Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili 

Sherehe ya Bikira Maria,Mkingiwa dhambi ya asili

Ni vema na ni haki kabisa kuamini kuwa Bikira Maria aliandaliwa na Mungu tangu nukta ya kwanza ya maisha yake kwa ajili ya mpango wake wa kuukomboa ulimwengu uliokuwa umezama katika dimbwi la dhambi na mauti.Alimuandaa mama huyu kwa kumkinga dhidi ya dhambi ya asili iliyoingizwa ulimwenguni kwa kosa la wazazi wetu wa kwanza Adam na Eva. Ni uzao wake Eva mpya ndio ulimponda kichwa shetani nasi tukakombolewa.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vaticani, tutafakari mafundisho ya Kanisa juu ya Bikira Maria katika sherehe ya kukingiwa dhambi ya asili. Katika mwaka wa kiliturujia Mama Kanisa ameweka siku za kumheshimu Bikira Maria katika adhimisho la Misa Takatifu katika hadhi tofautitofauti kama kumbukumbu za hiari na kumbukumbu za lazima, sikukuu na sherehe. Katika kumbukumbu zilizo za lazima ni: Bikira Maria malkia na mama yetu 22 Agosti, Bikira Maria mama yetu wa mateso 15 Septemba, Bikira Maria mama yetu wa Rozari Takatifu 7 Octoba na kutolewa hekaluni Bikira Maria mwenye heri 21 Novemba. Sikukuu tunazoadhimisha ni: kupashwa habari Bikira Maria kama atakuwa Mama wa Mungu 25 Machi, Bikira Maria kumtembelea Elizabeth 31 Mei na kuzaliwa Bikira Maria 8 Septemba. Sherehe tunazoziadhimisha ni: Bikira Maria Mama wa Mungu 1 Januari, Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni 15 Agosti na Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili 8 Desemba.

Tena kila Jumamosi isiyo na adhimisho maalumu, Kanisa huadhimisha kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Mungu. Kanisa linasisitiza pia kumheshimu Bikira Maria kwa mtu binafsi na katika jumuiya kwa kusali Rozari Takatifu kwani ndiyo ibada ya binafsi inayompendeza sana baada ya zile za kiliturujia hata akatokea sehemu mbalimbali duniani akihimiza tusali rozari ili tupate amani binafsi, kitaifa na kimataifa na pia kuepuka majanga mbalimbali ya asili, kivita na magonjwa kama katika kipindi hiki ambapo dunia hasa nchi za ulaya zinapoteseka kwa janga hili la homa kali ya mapafu inayosababishwa na kirusi cha korona. Kutokana na umuhimu na hadhi aliyonayo Mama Bikira Maria katika Kanisa na katika historia nzima ya wokovu, Kanisa limeweka pia mwezi wa tano kuwa ni mwezi wa Bikira Maria na mwezi wa kumi kuwa ni mwezi wa Rozari Takatifu.

Lakini tuchukue tahadhari katika ibada hizi zote zinazomhusu Bikira Maria hazina maana kuwa tunamuabudu yeye bali tunamtolea heshima ya juu kuliko watakatifu wengine wote. Ni Mungu tu tunampa heshima ya kuabudiwa tunayoiita latria, watakatifu tunawapa heshima tunayoiita dulia na Bikira Maria tunampa heshima tunayoiita yuper-dulia. Kukingiwa dhambi ya asili kwa Mama Bikira Maria ni fumbo la imani alilolifanya Mungu na kutufunulia katika mpango wa wokovu kwa ajili yake na kwa ajili yetu. Katika Injili ya Yohane Yesu alisema; “Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili, lakini atakapokuja huyo Roho wa ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote” (Yoh 16:12-13). Ni kwa msaada wa Roho Mtakatifu mafumbo ya imani juu ya Bikira Maria yamefunuliwa kwa Kanisa. Yeye mwenyewe Bikira Maria alitabiri kuheshimiwa kwake na vizazi vyote kama Mwinjili Luka anavyoandika; “Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mdogo, hivyo tangu sasa vizazi vyote wataniita mwenye heri” (Lk 1:48).

Kwa maongozi ya Roho Mtakatifu Kanisa linakiri na kusadiki wazi kuwa; Bikira maria alikingiwa dhambi ya asili tangu pale alipotungwa mimba. Kwasababu hiyo alizaliwa akiwa na neema ya utakaso. Hii ni zawadi ya pekee kutoka kwa Mungu ambapo kwa mpango wake aliamua kumchagua Bikira Maria na akamtakasa ili kupitia yeye Yesu Kristo azaliwe na ukombozi wetu uweze kutimia. Fundisho hili la Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili lina historia ndefu katika Kanisa. Ni fundisho ambalo limefunuliwa na Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa kwa kufanya tafakari ya fumbo la wokovu wetu kuanzia na fumbo la umwilisho ambapo Mungu mwenyewe alichukua hali ya mwili wetu wa kibinadamu kwa kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo mwilini mwa mama Bikira Maria na kwa tafakari ya kina ya fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Kihistoria tangu karne za mwanzo fundisho la Bikira Maria kutokuwa na dhambi ya asili lilifundishwa. Kanisa la Mashariki lilianza kusherehekea sikukuu ya Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili tangu karne ya 7 na 8. Mapokeo ya Kanisa yanaonyesha kuwa kwa Kanisa la magharibi maadhimisho ya Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili yalianza baadae na mnamo karne ya 19, baadhi ya Monasteri za Ujerumani na Roma walisherehekea sikukuu hii. Kanisa lilifikia hatua ya kutoa tamko na fundisho la Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili baada ya tafakari ya muda mrefu na majadiliano ya kina. Ndipo sasa mnamo 08/12/1854; Papa Pius IX alitoa tamko rasmi katika barua yake ijulikanayo kwa kilatini; ineffabilis Deus akisema: “Kwa uwezo wa Bwana wetu Yesu Kristo na wa mitume Petro na Paulo wabarikiwa na kwa uwezo wetu, tunatangaza, tunabainisha, tunaeleza wazi kuwa Bikira Maria amekingiwa na kuepushwa kabisa na dhambi ya asili, mara alipotungwa mimba, kwasababu alifadhiliwa na kupendelewa kabisa na Mungu Mwenyezi, yeye peke yake, kwa ajili ya mastahili ya Yesu aliye Mkombozi wa watu, basi tunatangaza kwamba mafundisho hayo yamefunuliwa na Mungu mwanyewe.”

Kumbe Bikira Maria ni mkingiwa dhambi ya asili toka siku ile ya kutungwa kwake mimba tumboni mwa mama yake kama matayarisho ya kuwa mama wa Mungu, alizaliwa akiwa na uzima wa neema ya utakaso na katika maisha yake Bikira Maria hakutenda dhambi wala hakuwa na doa lolote la dhambi. Bikira Maria alibaki Bikira daima kabla, wakati na baada ya kumzaa mkombozi kwani alichukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Mtaguso wa Efeso mwaka 431 ulitamka wazi kuwa Bikira Maria ni Mama wa Kristo kwa Kigiriki “Christokos” kwani mwili wake ulichukua mimba ya mkombozi wetu Yesu Kristo, na ni Mama wa Mungu kwa Kigiriki “Theotokos”, maana fumbo la umwilisho yaani Mungu kujifanya Mtu ulifanyika mwilini mwake. Kumbe ushirki mkamilifu wa Bikira Maria katika kazi ya ukombozi wetu na mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo ni sababu tosha ya yeye kukingiwa dhambi ya asili kwani asingeweza kushirika mapambano dhidi ya dhambi na mauti kama yeye mwenyewe angalikiwa katika hali ya dhambi.

Kumbe tunasadiki Bikira Maria tangu atungwe mimba Mungu alimkinga na kila doa la dhambi kwa kutazamia stahili za Yesu Kristo aliye Mkombozi wa binadamu wote. Yeye alikombolewa kwa namna bora zaidi kuliko wanadamu wote kwa kukingiwa dhambi ya asili ambayo wanadamu wote tunazaliwa nayo. Maisha yake yote hakutenda dhambi hata moja. Mapokeo ya Kanisa la mashariki yanamuita A Panagia yaani Mtakatifu tu. Mwaka 1858 Bikira Maria mwenyewe alijitambulisha huko Lurdi (Ufaransa) kwa Mtakatifu Bernadetta Soubirous kama Immaculata yaani asiye na doa. Tena huko Fatima (Ureno) tumefunuliwa moyo wake safi usio na doa.

Maandiko Matakatifu hayaweki wazi kuhusu jambo hili, lakini hata hivyo masomo tunayoyasoma katika sherehe hii yanatoa mwangwi wa fundisho hili la imani limhusulo Bikira Maria. Katika Injili mjumbe wa Mungu malaika Gabriel, aliyetumwa kumpasha habari Bikira Maria juu ya kumzaa mkombozi anamsalimia akisema; “Salamu uliyejaa neema, Bwana yu pamoja nawe.” Naye Bikira Maria anahoji; “Salamu hii ni ya namna gani?” Hofu na swali la Bikira Maria kwa malaika vinadhihirisha kuwa hata yeye hakujua mpango huu wa Mungu. Ni Malaika Gabriel ndiye aliyemfunulia ukweli huu kuwa ni mpango wa Mungu yeye Bikira Maria, kujazwa neema na Mungu kuwa naye na hivyo kuchukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu maana kitakachozaliwa ni kitakatifu, mwana wa Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo, Mkombozi na mfalme wetu. Bikira Maria anatii na kukubali akisema; “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema.” Maandiko Matakatifu yanaendelea kusema kuwa ni kwa uzao wa mwanamke Eva dhambi iliingia ulimwenguni na ni kwa uzao wa mwanamke Bikira Maria dhambi inaondolewa ulimwenguni. Ndivyo somo la kwanza kutoka kitabu cha mwanzo linavyosema kuwa; “Uzao wako (mwanamke) utakiponda kichwa cha nyoka….” Uzao wa mwanamke Eva mpya yaani Bikira Maria ndiye Bwana wetu Yesu Kristo aliyeshinda dhambi na mauti kwa ajili yetu.

Kimsingi Bwana wetu Yesu Kristo aliyezaliwa na Bikira Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu ndiye chanzo cha neema zote kutokana na umungu wake. Bikira Maria ambaye kwake Yesu alipata mwili, alishirikishwa umungu wake kwa namna ya ajabu kwa kuwa alimchukua mimba na baadaye akamzaa Mungu-mtu Bwana wetu Yesu Kristo. Hakika Bikira Maria aliandaliwa vilivyo na Mungu kwa ajili ya ukombozi wetu sisi wanadamu. Ni yeye tu na mwanaye Yesu Kristo ambao walizaliwa katika utakatifu kamili, yaani hawakuguswa na doa lolote la dhambi. Kumbe isingewezekana kabisa kwa mwana wa Mungu ambaye Yeye mwenyewe ni Mungu sawa na Baba achukuliwe mimba na kuzaliwa katika mazingira ya dhambi. Hii ndiyo sababu ya Kanisa kumheshimu na kumsifu Bikira Maria kama mama mtakatifu sana wa Mungu, mama mwenye usafi wa moyo, mama asiye na doa, mama asiye na dhambi.

Ni vema na ni haki kabisa kuamini kuwa Bikira Maria aliandaliwa na Mungu tangu nukta ya kwanza ya maisha yake kwa ajili ya mpango wake wa kuukomboa ulimwengu uliokuwa umezama katika dimbwi la dhambi na mauti. Alimuandaa mama huyu kwa kumkinga dhidi ya dhambi ya asili iliyoingizwa ulimwenguni kwa kosa la wazazi wetu wa kwanza Adam na Eva. Ni uzao wake Eva mpya ndio ulimponda kichwa shetani nasi tukakombolewa. Tumuombe basi Bikira Maria aliyekingiwa dhambi ya asili ili atuombee kwa mwanae nasi siku moja tuje tuungane naye pamoja na watakatifu wote huko mbinguni. Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili, UTUOMBEE.

BIKIRA MARIA MKINGIWA
07 December 2020, 09:26