaokuja kuuleta Yesu si tena ule wa kutoka kwa Farao bali ni kutoka katika dhambi ya ulimwengu. Wito ni ushuhuda. Na hatimaye ndugu zangu, wito ni udalali. Tunaweza kusema ule udalali mzuri, udalali wa kuwa kiungo cha kuwaleta watu kwa Kristo. Liturujia ya ubatizo inampaka mbatizwa Krisma takatifu ambayo pamoja na alama ya utakaso Krisma ni mafuta yenye harufu nzuri.

Mababa wa Kanisa wanaiona harufu hiyo nzuri kama mwaliko wa mkristo kuyaishi maisha yake ya ukristo kiasi cha kutoa harufu nzuri ya utakatifu, harufu itakayowavutia watu kumfuata Kristo. Na hii haikomei hapa tu, inakwenda hadi katika miito mbalimbali ya huduma ambayo tunaipokea katika kanisa. Kuiishi ili kuwavutia na wengine wapende kuiishi. Ndivyo alivyofanya Yohane Mbatizaji akawapeleka wafuasi wake mwenyewe kwa Kristo na ndivyo walivyofanya wafuasi wenyewe wakawaleta rafiki zao kwa Kristo. Tafakari hii inatuonesha tu kuwa maisha yetu yote kama wakristo ni wito ambao Kristo mwenyewe ametuitia.  Tuuishi basi wito wetu huo wa kuwa wakristo kwa kupenda kukaa karibu na Kristo, kwa kuwa mashahidi wake na kwa kuwarudisha wengi kwa Kristo hasa wale wasiomjua bado na wale waliojitenga naye kwa namna moja au nyingine.

Liturujia J2

                                                                                                

15 January 2021, 13:44