Domenika ya Nne ya kipindi cha Majilio Domenika ya Nne ya kipindi cha Majilio 

Neno la Mungu Domenika ya nne ya majilio mwaka B:Noeli imekaribia!

Noeli imekaribia.Kanisa linatualika kufanya maandalizi ili tumpokee Mwokozi katika maisha yetu,katika jumuiya zetu,katika familia zetu na zaidi sana katika nafsi ya kila mmoja wetu ili atujaze furaha na amani ya kweli. Tunaalikwa tukampokee kama Bikira Maria alivyompokea.Kwa unyofu tukitambua unyonge na utupu wetu,tujibidishe kutafuta mpango wa Mungu maishani mwetu na daima tutambue kwamba mpango wa Mungu ni mpango wa Upendo.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, Domenika ya nne ya majilio mwaka B wa Kanisa. Hii ni Domenika ya mwisho katika kipindi cha majilio. Kumbe kipindi cha majilio kiko ukingoni na Noeli imekaribia kama wimbo wa mwanzo toka kitabu cha Nabii Isaya unavyoimba: Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, mawingu na yammwage mwenye haki; nchi ifunuke, na kumtoa Mwokozi. Masomo ya Domenika hii yanatukumbusha jinsi mpango wa ukombozi wa mwanadamu ulivyoanza na kutilika kwake. Mungu alitangaza mpango wa kumkomboa mwanadamu mara tu alipoanguka dhambini kwa kumlaani Ibilisi akisema; “Kwa sababu umefanya hivyo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote na hayawani wa mwituni. Kwa tumbo utakwenda na kula mavumbi siku zote za maisha yako. Kisha Mungu akatangaza mpango wake wa kumkomboa mwanandamu kutoka ktika hila za shetani akisema: Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke na kati ya uzao wako na uzao wake, huo utakuponda kichwa na wewe utamgonga kisigino Haya tunayasoma katika kitabu cha Mwanzo 3:14-15. Maneno haya ya Mungu yamebeba ahadi ya Mkombozi atakayeishinda dhambi.

Somo la kwanza kutoka la kitabu cha pili cha Samweli ni mwendelezo wa ahadi ya Mungu ya kumleta mkombozi kwa njia ya uzao wa mwanamke. Somo hili linatusimulia mpango wa mfalme Daudi kutaka kumjengea Mungu nyumba. Mungu anakataa na badala yake anaahidi yeye mwenyewe kumjengea Daudi nyumba. Historia inasimulia kuwa Mungu alimteua Daudi kuwa Mfalme mahali pa Saul na kumuahidi kuwa ufalme wake hautakuwa na mwisho. Katika utawala wake, mfalme Daudi aliifanya Yerusalemu makao yake makuu [2Sam 2:1-4; 5:5-10; 1Sam 16:1-13], akalichukua na kulipeleka Sanduku la Agano walilopewa wana wa Israeli na Mungu kama alama ya uwepo wake Mungu, alama ya mshikamano wa waisraeli na Mungu, alama ya utii wao kwa Mungu. Sanduku hili lilikaa katika nyumba ya mapazi kama anavyosema Daudi mwenyewe; Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.  Hivyo Daudi akataka kujenga Hekalu ili kulihifadhi lile Sanduku la Agano. Nabii Nathani aliyekuwa Mshauri wake Daudi, alimtia moyo aendelee kulijenga Hekalu, lakini Mungu anamtokea Nathani na kumtuma kwa Daudi amwambie kuwa; Bwana anakuambia ya kwamba Bwana atakujengea nyumba. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele. Huu ni utabiri wa utawala wa Yesu atakayezaliwa na Bikira Maria kama tunasikia katika Injili.

Baada ya kifo cha Daudi, mwanae Solomoni alichukua utawala, akajenga hekalu zuri sana. Hiki kilikuwa kipindi cha utukufu kwa Israeli. Baada ya kifo chake wana wa Israeli walikengeuka wakaziacha njia za Bwana. Hii ikawa sababu ya kubomolewa kwa hekalu lao, kuangamizwa kwa mji wa Yerusalemu na wao kupelekwa uhamishoni Babeli. Na hata waliporudi kutoka uhamishoni bado hawakuwa na uhuru wa kisiasa maana waliendelewa kutawaliwa na dola zingine na hivyo wakaanza kujiuliza: “Je, Mungu ametuhadaa ya kwamba ufalme wa Daudi hautakuwa na mwisho.” Lakini Mungu hakawii kuitimiza ahadi yake. Mda ulipotimia akamtuma mwanae aliyezaliwa na Bikira Maria na hivyo ahadi ya Mungu kulijenga Hekalu litakalodumu milele inatimia katika yeye kwa kulisimika kanisa, ndilo hekalu lake takatifu na la milele.

Mtume Paulo katika somo la pili la waraka wake kwa Warumi anawaasa warumi wamshukuru Mungu kwa kuwaletea Mkombozi, Bwana wetu Yesu Kristo. Mtume Paulo anawaandikia Warumi na sisi pia kuwa lazima tuwe watu wenye shukrani kwa Mungu kwa kutuletea mkombozi aliyetutoa utumwani mwa shetani. Shukrani pekee ambayo tunaweza kumpa Mungu ni kutii amri zake kwa moyo wote tukijua kuwa ni yeye peke yake ndiye atupaye mahitaji yetu yote ya kiroho na kimwili.

Injili kama ilivyoandikwa na Luka inasimulia kutimia kwa ahadi ya Mungu kwa Daudi katika Yesu Kristo kwa kutupa simulizi la kuzaliwa kwake akianza na Yesu mwenyewe kupitia Daudi, akienda mpaka Abrahamu mpaka kufikia Adam ili kutuonesha kwamba Yesu ni mwana familia wa ukoo wa wanadamu wote. Kwamba Yesu anatoka kwa Adamu kama sisi tulivyo ni uzao wa Adamu lakini bila doa lolote la dhambi. Mungu anaikamilisha ahadi aliyotoa kwa Daudi kwa namna ya ajabu na isiyotegemewa kwa kumchagua msichana, Bikira Maria wa Nazareth, asiyejulikana na watu na hivyo anamuandaa ili awe mama wa Mkombozi, mama wa Mungu. Mungu anajishusha hata kumtaka shauri mwanadamu, Bikira Maria, awe mama wa Mkombozi. Ni unyenyekevu wa hali ya juu sana. Bikira Maria naye kwa unyenyekevu anasema; Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema. Tunaposoma majadiliano baina ya Bikira Maria na Malaika Gabrieli, tunaonja upole, unyofu na unyenyekevu wake, utakatifu na hekima yake. Malaika alipomsalimia; “Salamu Maria, umejaa neema, Bwana yu nawe, Bikira Maria alishangaa na kuogopa na kuhoji; salamu hii ni ya namna gani? Malaika anamwambia usiogope. Utachukua mimba na kumzaa mtoto mwanaume, utamwita jina lake Yesu maana ndiye atakaye wakomboa watu wake kutoka utumwa wa dhambi. Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake na ufalme wake hautakuwa na mwisho (Lk 1:31-33). Maria anatafuta uthibitisho wa maneno haya: “Litakuwaje neno hilo kwa maana simjui mume” (Lk 1:34). Malaika anamwondoa wasiwasi; “Roho wa Bwana atakushukia na nguvu za aliye juu zitakufunika kama kivuli kwani kitakachozaliwa ni kitakatifu, Mwana wa Mungu” (Lk 1:35).

Tukisoma kitabu cha Kutoka 40:34, tunaona jinsi Utukufu wa Bwana ulivyoijaza na kulifunika lile hema ambalo sanduku la Agano lilihifadhiwa, jambo lililojirudia hata baada ya Solomoni kujenga Hekalu la Yerusalem (1Wafal 6:10, 13). Hivyo maneno ya malaika Gabrieli kwa Bikira Maria kuwa Roho wa Bwana atamshukia kama kivuli toka juu ni uthibitisho kuwa Mungu ndiye takaye fanya haya yote ndani ya Bikira Maria ambapo Masiha atachukua mwili na damu kwake Bikira Maria. Kwa miezi 9 masiha ataishi ndani yake, hivyo mwili wake Bikira Maria unakuwa Hekalu takatifu na makao ya Mungu. Kumbe Bikira Maria anakuwa sanduku la agano, makao mapya ya Mungu kati ya watu. Bikira Maria anapokea mpango wa Mungu kwa moyo wote, akajitoa bila kujibakiza akisema: “Tazama mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe kadiri ulivyonena” (Lk 1:38). Luka anatumia maneno; Mimi ni Mtumwa na wala siyo Mimi ni Mtumishi. Mtumwa hakuwa na haki mbele ya Bwana wake. Maria anajihesabu kuwa Mtumwa mbele  ya Mungu. Ukweli juu ya mwana wa Mungu kuwa mtu ni fumbo. Akili zetu haziwezi kuelewa. Imani tu yaelewa. Mtume Paulo katika somo la pili la waraka wake kwa warumi anasema kuwa; Kristo kujimwilisha, kuwa mwana familia ya kibinadamu, mwana wa Adamu na mwana wa Mungu; mambo haya yote ni fumbo la upendo na fumbo la imani nasi hatuna budi kumshukuru Mungu kwa upendo wake kwetu sisi wanadamu.

Noeli imekaribia. Kanisa linatualika kufanya maandalizi ili tumpokee Mwokozi katika maisha yetu, katika jumuiya zetu, katika familia zetu na zaidi sana katika nafsi ya kila mmoja wetu ili atujaze furaha na amani ya kweli. Tunaalikwa tukampokee kama Bikira Maria alivyompokea. Kwa unyofu tukitambua unyonge na utupu wetu, tujibidishe kutafuta mpango wa Mungu maishani mwetu, na daima tutambue kwamba mpango wa Mungu ni mpango wa Upendo. Tuupokee mpango huo kwa furaha na kwa moyo wote pasipo kujibakiza. Mungu amekuwa akiendelea kumkomboa mwanadamu. Katika Noeli hii, Mungu anataka kuharakisha kazi hii ya ukombozi. Tumruhusu atande kazi hii mioyoni mwetu.

TAFAKARI NENO LA MUNGU JUMAPILI IV YA MAJILIO

 

18 December 2020, 15:14