Ujumbe wa Patriaki Bartholomeo wa kwanza kwa Noeli ya Mwaka 2020 unakazia utu, heshima na haki msingi za binadamu hasa wakati huu wa maambukizi makubwa ya ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Ujumbe wa Patriaki Bartholomeo wa kwanza kwa Noeli ya Mwaka 2020 unakazia utu, heshima na haki msingi za binadamu hasa wakati huu wa maambukizi makubwa ya ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. 

Patriaki Bartolomeo wa Kwanza: Ujumbe wa Noeli Kwa Mwaka 2020

Noeli ni Sherehe ya Fumbo la Umwilisho, changamoto na mwaliko kwa waamini kutambua na kuthamini tukio hili la kihistoria katika maisha yao ya kiroho. Fumbo la Umwilisho ni ufunuo wa historia, lengo na maana ya maisha ya binadamu, kadiri ya mpango wa Mungu. Huyu ni binadamu mwenye utu, heshima na haki zake msingi. Watu wote wamekombolewa kwa njia ya Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Bikira Maria alijiandaaa kikamilifu kumzaa Neno wa Mungu, akamtafakari alipozaliwa pale mjini Bethlehemu, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu wote. Maadhimisho ya Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2020 ni tofauti sana na Noeli za miaka mingine iliyopita. Hii inatokana na maambukizi makubwa ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Liturujia na Ibada Takatifu zimeguswa na kutikiswa sana na Virusi vya Corona, COVID-19. Jambo la msingi ni imani thabiti kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Kwa bahati mbaya sana, Maadhimisho ya Sherehe za Noeli, yamepoteza dira na mwelekeo wake wa kiimani na kugeuzwa kuwa ni kipindi cha ulaji wa kupindukia. Noeli ni Sherehe ya Fumbo la Umwilisho, changamoto na mwaliko kwa waamini kutambua na kuthamini tukio hili la kihistoria katika maisha yao ya kiroho. Fumbo la Umwilisho ni ufunuo wa historia, lengo na maana ya maisha ya binadamu, kadiri ya mpango wa Mungu. Huyu ni binadamu mwenye utu, heshima na haki zake msingi. Watu wote wamekombolewa kwa njia ya Kristo Yesu na kwamba, mbele ya Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, watu wote ni sawa. Hii ni kanuni msingi katika maadili na kwamba, maisha ya mwanadamu ni matakatifu kwa sababu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Sherehe ya Noeli ni ushuhuda wa Umungu na Ubinadamu wa Yesu ambaye aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kama ilivyoandikwa. Atarudi tena kuwahukumu wazima na wafu. Yesu ni hakimu mwenye haki na Mfalme wa utukufu. Waamini wanamtukuza Mwenyezi Mungu aliyejifunua kwa vinywa vya Manabii. Leo hii, Kanisa linamtangaza na kumshuhudia kwa watu wa Mataifa. Mwili wa Bikira Maria ukawa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno aliyefanyika mwili. Katika Sherehe za Noeli, Makanisa yamepambwa sana kuonesha Umungu na Ubinadamu wa Kristo. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2020 uliotolewa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol. Pamoja na madhara makubwa yanayoendelea kusababishwa na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVId-19, bado Malaika wanaendelea kuimba na kutangaza Habari Njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote, maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi ndiye Kristo Bwana.

Maadhimisho ya Sherehe za Noeli iwe ni fursa ya kusali na kuwaombea wale wote ambao wako hatarini, wameambukizwa au kufariki dunia kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Mama Kanisa anawashukuru na kuwapongeza wafanyakazi katika sekta ya afya, wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, wagonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-18 wataweza kuhudumiwa kwa kuzingatia utu, heshima na haki zao msingi. Wala idadi kubwa ya wagonjwa kisiwe ni kisingizio na sababu ya kuvunja kanuni msingi za kimaadili na utu wema. Wafanyakazi katika sekta ya afaya wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao wagonjwa. Wajisadake bila kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya ndugu zao wagonjwa. Wakleri wajitahidi na wao kutoa huduma za maisha ya kiroho kwa wagonjwa na waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19, kama kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Ugonjwa Corona, COVID-19 umegusa na kutikisa misingi ya imani, matumaini na mapendo. Mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu yamelegea sana. Hili ni janga linalopaswa kuisaidia Jumuiya ya Kimataifa kuungana na kushikamana, ili kupata suluhu ya kudumu. Majitoleo ya Msamaria mwema yawe ni mfano unaovuka mipaka ya kibinadamu. Mama Kanisa ataendelea kutoa huduma ya kiroho kwa wagonjwa na waathirika wote wa Virusi vya Corona, COVID-19, daima wakiwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Kristo Yesu, mganga mkuu wa maisha ya binadamu, ili aweze kuwaokoa na wale wanaofariki dunia, awajalie maisha ya uzima wa milele. Kwa bahati mbaya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa Mwaka 2020 haikuweza kutekelezwa barabara kwani mwaka 2020 ulikuwa umetangazwa kuwa ni Mwaka wa Vijana wa Kanisa la Kiorthodox ili kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Vijana wa kizazi kipya wanazo ndoto zao, mawazo na malengo, lakini pia wanayo maswali mazito kuhusu maana ya maisha na matumaini yanayosimikwa katika umoja na udugu wa kibinadamu.

Mama Kanisa anapenda kuwatangazia na kuwaomba vijana kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa ulimwengu mpya unaosimikwa katika misingi ya haki, amani na upendo. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol anahitimisha ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2020, akiwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu, kwa sababu Yeye ndiye chanzo na hatima ya maisha ya mwanadamu. Mengine yote yatakuja na kutoweka. Mwenyezi Mungu anaheshimu na kuthamini uhuru wa binadamu na kwamba, kila mtu anao wajibu wa kushiriki kikamilifu katika Fumbo la Wokovu. Ukweli katika uhuru katika Kristo Yesu umejaribiwa juu ya Msalaba na hii ndiyo njia inayoelekea kwenye Fumbo la Ufufuko. Anawaombea afya njema, upendo wa dhati, ustawi na maendeleo ya kweli wakati huu wa Noeli na kwa Mwaka Mpya wa 2021.

Ujumbe wa Noeli 2020
24 December 2020, 15:25