Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 2 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Utakatifu wa maisha ni wito mkuu unaotolewa kwa ajili ya waamini wote, ili wawe wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 2 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Utakatifu wa maisha ni wito mkuu unaotolewa kwa ajili ya waamini wote, ili wawe wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. 

Tafakari Jumapili 2 Mwaka B: Wito Kwa Wote: Utakatifu wa Maisha!

Tukumbuke: Wito ulio mkuu kuliko yote tulioitiwa sisi sote ni wito wa kuwa watakatifu kama Baba yetu wa Mbinguni alivyo Mtakatifu. Ni kwa ubatizo wetu tumefanywa kuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa, watu wateule warithi wa ufalme wa mbinguni. Tuuangali basi, tuutunze utakatifu wetu kwa maisha yenye kumpendeza Mungu na jirani ili mwisho wa yote tufike kwake Mbinguni.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 2 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Jumapili ya kwanza ya kipindi cha kawaida tuliadhimisha Ubatizo wa Bwana ambapo Mungu katika nafsi Tatu za Utatu Mtakatifu alijidhihirisha: Mungu Roho Mtakatifu katika alama na ishara ya njia, Mungu Baba kwa sauti yake iliyosikika ikimtambulisha Mungu Mwana kwetu sisi ikisema: Huyu ni Mwanangu Mpendwa, Msikilizeni yeye. Masomo ya domenika hii yanatupa nafasi ya kutafakari wito wetu wa kuwa watakatifu kwa kuisikiliza sauti ya Mungu, anapotuita ili tumtumike katika watu wake kama mtoto Samweli na Yohane Mbatizaji. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Nabii Samueli linasimulia wito wa mtoto Samweli. Jina Samueli maana yake ni “Niliyemwomba Bwana.” Hannah mama ya Samweli alikuwa mke wa pili wa Elikana naye alikuwa Tasa. Kutokana na utasa wake hakuwa na amani wala furaha ingawa mumewe alimpenda hata katika hali hiyo kwani alikuwa ni mchamungu. Hannah alienda hija huko Shilloh, mbele ya Sanduku la Agano akaomba mtoto wa kiume, ambaye atamtoa kama mtumishi hekaluni.

Mungu alisikiliza kilio chake, akamjalia mtoto mwanaume naye akamwita Samweli maana alimwomba kwa Bwana. Akiwa na umri wa miaka 3 hivi Hannah alimtoa mwanae Samueli hekaluni, akamkabidhi kwa kuhani Eli. Eli akamlea kama mwanae. Akiwa na umri wa miaka 12 Mungu alimtokea na kumwita Samueli, Samweli. Kwa maongozi ya Eli, Samweli anaitikia sauti ya Mungu akisema; “Nena Bwana kwa kuwa Mtumishi wako anasikia.” Samueli aliendelea kukua kwa kimo na busara. Mungu alikuwa pamoja naye, wala hakuacha Neno la Bwana lidondoke chini. Swali la kujiuliza na kutafakari kwa Wazazi katika nyakati zetu; tunaomba nini kwa Mungu kwa ajili ya watoto wetu? Tujifunze toka kwa Hannah tuwaombee watoto wetu waisikie sauti ya Mungu na kuitikia kama mtoto Samweli ili waweze kukua kwa kimo na busara kwa kufuata maongozi ya Mungu, watambue miito yao, waishii vyema ili kwayo waweze kuwa watakatifu.

Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho anatuasa tuitumie miili yetu kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu kwani kwa ubatizo miili yetu imekuwa hekalu la Roho Mtakatifu. Hivyo tusiiharibu miili yetu kwa yaliyochukizo kwa Mungu bali tuiheshimu, tuidhamini, tuitunze kwa kuvaa mavazi ya heshima kama wana wa Mungu, na sio kuichora kwa michoro ya ajabu na uiacha wazi katika hali ya utupu. Paulo anatuambia kuwa dhambi za uasherati, uzinzi, ushoga na ndoa za jinsia moja ni chukizo kwa Mungu zitatunyima kuingia Mbinguni. Katika ulimwengu wa sasa mambo haya yanadaiwa kuwa ni haki za binadamu. Hii si kweli hata kidogo maana Maandiko Matakatifu tangu enzi za Agano la Kale yanasema wazi kuwa matendo haya yote ni chukizo kwa Mungu yanatuchafua mwili na roho, ni kikwazo kwa wito wetu wa utakatifu, yanatufanya tusiwe watakatifu kama Mungu Baba yetu alivyo mtakatifu.

Katika Injili ilivyoandikwa na Yohane; Yohane Mbatizaji anawakabidhi wanafunzi wake kwa Yesu akisema; “Tazameni Mwanakondoo wa Mungu.” Wanafunzi wake wakamfuata Yesu naye Yesu alipowaona akawauliza “mnatafuta nini?” Wao wakamwuliza: “Mwalimu, unakaa wapi? Yesu akawaambia; “Njooni nanyi mtaona! Nao wakamfuata, wakakaa naye, wakajifunza kwake baadae wakawaleta wenzao kwa Yesu. Andrea alimleta Petro, Yohani alimleta Yakobo, Filipo akamleta Nathanaeli. Sisi nasi kwa Sakramenti ya ubatizo tumeitwa kuwa wamisionari, kuwaleta wengine kwa Yesu. Swali la kujiuliza; Tangu umebatizwa umewaleta wangapi kwa Yesu? Binadamu tumeumbwa kwa dhumuni maalum ambalo twaelekea bila kukwepa na hili si lingine ila la Kumtafuta Mungu kwa hali zote ili tuwezekuwa watakatifu kama yeye alivyo mtakatifu. Ili tuweze kuufikia utakatifu kila mmoja anapaswa kuuishi kiaminifu wito aliojaliwa na Mungu na kuupokea: uwe ni wito wa kazi katika kuwahudumia wengine kwa ajili sifa na utukufu wa Mungu. Au wito wa ndoa ambapo mwanaume na mwanamke wanaamua kwa makusudi kushirikiana na kwa upendo katika kutumikiana mpaka kufa, huku wakiwalea na kuwashirikisha imani yao watoto waliojaliwa na Mungu kwa upendo wao;

Kuna wito wa upadre na utawa ambapo padre au mtawa anayatolea maisha yake yote kwa ajili ya Mungu kwa kuwatumikia watu wake; au wito wa maisha ya pekee ambapo mtu anaamua kwa hiari yake, kutokuoa au kuolewa, si padre wala si mtawa bali anaacha yote ili awe huru kuwahudumia na kuwatumikia wengine. Lakini tahadhari ni kuwa; ikiwa mtu anayachagua maisha haya ili aepuke matatizo au apate raha na starehe fulani, huu ni ubinafsi na tena siyo wito. Licha ya kuwa wengine wanaishi hawajaoa wala kuolewa si kwa kupenda ila wamelazimika kuwa hivi nao wanapaswa kumshukuru Mungu kwa hali hiyo na kuishi usafi wa Mungu kwa ajili ya utakatifu wao. Ili mtu aweze kutambua wito wake uwe wa ndoa, upadre, utawa au wa kipekee, au aina ya kazi anapaswa awe na dhamiri safi na iliyo njema na hii inategemeana na malezi ya msingi aliyoyapata; kwanza kutoka kwa wazazi wake, pili viongozi wa dini, tatu kwa jamii inayomzunguka ikisaidiana na serikali. Ni malezi bora ya tangu utotoni ndiyo yanayompa mtu uwezo wa kusikia sauti ya Mungu, kung’amua aina ya wito ambao Mungu amemwita ili amtumikie.

Lakini nyakati hizi za kisasa tamaa ya maisha bora isiyozingatia maadili, imekuwa na tabia ya kumuondoa mzazi kutoka katika maisha ya familia. Wazazi wanakosa mda wa kukaa na watoto wao na hivyo kwa bahati mbaya sana watoto wao wanapata malezi kutoka kwa “watu wa mshahara” ambao nao pengine hawana msingi wa malezi bora na wengine walezi wao ni TV au simu ambazo haziwezi kuwa na mahusiano ya kujenga dhamiri iliyo hai na safi kwa watoto. Matokeo yake tunakuwa na familia na jamii isiyokuwa na mizani ya maadili. Kama familia ndio chanzo cha aina zote za miito katika maisha, kwa hali hii tumpateje baba au mama, mfanyakazi, mfanyabiashara, Padre au sista mwema na mwadilifu? Je watawezaje watoto wetu kuitambua sauti ya Mungu? Nani atawasaidia kuisikiliza na kuitambua sauti ya Mungu?

Jukumu la malezi ni wito na kazi ambavyo kila mzazi huipokea ili kuwalea na kuwaunda watoto wawe katika hali ya kujikubali na kukubalika katika  maisha yao ya kila siku. Mtoto kukosa malezi bora yenye upendo kwa kuwa yeye ni tunda la upendo kutoka kwa wazazi wake wawili baba na mama, anajeruhiwa kiroho, akilini na mwilini kiasi cha kujikataa mwenyewe na kuwakataa wengine. Ndio maana katika mang’amuzi ya kila siku tutakuta kuna watu ambao wanashindwa kuishi na wenzao au kufanya kazi na wengine hata yeye mwenyewe akiwa peke yake hawezi kufanya kazi zake vizuri. Kila atakapoishi na watu, ataleta mngongano pengine hata yeye mwenyewe haelewi ni kwanini yuko hivo. Lakini sababu ni kukosa msingi wa malezi kutoka kwa wazazi. Wazazi walikimbia wito wao na hivyo kuwa sababu ya majeraha haya. Wito wetu ni kwamba tuwasaidie ili wajitambue na tuwakubali tuwasaidie kuziunda upya dhamiri zao ili wamtambue Mungu.

Tukumbuke kuwa wito ulio mkuu kuliko yote tulioitiwa sisi sote ni wito wa kuwa watakatifu kama Baba yetu wa Mbinguni alivyo Mtakatifu. Ni kwa ubatizo wetu tumefanywa kuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa, watu wateule warithi wa ufalme wa mbinguni. Tuuangali basi, tuutunze utakatifu wetu kwa maisha yenye kumpendeza Mungu na jirani ili mwisho wa yote tufike kwake Mbinguni. Licha ya changamoto tulizonazo za kidunia zinazotuchanganya tudumu imara katika Imani tukisali na kumwomba Mungu atuangazie tutambue mwito wake wa Utakatifu wa maisha.

Jumapili Pili ya Mwaka B

 

15 January 2021, 11:21