Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 30 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa! Upendo kwa Mungu na jirani ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 30 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa! Upendo kwa Mungu na jirani ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu. 

Tafakari Jumapili 30 Mwaka A: Upendo Kwa Mungu Na Jirani!

Amri kuu ya Upendo: Sikiliza Ee Israeli; Bwana Mungu wako ni Mungu mmoja; Nawe Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote. Kisha Yesu anaongeza sehemu muhimu katika amri hiyo; mpende jirani yako kama nafsi yako (Wal 19:18). Akamalizia akisema; Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii. Mungu na Jirani!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 30 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Tunapokaribia mwisho wa mwaka wa kiliturujia wa Kanisa, Mama Kanisa anatukumbusha namna tunavyopaswa kuishi hapa duniani ili tuweze kuwa warithi wa uzima wa milele, na namna iliyo njema ni kumpenda Mungu na jirani. Somo la kwanza kutoka kitabu cha kutoka ni sehemu ya mkusanyo wa sheria zinazoeleza namna ya kuishi maisha yampendezayo Mungu, naye Mungu anasema: usimwonee mgeni, wala kumtendea jeuri, usimtese mjane aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima. Ukiwatesa watu hao nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake zenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima. Ukimkopesha mtu aliye maskini, usiwe kwake mfano wa mwenye kumdai; wala hutamwandikia faida. Ikiwa wewe kwa njia yoyote wapokea nguo ya jirani yako rehani, lazima utamrudishia mbele ya jua kuchwa; maana hiyo nguo ni kifuniko chake, hiyo peke yake ni nguo ya ngozi yake; je atalalia nini? Itakuwa hapo atakaponililia mimi, nitasikia; kwa kuwa mimi ni mwenye rehema.

Ijapokuwa sheria ya Musa ilikataza kuchukua riba katika mali waliyowakopesha ndugu zao, lakini bado wapo waliowatoza riba ndugu zao. Watu maskini walinyonywa haki zao, wajane walinyang’anywa urithi wao, na yatima waliuzwa na kuwa watumwa ndiyo maana Nehemia baadae anaeleza uhalisia huu akisema; Ndipo kukatokea kilio kikuu cha watu, na wake zao juu ya ndugu zao Wayahudi. Maana walikuwako watu waliosema: Sisi na wana zetu na binti zetu, tu wengi, na tupate ngano, tukale tukaishi. Tena walikuwako wengine waliosema: Tumeweka rehani mashamba yetu na mizazibu yetu na nyumba zetu tupate ngano kwa sababu ya njaa. Tena walikuwako wengine waliosema, tumekopa fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa kuweka rehani mashamba yetu na mizabibu yetu. Lakini miili yetu ni kama miili ya ndugu zetu, na watoto wetu kama watoto wao; kumbe tunawatia utumwani wana wetu na binti zetu kwa utumishi na baadhi zetu wamekwisha kutiwa utumwani, wala hatuwezi kujiepusha na hayo, maana watu wengi wana mashamba yetu na mizabibu yetu (Neh 5:1-5). Nasi tujiulize mioyoni mwetu, uovu huu katika jamii zetu, jumuiya zetu na familia zetu haupo? Je? Sisi nasi hatushiriki katika uovu huu? Basi, tunaonywa tusishiriki katika uovu huu, ili hasira ya Mungu isijewaka juu yetu.

Katika somo la pili la Waraka wake wa kwanza kwa Wathesalonike, Mtume Paulo anaeleza jinsi Wathesalonike walivyoipokea Injili kwa furaha licha ya upinzani mwingi hata wakapata sifa sehemu zote za Ugiriki. Mtume Paulo anasema kuwa wao wamekuwa kielelezo kwa watu wote waaminio. Maana kutoka kwao neno la Mungu limevuma, si katika Makedonia na Akaya tu, ila na kila mahali ambapo imani yao waliyonayo kwa Mungu imeenea. Mtume Paulo anashuhudia kuwa Wathesalonike walipomwongokea Mungu, waliziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai, na wa kweli wakiingojea hukumu ya mwisho. Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa kwa kila mbatizwa, kumwongokea Mungu na kusubiri kwa matumaini hukumu ya mwisho kwa furaha. Injili ilivyoandikwa na Mathayo inasimulia jinsi Mafarisayo walivyofanya shauri pamoja na kupanga kumuangamiza Yesu kwa kumuuliza swali la mtego kuhusu amri iliyo kuu katika torati ili wapate mashitaka juu yake. Tukumbuke, kuwa Mafarisayo walifundisha kuwa sheria zote 613 za Agano la kale zilizoziwekwa zina nguvu sawa kwani zote zimetolewa na Mungu. Ni wazi kuwa Mungu kupitia Musa aliwapa Waisraeli Amri 10 lakini hadi ujio wa Kristo Viongozi wa Dini walishaongeza amri hizo kufikia 613, ambapo amri 248 zinalihimiza wanayopaswa kufanya wana wa Israeli na amri 365 zilitoa makatazo ya mambo ambayo hawapaswi kuyafanya. Kwa hali hii wanasheria walifanya maisha kuwa magumu kwa watu wa kawaida. Ndiyo maana Yesu katika injili ya Mathayo 23:4 anasema; wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani, wasitake wenyewe kuigusa hata kwa ncha ya kidole chao.

Yesu anatoa jibu kwa swali lao kuwa kumpenda Mungu, na jirani ni msingi wa amri zote, tena amri zote hazina maana pasipo upendo.  Yesu anachukua amri hizi zote 613 na kuzifanya kuwa moja kwa kuziunganisha katika amri ya kumpenda Mungu na jirani. Sehemu ya kwanza ya jibu la Yesu ni sehemu ya sala ya Wayahudi na ilikuwa ni sehemu ya kukiri imani kwao iliyojulikana kama shema; Sikiliza Ee Israeli. Watoto walifundishwa sala hii na kuisali mara mbili kwa siku wakiibeba kifuani pao kama scapulari na ilionekana kuwa kinga kwa walioivaa. Yesu ananukuu mstari wa kwanza wa sala hii unaosema; sikiliza Ee Israeli; Bwana Mungu wako ni Mungu mmoja; Nawe Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote. Kisha Yesu anaongeza sehemu muhimu katika amri hiyo; mpende jirani yako kama nafsi yako (Wal 19:18). Akamalizia akisema; Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii. Kwa kuwa Wayahudi walifikiri jirani yao ni Myahudi swali lililofuata lilikuwa na jirani yangu ni nani? Ndipo hapo Kristo alipofundisha kuwa jirani yako ni mtu yeyote yule mhitaji kwa kutoa mfano wa msamaria mwema.

Kumbe, kumpenda Mungu na jirani ni amri zilizo sawa kabisa. Hakuna anayeweza kumpenda Mungu kama hampendi jirani yake na ukimpenda Mungu na Jirani, umekamilisha Maandiko, na kwa kufanya hivyo unakamilisha yote aliyoamuru Mungu katika ukamilifu wake, na unakuwa na uhakika wa kuingia katika Ufalme wake na kushiriki uzima wa Milele. Tutambue kuwa kumpenda jirani ni njia nyingine ya kumpenda Mungu. Amri hizi mbili ni nguzo na msingi wa sheria zote. Ukivunja moja ya amri hizi mbili umevunja zote. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii yaani maandiko yote matakatifu. Ampendaye Mungu na jirani, rohoni ametulia na ana uhakika wa uzima wa milele. Mwishoni mwa maisha yake hapa duniani, Yesu aliwaalika wafuasi wake kuweka maisha yao katika kiini cha upendo kwa Mungu na jirani. Tena akasema hii ni amri mpya, na akafupisha mafundisho yake akisema, pendaneni kama nilivyowapenda ninyi Yn 13:34, akasisitiza mkipendana watu watawatambua kuwa mu-wanafunzi wangu. Kumbe, upendo ni kitambulisho cha ufuasi wetu kwa Kristo. Mtume Paulo aliielewa vizuri amri hii ndiyo maana anainukuu katika barua yake kwa warumi akisema; ikiwapo amri nyingine yoyote, inajumlishwa katika neno hili; mpende jirani yako kama nafsi yako (Rum 13:9) na katika barua yake kwa Wakorinto anaorodhesha sifa za upendo 1 Kor.13:1-7).

Tukumbuke kuwa dini iliyo safi mbele ya Mungu Baba ni hii; kuwatazama yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda na dunia pasipo mawaa (Yak 1:27). Haya ni makundi dhaifu yasiyo na usalama. Kilio chao chasikika mbele ya Mungu kama alivyosema katika somo la kwanza kuwa atawatetea maskini na mafukara, atawashusha watesi katika hali ya utumwa kama wale wanaowatesa. Sisi nasi tunaelewa kinachotokea kwa wajane na yatima leo; wananyanyaswa, wananyang’anywa urithi wa wazazi zao, wanaishi maisha ya dhiki na utumwa. Maskini hana mtetezi ila Mungu. Tumeonywa kuwa tukiwatesa watu hao katika neno lolote; Mungu atasikia kilio chao, hasira yake itawaka moto atawaua kwa upanga wake watesi hao ili nao wawe wajane na watoto wao wawe mayatima, na matajiri maskini. Basi tufuate wosia wa Tobiti akisema; Wenye njaa uwape baadhi ya chakula chako, walio uchi uwape baadhi ya nguo zako. Sawa sawa na wingi wako utoe sadaka. Utoapo sadaka jicho lako lisiwe na choyo (Tob 4:16 ff). Huu ndio upendo tunaopaswa kuwanao kwa ndugu zetu ambao ndio kupimo cha maisha yetu ya ukristo na cha hukumu ya mwisho.

Jumapili 30 ya Mwaka A
21 October 2020, 12:05