2019.09.09 Ziara ya Kitume ya Papa Francisko nchini Msumbiji, Madagascar na Mauritius. 2019.09.09 Ziara ya Kitume ya Papa Francisko nchini Msumbiji, Madagascar na Mauritius. 

Afrika:Ujumbe wa Secam baada ya mwaka tangu ziara ya Papa Francisko!

Shirikisho la mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki SECAM wametoa ujumbe wao mara baada ya mwaka mmoja tangu Papa Francisko atembelee Afrika katika nchi ya Msumbiji,Madagascar na Mauritius tarehe 4-10 Septemba 2019.Ujumbe wa Maaskofu kwa ajili ya kuwatia moyo kama Papa mwenyewe alivyowaachia kazi ya kujikita nayo kwa ajili ya amani,matumaini na mapatano.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Mwaka mmoja uliopita Papa Francisko alifanya ziara yake ya kitume barani Afrika kuanzia tarehe 4 hadi 10 Septemba  2019 kwa kutembelea nchi ya Msumbiji, Madagascar na Mauritius. Baada ya siku 365 tangu kutokea tukio hili la furaha, kwa bara la Afrika, Shirikisho la Baraza la Maaskofu wa Afrika Mashariki na Madagascar (SECAM )wameandika ujumbe wao kwa waamini wote na wenye mapenzi mema. Ujumbe  wao uliotangazwa ni kwa ajili kuongeza nguvu na kuwatia moyo kama ulivyoachwa na Papa Francisko wakati wa ziara yake hasa ya kujikita kwa nguvu zote kutafuta amani, matumaini na mapatano.  “Tunarudia kutoa wito wa Papa Francisko ya kuwa wote tunapaswa kusema daima HAPANA  vurugu na NDIYO ya amani, kwa sababu kila kitu kinapotea katika vita na kila kitu kinapatikana katika amani”.

Maaskofu hawa wa SECAM aidha wanaandika kuwa: “Kwa sababu ya migogoro, watu wanaishia kutokuwa na nyumba kabisa za kuishi, chakula, shule za kuelimisha, hospitali za kutibu wagonjwa, makanisa kwa ajili ya kuunganika pamoja kusali na nyanja nyingi za kufanyia kazi”. Sio hiyo tu bali Secam pia inasisitiza juu ya janga la “maelfu na maelfu ya watu waliolazimika kuhama wakitafuta usalama na zana za kuweza kuishi”. Kwa njia hiyo ndipo maaskofu hawa wa Afrika na Madagascar wanatoa ushauri wa kutafuta amani kwa kuwa ndiyo utume unaowazingira wote na kuwaomba wafanye kazi kwa nguvu zote na mara zote bila kuchoka”.

Maaskofu wa SECAM vile vile wanasisitiza kwamba “amani siyo tu kutokuwepo kwa vita, lakini pia ni jitihada  bila kuchoka, hasa kwa wale walio na jukumu kubwa, la kuweza kutambua, kuhakikisha na kujenga upya kwa dhati hadhi, ambayo mara nyingi husahaulika au kupuuzwa kwa ndugu, kaka na dada, ili nao wahisi na kuwa wahusika wakuu wa hatima ya taifa lao na bara lao kwa ujumla.  Ni kwa njia ya amani tu, inawezekana kufikia upatanisho wanakumbusha Secam na ambayo inamaanisha kuwa na mchakato wa kila wakati unaohitajika, ambao kila kizazi kipya kinahusika na ambapo kuna haja ya ufunguzi wazi wa kukutana kweli, kutambuliwa kwa mwingine, kuimarisha uhusiano na kujenga madaraja” maaskofu wanasisitiza!

Hata hivyo kwa bahati mbaya Secam inafafanua kile kinachoendelea barani Afrika na kusema: “katika nchi tofauti  za Kiafrika, pamoja na Msumbiji iliyotembelewa na Papa Francisko, bado kuna vitendo vya kikatili, vya vurugu na katika bara zima hakuna ishara yoyote ya kuishi kwa amani au kwa usawa, umoja, usalama wa chakula na ulinzi wa mazingira”. Na hatimaye viongozi wakuu wa SECAM wanamshukuru Papa Francisko kwa kuwa mjumbe wa matumaini, mtangazaji wa amani na msaidizi wa upatanisho!

05 September 2020, 16:31