Tafuta

Shirika la Masista wa Upendo wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Kanda ya Malaika Mkuu Gabrieli, hivi karibuni limepata viongozi wapya ambao wako chini ya Sr. Jenipher Odira Muga, SCIC. Shirika la Masista wa Upendo wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Kanda ya Malaika Mkuu Gabrieli, hivi karibuni limepata viongozi wapya ambao wako chini ya Sr. Jenipher Odira Muga, SCIC. 

Masista wa Ivrea Afrika Mashariki Wapata "Majembe Mapya" Sr. J. Muga!

Masista wa Ivrea hivi karibuni wamefanya uchaguzi. Viongozi waliochaguliwa ni Sr. Jenipher Odira Muga, Mama mkuu wa Kanda Washauri wakuu ni: Sr. Koleta C. Samigune, Mama mkuu msaidizi wa Kanda, Sr. Caritas M. Kahiura, Sr. Beata F. Msuri pamoja na Sr. Jackline A. Wanga. Shirika limemteua Sr. Beatrice Aloyce Tarimo kushughulikia masuala ya fedha na uchumi katika ngazi ya Kanda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Masista wa Shirika la Upendo la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Ivrea maarufu kwa jina la “Masista wa Ivrea,” wanaendelea kuhimizwa na Mama Kanisa ili waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huduma ya upendo wa Mungu na kwa maskini, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya: upendo, furaha na matumaini Barani Afrika na sehemu mbalimbali za dunia. Masista wa Ivrea kama urithi wao kutoka kwa Mwenyeheri Mama Antonia Maria Verna, muasisi wa Shirika; wameachiwa: Ibada kwa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Fumbo la Ekaristi Takatifu na Msalaba kama nyenzo msingi za maisha na huduma ya Injili kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Hii ni changamoto, wito na mwaliko wa kukazia mchakato wa utakatifu wa maisha na unyoofu wa moyo, kama chemchemi ya Injili ya huduma ya upendo na matumaini kwa watu wanaoteseka kutokana na umaskini, ujinga na magonjwa.

Ni katika muktadha huu, Masista wa Ivrea, hivi karibuni wamefanya uchaguzi mkuu na kufanikiwa kuwapata viongozi wa Shirika, Kanda ya Malaika Mkuu Mikaeli inayoundwa na watawa wanaotekeleza utume wao nchini Kenya na Tanzania. Viongozi waliochaguliwa ni Sr. Jenipher Odira Muga, Mama mkuu wa Kanda anayelifahamu vyema Shirika la Ivrea Kanda ya Malaika Mkuu Mikaeli kwa sababu hii ni awamu yake ya pili ya uongozi katika ngazi ya Kanda. Washauri wakuu ni pamoja na Sr. Koleta Charles Samwigune, Mama mkuu msaidizi wa Kanda, Sr. Caritas Michael Kahiura, Sr. Beata Fokas Msuri pamoja na Sr. Jackline Akinyi Wanga. Shirika limemteua Sr. Beatrice Aloyce Tarimo kushughulikia masuala ya fedha na uchumi katika ngazi ya Kanda. Jopo zima la uongozi wa Kanda limeanza kutekeleza dhamana na utume wake rasmi kuanzia tarehe 16 Desemba 2020.

Mheshimiwa Sr. Raffaela Giudici, Mama mkuu wa Shirika la Upendo la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Ivrea anatumaini kwamba, viongozi wakuu wa Kanda ya Malaika Mkuu Mikaeli, wataweza kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa ukamilifu, ili waweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, wakiendelea kujizatiti katika ujenzi wa umoja na mshikamano wa kidugu na Mama mkuu wa Shirika pamoja na wasaidizi wake, ili kuendelea kupyaisha karama ya Shirika walioachiwa na Mwenyeheri Mama Antonia Maria Verna. Sr. Raffaela Giudici, Mama mkuu wa Shirika anapenda kuchukua nafasi hii, kuwashukuru na kuwapongeza Masista wote waliokuwa kwenye uongozi awamu iliyopita. Hawa ni pamoja na Sr. Enrica Giani, Sr. Jemma Issaka, Sr. Adolfina Mwambua pamoja na Sr. Rosaria Balestrucci kwa huduma na majitoleo yao. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awakirimie neema na baraka zake kutokana na majitoleo yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Shirika na Kanisa katika ujumla wake.

Mwenyeheri Mama Antonia Maria Verna, alipambana kwa imani thabiti dhidi ya umaskini wa hali, mali na utu. Alikuwa na imani thabiti kwa Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili, Mama wa Yesu na Mama wa Kanisa: Chemchemi isiyokauka ya: imani, neema na matumaini. Ni mang’amuzi ya maisha ya mwanamke ambaye hakuogopa kupenda. Mwenyeheri Mama Antonia Maria Verna, Dada wa upendo alikuwa huru katika kusema “Ndiyo” kwa Bwana, kwa ajili ya utumishi wa upendo kwa Mungu na kwa jirani.  Alitangazwa na Mama Kanisa kuwa ni Mwenyeheri hapo tarehe 2 Oktoba 2011, katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Aliyepalizwa mbinguni, jimboni Katoliki la Ivrea, nchini Italia. Ibada hii pia ilihudhuriwa na Maaskofu kadhaa kutoka katika Majimbo ambamo Masista wa Ivrea wanatekeleza dhamana na utume wao. Maisha ya Mama Antonia Maria Verna yamekuwa ni nuru angavu inayowafungulia watu wa Mungu upeo wa: imani, matumaini na mapendo, katika uhuru kwa ajili ya kumpenda na kumtumikia Mwenyezi Mungu pamoja na watu wake! Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili ambaye alisema ndiyo bila masharti, anaendelea kuwafunda watawa wake kutokuwa na mipaka katika utume wao.

Ni katika muktadha huu, tangu mwanzo kabisa wa maisha na utume wa Shirika la Ivrea, kutoka nchini Italia wamejizatiti katika safari ya umisionari kuelekea Mashariki: yaani Uturuki, Lebanoni na Israeli, ili kushiriki katika majadiliano ya kidini, kitamaduni na kiekumene kwa kuheshimu na kuthamini: imani na tamaduni tofauti za watu, kwa sababu upendo ni amri ya Yesu. Masista wameelekea pia nchini Libya ambako kwa takribani zaidi ya miaka 50 wamewahudumia watu wa Mungu nchini humo katika Hospitali, lakini kwa sasa utume huu umesitishwa kutokana na machafuko ya kisiasa na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea nchini humo. Masista walifunga safari pia kuelekea nchini: Argentina, Pennsylvania, Tanzania, Kenya na mwisho Albania na Mexico kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo, matumaini na furaha inayobubujika kutoka katika Msalaba wa Kristo Yesu.

Viongozi wapya SCIC

 

 

 

11 January 2021, 15:35