Tafuta

Vatican News
2020.08.01 Kusoma maandiko matakatifu 2020.08.01 Kusoma maandiko matakatifu  

Sudan Kusini:Limetangazwa toleo jipya la Biblia kwa lugha ya Pazande!

Askofu wa Jimbo la Tombura-Yambio nchini Sudan Kusini anawaalika mapadre kufikiria tukio la Biblia mpya ya lugha ya ‘Pazande’ kama wito wao kuwa wahudumu wa Neno.Katika maadhimisho ya Misa,Askofu Hiiboro amewaalika wakristo kuendelea kusali kwa ajili ya kupambana na virusi vya corona linaloendelea kutesa ulimwengu na kufuata kanuni zilizotolewa kuzuia kuenea kwa virusi.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Ni hatua muhimu sana iliyofikiwa kwa hitimisho la miaka ya kazi ngumu, ya uvumilivu katika huduma ya kimisionari. Kwa maana hii, tarehe 14 Septemba 2020 katika Jimbo la Tombura-Yambio imewakilishwa Toleo jipya  la kwanza la ‘Biblia’ katika lugha mahalia ya Pazande. Hii ni hatua muhimu kwa jimbo hilo, ambalo limekuwepo kwa zaidi ya miaka mia moja. Kama ilivyonukuliwa na Shirika la habari za kimisionari Fides kuhusu tukio hilo la kihistoria lililofanyika katika fursa ya kumbukizi la miaka 6 tangu  kifo cha Askofu Joseph Gasi Abangite,aliyekuwa wa  kwanza kupewa jimbo hilo.

Tukio hilo limeongozwa na kauli mbiu iliyochukuliwa katika Zaburi: “Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu”. Katika barua yake ya kichungaji ya Askofu Eduardo Hiiboro, wa jimbo hilo kwa sasa, amesisitiza umuhimu kuwa toleo la ‘Andiko Takatifu’ ambalo  linaleta pamoja zaidi ya waamini milioni nne ambao wanazungumza lugha ya Pazande nchini ya Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kwa mujibu wa Askofu wa Jimbo amesema :“Shauku yangu kama kiongozi wa Jimbo katoliki ya Tombura-Yambio, ni ile ya kuadhimisha, kusoma, kueneza na kuishi Neno la Mungu kwa namna ya kugeuka kuwa kitovu cha mantiki yote ya maisha.” Ni matarajio kuwa Biblia inageuka kuwa sehemu ya kimbilio na kiini cha maisha ya kila mwaamini na kwa ajili ya Kanisa la Tombura-Yambio, ambalo linaendelea kuadhimisha, kusoma, kusali na kushirikisha Neno la Mungu”.

Askofu Hiiboro kwa kuhitimisha anawaalika mapadre kufikiria tukio hili kama wito wao kuwa wahudumu wa Neno. Katika maadhimisho ya Misa, Askofu Hiiboro amewaalika pia wakristo kuendelea kusali kwa ajili ya kupambana na virusi vya corona linaloendelea kutesa ulimwengu, vile vile kuzingatia kanuni zilizotolewa za kuzuia kuenea kwa virusi. Katika maadhimisho ameshiriki hata kiongozi wa Serikali ya Ikweta ya Mashariki Jenerali, Alfred Futuyo, ambayo amewaalika wazalendo kukumbatia amani na kuungana kwa ajili ya maendeleo ya serikali na Nchi kwa ujumla.

17 September 2020, 16:51