Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Inàcio Saùre wa Jimbo kuu la Nampula, Msumbiji ameandika Waraka wa Kichungaji kukumbukia Mwaka mmoja tangu Papa Francisko alipotembelea Msumbiji tarehe 4-6 Septemba 2019. Askofu mkuu Inàcio Saùre wa Jimbo kuu la Nampula, Msumbiji ameandika Waraka wa Kichungaji kukumbukia Mwaka mmoja tangu Papa Francisko alipotembelea Msumbiji tarehe 4-6 Septemba 2019.  (Vatican Media)

Waraka wa Kichungaji Kutoka Msumbiji: Upatanisho, Amani na Matumaini!

Askofu mkuu Inácio Saúre, anasema, mchakato wa ujenzi wa amani ya kudumu ni changamoto inayopaswa kupokelewa kwa: Imani, moyo mkuu na ujasiri. Amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini inawahusisha na kuwashirikisha wote. Utamaduni wa ujenzi wa haki, amani na upatanisho ni mchakato unaohitaji toba na wongofu wa ndani, ili kuondokana na utamaduni wa kifo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji kuanzia tarehe 4-6 Septemba 2019 iliongozwa na kauli mbiu “matumaini, amani na upatanisho.” Hija hii ilifanyika wakati muafaka, Msumbiji ilipokuwa inamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa ajili ya amani, ustawi na maendeleo ya watoto wake baada ya patashika nguo kuchanika kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyo sababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji amedhamiria na anataka kuhakikisha kwamba, Msumbiji inajenga na kudumisha misingi ya haki, amani na umoja wa kitaifa, ndiyo maana hivi karibuni, Chama cha FRELIMO kimewekeana tena sahihi Mkataba wa Amani na Chama cha RENAMO, ambacho kwa sasa kinaongozwa na Bwana Ossufo Momade. Lengo ni kusitisha vita na mashambulizi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia; pamoja na kuhakikisha kwamba, ulinzi na usalama wa Msumbiji unaendelea kuimarishwa. Mkataba huu, unaweka matumaini makubwa katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa.

Baba Mtakatifu akiwa nchini Msumbiji alipata bahati ya kumtembelea Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji pamoja na kufanya naye mazungumzo ya faragha. Baadaye, Baba Mtakatifu akakutana na kuzungumza na viongozi wa serikali, wanadiplomasia, viongozi wa kisiasa pamoja na vyama vya kiraia. Itakumbukwa kwamba, majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni kati ya vipaumbele vinavyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu alikutana na kuzungumza na vijana kutoka dini na madhehebu mbali mbali nchini Msumbiji, ili kuwaimarisha katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama sehemu pia ya mchakato wa kuganga na kuponya madonda ya vita na kinzani, zilizoipekenya Msumbuji kwa miaka mingi. Baba Mtakatifu alikutana na kuzungumza na Maaskofu, Mapadre, Watawa, Makatekista, Waseminari pamoja na walezi wao kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili, Jimbo kuu la Maputo, Msumbiji.

Ijumaa, tarehe 6 Septemba 2019, Baba Mtakatifu asubuhi kabla ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa Zimpeto, alitembelea Hospitali ya Zimpeto na kusalimiana na wagonjwa. Baada ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu akawa amehitimisha hija yake ya kitume nchini Msumbiji kama hujaji wa matumaini, amani na upatanisho. Katika kumbukizi la mwaka mmoja tangu Baba Mtakatifu Francisko alipofanya hija ya kitume nchini Msumbiji, Askofu mkuu Inácio Saúre, wa Jimbo kuu la Nampula ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji, ameandika Waraka wa Kichungaji kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji mintarafu hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo. Anasema, anapenda kuchukua fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyebariki na hatimaye, kufanikisha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji. Kwa hakika, amekuwa ni alama ya uwepo wake wa karibu, upendo na mshikamano kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji, lakini zaidi,  kwa wale wananchi walioathirika zaidi kutokana na kimbunga cha Idai na Kenneth; wahanga wa vita ya wenyewe kwa wenyewe Kaskazini na Kati kati ya Msumbiji.

Mtakatifu Paulo VI alikuwa ni kiongozi aliyeitakia Msumbiji amani na ustawi kwa kukazia umuhimu wa mshikamano na uhuru wa kweli kwa wananchi wa Msumbiji waliokuwa bado wanaelemewa na kongwa la ukoloni na miaka mitano baadaye,  yaani mwaka 1975 Msumbiji ikajipatia uhuru wake wa bendera. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1988 alitembelea Msumbiji ambayo ilikuwa bado imezama katika vita ya wenyewe kwa wenyewe. Hili ni janga ambalo limepelekea maelfu ya wananchi kupoteza maisha; kukimbilia uhamishoni na wengine kupata vilema vya kudumu. Vita ilivuruga umoja, mshikamano na mafungamano ya jamii kitaifa; familia zikasambaratika, uchumi ukachechemea na vijana wengi wakajikuta hawana tena fursa ya masomo na ajira. Baba Mtakatifu ametembelea Msumbiji baada ya kuathiriwa sana na Kimbunga cha Idai kilichopiga nchini Msumbiji mwezi Machi, 2019 na Kenneth kilichosababisha maafa makubwa mwezi Aprili 2019. Ni katika muktadha huu, familia ya Mungu nchini Msumbiji katika unyonge wake, ikaonja ukarimu, upendo na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa, iliyofufua tena matumaini kwa wananchi wa Msumbiji.

Kauli mbiu ya “Matumaini, amani na upatanisho” ni mbinu mkakati wa maisha na utume wa Kanisa nchini Msumbiji, ili kuendelea kusoma alama za nyakati hata kwa wakati huu. Kwa hakika, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kuwakumbuka watu wa Mungu nchini Msumbiji katika sala na sadaka yake. Kinachomsikitisha Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu ni vitendo vya kigaidi kimataifa vinavyofanywa dhidi ya wananchi wa Msumbiji hasa huko Cabo Delgado. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 23 Agosti 2020 mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa mara nyingine tena alipenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji na kwa namna ya pekee wale ambao wako Cabo Delgado, Kaskazini mwa Msumbiji, wanaoteseka kutokana na vitendo vya kigaidi kimataifa. Baba Mtakatifu amesema, amewataja watu wa Mungu kutoka nchini Msumbiji, kwa kukumbuka hija yake ya kitume nchini Msumbiji kuanzia tarehe 4-6 Septemba 2019 iliyoongozwa na kauli mbiu “Matumaini, amani na upatanisho.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso ya wananchi wa Msumbiji, hivi karibuni, alimpigia simu Askofu Fernando Lisboa wa Jimbo Katoliki la Pemba, Msumbiji, ili kumfariji na kutaka kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji. Alisema, anafuatilia matukio yote ya Cabo Delgato kwa wasi wasi mkubwa na kwamba, daima amewaweka katika sala zake. Katika hali ngumu na wasi wasi wa maisha, kamwe wasisite kumpatia taarifa mapema. Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 12 Aprili 2020, aliadhimisha Sherehe ya Pasaka ya Bwana, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baadaye, akatoa ujumbe wa Pasaka: “Urbi et Orbi”. Alisikika akisema kwamba, dharura ya wakati huu kutokana na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 isiifanye Jumuiya ya Kimataifa ikasahau majanga mbali mbali yanayoendelea kuwakumba watu wengi sehemu mbali mbali za dunia.

Askofu mkuu Inácio Saúre, wa Jimbo kuu la Nampula ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji katika Waraka wake wa Kichungaji kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji anasema, mchakato wa ujenzi wa amani ya kudumu ni changamoto inayopaswa kupokelewa kwa: Imani, moyo mkuu na ujasiri. Amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini inawahusisha na kuwashirikisha wananchi wote wa Msumbiji pamoja na taasisi zake. Kamwe, vita na ubaya wa moyo visiwe ni hatima ya maisha ya wananchi wa Msumbiji. Mambo yote yatakwenda vyema, kwa wale wote wanaompenda Mungu na jirani zao. Utamaduni wa ujenzi wa haki, amani na upatanisho ni mchakato unaohitaji toba na wongofu wa ndani, ili kuondokana na utamaduni wa kifo, unaowasukuma baadhi ya wanasiasa kutaka kukimbilia mtutu wa bunduki kama silaha ya suluhu ya matatizo na changamoto za maisha. Umefika wakati kwa watu wa Mungu nchini Msumbiji kusimama kidete kujenga na kudumisha Injili ya Amani dhidi ya Utamaduni wa kifo, kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kukuza na kudumisha demokrasia shirikishi.

Ulinzi na usalama ni kazi ya wananchi wote wa Msumbiji na wala si dhamana ya FRELIMO wala RENAMO peke yao. Uongozi uwe ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa Katoliki nchini Msumbiji, linapania kuendeleza mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu nchini Msumbiji. Baba Mtakatifu Francisko anasema, siasa safi ni msingi wa maendeleo endelevu na fungamani; demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, yanayowashirikisha wadau mbali mbali mbali katika jamii; marika pamoja na tamaduni, daima wakijitahidi kujenga imani kati yao kama sehemu ya kukuza na kudumisha amani. Amani ya kweli inapata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu. Lakini, wakati mwingine, moyo huu unasheheni maovu kama vile: rushwa na ufisadi; uvunjaji wa haki msingi za binadamu; vita katika mifumo mbali mbali; utumiaji mbaya wa madaraka na uongozi mbovu usiozingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi na matokeo yake ni: ukosefu wa fursa za ajira, huduma mbovu za kijamii katika sekta ya elimu, afya na makazi; njaa na ukosefu wa maji safi na salama; uhamiaji wa shuruti; sera za ubaguzi wa rangi; uchafuzi wa mazingira na matumizi mabaya ya rasilimali na utajiri wa nchi.

Waraka Msumbiji
25 August 2020, 13:57