Tafuta

Askofu Mstaafu JB Kagwa: 23 Machi 1943 hadi 20 Januari 2021: Kiongozi wa Kanisa aliyejipambanua kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu nchini Uganda. Sasa Apumzike kwa Amani. Askofu Mstaafu JB Kagwa: 23 Machi 1943 hadi 20 Januari 2021: Kiongozi wa Kanisa aliyejipambanua kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu nchini Uganda. Sasa Apumzike kwa Amani.  

Askofu JB Kagwa wa Jimbo la Masaka Awaliza Wengi! COVID-19

Askofu mstaafu JB Kaggwa amewaongoza, amewafundisha na kuwatakatifu watu wa Mungu kama Padre kwa wa miaka 49 na kama Askofu kwa wa miaka 25. Tarehe 16 Aprili 2019 akang’atuka. Amefariki dunia akiwa anajiandaa kuadhimisha miaka 78 tangu alipozaliwa. Sasa amelala kwenye usingizi wa amani, huku akiwa na tumaini la ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Machozi na majonzi makubwa yaliwakumba watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Masaka, Uganda Jumamosi tarehe 23 Januari 2021, wakati mwili wa Marehemu Askofu mstaafu John Baptist Kaggwa, maarufu kwa jina la JB Kagwa ulipokuwa unashushwa taratibu kaburini. Askofu mstaafu Kaggwa amefariki dunia tarehe 20 Januari 2021, baada ya kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kwa muda wa miezi miwili. Alikuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Mulago, Jijini Kampala. Askofu mstaafu JB Kaggwa anakumbukwa na wengi kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu nchini Uganda. Daima, amekuwa ni kiongozi wa Kanisa aliyependa kuona utawala wa sheria ukizingatiwa na wote. Katika maisha na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, alijifunga kibwebwe kupambana na ujinga, umaskini na maradhi kwa kuwekeza zaidi katika miradi ya kiuchumi na kijamii. Mradi wa Maendeleo Jimbo Katoliki la Masaka, MADDO, umwekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kilimo na ufugaji wa Ng’ombe wa kisasa.

Mradi huu umewahakikishia watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Masaka: Kilimo bora na cha kisasa na hivyo kuwa na uhakika pamoja na usalama wa chakula kwa wakazi wake na chanzo cha ajira na mapato kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Masaka. Anakumbukwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA kwa kuonesha mfano bora wa kuigwa katika kujenga na kudumisha mshikamano na udugu wa kibinadamu miongoni mwa watu wa Mungu ndani na nje ya AMECEA.Askofu mstaafu JB Kaggwa alipenda kusogeza huduma ya maisha ya kiroho karibu zaidi na maisha ya waamini wake. Hadi kufikia mwaka 2021 Jimbo Katoliki la Masaka lina Parokia 55. Nyingi ni zile zlizoanzishwa na Askofu mstaafu JB Kaggwa enzi ya uongozi wake. Wakati anang’atuka madarakani, Jimbo Katoliki la Masaka, kwa sehemu kubwa liliweza kujitegemea kwa rasilimali watu na vitu! Alikuwa ni mhubiri mzuri na “mjasiriamali wa kutupwa”. Alipenda kutoa kipaumbele kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kuwatambua kuwa ni rasilimali na walengwa wakuu wa mchakato wa Uinjilishaji mpya. Ni kiongozi aliyethamini rasilimali muda, kiasi kwamba, alikuwa anawahi eneo la tukio kuliko hata waandaaji wenyewe, ili kuonesha umuhimu wa kuzingatia rasilimali muda kama kichocheo cha maendeleo fungamani ya binadamu.

Askofu mstaafu JB Kaggwa alithamini na kuwekeza katika mchakato wa uinjilishaji wa kina, kwa njia ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, kwa kuanzisha Kituo cha Radio cha Centenary, 88.1 FM, ili kwamba, Habari Njema ya Wokovu iweze kuwafikia watu wengi zaidi mahali walipo! Lakini yote haya aliyafanya kwa moyo wa unyenyekevu kabisa. Marehemu Askofu mstaafu John Baptist Kaggwa, amezikwa kwenye Kikanisa cha Seminari Ndogo ya Bukalasa, Jimbo Katoliki la Masaka. Itakumbukwa kwamba, Askofu mstaafu JB Kaggwa alizaliwa tarehe 23 machi 1943 huko Bulenga, Wakiso Mkoani Buganda. Ni kati ya wanafunzi “machachari sana” waliosoma Falsafa kwenye Seminari ya Katigondo. Kunako mwaka 1965 alipelekwa mjini Roma ili kuendelea na masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana. Mwezi Mei 1971 akapewa Daraja ya Ushemasi. Tarehe 12 Desemba 1971, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre akiwa na umri wa miaka 28. Akabahatika kuteuliwa kuwa Gambera Msaidizi Chuo Kikuu cha Kipapa cha “San Paolo Roma”.

Askofu mstaafu JB Kaggwa, aliwahi kuwa Gambera wa kwanza wa Seminari kuu ya “St. Mbaaga iliyoko Ggaba, Jimbo kuu la Kampala, Uganda. Tarehe 19 Desemba 1994 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu Mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo Katoliki la Masaka. Tarehe 24 Juni 1995 akawekwa wakfu kuwa Askofu. Tarehe 10 Januari 1998 akasimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo la Masaka. Kwa ufupi amewaongoza, amewafundisha na kuwatakatifu watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Masaka kama Padre kwa muda wa miaka 49 na kama Askofu kwa muda wa miaka 25. Tarehe 16 Aprili 2019 akang’atuka kutoka madarakani. Askofu mstaafu John Baptist Kaggwa amefariki dunia akiwa anajiandaa kuadhimisha miaka 78 tangu alipozaliwa. Sasa amelala kwenye usingizi wa amani, huku akiwa na tumaini la ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele!

Askofu Jb Kaggwa

 

26 January 2021, 15:13