Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe limeandika Waraka wa Kichungaji wa Mwaka 2020 kuhusu hali halisi ilivyo nchini mwao na kuitaka Serikali kusikiliza na kujibu kilio cha watu wake. Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe limeandika Waraka wa Kichungaji wa Mwaka 2020 kuhusu hali halisi ilivyo nchini mwao na kuitaka Serikali kusikiliza na kujibu kilio cha watu wake. 

Waraka wa Kichungaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe 2020

Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe katika Waraka wa Kichungaji, linayaangalia: Matukio ya wakati huu, saratani ya rushwa na ufisadi, umuhimu wa kuenzi siku ya mashujaa. Maaskofu wanakazia umuhimu wa mchakato wa mageuzi kama sehemu ya mapambano dhidi ya umaskini na umuhimu wa kuunda jukwaa litakalojadili vipaumbele vya familia ya Mungu nchini Zimbabwe. Aman!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe, ZCBP limeandika Waraka wa Kichungaji wa Mwezi Agosti 2020 unaofanya upembuzi yakinifu kuhusu fursa, matatizo na changamoto zinazoendelea kuwapekenya watu wa Mungu nchini Zimbabwe. Maaskofu wanasema, mapambano bado kabisa yanaendelea kwa sababu maisha ya wananchi wa Zimbabwe ni muhimu sana na wala mchakato wa kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, kamwe hauna kikomo. Kila kizazi kinawajibika kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa sanjari na kuendelea kujikita katika mchakato wa kudumisha misingi ya amani. Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe katika Waraka wa Kichungaji wa tarehe 14 Agosti, 2020 linayaangalia matukio ya wakati huu, saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma, umuhimu wa kuenzi siku ya mashujaa na vikosi vya ulinzi na usalama. Maaskofu wanakazia umuhimu wa mchakato wa mageuzi makubwa kama sehemu ya mapambano dhidi ya umaskini na kwamba, kuna umuhimu wa kuunda jukwaa litakalojadili vipaumbele vya familia ya Mungu nchini Zimbabwe.

Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe linasikitika kusema kwamba, kwa sasa Zimbabwe inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, kuna ongezeko kubwa la umaskini wa hali na kipato; kuna ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula. Saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma unaendelea kuwapekenya watu wa Mungu nchini Zimbabwe, kiasi kwamba, haki msingi za binadamu si kati ya vipaumbele nchini Zimbabwe, hali ambayo imepelekea hata baadhi ya viongozi wa Serikali kuanza kutumia madaraka yao vibaya na kusahau utawala wa sheria. Haya ni matatizo na changamoto zinazohitaji kupewa suluhu ya haraka kabla ya mambo hayajaharibika zaidi. Maandamano na migomo ni dalili kwamba, wananchi wa Zimbabwe wamechoka na hali wanayokabiliana nayo na sasa wanataka kuona mageuzi makubwa katika medani mbali mbali za maisha. Kuna matatizo kama “Gukurahundi” ambayo hayakupewa ufumbuzi wa kudumu, na sasa yanaendelea kuwatesa vijana wa kizazi kipya. Itakumbukwa kwamba, “Gukurahundi” ni mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Jeshi la Serikali dhidi ya wananchi wa kabila la Wandebele kati ya mwaka 1983 hadi mwanzoni mwa mwaka 1987.

Viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa wameonesha wasi wasi wao kutokana na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu nchini Zimbabwe, lakini bado shutuma hizi hazijafanyiwa kazi na Serikali ya Zimbabwe. Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe linasema kwa hakika maisha ya watu wa Mungu nchini humo ni muhimu sana. Kuna haja kwa Serikali kuheshimu uhuru wa watu kutoa mawazo yao na kwamba, tofauti ya maoni, mtazamo na vipaumbele, kisiwe ni chanzo cha kinzani na mipasuko ya kijamii nchini Zimbabwe, bali fursa ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa unaofumbatwa katika misingi ya utofati na wala si uadui. Vinginevyo, watu wenye mawazo tofauti watachukuliwa daima kuwa ni wapinzani wa Serikali ambao hawana haki ya kuwepo nchini Zimbabwe, hali ambayo ni hatari sana, kwani hiki ni kielelezo cha matumizi mabaya ya madaraka ya umma. Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe katika Waraka wake wa kichungaji linasikitika kusema kwamba, rushwa na ufisadi ni saratani inayoendelea kuwapekenya watu wa Mungu nchini Zimbabwe. Rushwa inaendelea kufifisha uchumi na haki msingi za binadamu na matokeo yake waandishi wa habari wanaofunua saratani hii, wameishia “kutupwa lupango” na huko wanakiona cha mtema kuni!

Mama Kanisa katika maisha na utume wake wa kinabii, anao wajibu wa kutangaza na kushuhudia haki inayofumbatwa katika huruma, daima likiwa linatafuta: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rushwa, uchu wa mali na madaraka, ni mambo ambayo yamewafanya baadhi ya viongozi wa Serikali, kuendelea kuwa jeuri, kwa ajili ya kulinda masilahi yao binafsi na wale wanaowazunguka! Kuna haja kwa familia ya Mungu nchini Zimbabwe kutambua kwamba, uongozi ni huduma inayotekelezwa kwa unyenyekevu pasi na makuu! Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe katika Waraka wake wa kichungaji linasema, kuna haja ya kuendelea kuadhimisha kumbukumbu ya mashujaa na vikosi vya ulinzi na usalama kwa mchango wake mkubwa katika ukombozi wa Zimbabwe, bila kuwasahau wananchi wa kawaida waliochangia katika mchakato mzima wa kutafuta na hatimaye, Zimbabwe ikajipatia uhuru wake. Maaskofu wanawataka wanasiasa kuwa ni vyombo na wajenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa; vyombo vya ulinzi na usalama viwe ni kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao na kamwe visitumiwe na Serikali ya Zimbabwe kwa ajili ya kuwanyanyasa raia wake. Kuna baadhi ya wanasiasa wanaoendelea kuunda mazingira ya vita na mipasuko ya kijamii kati yao na wananchi, jambo ambalo ni hatari sana kwa mafungamano ya kijamii nchini Zimbabwe.

Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe linawaalika viongozi wa Serikali na wanasiasa kusoma alama za nyakati na kufanya mageuzi makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya watu wa Mungu nchini Zimbabwe. Wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini kilio cha watu wao na kukipatia majibu muafaka. Viongozi wawe na ujasiri wa kujadiliana na raia wao katika misingi ya ukweli na uwazi, bila vitisho, dharau wala kejeli! Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni kati ya mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na viongozi wa Serikali na kisiasa, huku wakiongozwa na dhamiri zao nyofu. Viongozi wa Serikali wawe na ujasiri wa kubainisha mafanikio, mapungufu na changamoto wanazokabiliana nazo na wala si busara kukimbia matatizo. Viongozi wa Serikali na kisiasa kushindwa kujenga utamaduni wa kusikiliza na kujadiliana katika misingi ya ukweli na uwazi, leo hii, Zimbabwe imefikia katika hali kama hii, kiasi cha wananchi kuanza kufikiri kwamba, Serikali yao, imewageuzia kisogo! Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe linasema, kuna haja kwa Serikali kujenga jukwaa litakaloweza kufanya upembuzi yakinifu kuhusu matatizo, changamoto na fursa, hili hatimaye, kubaini vipaumbele vya watu wa Mungu nchini Zimbabwe vinavyopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, sheria za kitaifa na kimataifa zinazingatiwa, utawala wa sheria unapewa kipaumbele pamoja na kuendea kufufua urafiki na mataifa ambayo yamefunga uhusiano wake wa kidiplomasia na Zimbabwe. Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe, mwishoni mwa Waraka wake wa kichungaji linakaza kusema, janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, litaendelea pia kusababisha matatizo na changamoto mbali mbali nchini Zimbabwe.

Maaskofu Zimbabwe
17 August 2020, 14:00