Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Majilio: Habari Njema ya Wokovu: Injili Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Majilio: Habari Njema ya Wokovu: Injili 

Tafakari Jumapili 2 Kipindi cha Majilio: Habari Njema ya Wokovu!

Injili ya Marko ni ya kwanza kwa kuandikwa katika Injili nne tunazokuwa nazo katika Agano Jipya. “Ἀρχη του ευαγγελιου Ἰησου Χριστου υιου του Θεου.” “Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.” Marko 1:1. Labda tunajiuliza kwa nini Mwinjili anaamua kuanzia na sentensi hii ya kutuambia ni “Mwanzo wa Injili”. Huu ni mwaliko wa kumjifunza Marko katika Injili yake!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Liturujia ya Dominika ya leo, tunasoma sura ile ya kwanza ya Injili ya Mwinjili Marko, na ndio Injili itakayotusindikiza katika kipindi cha mwaka mzima wa kiliturujia tuliouanza Dominika ile ya kwanza ya Majilio. Injili ya Marko ni ya kwanza kwa kuandikwa katika Injili nne tunazokuwa nazo katika Agano Jipya.  “Ἀρχη του ευαγγελιου Ἰησου Χριστου υιου του Θεου.” “Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.” Marko 1:1. Labda tunajiuliza kwa nini Mwinjili anaamua kuanzia na sentensi hii ya kutuambia ni “Mwanzo wa Injili”, wakati anajua kuwa tunajua kwa hakika kuwa tupo mwanzoni mwa Injili aliyotuandikia? Mwinjili Marko, hatumii maneno hayo kwa bahati mbaya tu. Hivyo, niwaalike tunapotafakari Injili ya Mwinjili Marko mwaka huu, tangu mwanzo kujifunza pia aina za uandishi na kwa nini anaandika katika mtindo huo na hata baadhi ya maneno anayoyatumia.

“Mwanzo wa Injili…”, ni maneno yenye kutualika kutafakari juu ya mwanzo ule wa uumbwaji wa ulimwengu. Na sio mwanzo katika muda bali mwanzo wa uwepo wa vyote vilivyopo kutoka kutokuwepo kabla, yaani uumbaji “ex nihilo”. Ni uwepo ule unaopata maana tu kwa kuwa Mungu yupo. Hivyo ni mwanzo anaouzungumzia Mwinjili Marko ni “Principium” wa kila kitu kilichopo. “Hapo mwanzo, Mungu aliumba mbingu na dunia.” Mwanzo 1:1. Ulimwengu umeumbwa kutoka mikono ya Mungu, ni matunda ya wema na upendo wake, na ulimwengu kutoka mikononi mwa Mungu, tazama kila kitu ni chema na kizuri. Ni kupitia mwanadamu, kutokana na ukaidi wake basi dhambi ikaingia duniani. Na ndio tunaona ahadi ya Mungu kupitia nabii Isaya: “Sasa, naumba mbingu mpya na dunia mpya. Mambo ya zamani hayatakumbukwa tena.” Isaya 65:17

Na ndio tunaona leo Mwinjili Marko anapozungumzia huu mwanzo mpya, anatoa tangazo la furaha, tangazo la Habari Njema ya Furaha! Kwa kweli neno la Kigiriki linalotumika hapa “euangeliou”, mwanzoni halikuwa na maana tunayokuwa nayo leo, kumaanisha zile Injili nne. Ni neno lenye maana ya “Habari Njema ya Furaha”, ingeweza kuwa ni tangazo la kuzaliwa mfalme, tangazo la kushinda vita, au tangazo lingine lolote lenye kuleta furaha na matumaini makubwa, kila tangazo la furaha liliitwa ni habari njema, yaani kwa Kigiriki ndiyo “euangeliou”.  Jumuiya ile ya kwanza ya wakristo katika karne ya kwanza, walikuwa wanajiuliza; Ni lini na kwa namna gani basi wanaingia katika ulimwengu mpya kwa njia ya imani waliyoipokea? Ni katika kujaribu kujibu swali hili, mnano karne ile ya kwanza wakati wakiwepo wengi waliomuona na kushuhudia fumbo la Kristo, yaani maisha yake, mateso, kifo na ufufuko wake. Waamini wale waliona haja ya kukusanywa na kuwekwa katika maandishi, “Tangazo la Habari Njema ya Wokovu”, tangazo lilionesha mwanzo wa uumbwaji mpya,

Marko Mwinjili, ambaye mapokeo yanamtaja kuwa alifuatana na Mtume Petro na alikuwa kijana aliyeheshimika katika jumuiya ile ya waamini, akateuliwa kuyakusanya na kuyaweka katika Maandiko. Na hata mapokeo yanasema yawezekana ni nyumbani kwa akina Marko, Yesu Kristo na mitume wake waliila karamu ile ya mwisho. Na hata jumuiya ya kwanza ya waamini kule Yerusalemu, walikuwa wanakusanyika na kuadhimisha Neno na Ekaristi, nyumbani kwa akina Marko. Nyumbani hapo ambapo hata msichana wa kazi wa familia ile aliijua sauti ya Mtume Petro na hata kumfungulia baada ya kutoka gerezani (Matendo 12:12-17). Marko huyu, yawezekana pia ndiye yule anayetajwa kuwepo pale Getsemani wakati askari wakimkamata Yesu, naye shuka alilokuwa amejivika likashikwa na mmoja wa maaskari na kumpasa kukimbia uchi (Marko 14:51).

Marko Mwinjili kwa kutumia mtindo wa masimulizi anajaribu kukusanya na kuyaweka pamoja katika maandishi yale yule aliyoyaona ni muhimu katika “Tangazo la Habari Njema”. Mwinjili Marko anatuonesha, Habari Njema ilianza pale Yohane Mbatizaji alipoanza kutangaza ubatizo wa toba kule jangwani, akiwaalika watu kutubu na kugeuza maisha yao, kuwaalika kumrudia Mungu, ni hapo mwanzo mpya, ni hapo kunakuwa na uumbaji mpya, ulimwengu mpya unaanza pale tunapokiri dhambi zetu na kuamua kuacha maisha ya dhambi. Ni hapo jangwani katika kuacha dhambi, ndio mwanzo wa historia yetu, ndio mwanzo wa Habari Njema, yaani, mwanzo wa Injili.

Kama nilivyoonesha hapo juu kabla, neno “Injili” mwanzoni, halikuwa na maana ile tunayokuwa nayo leo, ya kumaanisha Injili au vitabu vile vinne vya Agano Jipya. Injili kwa maana ya “Tangazo la Habari Njema”, liliweza kumaanisha habari ya ushindi wa vita, habari ya mafanikio kama kuweka makubaliano ya kuacha vita na kuishi kwa amani, kuzaliwa au kusimikwa kwa mfalme, yaani Kaisari wa Kirumi nyakati zile, kwani habari hizi za furaha ziliwahakikishia ustawi wao, afya na hata amani. Ni habari ambazo kwa kila aliyezisikia basi, alijawa na furaha na matumaini.  Mwinjili Marko leo pia anatumia neno hilo “Injili” akilipa maana nyingine mpya. Ni kutuambia kuwa Habari Njema ya kweli ni ya ujio wake Yesu Kristo, ni kukubali Yesu Kristo azaliwe na abadili na kuyapa maana maisha yetu, kwa kutuonesha jinsi ya kuenenda na kuishi. Habari Njema ni Yesu Kristo mwenyewe, Masiha, Mpakwa mafuta wa Mungu, ndiye Kristo wa Mungu.

Mwinjili Marko, mara baada ya sentensi ile ya kwanza ya Injili anamtambulisha mara moja Yohane Mbatizaji. Ni mtu anayeishi maisha ya kujikatalia na kujinyima jangwani, anayeishi mbali na jamii ile iwe kisiasa na hata kidini. Ni mmoja kati ya wana wa Taifa lile ambalo kwa miaka bado wangali safarini kuelekea nchi ile ya ahadi, nchi ya uhuru wa kweli; Kwani walitoka Misri na kuelekea katika nchi ile ya ahadi, lakini bado walichukuliwa tena mateka huko Babeli na baadaye kuongozwa na Mungu kurejea tena Yerusalemu. Hata sasa walipoamini kuwa ni watu huru, hapo anatokea Yohane Mbatizaji na kuanza kuwatangazia tena habari kama ile ya Nabii Isaya.

“Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake.” Ndio maneno ambayo kwa namna ya pekee tunayasikia katika somo la kwanza na la Injili ya leo. Ni maneno ya nabii yule aliyeyatamka wangali uhamishoni Babeli, ili kuwaalika na kuwatia faraja wale waliokuwa wamekata tamaa. “Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo, watu wangu, asema Mungu wenu.” Ni tangazo la kinabii la furaha kwani liliwahikishia mwisho wa mateso yao, hivyo, kuwa na hakika kuwa Mungu anarejea na kuanza kutembea nao tena katika historia yao. Na ndio mwaliko anaoutoa pia Yohane Mbatizaji kwa watu wake kubadili maisha yao kwa kuacha dhambi na kuongoka kwa njia ya kupokea ubatizo ule wa maji.

Wengi wanaitikia wito huo wa Yohane Mbatizaji, wanatoka mijini na kwenda jangwani kuupokea ubatizo ule wa toba. Wanatambua kuwa ni lazima kufanya tena safari ile ya kutoka, ili waweze kufikia nchi kweli ya ahadi, ambayo sio Palestina bali ni nchi ya kuingia katika mahusiano mapya na Mungu kwa kuziacha njia zile zisizofaa wala kumpendeza Mungu. Ili Mungu aweze kuwatangulia na kuwaongoza kama wakati wa tukio la kutoka utumwani Misri, basi hawana budi; “Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu” (Isaya 40). Lazima kuachana na njia zao za zamani na Mungu mwenyewe atawaongoza kutoka nchi ile ya mateka na kuwarejesha tena Yerusalemu.

Ni kwa njia ya Musa mpya, Mungu atawaongoza katika nchi ya ahadi ya kweli, katika maisha mapya ya furaha na amani ya kweli, katika mwanzo mpya wa historia yao. Ni kwa njia ya Mwinjili Marko anategua kitendawili si tu kwao bali hata kwetu leo. Mwinjili Marko anamleta mara moja mwanzoni kabisa mwa Injili yake, Yohana Mbatizaji, ni Yohane Mbatizaji anayekuwa kama kidole kinachomtambulisha na kutuelekeza sisi sote kwa yule aliye “Habari Njema, yaani, Yesu Kristo mwenyewe.” “Na Yohane alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiuoni mwake, akala nzige na asali ya mwitu.” Yohana Mbatizaji hakuvaa mavazi meroro kama wanayovaa wafalme na watu wenye hadhi katika uso wa dunia hii bali singa za ngamia na mshipi wa ngozi na hata chakula chake ni kile cha mwitu. Ndio kusema alikataa kabisa kushiriki uovu na uozo ulikuwepo katika jamii yake, jamii iliyokuwa mbali na Mungu kwa kuishi katika madhambi na uovu mkubwa.

Yohane Mbatizaji kama nabii, kama kidole kile kinachotuelekeza kwa Masiha, anavaa kabisa unabii wake kwa kuishi maishi ya kujikatalia na kujitenga na kila uovu, ni mjumbe anayekuja na kutualika kuandaa njia ya Bwana, na ndio kubadili maisha yetu, kujitenga nasi na uovu na madhambi. Leo tunaishi katika ulimwengu unaoongozwa na falsafa ya kila mmoja ni sahihi maadamu tu haingilii maisha ya mwingine, kila mmoja ni sahihi kwa mtazamo au muono wake, ni ulimwengu wa mkwamo wa maisha adilifu. Ni ulimwengu ambapo mwanadamu amechukua nafasi ile ya Muumba wake, nafasi ile ya Mungu ambaye anapaswa kutuongoza na hivyo hatuna budi kumtii na kulishika Neno lake. Ni Neno lake linalopaswa kuwa taa ya miguu yetu na kutuongoza na kinyume chake ni kuendelea kutembea katika giza nene.

Yohane Mbatizaji kama mmojawapo wa manabii alikuwa na utume maalum; na ndio kuandaa njia ya kutufanya sote kukutana na mapendo ya Mungu kwetu. Mavazi yake yalimtambulisha utume na kazi yake ya kinabii: “Siku hiyo, kila nabii atayaonea aibu maono yake anapotabiri. Hawatavaa mavazi ya manyoya ili kudanganya watu” (Zakaria 13:4). Na hata Eliya kama Yohane; “Alikuwa amevaa vazi la manyoya na mshipi wa ngozi kiunoni” (2 Wafalme 1:8). Labda yafaa tena turejee nyuma na kuona hasa kazi nyingine ya Yohane Mbatizaji; “Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba iletayo ondoleo la dhambi. Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto Yordani, wakiziungama dhambi zao” Kazi kubwa hapa ni kubatiza kwa maondoleo ya dhambi.

Neno “Ubatizo” ni neno linalotokana na lugha ya Kigiriki likiwa na maana ya “kuzamisha majini”, kwa tafsiri sisisi. Lakini pia lilikuwa na maana nyingine, hasa lilipotumika katika muktadha wa kidini hasa ya Kiyahudi. Ni katika muktadha wa Kiyahudi likaanza kutumika likiwa na maana ya kunawa au kutawadha kwa sababu za kujitakasa na najisi za kimwili, mfano mmoja: aliyegusana na mpagani ilimpasa kutawaza, ilimpasa kunawa ili aondokane na najisi hiyo. Lakini pia likaendelea kutumika hata pale mpagani alipoomba kujiunga na dini ya Kiyahudi, basi alibatizwa kwa maji, ndio kusema neno hili tangu mapema likatoolewa na kuanza kutumika katika muktadha wa kidini na kiimani hata kati ya wayahudi.

Lakini Ubatizo wa Yohane ulikuwa tofauti na aina ya ubatizo uliofanyika na Wayahudi kwa ajili ya kujitakasa na najisi mbali mbali. Ubatizo wa Yohane haukuwa kwa ajili ya kuondoa unajisi bali kuwatoa katika maisha ya dhambi, ni wa kubadili maisha yao. Ni ubatizo uliomtaka mmoja kufanya mabadiliko sio ya nje au ya juu juu tu, bali mabadiliko ya ndani, mabadiliko ya maisha. Lakini zaidi sana, tunaona tangu mwanzo mwa Injili ya Marko, kuwa muhusika mkuu sio Yohane Mbatizaji, aliyekuwa ni mtangulizi, ni muandaaji na hata anakiri na kuhubiri Yohane Mbatizaji mwenyewe. “Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake. Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.” Yohana kama nilivyotangulia kusema ni kidole kinachotuonesha na kutueleza kule iliko Habari Njema, kule iliko Injili, yaani kwa Kristo mwenyewe.

Yohane anatuonesha kuwa anayekuja ana nguvu kuzidi yeye na pia mtoaji wa Roho Mtakatifu. Yohana anatuonesha kuwa yeye mfano wa yule anayekuja, Yohana alibaki nyikani akihubiri ubatizo wa toba, bali ajaye atakuwa kati ya wadhambi akiwahubiri toba, lakini zaidi sana kuwapa zawadi ya Roho Mtakatifu. Yohane naye ingawa atateseka na kuuwawa lakini tofauti na yule ajaye kwani baada ya kufa, atafufuka siku ya tatu, na zaidi sana Ubatizo wake, hautakuwa wa maji tu bali katika Roho, katika maisha na mahusiano mapya na Mungu. Ndio kusema kila anayepokea Ubatizo wake Yesu Kristo, sio tu anaondolewa dhambi bali anapata cheo cha kuwa mwana na mrithi pamoja na Mwana pekee wa Mungu. Ni kuwa si tu mtu mwema bali mwana wa Mungu. Ni Habari Njema ya furaha kufanyika si tu watu wema bali wana wake Mungu kwa njia ya Ubatizo wetu katika Roho Mtakatifu. Ni Habari Njema na yenye kutustaajabisha sana! Ukristo sio tena dini tu bali ni mahusiano na Mungu, na ndio maana hata tunaposali, tunapaswa kutambua kuwa tunakuja kukutana na Mungu anayetupenda na kutuhurumia, sala ni mazungumzo na Mungu aliye Baba yetu Mwema wa mbinguni, ni kumsikiliza Mungu na pia nasi kuweza kwa msaada wa Roho kuongea naye. Imani yetu wapendwa inatuanzishia mahusiano mapya na Mungu.

Katika Ubatizo si tu tunaondolewa dhambi zetu na kufanyika viumbe wapya, bali tunazamishwa katika Roho Mtakatifu, katika Roho wa Upendo wa Mungu. Ndio kushiriki kikamilifu katika maisha ya Kimungu, maisha ya neema na utakatifu, maisha ya upendo wa kweli usio na masharti, maisha ya kuongozwa na Mungu mwenyewe kwa njia ya Neno lake na masakramenti, maisha ya kuwa wajumbe wa upendo wa Mungu kwa Mungu mwenyewe na pili kwa jirani kama Kristo, kama Mungu anavyotupenda. Ni maisha ya kuishi ikiwa ni Mungu pekee ndio kipimo chetu, ndio standard yetu, na hilo hatuwezi kwa nguvu wala utashi wetu bali kwa msaada wa Mungu mwenyewe, na ndio neema zake.  Hivyo, Injili ya Marko anatuonesha kuwa Yohane Mbatizaji hakuwa muhusika mkuu wa Injili bali anasimama kama kidole kinachotuonesha na kutuelekeza ilipo Habari Njema ya Furaha, Injili yenyewe, na ndio Yesu Kristo aliye mkuu kuzidi yeye, anayepaswa kuongezeka na yeye kupungua. Nawatakia Dominika na tafakuri njema.

14 December 2020, 09:20