Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 19 ya Mwaka A wa Kanisa. Ujumbe mahususi: Shindeni hofu ya imani na imani, kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 19 ya Mwaka A wa Kanisa. Ujumbe mahususi: Shindeni hofu ya imani na imani, kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. 

Tafakari Jumapili 19 ya Mwaka A: Shindeni Hofu za Imani na Maisha

Kitendo cha Petro kuzama kwa hofu ni mwaliko wa wafuasi wa Yesu kuishinda hofu za imani na hofu za maisha inayoweza kuwapoteza kutoka katika kulishika Neno la Yesu na hivyo kuangamia. Mtumbwi ni alama ya Kanisa lililo daima safarini. Ni mwaliko wa Kanisa kuendelea kuutunza utambulisho wa Kristo ndani yake ili kuyashinda mawimbi na misukosuko katika safari yake ya wokovu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya 19 ya mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (1Fal 19:9a, 11-13a) ni kutoka kitabu cha kwanza cha Wafalme. Ni somo linaloelezea tukio la Eliya kukutana na Mungu katika mlima ulioitwa Horebu. Kilichotokea ni kuwa Eliya alikuwa amemaliza kupambana na manabii wa miungu ya kigeni na kuwashinda katika mlima Karmeli. Tukio hilo lilimjengea uadui mkubwa hadi akatishiwa kuuwawa. Akakimbia kuinusuru nafsi yake lakini pia kukimbia kwake huku kuliashiria pia kukata tamaa. Eliya hakuelewa ni kwa nini baada ya kumtolea Mungu ushuhuda mkubwa namna hii, Mungu hamhakikishii ulinzi wala usalama na tena badala ya kupata sifa machoni pa watu yeye anaambulia vitisho vya kuuwawa. Akafika Horebu mlima wa Mungu akamsubiri Mungu atokee kama alivyokuwa amemwahidi. Ukapita upepo mkali unaopasua milima na miamba lakini Bwana hakuwamo katika upepo huo, likapita tetemeko, ukaja na moto lakini Bwana hakuwapo katika vyote hivyo. Hatimaye ikaja sauti ndogo na ya utulivu, na humo ndimo alimokuwamo Bwana. Naye Eliya kwa kutambua uwepo wa Bwana akajifunika uso wake. Somo hili linatuonesha namna ulivyo utendaji wa Bwana. Ni utendaji wa unyenyekevu, usiotafuta kujionesha au kama tunavyoweza pia kusema, ni utendaji usio wa mbwembwe. Haujipambanui katika mbwembwe bali una njia na namna yake ambayo si mara zote itaendana na matazamio ya kibinadamu.

Somo la pili (Rum 9: 1-5) ni kutoka katika waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika somo hili Paulo anazungumzia suala la Wayahudi kumkataa Kristo na kutokumpokea kama njia pekee ya wokovu. Ni kwa nini wayahudi walimkataa Yesu? Walimkataa kwa sababu kitendo cha Mungu kujifunua kwanza kwao na kuingia nao Agano, akawapa Torati na kuwafanya watoto wake walishindwa kukitafsiri katika mpango mzima wa wokovu. Njia hiyo ya Wayahudi ni njia sahihi ya wokovu lakini ni njia iliyokuwa inasubiri kukamilishwa na ujio wa Kristo.  Kubaki katika njia ya Agano la Kale pekee bila kumpokea Kristo ni kuhatarisha wokovu wao. Mtume Paulo mwenyewe hapo mwanzo alifikiri hivyo na aliwatesa sana wakristo hadi hapo Kristo mwenyewe alipomtokea katika njia ile ya Damasko. Tangu hapo, Mtume Paulo ambaye alijikita kuwa mhubiri wa watu wa Mataifa hakuacha kuwaalika na wayahudi wenzake kumuongokea Kristo. Katika somo la leo Mtume Paulo anaonesha waziwazi kinachomuumiza kuhusu hao ndugu zake wayahudi. Anasema moyo wake unajaa uchungu kwa ajili yao hadi yuko radhi yeye mwenyewe asiokolewe ili ndugu zake wayahudi wapate kumjua Kristo, wamkiri na wapate wokovu. Kwa maneno hayo Mtume Paulo anawasikitia Wayahudi kwa kushindwa kumtambua Kristo. Hapo hapo anawaalika watambue kuwa pamoja na ufunuo wa Mungu waliokwisha kuupata, Kristo ndiye ukamilifu wa ufunuo na ndiye njia pekee ya wokovu. Wampokee.

Injili (Mt 14:12-33) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo.  Inaelezea muujiza wa Yesu kutembea juu ya maji.  Katika tukio hilo, wanafunzi wa Yesu wanapanda mashua na kuanza safari wakati yeye bado yupo mlimani akisali kama ilivyokuwa desturi yake. Anamaliza kusali anawafuata akitembea juu ya maji. Petro anapomtambua na kujihakikishia kuwa ni yeye, anaomba naye atembee juu ya maji. Anaanza kweli kutembea lakini muda tu anazama kwa hofu. Yesu analitafsiri tukio hili kama ukosefu wa imani na anamuuliza Petro, “ewe mwenye imani haba kwa nini ulitia shaka?”. Muujiza huu una alama nyingi zinazoweza kutusaidia kuupatia tafsiri. Tunapoyaangalia maji kama alama ya nguvu za giza na nguvu za uharibifu, kitendo cha Yesu kutembea juu ya maji ni ishara kuwa Yesu yu na nguvu kuliko nguvu hizo za uharibifu zinazowakilishwa na maji. Petro anapoomba na yeye kutembea juu ya maji Yesu anamwambia njoo. Na kwa neno hilo la Yesu Petro kweli anatembea juu ya maji. Yesu hapa anapenda kutuonesha kuwa kwa Neno lake hata wanafunzi wake watakuwa na uwezo wa kushinda nguvu za giza na za uharibifu. Kitendo cha Petro kuzama kwa hofu ni mwaliko wa wafuasi wa Yesu kuishinda hofu za imani na hofu za maisha inayoweza kuwapoteza kutoka katika kulishika Neno la Yesu na hivyo kuangamia. Mtumbwi ni alama ya Kanisa lililo daima safarini. Yesu anapoingia mtumbwini, hapo hapo upepo mkali na mawimbi yanakoma. Ni mwaliko wa Kanisa kuendelea kuutunza utambulisho wa Kristo ndani yake ili kuyashinda mawimbi na misukosuko katika safari yake ya wokovu.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kuyasikiliza na kuyafafanua masomo ya dominika hii ya 19 ya mwaka A wa Kanisa, nawaalika tuielekeze tafakari yetu ya leo katika njia ya imani aliyoipitia nabii Eliya kama tulivosikia katika somo la kwanza. Eliya alifanya mambo makubwa sana kwa ajili ya kuwaonesha Waisraeli yupi ni Mungu wa kwelli. Unabii wake ulijaa alama kubwa kubwa za ushuhuda. Mfano ni ile alama aliyoifanya mlima Karmeli alipowakusanya manabii wa miungu baali akawaambia watengeneze altare na waweke sadaka yao na yeye atengeneze altare aweke sadaka yake waone ni Mungu yupi atakayejibu kwa moto. Namna hii ya kuiishi imani imekuwa pia ni namna ya Wakristo walio wengi. Wengi wamekuwa ni wakristo wa kutafuta ishara, miujiza, utukufu na mambo mengine kama hayo. Namna hii pia imewaingia baadhi ya viongozi wa dini na wahubiri. Matokeo yake Makanisa yanaanza polepole kugeuzwa kuwa ni mahala pa kuonesha miujiza na ishara nyingine nyingi za kuvutia hisia za watu. Badala ya wahubiri kumtangaza Kristo, zimetangazwa zaidi ahadi za kupokea utajiri, uponyaji na miujiza.

Leo, katika somo letu la kwanza, Mwenyezi Mungu anapoamua kujitokeza kwa Eliya anaamua makusudi mazima kwanza kupitisha mbele yake upepo mkali unaoweza kupasua milima na miamba. Lakini yeye hawi katika upepo huo. Anapitisha pia tetemeko lakini hawi katika hilo tetemeko. Anapitisha moto uwakao lakini pia hawi katika moto huo. Badala yake anakuwa katika sauti ndogo na ya utulivu.  Humo katika sauti ndogo isiyoleta hamaki wala taharuki na tena sauti ya utulivu kabisa ndimo Mungu anakuwamo. Anamwonesha Eliya na kutuonesha nasisi pia kuwa hiyo ndiyo namna ya kujifunua kwake Mungu. Kumbe nasi tunapomtafuta Mwenyezi Mungu katika sala na maombi au nasi tunapomhubiri na kumtangaza kwa wengine tuyafanye yote hayo kwa huo utulivu anaopenda yeye mwenyewe kujifunua kwetu. Tusizikimbilie ishara, tusitafute maajabu, tusitangaze “mbwembwe”. Tujivike namna hiyo ya Mungu na yeye akipenda kututendea ishara atatenda kwa wakati wake.

Jumapili 19 ya Mwaka A wa Kanisa
07 August 2020, 14:13