Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Japan: Ujumbe wa Siku 10 za Kuombea Amani Duniani 2020: Linda Maisha Yote, Amani ni Safari ya Matumaini. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan: Ujumbe wa Siku 10 za Kuombea Amani Duniani 2020: Linda Maisha Yote, Amani ni Safari ya Matumaini. 

Ujumbe wa Baraza La Maaskofu Japan Siku 10 za Kuombea Amani 2020

Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linapenda kukazia kuhusu madhara ya vita huko Okinawa; Msimamo wa Kanisa kuhusu kuenzi Injili ya amani duniani; Ujumbe wa Amani kutoka kwa Papa Francisko na kwamba, amani ni safari ya matumaini. Changamoto katika ulimwengu mamboleo ni vita baridi inayotishia amani duniani, athari za mabadiliko ya tabinchi na Virusi vya COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Amani inatishiwa sana na mashindano, utengenezaji, biashara pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani ambayo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu! Baraza la Maaskofu Katoliki Japan katika ujumbe wake wa Siku 10 za kuombea Amani Duniani, kwa mwaka 2020 linasema: Linda maisha yote, Amani ni safari ya Matumaini. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, CBCJ, kwa nyakati mbali mbali limekuwa likitoa ujumbe kwa ajili ya kumbukumbu ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Leo hii, bado kuna vita baridi, amani inaendelea kutishiwa kwa sababu ya utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha za nyuklia sanjari na athari za mabadiliko ya tabianchi na sasa janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Katika ujumbe wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linapenda kukazia kuhusu madhara ya vita huko Okinawa; Msimamo wa Kanisa kuhusu kuenzi Injili ya amani duniani; Ujumbe wa Amani kutoka kwa Papa Francisko na kwamba, amani ni safari ya matumaini.

Maaskofu Katoliki Japan wanasema mapambano kati ya Japan na Marekani kwenye Kisiwa cha Okinawa yalisababisha maafa makubwa na wananchi Kisiwani hapo, wakakusanyika ili kusali, kumwomba Mungu aweze kusitisha vita hiyo na amani kurejea tena kati yao. Mwanadamu daima amekuwa ni chanzo cha vita, kumbe, ni wajibu wake, kujiwekea sera na mikakati ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Vita daima itaendelea kuwa ni kashfa kubwa katika maisha ya binadamu. Lakini maisha ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kurutubishwa kwa njia ya mchakato wa ujenzi wa umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu, haki na uaminifu kwa jirani. Amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha mwanadamu.

Kunako mwaka 1981, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema: kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani huko Hiroshima na Nagasaki nchini Japan. Tangu wakati huo, familia ya Mungu nchini Japan kuanzia tarehe 6 hadi 15 Agosti ya kila mwaka imekuwa ikisali kwa ajili ya kuombea amani duniani. Huu ni muda muafaka wa kusali na kutafakari kuhusu Injili ya amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Majadiliano katika ukweli na uwazi, yasaidie kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani. Baba Mtakatifu Francisko anasema sala ni silaha nzito kwa ajili ya kusaidia mchakato wa majadiliano kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ili aweze kusaidia kuenzi ujenzi wa dunia inayosimikwa katika haki na mshikamano kama kielelezo cha amani ya kudumu. Tarehe 20 Septemba 2017 Vatican ikaridhia Mkataba wa Kimataifa unaopiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia.

Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Japan Mwezi Novemba 2019, alikazia umuhimu wa kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani. Aliwataka vijana kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutafuta na kudumisha amani. Rasilimali fedha inayotumika kwa ajili ya kutengeneza, kuboresha na kuhifadhi na hatimaye, kuuza silaha za maangamizi, nyuma yake kuna kilio cha watoto na familia nyingi duniani. Watu wanatamani amani ya kudumu ili kuondokana na vitisho vya silaha za maangamizi na kwamba, hii ni changamoto inayowahusisha watu wote; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuaminiana na wala si katika tabia ya kupimana nguvu. Kuna haja ya kudhibiti biashara ya silaha kimataifa na maendeleo makubwa ya teknolojia kuhusu masuala ya kijeshi. Hii ni dharura inayohitaji kushughulikiwa na viongozi wote wa Jumuiya ya Kimataifa.

Baba Mtakatifu anasema, dunia bila kuwa na silaha za kinyuklia inawezekana kabisa na ni muhimu sana na kwamba, silaha hizi za maangamizi kamwe haziwezi kuwasaidia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika wa usalama wa raia na mali zao kitaifa na kimataifa. Kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu madhara yake katika maisha ya watu sanjari na mazingira; kwa kuondoa hofu, mazingira ya kutoaminiana, chuki na uhasama vinavyozungumza “dhana ya silaha za nyuklia”. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linasema amani ni safari ya matumaini, mwaliko kwa wananchi wa Japana kuendelea kuwajibika kulinda na kudumisha amani, umoja na udugu wa kibinadamu unaofumbata majadiliano katika ukweli na uwazi. Maaskofu wanawataka watu wa Mungu nchini Japan kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya amani, ili amani ya Kristo iamue miyoni mwao.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Katiba ya Kitume “Fidei depositum” iliyoridhia kuchapishwa kwa Katekisimu ya Kanisa Katoliki anasema, Katekisimu ya Kanisa Katoliki inakazia kwamba, hatima na kiini chote cha mafundisho ya imani vinaelekezwa katika upendo ambao hauna kikomo. Iwe inaelekezwa kwa ajili ya ukweli wa imani au, matumaini au wajibu wa utendaji wa maadili, upendo wa Mungu utadumu daima.  Kanisa kwa kusoma alama za nyakati, linataka kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na uhai wa binadamu dhidi ya adhabu ya kifo inayokumbatia utamaduni wa kifo. Mwenyezi Mungu anawapatia waja wake nafasi ya kutubu na kumwongokea, ili aweze kuwakirimia msamaha na kuwaonjesha tena huruma na upendo wake usiokuwa na kifani! Papa Francisko anasema adhabu ya kifo haikubaliki kwa sababu inadhuru haki na utu wa mtu. Haitoi nafasi ya mtu kujitetea mbele ya vyombo vya sheria. Kutokana na mwelekeo huu Kanisa linawataka viongozi wa Serikali kusimama kidete kulinda na kutetea uhai wa binadamu kama ambavyo inafafanuliwa kwenye kipengele cha 2265 na 2266.

Baba Mtakatifu Francisko anafafanua kwamba, hapa hakuna kinzani na Mafundisho ya Kanisa yaliyopita, kwani jambo la msingi ni kusimama kidete kulinda uhai wa binadamu tangu pale anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika mtu kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni mwendelezo wa uelewa wa kina wa Mafundisho tanzu ya Kanisa kwani, adhabu ya kifo ina madhara makubwa kwa utu na heshima ya binadamu. Hivyo, Kanisa katika mafundisho, maisha na ibada zake, linaendelea daima na kuvirithisha vizazi vyote ukweli juu yake, na juu ya yale anayoyaamini. Huu ni muhtasari wa asili na utume wa Kanisa unaofafanuliwa katika mafundisho na maisha yake, kama chachu muhimu inayowaunganisha na kuwawezesha waamini kuwa ni watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, “Amana ya imani” ni endelevu kama lilivyo pia Neno la Mungu, linalokuwa na kuendelea kukomaa katika maisha ya waamini na kamwe haliwezi kudumazwa na binadamu kama anavyobainisha Mtakatifu Vincent wa Lèrins kwani hii ni sehemu ya ukweli mfunuliwa unaotangazwa na kurithishwa na Mama Kanisa na wala si mabadiliko ya Mafundisho tanzu ya Kanisa, kwani hii pia ni kazi ya Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa.

Kama ilivyokuwa wakati wa Agano la Kale Mwenyezi Mungu ambaye alinena zamani na mababa katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi na sasa anazungumza kwa njia ya Mwanaye Kristo Yesu, mwaliko kwa waamini kuisikiliza sauti hii kwa umakini, ili kuliwezesha Kanisa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu kama ilivyokuwa wakati wa Kanisa la mwanzo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kuhimiza umuhimu wa watu wa Mataifa kudumisha amani. Kanisa linaunga mkono Kanuni ya Sheria ya Kimataifa kuhusu Silaha za Nyuklia, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani. Amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujielekeza zaidi katika kubuni sera na mikakati itakayosaidia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Kunako mwaka 1964, Mtakatifu Paulo VI alishauri kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo kwa Nchi Maskini, ambao ungechangiwa kwa kuchukua sehemu ya bajeti ya serikali mbali mbali kwa ajili ya matumizi ya kijeshi. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutengeneza mazingira ya kuaminiana, kwa sababu hii ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Umefika wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa kujenga na kuimarisha utamaduni wa majadiliano; toba na wongofu wa ndani, ili utamaduni wa uhai, upatanisho na udugu viweze kutawala katika akili na nyoyo za watu. Ifuatayo ni Sala ya Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa ajili ya kuombea amani duniani: Ee Bwana unifanye kuwa chombo cha amani. Palipo chuki nieneze upendo. Palipo na mashaka pawe na imani. Palipo na tumaini pawe na matumaini. Palipo na giza pawe na mwanga. Palipo na huzuni pawe na furaha. Ee Bwana Mungu,unijalie; Nisitafute kufarijiwa bali kufariji Nisitafute kupendwa bali kupenda. Kwani ni katika kutoa ndipo tunapopokea Ni kwa kusamehe ndipo tunaposamehewa. Na ni kwa kufa ndipo tunazaliwa katika uzima wa milele, AMINA.  Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu: kutubu, kuongoka na kujiaminisha mbele yake, ili aweze kuwageuza kuwa ni vyombo vya amani na hivyo kutorudia tena kwenye makosa ya kihistoria.

Maaskofu Katoliki Japan

 

06 August 2020, 14:04