Domenika ya Neno la Mungu: Neno la Mungu linalosomwa, kutafakariwa na kumwilishwa katika maisha ya kila siku, kama kielelezo cha imani tendaji! Domenika ya Neno la Mungu: Neno la Mungu linalosomwa, kutafakariwa na kumwilishwa katika maisha ya kila siku, kama kielelezo cha imani tendaji! 

Dominika ya Neno la Mungu: Neno la Mungu Katika Maisha ya Watu!

Ni katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, tunaona nafasi na umuhimu wa Neno la Mungu. Ni kwa njia ya Neno lake, tunajifunza Neno la Mungu, tunaingia katika mahusiano na mafungamano na Mungu mwenyewe, Dominika ya Neno la Mungu iamshe ndani mwetu kiu ya Neno la Mungu, kulisoma, kulitafakari na kujifunza kwa bidii, ili liweze kuwa ni taa na dira ya maisha yetu!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na salama. Leo ikiwa ni Dominika ya tatu ya mwaka wa Kanisa, pia ni Dominika ya Neno la Mungu, hivyo nawaalika kuzingatia katika tafakuri zetu za kila Dominika kuzama zaidi na zaidi katika hilo Neno kwani ni katika Neno tunakutana na Mungu, anayenena nasi, lakini pia anayesubiri jibu kutoka kwa kila mmoja wetu. Neno la Mungu ni mdahalo wenye pande mbili, ni majadiliano kati ya marafiki wawili, yaani Mwenyezi Mungu na kila mmoja wetu. Na ndio tutaona pia katika tafakari yetu ya leo majadiliano na mdahalo huo wa kirafiki kati ya Yesu wa Nazareti na wafuasi wake wale wa kwanza. Dominika ya Neno la Mungu, kama anavyotualika Baba Mtakatifu Fransisko uadhimishwa kila Dominika ya tatu ya Mwaka wa Kanisa kadiri ya Barua yake ya Aperuit Illis (Aliwafunulia akili zao) ya mwaka 2019, Septemba 30, kwayo anatutaka sote, yaani wachungaji na waamini walei, kuona umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya kila mwamini, na pili kuangalia mahusiano ya ndani kabisa ya Neno la Mungu na Maadhimisho yetu ya Kiliturujia.

Sisi kama waamini wakristo, ni watu tunaosafiri katika historia, na daima tunasafiri si peke yetu, bali na Mungu kati yetu, anayebaki pamoja nasi akinena nasi kwa njia ya Neno lake na kutulisha kwa Sakramenti zake. Kuwa na siku moja kama Dominika ya Neno la Mungu, haimaniishi Neno la Mungu linakuja kwetu mara moja kwa mwaka, bali mara moja kwa mwaka mzima, kwa kuwa tunao uhitaji wa lazima wa kulijua Neno la Mungu, wa kumjua Yesu Kristo Mfufuka, ambaye daima anajifunua kwetu kila linapomegwa Neno lake na Mwili wake katika Maadhimisho yetu ya Kiliturujia. Ni katika Liturujia zetu tunaona nafasi na umuhimu wa Neno la Mungu. Ni kwa njia ya Neno lake, nasi kwa kujifunza Neno la Mungu tunaingia katika mahusiano na Mungu mwenyewe, kinyume chake mioyo yetu inabaki kuwa baridi na macho ya mioyo yetu inabaki katika upofu, kama ilivyo ada tunavyoona upofu wa aina mbali mbali katika ulimwengu wetu wa leo. Dominika ya Neno la Mungu iamshe ndani mwetu kiu ya Neno la Mungu, kulisoma na kulitafakari na kujifunza vema Maandiko Matakatifu.

Ni kwa njia Liturujia ya Neno ya Mungu yaani masomo ya Misa, tunaona Mungu anaongea na watu wake na Kristo kwa namna ya pekee anapotangaza Injili yake, Habari Njema ya Wokovu wetu. Ni katika Injili tunafikia kilele na tamati ya Ufunuo wa Mungu kwetu wanadamu. Na ndio maana katika Maadhimisho ya Kiliturjia Mama Kanisa anahimiza umuhimu wa kuwa na Kitabu cha Injili, nacho ndio kinabebwa kwa heshima wakati wa maandamano ya kuingia kabla ya Ibada ya Misa Takatifu.  Katika baadhi ya makanisa yetu, tunaona kuna mahali maalumu ambapo hapo Injili ya Kristo ufunuliwa kila siku. Mama Kanisa anatualika, kwa njia ya kutafakari vema masomo yote ya Misa kadiri yalivyopangwa kiliturjia na kutuhimiza kuheshimu na kuwa waaminifu bila kuyabadilisha, kwani yamepangwa kwa namna ya kutusaidia kuingia na kumjifunza Mungu na Bwana wetu Yesu Kristo, kwa njia ya Neno la Mungu.

Kutokana na umuhimu huo tunaona Kwa Barua hii binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Spiritus Domini” yaani “Roho wa Bwana”: Utume wa Waamini Walei kutoka katika Ubatizo”, kuanzia sasa wanawake wenye sifa wanaweza kupewa huduma ya usomaji na utumishi Altareni. Baba Mtakatifu amepanua wigo, leo si tu wanaume bali hata wanawake wenye kuonekana na sifa stahiki kuwa watangazaji wa Neno la Mungu, kwa kusimikwa rasmi kama watangazaji wa Neno, yaani Lectors. Watangazaji wote wa Neno la Mungu, wanaalikwa kujiandaa vema kabla ya kulitangaza hilo Neno la Mungu. Ni utume unaotokana na nguvu ya Roho Mtakatifu tuliyempokea kwa mara ya kwanza siku ya Ubatizo wetu. Kila mbatizwa anaalikwa kuwa mtangazaji wa Neno la Mungu iwe kama msomaji lakini zaidi sana kwa mifano mema ya maisha yetu ya siku kwa siku, kuwa mashahidi wa Neno la Mungu kwa njia ya maisha yetu.

Kiti cha Neno la Mungu au mimbari (ambo), hakina budi kupewa heshiwa stahiki, na kamwe isitumike kama mahali pa matangazo au mambo yanayokuwa nje ya kulitangaza Neno la Mungu. Mama Kanisa leo anatualika kuzingatia kuwa mimbari ni meza ambapo Neno la Mungu linatangazwa, kuimba wito wa katikati, mbiu ya Pasaka, mahubiri, nia za Misa na sala za waamini, na anatuangalisha kuwa kamwe tusitumie mimbari ya Masomo kwa ajili ya uratibishaji wa Liturjia au matangazo au mambo ya namna hiyo. Ni vema kulizingatia hili katika makanisa yetu yawe ya kigango au kiparokia. Mama Kanisa kwa kuzingatia umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya kila mwamini, kuwepo na mikakati ya kuwasaidia waamini kujifunza Neno la Mungu, labda kijimbo, kiparokia na hata katika jumuiya zetu ndogo ndogo za Kikristo.

Tunaalikwa pia kuona uhusiano uliopo wa Neno la Mungu na Maadhimisho mengine ya kiliturjia kama sala za masifu, na hata kuhimiza kuwepo na desturi ya kusali sala ya Kanisa kwa pamoja katika jumuiya zetu mbali mbali iwe za kiparokia, jumuiya ndogo ndogo na hata katika familia zetu majumbani.Baba Mtakatifu anamuweka mbele yetu kama mfano wa mtakatifu aliyependa kwa dhati Maandiko Matakatifu, Mt. Jerome. Mtakatifu Jerome alijifunza kwa bidii Maandiko Matakatifu, aliyafasiri, aliyaelezea maana yake hasa inayozingatia lugha za Kibiblia, na aliyekuwa na kiu na hamu kubwa ya kuwafundisha wengine Neno la Mungu na kulisambaza. Ndio nasi leo tunaalikwa kuiga fadhila hizi za Mtakatifu Jerome, hasa kwa kutenga muda ikiwezekana kila siku kulisoma na kulitafakari Neno la Mungu na kuwa tayari pia kulisambaza kwa njia ya maisha yetu yanayoakisi Neno hilo la Mungu.

Taifa la Wanawaisraeli baada ya kuchagua kuongozwa na wafalme kama watu wa mataifa mengine, walibaki na mateso makubwa kwa miaka mingi. Ni baada ya kuwa na wafalme waliowafanya kuwa mbali na Mungu wao aliyewateua na kuwakomboa kutoka utumwani Misri. Hivyo katika Injili ya leo Yesu Kristo anapowahubiria juu ya ufalme wa Mungu, wasikilizaji wake walielewa vema kuwa sasa baada ya kuona wafalme wao wameshindwa kuwalinda na kuwatetea dhidi ya maadui wao, ni Mwenyezi Mungu pekee anayeweza kulinda na kuongoza watu wake. Taifa la Israeli kwa miaka mingi lilibaki kusubiri ahadi ya Mungu mwenyewe na hasa ufalme wake kurudi katikati yao. Wakati umefika sasa ambapo Mwenyezi Mungu amefika kuwakomboa watu wake.  Muda wa kusubiri umekwisha na sasa imefika saa ile ya kufarijiwa na amani, saa ya ufalme wa Mungu na ahadi zake kwa watu wake umewadia.

Neno Injili linatokana na neno la Kigiriki ευαγγλιον (eungelion) likimaanisha habari njema. Hivyo kila habari njema ilikuwa inaitwa euangelion mathalani, ushindi wakati wa vita, kupona maradhi fulani, kuzaliwa kwa mfalme, kuhitimsihwa kwa vita. Na ndio mwinjili Marko anamtambulisha Yesu kuwa ndiye amekuja kuleta Habari njema ya ufalme wa Mungu. Ni upendo wa ujio wa Mungu kati yetu, ni Mungu anayekuja kusimika ufalme wake ulimwenguni. Ni Habari njema hivyo kila anayeisikia Habari hiyo hujawa na furaha na amani ya kweli. Ndio Injili maana ni Habari ya Upendo wake Mungu kwa mwanadamu. Neno la Mungu ni Habari Njema kwani ni Habari ya Furaha na Matumaini kwa kila mmoja wetu. Ni Neno linalouhisha tena maisha ya kila muumini. Habari Njema inatualika mimi na wewe pia kutubu na kuamini. Toba anayozungumzia Marko Mwinjili sio tu tendo la kuacha dhambi bali ni kubadili mtazamo wetu kumuhusu Mungu, mwanadamu, ulimwengu na historia.  Mara nyingi tunasisitiziwa sana juu ya kubadili tabia zetu ila tunasahau kuwa Mungu wetu anataka hasa tuwe na mahusiano ya upendo kati yetu na yeye.

Kumwona Mungu siyo kama hakimu au mtungaji wa sheria na amri tu bali anataka kuwa na mahusiano ya baba na mwana na watu wake. Ni mahusiano ya upendo na urafiki. Neno linalotumika katika kwa kigiriki ni μετανοειτε (Metanoeite) likimaanisha tubuni, ni amri au agizo la kututaka kubadili namna yetu au mtazamo wetu kumhusu Mungu. Ni kubadili kichwa! It is the change of attitude! Ni kwa njia hiyo hapo tunaweza kusema Neno lake ni Habari Njema, kwani ni Habari inayotujaza furaha na tumaini tena. Yesu Kristo anatualika mimi na kuwa kuwa na kichwa kipya, kwa maana mtazamo wetu mpya kumuhusu Mungu. Mungu ni Baba yetu anayetupenda. Ni mwaliko kwetu pia kumpenda Mungu na kuwa daima karibu naye. Toba ya kweli ni kuwa na URAFIKI na MUNGU, ni UPENDO kwa Mungu. Ni kukaa na Mungu katika maisha yetu ya siku kwa siku.Toba ya kweli ni mahusiano yetu na Mungu na wenzetu, ni kuingia katika mahusiano ya mapendo kwa Mungu na kwa jirani.

Kuamini pia Injili, kitenzi neno la Kigiriki linalotumika ni πιστευετε (Pisteuete) ni kuwa na hakika katika HABARI NJEMA, siyo habari ya kubahatisha ni hakika kuwa Mungu anatupenda na anataka kuwa na mahusiano ya upendo na kila mmoja wetu. Ni ahadi ya Mungu aliye daima mwaminifu na hivyo kamwe hatutahadaika na Habari hii njema.Tunaalikwa kuamini Neno lake kwani Yeye daima ni mwaminifu kwetu, hata mara moja hatakwenda wala kutenda kinyume na Neno lake, ni Neno la Mungu linamuakisi Mungu mwenyewe.    Sehemu ya pili ya Injili ya leo ni kuhusu wito wa wale wafuasi wanne wa kwanza, ni ndugu wale wanne, yaani, Simone na nduguye Andrea na pia Yakobo na nduguye Yohane. Tofauti na Mwinjili Yohane (Yoh 1:35-51), Mwinjili Marko lengo na shabaha yake sio kutueleza hasa kwa mapana jinsi au mazingira waliyoitwa wale wafuasi wa kwanza. Mwinjili Marko hatuelezi kama walimsikia kwanza Yesu Kristo kabla ya wito wao au la, hatuelezi ni kwa nini wanakubali kumfuasa Yesu Kristo bila kuweka pingamizi au swali lolote.

Marko mwinjili anataka hasa kutuonesha ni kwa jinsi gani wewe na mimi katika maisha yetu ya siku kwa siku tunakutana na Yesu Kristo na anatualika sote kumfuasa, kuenenda katika urafiki na mahusiano ya upendo pamoja na Yesu Kristo. Ni Yesu hasa tunayekutana naye katika meza ya Neno na Mwili wake. Sehemu ya Injili ya leo haitupi picha kamili maana ni kama inatoka sehemu moja kwenda nyingine kwa haraka bila matayarisho ya kutusaidia kujenga picha kamili ya matukio. Lengo la mwinjili Marko ni kuonesha kuwa hakuna muda wa kupoteza maana ile ari na shauku ya kutangaza HABARI NJEMA ni kubwa hivi hatupaswi kupoteza muda, ni wakati umekamilika, ile saa imefika ya ufalme wa Mungu na hivyo Yesu Kristo anatualika kwa haraka kwenda nasi kumfuasa. Ni wakati wa neema, ni fursa adimu, hivyo kila mmoja wetu hanabudi kutumia fursa hiyo, ni καιρος (kairos) yaani muda muafaka, ni fursa. Wakati au muda anaozungumzia Yesu Kristo sio ule wa kawaida kwa maana ya κρονος (kronos) bali ni καιρος(kairos). Kwa wale wanaosoma tafakari hizi tangu mwaka jana labda sasa wanaanza kidogo kidogo kuzoea maneno haya ya Kigiriki maana tuliyatumia katika Dominika zile za Majilio.

Na ndio Mwinjili Marko anatupatia pia picha ya Yesu kuwa hasimami na kugeuka nyuma kuangalia kama wale aliowaita wameitika wito wake au la. Hakuna kupoteza muda, ni muda wa kutangaza ufalme wa Mungu na hivyo kila mmoja wetu awe na hamu na shauku ya kutangaza Injili. Dominika ya Neno la Mungu, inatualika nasi leo kujawa na shauku hiyo hiyo ya kuwashirikisha wengine Habari Njema, iwe katika familia zetu, jumuiya zetu, mitaa yetu, mahali pa kazi na kadhalika na kadhalika, ni kwa njia ya maisha yetu kila mmoja anaalikwa kuwa shahidi wa Habari Njema, yaani wa Neno la Mungu. Labda cha kutafakarisha tena ni kuwa wafuasi wale wa kwanza, Yesu Kristo haendi kuwaita kutoka hekaluni au katika masinagogi, bali anakutana nao katika mazingira yao ya kazi zao za kila siku.  Ni kama Musa anaitwa wakati anachunga kondoo wa baba mkwe wake. Hivyo Yesu Kristo anatualika sote katika sehemu zetu mbali mbali na shughuli zetu mbali mbali kumfuasa yeye, maana yake ni kuwa na mtazamo mpya na kuanza kutangaza nasi Habari hiyo njema ya furaha.

Neno lake linatujia na kutualika katika hali zetu za kila siku, Neno la Mungu pamoja na kulisoma na kulitafakari hapa Kanisani, bali pia halina budi kuwa ndio taa ya maisha ya kila mmoja wetu katika nyanja na hali zote. Wafuasi wale wanaacha mara moja nyavu zao. Nyavu pia inaweza kueleweka kama lugha ya picha ya kuacha nyuma yale yote yanayotuzua kumfuasa Yesu Kristo, nyavu zinatufunga na kutufanya kushindwa kumfuasa Yesu Kristo. Kila mmoja wetu kwa namna moja au nyingine anazo nyavu zake zinazomzuia kuwa na uhusiano wa upendo na kirafiki na Mungu. Ni mwaliko wa kuziacha mara moja. Nyavu zinatufanya tushindwe kusonga mbele, kukua katika mahusiano yetu kwa Mungu na kwa wenzetu. Waliacha pia watumishi wao nyuma maana ni wao sasa wanaalikwa kuwa watumishi wa Habari Njema ya Wokovu. Ni mwaliko wa kutumikia. Waliacha pia baba yao Zebedayo, baba ni ishara na alama ya mapokeo.

Kuacha baba ni kuacha mtazamo ule wa kimapokea na kuanza mtazamo mpya wa mahusiano ya upendo kati yetu na Mungu Baba. Mungu ni upendo! Ni kukubali kuanza maisha mapya, kimtazamo na hata kiutendaji. Kila anayekutana na Mungu katika Neno lake, anaalikwa kuacha nyavu, kuacha nyuma baba na watumishi wake, ndio kusema kuanza aina na mtindo mpya wa maisha, kuanza kuongozwa na mantiki sio ile ya kibinadamu bali ya Mungu mwenyewe. Wito wa Yesu ni Kristo ni kumfuasa hivyo kutoka katika hali zetu za awali na kuanza kumfuasa kwa maana ya kuwa na mahusiano mapya. Tofauti na walimu wengine ambao wanafunzi walienda kwao kujifunza, Yesu anatualika Yeye tumfuase. Hivyo wewe na mimi hatuna budi kuacha nyavu, baba au watumwa wetu na kuanza kumfuasa Yesu mara moja bila kupoteza wakati. Wakati umetimia wa kuujenga ufalme wa Mungu hapa duniani. Ni καιρος! Ndio saa ile ya neema! Nawatakia Dominika njema ya Neno la Mungu na tafakuri njema ya kuitikia wito wa Mungu, yaani Habari Njema katika maisha yetu.

22 January 2021, 08:27