Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, tarehe 5 Desemba 2020 amefungua na kubariki Seminari kuu ya Nazareth, Mwendakulima, Jimbo Katoliki la Kahama. Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, tarehe 5 Desemba 2020 amefungua na kubariki Seminari kuu ya Nazareth, Mwendakulima, Jimbo Katoliki la Kahama. 

Wosia wa Kardinali Pengo: Ufunguzi wa Seminari Kuu ya Nazareth, Jimbo Katoliki la Kahama

Kardinali Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, hivi karibuni amebariki na kuzindua rasmi Seminari kuu ya Nazareth, iliyojengwa huko Mwendakulima, Jimbo Katoliki la Kahama. Amelitaka Kanisa la Tanzania kumtegemea Mungu, kuwa na mwelekeo chanya katika maisha; kusali na kujiaminisha kwa Mungu, kwa kuchangia kwa hali na mali! Inawezekana.

Na Padre Alfred Stanslaus Kwene, -Kahama, Tanzania.

Katika homilia yake, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, alianza kwa kuelezea upekee wa siku hiyo, kwa kutanabahisha kuwa ilikuwa ni siku ya furaha, shangwe na shukrani kwa Mungu kwa baraka kuu aliyolijalia Kanisa la Tanzania kwa kuweza kufungua Seminari Kuu mpya ya Nazareth – Mwendakulima. Huku akifanya rejea katika masomo ya siku hiyo, alisisitiza kuwa Somo la Kwanza na Injili ya siku hiyo kuwa yanadhihirisha hali ya hofu na wasiwasi inayomkumba nabii hivi kwamba anajiona hawezi kutekeleza kazi aliyopewa kwa hoja kuwa yeye ni mtoto. Lakini Mwenyezi Mungu anamuimarisha kwa neno hili: Tazama niko pamoja nawe nikuokoe! Alikaza kusema kuwa neno hilo la hofu na mashaka tunalikuta tena katika Injili Takatifu ya siku hiyo, pale ambapo wafuasi wa Bwana wanakwenda Galilaya kwenye mlima ule ambao Yesu alikuwa amewaagiza na anajitokeza kwao. Katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu, Mwinjili anakariri kuwa baadhi yao (wafuasi) walitia shaka. Japo, Mwinjili haweki wazi ni nini ilikuwa sababu ya mashaka yao, lakini kila mmoja wetu ndani ya moyo wake angeweza kuifikiria sababu hiyo, yaani, huyu anayejitokeza kwetu – Yesu – mbona alikubali akauawa? Mbona alifanya makubwa lakini mwishowe akafa? Anaonekana mbele yetu, kweli ni yeye?  Kwa maneno mengine, wanachokuwa na mashaka nacho ni juu ya uwepo wa Yesu kati yao.  

Katika mazingira hayo ya hofu na mashaka, Bwana wetu Yesu Kristo aliwaimarisha kwa maneno yaleyale ambayo Mungu alimwimarisha nabii katika Agano la Kale: Nendeni ulimwenguni mwote, lakini kumbukeni kuwa niko pamoja nanyi siku zote hadi ukamilifu wa dahari. Kardinali Pengo aliendelea kusisitiza kuwa maneno haya ya faraja/matumaini toka Kwa Yesu nasi tunayahitaji sana katika siku ya leo (ya uzinduzi). Tunapaswa kuwa na uthabiti wa Imani kwamba katika tendo hili la kuanzishwa Seminari Kuu, Mungu yuko pamoja nasi. Hili ni neno muhimu ambalo tunatakiwa tulijenge mioyoni mwa kila yule anayehusika – kuanzia maaskofu walioamua kuanzisha tendo hili. Aliwaalika Maaskofu wakumbuke kuwa uzinduzi wa Seminari hiyo sio tendo lao, bali la Mungu; Mungu yuko pamoja nao. Kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa kwanza wa Yesu, nasi twaweza kugubikwa na hofu, hali ambayo huenda inawakumba hata baadhi ya maaskofu. Hivyo, lazima kumtegemea Mungu. Tofauti na Mitume wa Kwanza, alitualika tujifunze kutazama na kuwa na mwelekeo chanya (positive) katika maisha yetu. Msingi wa hofu na mashaka yao (Mitume) ilikuwa ni katika kumwona Kristo anajiachia ateswe na afe Msalabani hivi kwamba ilikuwa vigumu kuamini kuwa kafufuka, yu hai.

Mitume walitia shaka kwa sababu walitazama katika upande wa mateso na kifo cha Kristo. Magumu aliyopitia Bwana Yesu Kristo ndiyo waliyoyakazia macho hivi kwamba wakashindwa kuamini kile ambacho wanakiona. Huyu alizikwa baada ya kuteswa na kuuawa, ubavu wake ukachomwa kwa mkuki, awezaje kuwa hai tena? Walielekeza macho yao katika upande ule tunaoweza kuuita NEGATIVE – mapungufu, magumu, n.k na hivi wakawa na sababu ya kutia shaka! Huku akirejea katika historia, Kardinali Pengo alishirikisha furaha yake kubwa ya kupewa fursa na Maakofu na kuwa Kiongozi wa Ibada hiyo ya Misa ya Ufunguzi wa Seminari Kuu ya Nazareth. Aidha, alidokeza ni nini hasa iliamini ilikuwa sababu ya Maaskofu kumwalika yeye kwa nafasi hiyo. Kwa kutambua kuwa hakutegemewa aalikwe kwa ajili ya kutoa fedha (ambazo hata hivyo inajulikana kuwa hana), pamoja na kuwa yaweza kuwapo sababu nyingine asiyoijua yeye; ila aliamini kabisa mwaliko huu ulikuwa na msingi wake katika historia. Imani yake ilimtuma kufikiri kuwa katika ufunguzi wa Seminari ya Nazareth, mawazo ya Maaskofu yalienda katika ufunguzi wa Seminari Kuu nyingine katika miaka ile ya ’70 mwishoni, wakati ule Maaskofu walipoamua kuanzisha Seminari Kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga – Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Hiyo ndiyo ilikuwa ya mwisho kujengwa hadi sasa. Maaskofu wakafikiri kuwa, kama kulikuwa na mtu aliyekuwa anashika nafasi ya kueleweka wakati huo, pasipo kujali angefika kusema nini, basi ni vema akawepo hapa kwa ajili ya kutoa ushuhuda kuwa – kama iliwezekana wakati ule, kwanini isiwezekane sasa.

Kwa namna ya pekee, Kardinali Pengo alikazia kuwa huo ndio ambao angependa upokeleke kuwa ujumbe wake msingi (neno lake) kwa siku hiyo, yaani ushuhuda kuwa: kama iliwezekana wakati ule wa kuanzisha Seminari Kuu ya Segerea, kwanini isiwezekane sasa? Miaka ile inaanzishwa Seminari Kuu ya Segerea kilikuwa ni kipindi chenye changamoto nyingi, kama vile: uwepo wa vita vya Tanzania na Uganda – vilivyofanya nguvu nyingi za taifa kuelekezwa huko; ukosefu wa mahitaji msingi ya kibinadamu mintarafu chumvi hata mikate; ubovu wa miundombinu ya barabara ambayo wakati mwingine ilisababisha kukosekana kwa mawasiliano kati ya Seminari na Askofu wa Jimbo; kupungua kwa misaada toka kwa wahisani – kwani wakati huo majimbo yote isipokuwa moja pekee yalikuwa chini ya maaskofu wazawa ambao iliwapasa kuhangaika ili kuyategemeza majimbo yao na Seminari Kuu mpya pia. Bado hata katika mazingira hayo Seminari iliweza kuanzishwa tu.  Ni dhahiri kuwa katika mazingira kama hayo kusema inaanzishwa Seminari Kuu mpya halikuwa jambo rahisi. Ilihitaji ujasiri mkubwa wa maaskofu.

Kardinali Pengo aliwakumbusha Maaskofu ya kuwa, kama iliwezekana wakati ule pamoja na magumu yote yaliyokuwepo, kwa nini leo tushindwe kuanzisha Seminari ya Nazareth jimboni Kahama? La muhimu, kama vile ilivyokuwa kwa Seminari ya Segerea, neno kuu ni kujiweka mikononi mwa Mungu – kutambua kuwa hii shughuli sio ya mtu binafsi, bali yake Mwenyezi ambaye yuko pamoja nasi hadi utimilifu wa dahari. Imani hii lazima ieleweke katika matendo ya kila siku. Vile ilivyokuwa kwa Maaskofu wa wakati ule, kwamba waliguswa na mahitaji ya seminari (concerned), vivyo hivyo na leo hii kwa Seminari ya Nazareth. Alikaza kusema kuwa, ni wazi haitakuwa sawa maaskofu wakawa wanafanya vitu vingine na huku vijana wetu wanakosa hata chunvi kwa ajili ya chakula chao cha kila siku, na wao (Maaskofu) wakawa wanaendelea na miradi mingine ambayo haina uhusiano na uinjilishaji. Haiwezekani tukahalalisha kitendo kama hicho. Alisisitiza kuwa: “Kama tumeamua kuanzisha seminari hii, inabidi sisi wenyewe tudhihirishe kwamba tunaamini ni uamuzi wake Mwenyezi na kwa sababu ni wake, sisi hatuna kingine isipokuwa kuweka nguvu zetu na mioiyo yetu katika shughuli hii”.

Aidha, Kardinali Polycarp Pengo aliendelea kuhimiza kuwa, kwa sababu kazi hii ni ya Mungu, neno la kwanza na la muhimu kabisa ni SALA. Mwenyezi Mungu haongei na binadamu kwa maneno ya blabla au kwa mikutano. Mwenyezi Mungu anaongea na sisi kwa njia ya SALA. Neno la kwanza kwa kila yule anayehusika na Seminari ya Nazareth ni kupiga magoti mbele ya Mwenyezi, tukikiri kuwa yuko pamoja nasi na kumwomba afanikishe shughuli hii ambayo imeanza kwa jina lake. Kundi la kwanza katika kutimiza wajibu huu wa kusali ni maaskofu. Japo wataombwa michango na vitu vingine, cha muhimu zaidi ni roho ya SALA. Vile Vile aliwageukia waamini kokote waliko nchini Tanzania na kuwakumbusha kuwa, watazidi kuombwa misaada na huu hautakuwa mwisho, kwani kama ambavyo kila aliyehuduria siku hiyo alivyoshuhudia, huu ni mwanzo tu. Kwa yeyote yule anayezifahamu seminari kuu zingine, mfano Segerea, wanapoiona hii ya Nazareth wanatambua kuwa huu ni mwanzo tu. Ni dhahiri kuwa waamini watazidi kuombwa, wasisite kutoa kwa moyo, lakini wazingatie kwanza SALA - tukimshukuru Mungu kwa zawadi hii ya yeye kuwa pamoja nasi hadi ukamilifu wa dahari hata katika miradi kama hii. Sote tunahitaji kudhihirisha kwamba Mungu yuko pamoja nasi na kwamba shughuli hii ni ya Mwenyezi. Tutoe michango – sawa, ushauri – sawa, lakini tusisahau kuyafanya yote ndani ya sala pamoja na Mwenyezi.

Mwishoni Kardinali Polycarp Pengo, alihitimisha tafakari yake kwa kuiombea tena baraka ya Mungu Seminari Kuu Mpya na kila yule atakayehusika katika kuifanya ikue na kustawi. Alimwomba Mwanyezi Mungu aendelee kuibariki seminari yetu, asikilize dua na sala zetu, Mwenyezi Mungu ailainishe mioyo yetu na kuielekeza kwake. Alituasa tusiwe kama Petro alipokuwa anatembea juu ya maji, badala ya kukaza macho kwa Yesu alitazama pembeni, na hatimaye akaanza kuzama. Alisisitiza: “Na sisi wapendwa, tukianza kuhesabu magumu na shida tutazama. Lakini tukumbuke kuwa Yeye daima yuko pamoja nasi, hata katika dhoruba tukaze macho yetu kwa Yesu aliyemo hata ndani ya dhoruba na kwa njia hiyo tutaweza kufanikisha mambo mazuri tunayokusudia kuhusu seminari yetu”. Pamoja na kuhimiza juu ya kumtegemea Mungu, aliwashukuru tena Maaskofu kwa wazo lao na kwa moyo wao wa kuwa tayari ili kufanikisha shughuli hii. Aliwaombea akisema: “Mwanyezi awabariki ninyi na shughuli zote mnazozifanya kwa ajili ya Kanisa la Tanzania”. TUMSIFU YESU KRISTO.

14 December 2020, 11:13