Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XXIII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa katika mchakato mzima wa msamaha na upatanisho wa kidugu! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XXIII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa katika mchakato mzima wa msamaha na upatanisho wa kidugu!  (ANSA)

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XXIII: Hatua za Upatanisho!

Mama Kanisa katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXIII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa, anaweka mbele ya macho ya waamini umuhumu wa kutubu na kumwongokea Mungu sanjari na kujipatanisha na jirani. Injili inaonesha kwa namna ya pekee kabisa hatua mbalimbali zinazopaswa kuchukuliwa ili mwamini aweze kupata msamaha na upatanisho wa kweli na wa kidugu!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Ili tuweze kupata vema ujumbe kusudiwa utokanao na somo la Injili ya Dominika ya leo, ni vema kuangalia tangu mwanzoni muktadha wake. Sehemu hii ya Injili kutoka sura ile 18 ya Mwinjili Mathayo, sura nzima ya 18 inazungumzia juu ya mahusiano kati ya waamini wa jumuiya (ekklesia) ya Wakristo: Juu ya nani aliye mkubwa, kuepuka kukwaza walio wadogo au wengine, mfano wa kondoo aliyepotea ndio kusema jinsi ya kumrejesha mmoja anayepotea au kuwa mbali na imani na Kanisa, kusahihishana kwa mapendo ya kidugu, na kuwa watu wa msamaha kwani nasi tunasamehewa madeni makubwa ya dhambi na makosa yetu. Ni sura inayotoa maelekezo ya nini kifanyike ili kulinda upendo na umoja wa jumuiya ya waamini yaani Kanisa (ekklesia). Na ndio hapo tunaona sehemu ya Injili ya leo inatoa nafasi ya kuona jinsi ya kuenenda hasa pale mmoja wetu anapokosea, anapopotoka na kuenenda kinyume na Injili, kinyume na mapenzi ya Mungu, kinyume na Kanisa. Lengo kuu daima ni kumrejesha kwa upendo, ni kumpata tena ndugu yetu kwa kumtoa katika utamaduni wa kifo na kumrejesha kwenye maisha ya uzima wa kweli, maisha ya muunganiko na Mungu na jumuiya ya wanakanisa(ekklesia). Masahihisho lazima yawe na lengo la kumpata tena, na hivyo daima lazima yasukumwe kwa upendo na kamwe isiwe nafasi ya kumshusha au kumdhalilisha mwingine, kwani huko ni sawa na kumuua na kumpoteza zaidi mwingine.

Naomba pia niweke wazi tangu mwanzo kuwa katika tafsiri yetu ya Kiswahili imetumia maneno ambayo hayapo katika tafsiri nyingi za zamani. ‘’Ndugu yako akikukosea…’’ maneno ‘’εις σε’’ yakiwa na maana dhidi yako, kwa kweli maneno haya yapo katika mabano, hivyo kwa kweli tafsiri nyingine inayobaki pale ni ‘’Ndugu yako akikosea au akitenda dhambi”, na ndiyo haswa nitaomba tuitumie zaidi katika tafakuri yetu ya leo. Ni nini napaswa kufanya pale ninapoona ndugu yangu, na ndugu hapa inamaanisha kila mbatizwa, kila muumini anapokuwa mbali na Injili, mbali na Kanisa kwa kuenenda kinyume na imani yetu. Ni nini wajibu wangu kwa ndugu yangu anayepotoka katika imani? Yesu leo anatuelekeza kila mmoja ni nini, na jinsi ya kumpata ndugu yangu aliyepotea, anayekuwa mbali na Mungu na jumuiya pia ya waamini yaani Kanisa (ekklesia). Ili kupata ujumbe vema nawaalika tuanze kusoma aya ile iliyotangulia sehemu ya Injili ya leo yaani aya ya 14; ‘’Hali kadhalika, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmoja wa hawa wadogo apotee’’. Ni aya inayotusaidia kuona lengo la kusahihishana ni katika kutimiza mapenzi ya Mungu Baba yetu kuona kila mmoja wetu anapata maisha tena, anarudi na kuwa katika muungano naye na jirani na Kanisa.

Ni wazi ni wajibu wa mchungaji kuhakikisha anampata tena kondoo aliyepotea, lakini huu ni wajibu wa kila mbatizwa, wa kila mkristo kuwa mchungaji wa mwingine, kuwa msaada kwa mwingine katika kuoneshana njia iliyo sahihi, njia inayotupeleka uzimani na si katika maangamio. Hatupaswi kuwa kama Kaini aliyelalamika na kusema: ‘’Mimi sijui! Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?’’ Mwanzo 4:9. Sisi sote kama wabatizwa hatuna budi kutambua wajibu wetu na hasa kwa kuiishi amri ile kuu ya mapendo, inayotusukuma kila mara kuwapenda wengine, kuhakikisha kuwa kwa upendo tunawasaidia wengine kutembea katika njia ya haki, njia ya urafiki na Mungu na jirani. Pamoja na hilo bado Yesu leo anatuelekeza hata jinsi ya kutimiza wajibu huo. Angalisho kwetu tunapotimiza wajibu huo kukumbuka kuwa tufanye yote tukiongozwa na amri ya mapendo na si kinyume na hapo. Hivyo tunawajibika kulinda utu na heshima ya ndugu yetu kwa kuepuka masengenyo, kufurahia maovu ya wengine na kuona fahari kuyaanika au kuyatangaza kwa wengine, kwani huo ni sawa na uuaji, ni kumshusha na kuzidi kumweka mbali ndugu aliye mdhambi, ni kuua mahusiano yetu naye, na hapo nasi tunaingia katika anguko letu, kwani nasi tunaingia dhambini badala ya kuwa msaada wa kumtoa ndugu katika shimo alimo; sisi pia tunatumbukia katika shimo refu na la hatari zaidi.

Yawezekana kuingia katika kishawishi cha kudhania kuwa kwa kusema ukweli basi hapo nitabaki na amani ya roho. Ila ikumbukwe kuwa kilicho na thamani ya juu katika maisha ya mkristo sio ukweli au kusema ukweli bali ni upendo. Ukweli unaweza kwenda kinyume na upendo, na hapo inayochukua nafasi ya kwanza daima ni upendo. Ukweli si kila mara utalinda utu wa mwingine au kulinda umoja wa wanakanisa kwani waweza kutugawa na kutusambaratisha zaidi, na hata kujeruhi wengine, hivyo sisemi kuwa tusiwe wakweli ila katika kuusema au kuusimamia ukweli hatuna budi kuongozwa na kufanya yote kwa upendo. Hekima ya Yoshua Bin Sira 28:17 tunasoma: ‘’Pigo la mjeledi hubakiza kovu, lakini pigo la ulimi huvunjavunja mifupa’’. Ulimi hauna mfupa; lakini unasambaratisha mifupa, kwa maneno yetu tunaweza kuwaumiza na kuwajeruhi wengine. Papa Francisko kila mara anatukumbusha waamini wakristo kuwa makini na dhambi ya ulimi, tunaona jinsi ulimi unavyoangamiza familia zetu, jumuiya zetu hata za kati ya wahudumu wa Neno la Mungu kwa maana makasisi na watawa, jumuiya zetu ndogo ndogo za kikristo, jumuiya za vyama vya kitume na hata maparokiani na majimboni mwetu.

Tunaalikwa leo kujitafakari na kuangalia ni kwa namna gani nimetumia ulimi wangu kuua nafsi au maisha ya mwingine, kwa masengenyo na katika kuanika na kuutangaza uovu au ubaya wa mwingine. Yafaa tukumbuke tunatumbukia katika shimo refu na la hatari zaidi kuliko hata la yule aliye katika uovu kwa kutenda uovu huo kwani ni sawa na uuaji. Ukweli usiojengeka wala kusukumwa na upendo kwa kutupelekea zaidi katika magomvi, kudharirisha na kumwangamiza mwingine, huo hatuna budi kuuepuka na kuwa macho nao. Kila jambo ninalolitenda ili kumsaidia ndugu yangu lazima kujiuliza kama ninalifanya hilo kwa upendo, na kama siyo basi naalikwa kubadili namna yangu ya kufikiri na kutenda. Kila jambo ninalolifanya halina budi kusukumwa na upendo wa kweli kwa ndugu yangu. Si kila ukweli ninaoujua au kuufahamu kuhusu ndugu yangu lazima niuseme hasa ninapotambua kuwa ninapousema basi hapo ninamwangamiza ndugu yangu. Ukweli unaoangamiza na kuua huo ni sawa na uovu, unatoka kwa yule muovu. ‘’Nyingi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka kutelekeza tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile, maana yeye ni mwongo na baba wa uongo’’ Yohane 8:44.

Yesu leo anatuelekeza hatua tatu za namna ya kumpata tena ndugu anayekuwa katika makosa, anayekuwa dhambini, kwa maana mbali na Mungu na jumuiya ya wanakanisa.  Hatua ya kwanza ndio ile inayokuwa ngumu katika utekelezaji wake lakini ya muhimu haswa ndiyo kuongea naye uso kwa uso, mtu kwa mtu bila kuanza kumzunguka kusambaza uovu wake kwa watu wengine. Ni sawa na kusema hatua ya kwanza yafaa ifanyike sirini, iwe ni siri kati yenu bila kuanza kufanya wengine wajue. Na ndio maana nimesema kuwa ni hatua ngumu lakini ya kikristo. Ni rahisi kutoka na kuanza kumtangaza na kumvua nguo na kumuanika kwa wengine na hata kuona furaha kuanika ya mwingine. Ni kilema cha wengi wetu kupenda kuwavua kwa kusimulia mabaya au maovu ya wengine iwe kwa mwingine na hata mara nyingine mabarazani na kwenye vijiwe vyetu vya kila siku. Ndugu zangu tuwe daima walinzi wa ndimi zetu, kuangalia naongea nini kumhusu mwingine kama nikijua nisingependa hilo liongelewe juu yangu basi ni vema kukaa kimya, maana kuendelea kulifanya hilo ni kushiriki katika kumuangamiza na kumuua mwingine.

Ni kwa msaada wa somo letu la pili la leo, Mtume Paulo anatuonya nasi: ‘’Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana…Pendo halimfanyii jirani neno baya, basi upendo ndio utimilifu wa sheria’’ Warumi 13:8-10. Ni maneno yanayotutaka kila mara kutambua maisha ya ukristo yanapata umaana na uhalali wake katika upendo na kamwe sio nje ya hapo. Deni la kila mmoja wetu kila tunapoamka asubuhi na kusafiri kwa siku nzima si kitu kingine bali kupenda kama Mungu anavyotupenda, iwe tunasali, iwe tunatimiza wajibu wetu, iwe tuna furaha na kujumuika na wengine, kila mara hatuna budi kutambua kuwa tunadaiwa neno moja tu nalo si jingine bali ni upendo. Yesu anakwenda mbali zaidi na kusema kama hatua hii ya kwanza haitatupatia matunda mazuri basi twende hatua ya pili. Ni kwa kuwashirikisha ndugu mmoja au wawili wenye hekima na busara katika jumuiya ya wanakanisa. Ndio kusema bado tunawajibika kulinda utu na heshima ya mkosaji, kutenda kwa uangalifu mkubwa hivi kutokumwangamiza mwingine kwa kuua nafsi yake.

Ni kusahihisha kunakosukumwa na upendo kwa mwingine na ndio maana hao wengine wanaweza kushirikishwa kwa nia ya kumpata ndugu anayekuwa mbali katika uovu. Ni kuwashirikisha wale watu ambao tunakuwa na hakika kuwa wanamtakia mema, wanamtakia uzima wa kweli, wanamtakia lililo jema kwa upande wa mkosaji. Daima tukumbuke kinamchomrudisha ndugu aliye mbali si kingine bali ni upendo wetu, ni jinsi anavyoonja maumivu yetu kwa kumuona anakuwa mbali na Mungu na jirani. Daima hata katika familia zetu tunashindwa kuwasaidia wengine kwani wanakosa kuonja upendo wetu kwao, tunatanguliza mara nyingi hukumu kuliko hata kuwasikiliza na kuwasaidia kwa upendo. Ni changamoto katika familia zetu na hata katika jumuiya za wanakanisa. Baada ya kushindikana hatua hizi mbili za awali, Yesu anatualika kushirikisha Kanisa. Kanisa ni mama kwa kila mmoja wetu. Ni wajibu wa mama kanisa kukusanya wanae, kusali kwa ajili ya wanae na hasa kuona kila mwanakanisa anasaidiwa kwa upendo ili kurudi katika muungano na Mungu na ekklesia.

‘’Na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru’’ maneno haya ya Yesu kama tunayachukulia jinsi yalivyo hakika tunabaki na maswali magumu bila majibu. Ni Yesu anayetuambia katika aya ile ya 10 ya sura ya 18 ya Injili ya Matayo akisema: ‘’Jihadharini! Msimdharau mmojawapo wa wadogo hawa’’.  Na hata twajiuliza yawezekanaje rafiki wa watoza ushuru na wadhambi kutoa hukumu kali namna hii? ‘’Mwangalieni huyu, mlafi na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi’’ (Mathayo 11:19). Na hata tukirejelea Injili ya Matayo tunabaki na mshangao kwani kila mara mwinjili anatukumbusha kuwa kanisa sio jumuiya ya wakamilifu au watakatifu bali ni pia ya wadhambi na wakosefu. Ni shamba lenye mchanganyiko wa ngano na magugu, ni wavu wenye kuvua samaki wazuri na wabaya, ni karamu walimoalikwa na kushiriki wema kwa waovu. Kama ndivyo basi kwa nini leo Yesu anaruhusu kuwatenga wale wanaoshupaa katika uovu?

Kauli hii ya Yesu isitupelekee kukosa kumuelewa vema Yesu na hivyo kujikuta katika matata ya kufafanua Neno la Mungu kama Habari Njema ya wokovu, Habari ya matumaini na upendo wa Mungu kwa kila mwanadamu bila upendeleo wala ubaguzi wa aina yoyote ile. Ni wajibu wa kanisa kama mama kuhakikisha halimpotezi hata mwana wake mmoja, bali wote wafikie ukamilifu na kuwasindikiza kwa huruma na upendo. Ni katika kutimiza wajibu huo mama kanisa linaweza kutumia njia ya kumsaidia mtu kutambua kuwa yupo mbali na Mungu na Kanisa. Ni wajibu wa mama kanisa kufundisha wana wake na kuwaonesha pale wanapoishi kadiri ya Injili na hivyo wajibu wa kuonya na kusahihisha wana wake pale wanapopotoka ila likifanya yote kwa upendo. Ni wajibu wake kusahihisha, kuonya na hata kuadhibu inapobidi ila daima likisukumwa na upendo ili kumsaidia huyu anayekuwa katika uovu kubadili njia yake na kupata uzima. Kanisa halipaswi kubaki kimya au kuvumulia au kuufumbia macho uovu wa wana wake, na huo ni wajibu wa kila mbatizwa katika kuona anamsaidia mwingine kurudi katika njia iliyo sahihi.

Ni changamoto kubwa katika ulimwengu wetu wa leo. Ulimwengu wa utamaduni wa kila mmoja ni kipimo cha ukweli, kila mmoja aamue nini jema na nini ovu, hakuna ukweli mmoja bali kila mmoja ni ukweli kutegemeana na yeye. Ni ulimwengu kila mmoja yupo sawa kwa mtazamo wake na maonjo na mazingira yake, ukweli hautokani tena na Neno la Mungu. Ni changamoto hata kwetu wahubiri na wanakanisa, pale tunapopotoka kwa kudhani kila mmoja aone na aamue yeye mwenyewe, Kanisa linawajibishwa leo, linaalikwa kujitathimini na kuona nafasi yake ni nini katika kuwaelekeza watu katika ukweli, yaani kwa Mungu kwa msaada wa Neno la Mungu. Nchini kwetu Tanzania tupo katika siku muhimu na nyeti, siku za michakato ya kuelekea uchaguzi mkuu. Nini wajibu wa Kanisa? Je, ni kuchukua upande kwa kukinenea vema na mazuri chama kimoja tu, au mgombea anayekuwa ni wa kwetu tu, au ndugu au wa kabila au imani yangu tu, je, tunatambua wajibu wa kulinda na kuwa watetezi wa haki bila kujali itikadi zetu na tofauti zetu mbali mbali, je sisi ni waamini wa haki? Ni maswali kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza. Je, kama kiongozi ninasimamia haki, ni muumini wa haki? Kama mwamini mlei,  Je, nashiriki haki yangu ya kiraia kwa kusukumwa na haki?

Haki ni msingi wa amani, haki inatokana na kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake kama raia na zaidi sana basi watumishi na viongozi wa dini kuwa watetezi wa haki, kuwa wasemaji wa wale wasiokuwa na sauti, wanaokuwa wanyonge na wadogo. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na vile vya kusimamia haki, je wanasukumwa nao na kuongozwa katika kuhakikisha wanalinda haki za kila raia bila upendeleo au ubaguzi? Je, tume yetu ya uchaguzi inasimamia haki kwa wagombea wote bila upendeleo au kugandamiza baadhi wanaokuwa wanyonge? Kila mmoja leo anaalikwa kujiuliza, Je, mimi ni muumini wa haki katika familia, kazini, jumuiyani, kigangoni, parokiani, uraiani na ulimwenguni? Je, natenda na kutimiza wajibu wangu kwa kusukumwa na upendo kwani ndio sheria kuu, ndio ukamilifu wa yote tunayodaiwa kuyatenda kama wakristo. Hata tunapotimiza wajibu wetu wa kumsahihisha mwingine, daima Kanisa linatuhimiza na kutukumbusha maneno ya Kristo mwenyewe: ‘’Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako, na huku huioni boriti iliyoko katika jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe! Toa kwanza boriti iliyoko jichoni mwako, na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako’’ (Luka 6:42).

Kanisa daima limetambua wajibu wake huo wa kusahihisha na kuwasaidia wana wake kubaki katika urafiki na Mungu na jumuiya ya wanakanisa. Kanisa linajifunza na kuona kila mara jinsi bora zaidi ya kulitekeleza hilo. Mtume Paolo katika waraka wake wa kwanza wa Wakorintho sura ile ya tano anawaandikia na kuwaonya lakini haswa kuwaelekeza kumtenga yule aliyekuwa anaishi na mke wa baba yake. Kanisa halifurahi kutenga wanae bali inatumika kama mbinu na njia ya kumfanya mmoja aguswe ili kubadili njia zake na ndio maana kila mara Kanisa linatualika kukumbuka kuwaombea wale wote wanaokuwa mbali na ushirika na Mungu na Kanisa. Ni wajibu wetu kila siku tunapopiga magoti kusali na kuwaombea wale wote wanaoshupaa katika uovu ili neema ya Mungu iwaguse na kukubali kubadilika kwa kuongozwa na Injili ya Kristo. Kanisa tangu mwanzo linafundisha juu ya wajibu wa kulinda mafundisho sahihi kwa kuwaonya na kuwakaripia na hata kuwafundisha kwa njia ile ngumu ya kuwatenga wazushi wa imani. ‘’ Mtu anayesababisha mafarakano mpe onyo la kwanza na la pili, kisha achana naye’’ (Tito 3:10). ‘’Tutakiane amani’’, ni maneno tunayoyasikia katika kanuni ya kila adhimisho la Misa Takatifu.

Yafaa tutambue umuhimu na maana ya maneno yale, mkono wa amani kwa jirani ambaye yawezekana hata akawa ni mtu nisiyemfahamu ni kunikumbusha maneno ya leo ya Yesu anapohitimisha sehemu ya Injli ya leo. ‘’Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu wakatapopatana duniani katika jambo lo lote wakataloomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni…’’ Ni hakika kuwa sala ya kweli lazima isaliwe tunapokuwa na amani, tunapomaliza tofauti zetu na wengine, sala ni kitendo cha upendo sio tu kwa Mungu bali pia kwa jirani. Kama kweli tunataka kusali kweli na vizuri hatuna budi kupenda kwanza, sala ni muunganiko wetu na Mungu na pia kati yetu. Ni kitendo kinachoonesha kuwa nipo pamoja na Mungu na ndugu yangu, na jirani yangu. Sala kamwe sio kitendo cha ubinafsi na ndio maana tunakumbushwa tunaposhiriki adhimisho la Misa Takatifu kutakiana amani, sala ni kitendo kinachopaswa kunileta karibu na Mungu na jirani, ni maneno na ishara tunayoifanya kabla ya kumpokea Yesu wa Ekaristi, nina amani na jirani na hivyo namuona Kristo katika sura ya mwingine na kwa kuwa nakiri hilo basi sasa nakuwa tayari kumkaribisha Yesu aingie ndani mwangu katika maumbo yale ya mkate na divai. Nawatakia Dominika na tafakari njema.

05 September 2020, 14:21