Vatican News
Tangu mwanzo wa maisha na utume wake, Kanisa limepitia vipindi vigumu na mawimbi mazito katika maisha na utume wake: Jambo la muhimu ni kutambua uwepo endelevu wa Kristo ndani ya Kanisa. Tangu mwanzo wa maisha na utume wake, Kanisa limepitia vipindi vigumu na mawimbi mazito katika maisha na utume wake: Jambo la muhimu ni kutambua uwepo endelevu wa Kristo ndani ya Kanisa.  (AFP or licensors)

Tafakari Jumapili 19 ya Mwaka A wa Kanisa: Kanisa na Mawimbi Mazito!

Ndani ya mashua kuna Mitume wenye uzoefu na mang'amuzi ya mapungufu yao ya kibinadamu, wasi wasi na mashaka, lakini kwa pamoja wanajisikia wamoja katika imani wakimzunguka Yesu Kristo. Hii ndiyo sura ya Kanisa ambalo halina budi kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha. Imani inawahakikishia waamini uwepo endelevu wa Kristo katika maisha yao! Imani thabiti!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Muktadha wa somo la Injili ya leo unatokana na muujiza ule wa Yesu kuwalisha makutano mikate ile mitano na samaki wawili, wakala wakashiba na hata kusaza vikapu kumi na viwili. Ni Injili tuliyotafakari Dominika iliyopita kutoka Mwinjili Mathayo 14:13-20. Ni baada ya kuwalisha leo Yesu anawaaga makutano na pili anawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo. Yafaa tangu mwanzo kuweka wazi kuwa tukiisoma sehemu hii ya Injili kama masimulizi ya matukio ya kihistoria hapo tutajikuta tunabaki na maswali mengi na tena magumu kupata majibu yake. Kwa nini Yesu anawalazimisha waende peke yao bila yeye kuwepo pamoja nao? Ilishakuwa jioni au usiku kulikuwa na ulazima gani wa kuwaamuru kupanda chomboni na wapi hasa walipaswa kwenda kwa kumtangulia? Na hata kwa wanaolifahamu ziwa lile Galilaya bado tunajiuliza ni kwa nini iliwachukua usiku mzima kutoka ng’ambo moja kwenda ng’ambo ya pili? Petro anamuomba Yesu atembee naye juu ya maji, na anajikuta anaomba msaada kutoka kwa Yesu ambaye yawezekana kabisa hakuwa anajua kuogelea kama Petro aliyezaliwa maeneo yale ya ziwani. (Yohane 21:7)

Ni kutokana na maswali ya namna hii tunaalikwa kuona kuwa Mwinjili Matayo hapa hakuwa na nia ya kutupa masimulizi ya muujiza wa kihistoria uliojiri na kutokea siku zile bali nyuma yake ni mafundisho ya kiteolojia anayotualika kuyachota kutoka simulizi hili. Ni simulizi lenye lugha ya picha ili kupata ujumbe kusudiwa kutoka kwa Mwinjili Mathayo. Ilikuwa jioni au pale anaposema zamu ya nne ya usiku, ndio kusema wakati kungali bado giza; usiku katika Maandiko ni wakati ule wa giza pasipokuwa na mwanga wala nuru. Usiku unabeba hasa maana hasi, ni sawa na kusema saa ile mwanadamu anaposafiri bila uwepo wa Mungu pamoja naye, anapokuwa mbali na Mungu, ni wakati wa mateso na mahangaiko makubwa. Kilio cha mzaburi saa ile ya usiku; Zaburi 22:2 ‘’Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu; napiga yowe usiku, lakini nafuu sipati’’. Ni saa ngumu na mateso kwa mwanadamu, ni saa ya kilio na mayowe kama asemavyo Mzaburi na ndio saa ya madhulumu na nyanyaso ya kila aina kwa wafuasi wake Kristo. Ni saa ambayo kwa hakika kila mmoja katika safari yake ya ufuasi anakutana nayo.

Ni saa ambayo kila mmoja wetu katika uduni na udhaifu wetu tunatamani kuiepuka na ndicho haswa walichofanya Mitume na wafuasi wa Yesu wa nyakati zile. Tunasikia leo Yesu anawalazimisha kupanda chomboni na kumtangulia kwenda ng’ambo. Linatumika neno ‘’aliwalazimisha’’ sio kwa ajali bali ndio neno haswa linalobeba maana katika tafakari yetu ya leo. Ni baada ya kula na kushiba na hata kusaza walitamani wabaki katika hali ile daima, katika wakati ule wa shibe na furaha, hali ya kutopungukiwa wala mateso, ni hali ambayo mara nyingi mimi na wewe tunaipenda na kuona inafaa katika safari yetu ya ufuasi.  Vilibaki vikapu kumi na viwili baada ya muujiza ule wa kuwalisha mikate na samaki, ni zamu yao sasa kila mmoja kutwaa kikapu kimoja na kwenda ng’ambo, ni zamu ya utume na utumishi tunayoitiwa nayo kila mmoja wetu baada ya kukutana na Kristo Mfufukata katika meza ile ya Neno na Mwili na Damu yake Azizi. Ni wito wa kuwa mashuhuda wa Kristo Yesu baada ya kukutana naye, ni utume tunaopewa sisi sote wabatizwa kupanda chomboni na kwenda ng’ambo. Daima tunaalikwa na kulazimishwa kupanda chomboni, chombo hapa sio mashua au mtumbwi bali ni Jumuiya ya wanakanisa, ndio kusema kutenda na kufanya yote pamoja na Jumuiya ya Kanisa, kadiri ya mafundisho ya Kanisa yatokanayo na Neno la Mungu kwa nafasi ya kwanza na mapokeo ya Mababa wa Kanisa. Utume wa Kristo mfufuka sio jambo langu binafsi bali ni utume wa Kanisa zima ninaoalikwa kuushiriki na kuutelekeza.

Yesu hakuwa nao kimwili chomboni ndio kusema giza likazidi kuwa kubwa na hata upepo wa mbisho. Yesu badala yake anapanda mlimani faraghani, ndio kusema anajitenga na Kanisa lake, hayupo tena kimwili pamoja nao, ni saa ile ya kupaa kwake mbinguni, saa ambapo wanafunzi wanabaki na hofu na mashaka makubwa ya kusafiri wenyewe bila uwepo wa kimwili wa Bwana na Mwalimu wao. Ni saa ile baada ya mateso na kifo wanabaki na mashaka na wasiwasi mkubwa na hata kujifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi. Giza na upepo wa mbisho ndio hali wanayokuwa nayo wafuasi wa Yesu pale wanaposhindwa kutambua uwepo wa Kristo kati yao. Ndio hali ambayo hata nasi tunajikuta nayo mara nyingi kwa kushindwa kwetu kuutambua uwepo wa Kristo mfufuka pamoja nasi katika Neno lake, Kanisa lake na kwa njia ya pekee katika Sakramenti za Kanisa alizotuachia. Ni saa ya giza pale hata wale wenye imani wanapojikuta katika mateso na shida kubwa katika maisha yao ya ufuasi na kiasi cha kumlilia Mungu na kupiga mayowe. Ni haki kabisa kulia na hata kupiga mayowe kuomba msaada na uwepo wake maana tunajua tukibaki peke yetu hatuwezi kitu kamwe, hatuwezi kulishinda lile giza wala upepo ule wa mbisho.

Mtume Paulo anawaandikia Waefeso 4:14 ‘’Basi, hatutakuwa tena kama watoto, tukitupwa na kupeperushwa huko na huko kwa kila upepo wa mafundisho wanayozua watu wadanganyifu ili wawapotoshe wengine kwa hila’’ Ndio kusema upepo hapa yawezekana pia ukawa ndio mafundisho yale yanayokuwa kinyume na Kristo Mfufuka. Tupo katika ulimwengu ambapo ukweli hausimami tena wenyewe bali kila mmoja wetu ni ukweli, ndiye chanzo ndiye mwamuzi wa nini cha kweli na nini sio cha kweli. Ulimwengu ambapo hautaki tena Mungu awe ndio ukweli wetu wa kutuongoza katika maisha yetu, ni kibuli cha akili zetu na mantiki zetu za kibinadamu na utaalamu wa kisayansi na kiteknolojia. Kama Mtume Paulo anavyowaasa na kuwasisitiza wakristo wale wa Efeso kuwa sisi sio tena watoto kuanza kuyumbishwa na upepo huo wa mafundisho bali tubaki imara katika Injili. Leo kuna wimbi la waamini wakatoliki wanaoyumbishwa na mafundisho ya uongo, wanaozunguka na kumaliza kila kikundi na kusahau kuwa Kanisa la Kristo ni Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume.

Hakuna hata mmoja anayetumwa kupanda chomboni au kwenda peke yake bali wito na utume wetu ni ule wa Kanisa zima na hivyo hatujitumi bali tunatumwa na Kristo mwenyewe kwa njia ya chombo chake yaani Kanisa. Mafundisho yetu sio matashi ya mtu mmoja mmoja bali ya Kristo mwenyewe kwa njia ya Kanisa lake.Maji hasa katika Agano la Kale, ni ishara ya umauti na kifo. Tunasoma mzaburi pale alipoathirika na maradhi makubwa ambayo yangeliweza hata kumpelekea kupoteza uhai wake anasali na kuomba, Zaburi 144:7-8 ‘’Unyoshe mkono wako kutoka juu, uniokoe na kuniondoa katika maji haya mengi; uniondoe makuchani mwa wageni, ambao husema maneno ya uongo, hunyosha mkono kushuhudia uongo’’ Na hii tunaisoma pia katika Zaburi 18:4,16 ‘’Kamba za kuzimu zilinizunguka, mitego ya kifo ilinikabili…Mungu alinyosha mkono kutoka juu akanichukua, kutoka katika maji mengi alininyanyua’’. Lakini Mwenyezi Mungu anawaahidi watu wake kutokuwaacha na daima kuwa nayo hata wanapopita katika bonde lile la uvuli wa mauti. Isaya 43:1-2 ‘’…Msiogope…mkipita katika mafuriko, mimi nitakuwa pamoja nanyi…’’ Ni Mungu anayekuwa pamoja na watu wake nyakati zote iwe zile nyepesi lakini pia hata wakati wa mapito magumu na yenye kuogofya Mungu anabaki kuwa mwaminifu hakuna hata saa moja hatakuwa mbali nasi.

Maji kwa Wayahudi yalikuwa ni ishara ya kifo na umauti, ni ishara ya yule muovu na nguvu zake, hivyo Mwinjili anapotumia ishara hii hatuna budi kuelewa sasa ujumbe kusudiwa kwetu kwa wasikilizaji wa Injili hii. Wanafunzi waliogopa maji na upepo wa mbisho, waliogopa hatari kubwa itokanayo na yule muovu na nguvu zake, ni jumuiya ya waamini anayowaandikia Mwinjili Matayo baada ya miaka zaidi ya hamsini baada ya ufufuko wake Kristo, ni jumuiya iliyokuwa ikipitia magumu na mateso na mahangaiko mengi kiasi cha kupoteza imani kwani walikosa kuutambua uwepo wa Kristo mfufuka katikati yao. Chombo kilikuwa kinaatabika katikati ya bahari. Kitenzi kinachotumika hata kutoka lugha ya Kigiriki ni ‘’basanizo’’, kikiwa na maana hasa ya kupitia majaribu au vishawishi, ndio hali ya Kanisa lile la mwanzo na hata leo katika nyakati zetu kuna mahali tunajikutaka kama Kanisa na hata kama mwamini mmoja mmoja. ‘’Basanos’’ neno la Kigiriki likiwa na maana ya jiwe gumu lilitumika katika kujaribu kuona kama chuma kimeiva kweli au la, hivyo kilipigwa kwa nguvu sana kwa kutumia jiwe hilo. Ni kipimo cha uimara wake wa chuma, na ndio tunaona pia hata maisha yetu ya imani na ufuasi daima tutapitia magumu mengi ili kupima uimara na ubora wetu wa urafiki wetu kwa Mungu na kwa jirani.

Mawimbi yalikitaabisha chombo kile, na kwa kweli hakuna hata wakati mmoja ambapo Kanisa halijapitia misukosuko ya kila aina. Hata mwanzo kabisa wa uwepo wake tayari tunaona lilipitia magumu na mateso makali kabisa sio tu kutoka nje yake bali hata ndani yake, na hata leo tunaona Kanisa bado halijawahi kukosa kutaabishwa na mawimbi ya kila aina. Ni kwa kukosa kwetu kutambua uwepo wa Yesu katikati yetu katika Neno lake na masakramenti yake na kwa namna ya pekee katika maumbo yale duni kabisa ya Mkate na Divai anabaki akisafiri pamoja nasi. Yesu anabaki nasi katika tabernakulo za makanisa yetu, ni mara ngapi tunasaka nafasi ya kwenda na kukaa mbele yake na kuongea na kumwambia yote yanayotusonga katika maisha yetu iwe mtu binafsi, maisha ya ndoa na familia, maisha ya jumuiya zetu, maisha ya kikazi na shughuli zetu za kila siku, mahusiano yetu na Mungu na hata wenzetu, magumu yetu ya kila aina. Leo hatuna sababu ya kusafiri umbali mrefu ili tukaonane na Kristo Mfufuka kwani yupo katika makanisa yetu iwe ya parokia au yale ya jumuiya, yumo katika maumbo yale ya mkate na divai, yumo katika ukimya na tafakuri na faragha, tujifunze kukutana na Yesu faraghani!

Tabernakulo ni faraghani, ni mahali ambapo tunaweza kukutana na Yesu na kumuangalia na kuongea naye, ila hatuna budi kujifunza kujadiliana naye hivyo sisi tuongee ila tumpe nafasi naye aongee nasi, ni katika kusikiliza zaidi tunaweza kupata majibu ya maswali na magumu yetu. Ni kwa kusikiliza tunakuwa wanafunzi maana mwalimu wetu ni Kristo mwenyewe. Ni katika kusikiliza Mungu ananena nasi! Ni mwaliko wa kujifunza kuwa faraghani, faraghani ni sehemu ya kuwa wenyewe bila uoga kwani ni Mungu pekee anayetuona sirini anapata nafasi ya kujadiliana na kila mmoja wetu. Inapokuwa zamu ya nne ya usiku ndio kusema kunapokaribia alfajiri Yesu akawaendea juu ya maji. Ni Yesu pekee aliye mshindi wa yule muovu shetani na nguvu zake. Ni Yesu anayetembea juu ya huyo muovu na nguvu zake, ni Yeye anayetuhakikishia usalama wetu. Wanafunzi kama siku ile ya ufufuko wanashindwa kumtambua na kudhani kuwa wanaona kivuli, ndio maana walibaki kuwa katika giza nene la kiimani, ni giza la kushindwa kumtambua Kristo, kushindwa kuuona uwepo wake katika maisha yetu na kwa namna ya pekee ugumu wa kumtambua Yesu anayekuja kwetu kila siku katika maumbo yale ya mkate na divai, yaani Ekaristia.

Mwinjili Mathayo katika somo la leo sio lengo lake kutupa masimulizi ya kihistoria bali ni katekesi iliyojaa utajiri mkubwa wa Kitaalimungu. Ndio hali ya jumuiya ile ya waamini waliyokuwa wanaipitia nyakati zile, nyakati ngumu na za majaribu, nyakati za misukosuko ya upepo na mawimbi ya bahari. Kushindwa kuutambua uwepo wa Kristo mfufuka katikati yetu hapo tunabaki kumwona kama kivuli na kubaki katika mashaka na wasiwasi mkubwa. Luka 24:37 ‘’Wakashtuka na kushikwa na hofu wakidhani wameona mzimu’’ Sio kwa macho ya nyama tunaweza kumuona na kumtambua Kristo mfufuka isipokuwa kwa macho tu ya imani. Ni kwa msaada wa neema zake nasi tunaweza kukua kiimani na kuweza kuutambua uwepo wake na hivyo kuwa na hamu na shauku kila mara ya kwenda na kukutana naye katika Neno lake na pia na kwa namna ya pekee katika maumbo yale duni kabisa ya mkate na divai, yaani Mwili na Damu yake Azizi. Sehemu ya mwisho ya somo la Injili ya leo ni mazungumzo ya Yesu na mwanafunzi yule Mtume Petro. Ni Mtume Petro bado katika hali ya mashaka anaweka ombi lake kwa Bwana, ‘’Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji’’ (Aya 28) Kwa anayechukulia tukio hili kama simulizi la kihistoria anaweza kupata ugumu wa ombi la Mtume Petro ila kwa kutambua nafasi ya Petro kama wakili wa Kanisa lake Kristo, kwa nafasi yake naye anaomba anywee kikombe kile cha wokovu kwa nafasi ya kwanza, yaani kukubali kubeba msalaba na hata kufa kwa ajili ya Kristo na Injili.

Ni ombi la kuwa tayari kutoa maisha yake kwa nafasi ya kwanza, lakini Petro anashindwa kutembea juu ya maji kwani badala ya kumkazia macho Kristo anayemwita anakazia macho maji, mawimbi na upepo. Hata nasi kila mara kama kweli tunataka kumfuasa Kristo hatuna budi kumkazia macho Yesu anayetuita na kamwe isiwe misukosuko na mawimbi katika maisha ya ufuasi. Ni kwa kumkazia macho Yesu hapo imani yetu inaimarika na kukua, ila kila tunapokazia macho malimwengu na nguvu za yule muovu hapo imani yetu inajikuta ikitaabika na kuyumbishwa na kujikuta tunaanza kuzama katika bahari ya yule muovu na uovu.  Kristo mfufuka anamwambia kila mfuasi wake; ‘’Njoo’’. Na analisema hili hata tunapopitia nyakati ngumu na zenye kuogofya katika maisha yetu. Ni wito katika Dominika hii ya leo kuwa Kristo Mfufuka anamuita kila mmoja wetu kwenda kwake na hivyo salama yetu inapatikana pale tunapomtambua na kumkazia macho yeye peke yake. Ni kwa kumtambua na kumkazia macho tunaweza kama chombo yaani Kanisa kuvuka salama na kwenda ng’ambo ya pili yaani kwenye maisha ya heri na umilele, maisha ya kuunganika na Mungu. Nawatakia Dominika na tafakari njema.

08 August 2020, 07:56