Tafuta

Askofu mkuu mwandamizi Abel Gabuza wa Jimbo Kuu la Durban Afrika ya Kusini amefariki dunia jumapili tarehe 17 Januari 2021 baada ya kupambana na Corona kwa juma zima huku akiwa "ICU" Askofu mkuu mwandamizi Abel Gabuza wa Jimbo Kuu la Durban Afrika ya Kusini amefariki dunia jumapili tarehe 17 Januari 2021 baada ya kupambana na Corona kwa juma zima huku akiwa "ICU" 

Askofu Mkuu Mwandamizi Abel Gabuza: COVID-19 Yakatisha Maisha Yake!

Askofu mkuu mwandamizi aliyekuwa na haki ya kurithi Jimbo kuu la Durban Abel Gabuza amefariki dunia, tarehe 17 Januari 2021 nchini Afrika ya Kusini. Askofu mkuu Abel Gabuza amepambana kiume kwa muda wa juma zima dhidi ya Virusi vya COVID-19, akiwa amelazwa katika chumba cha uangalizi maalum Hospitalini hapo, ICU. Sasa anapumzika kwenye usingizi wa amani. RIP. Amina!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Wilfrid Fox Napier, OFM, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Durban, Afrika ya Kusini, anasikitika kutangaza kifo cha Askofu mkuu mwandamizi aliyekuwa na haki ya kurithi Jimbo kuu la Durban Abel Gabuza kilichotokea kwenye Hospitali ya Hillcrest, Jumapili tarehe 17 Januari 2021 huko nchini Afrika ya Kusini.  Askofu mkuu Abel Gabuza amepambana kiume kwa muda wa juma zima dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, akiwa amelazwa katika chumba cha uangalizi maalum Hospitalini hapo, ICU. Juhudi za madaktari kutaka kuokoa maisha yake, zimegonga mwamba. Marehemu Askofu mkuu mwandamizi Abel Gabuza amekuwepo Jimbo kuu la Durban kwa muda wa miaka miwili sasa. Sasa Mwenyezi Mungu amemwita, ili akampumzishe kwenye usingi wa amani, akiwa na matumaini ya ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele!

Katika kipindi hiki kifupi, watu wa Mungu Jimbo kuu la Durban walianza kuonja, wema, upole na majitoleo yake kama mchungaji mwema na mwaminifu. Atakumbukwa na wengi kutoka Pretoria mahali alikozaliwa; Jimbo Katoliki la Kimberley alikofundisha, akaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu na sasa Jimbo kuu la Durban. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 9 Desemba 2018, alimteuwa Askofu Abel Gabuza kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Durban, Afrika ya Kusini. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu mwandamizi Gabuza alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Kimberley, Afrika ya Kusini. Ni kiongozi wa Kanisa aliyejipambanua na akasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Hakuwafumbia macho wala rushwa nchini Afrika ya Kusini. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mwandamizi Gabuza alizaliwa kunako tarehe 23 Machi 1955 huko Alexandra, Pretoria, Afrika ya Kusini wakati ambapo sera za ubaguzi wa rangi zikiwa zimepamba moto Afrika ya Kusini. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, kunako tarehe 15 Desemba 1984 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 23 Desemba 2010 akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kimberley na hatimaye, kuwekwa wakfu tarehe 19 Machi 2011. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 9 Desemba 2018 akamteuwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Durban, Afrika ya Kusini!

Na habari zaidi kutoka Afrika ya Kusini zinabainisha kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, kuanzia Jumanne tarehe 19 hadi 22 Januari 2021 linafanya mkutano wake mkuu kwa njia ya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Hii inatokana na wimbi kubwa la maambukizi ya gonjwa la Corona, COVID-19 nchini Afrika ya Kusini. Hadi kufikia tarehe 18 Januari 2021 majira ya mchana, watu milioni 1.34 walikuwa wameambukizwa Virusi vya Corona, COVID-19. Kati ya wagonjwa hawa, waliopona ni milioni 1.1. Watu waliofariki dunia ni 37, 105.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, SACBC limesema kwamba, Askofu Xolelo Thaddaeus Kumalo aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Novemba 2020 kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Witbank, hataweza kusimikwa tena tarehe 24 Januari 2021 kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali. Itakumbukwa kwamba, Askofu Xolelo Thaddaeus Kumalo alizaliwa tarehe 2 Julai 1954 na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 10 Oktoba 1991 kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Bethlehemu, Afrika ya Kusini. Tarehe 11 Machi 2008 akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Eshowe na hatimaye, kuwekwa wakfu tarehe 7 Juni 2008. Tarehe 25 Novemba 2020 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Witbank, Afrika ya Kusini.

Naye Askofu mteule Robert Mogapi Mphiwe, aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Novemba 2020 kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rustenburg, Afrika ya Kusini, hataweza kusimikwa hapo tarehe 7 Februari 2021 kama ilivyokuwa imepanga hapo awali kutokana na kuibuka kwa wimbi kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Askofu mteule Robert Mogapi Mphiwe alizaliwa tarehe 14 Machi 1972 Jimbo kuu la Pretoria, Afrika ya Kusini. Alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 1 Novemba 1997. Tarehe 25 Novemba 2020, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Rustenburg.

Askofu mkuu Gabuza
18 January 2021, 15:31