Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili 21 ya Mwaka A wa Kanisa: Ukulu wa Mtakatifu Petro na Kiri ya Imani inayojenga mahusiano ya dhati kabisa na Kristo Yesu. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili 21 ya Mwaka A wa Kanisa: Ukulu wa Mtakatifu Petro na Kiri ya Imani inayojenga mahusiano ya dhati kabisa na Kristo Yesu.  (Vatican Media)

Tafakari Jumapili 21 ya Mwaka A. Ukulu wa Mt. Petro: Kiri ya Imani

Masomo ya leo yanatufundisha juu ya Ukulu wa mtume Petro umejikita katika kumjua na kumkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai kwa ufunuo wa Mungu Baba na kwa sababu hiyo Kanisa likajengwa juu yake.. Yesu akawauliza wanafunzi wake; Je, nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Nasi swali hili litusaidie kumtambua Kristo ni nani katika maisha yetu ya sasa na yajayo.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa radio Vatikani, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 21 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya leo yanatufundisha juu ya Ukulu wa mtume Petro umejikita katika kumjua na kumkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai kwa ufunuo wa Mungu Baba na kwa sababu hiyo Kanisa likajengwa juu yake. Haya yanatokea baada ya Yesu kuwauliza wanafunzi wake; Je nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Nasi swali hili litusaidie kumtambua Kristo ni nani katika maisha yetu ya sasa na yajayo. Katika somo la kwanza, Nabii Isaya anamlaumu Shebna, mtunza hazina, na anatabiri kuwa Mungu ataweka funguo mabegani mwa Eliakimu mwana wa Hilkia naye atashika kazi ya Shebna na kuchukua nafasi yake, atapewa funguo za kufunga na kufungua milango ya nyumba ya Mungu. Huu ni utabiri unaotimia kwa kusimikwa kwa Kanisa juu ya Mtume Petro Khalifa wa Yesu Kristo. Maneno haya “kupewa funguo” ni ishara ya mamlaka anayokabidhiwa mwanadamu na Mungu kwa mambo yamhusuyo Mungu ndiyo yanatumiwa na Yesu katika Injili ya domenika hii kuonyesha ukulu wa mtume Petro katika kukabidhiwa madaraka ya kuliongoza Kanisa.  Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake kwa Warumi anaisifu na kuitukuza hekima ya Mungu inayopita ufahamu wa kibinadamu. Hekima hii inajionyesha kwa kuwaokoa watu wote wayahudi na wasio wayahudi kwa njia ya mwanae mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo.

Mtume Paulo anatuambia; Ni hekima ambayo watawala wa dunia hii hawakuielewa; maana wangaliielewa hawangalimsulibisha Bwana wa utukufu (1Kor 2:8). Akionyesha umuhimu wa kumjua Mungu. Kristo alisema; na uzima wa milele ndio huu: kukujua wewe uliye peke yako Mungu wa kweli; na kumjua Yesu Kristo uliyemtuma (Yoh 17:3). Injili ilivyoandikwa na Mathayo inasimulia jinsi Petro alivyoungama wazi kuwa Yesu ni Masiya, Mwana wa Mungu aliye hai na kwa sababu ya imani hiyo Yesu anampa mamlaka ya kuwa kiongozi wa Taifa Jipya teule la Mungu yaani Kanisa na kumkabidhi funguo kama alama ya ukuu, mamlaka na utumishi wake. Mamalaka haya ndiyo anayonakuwanayo kila Baba  Mtakatifu anayechagualiwa kuliongoza Kanisa kwani ni halifa wa Mtume Petro. Kiri ya imani ya Petro kuwa Yesu ni mwana wa Mungu aliye hai ni ufumuo wa Mungu kwa mwanadamu ndiyo maana Yesu anamwambia; heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala mifunguo ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.

Historia inaonesha kuwa Kaisaria-Filipo palikuwa na miungu wengi wa Kigiriki, na wa Siria na Herode Mkuu alikuwa amejenga hekalu kubwa kuonesha umungu wa Kaisari kama shukrani kwa Kaisari wa Roma baada ya kuwa amemwongezea Herode eneo hilo alitawale. Filipo mtoto wa Herode aliongezea jina lake pakaitwa Kaisaria-Filipo. Eneo hili lilikuwa na miungu wengi wa asili. Yesu akiwa katika eneo hili la Kaisaria Filipo anawauliza wanafunzi wake swali; watu wanasema mimi ni nani na kisha anawauliza wao; na ninyi je, mwasema mimi ni nani? Msingi wa hili swali ni kujua kama watu wengine pamoja na wanafunzi wake wamekuwa na uelewa kuwa yeye ni nani na mafundisho yake juu ya ufalme wa Mungu ulivyo tofauti na falme za miungu mingine. Swali hili ni la maana sana kwa sababu kujua ndio msingi wa mambo yote. Huwezi kupenda wala kuamini usichokijua. Lazima kwanza watu wamjue Kristo ndipo wamwamini na kumpenda. Paulo anasema “Basi watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena watamwaminije kama hawajapata kumsikia?” (Rom 10:14). Hii haimaanishi kwamba kwanza tujue kila kitu kuhusu Mungu ndipo tumwamini; hapana. Hii haitakuwa imani tena. Lakini tunahitaji walau kujua kuwa kuna Mungu, tunajua – tunaamini –na tunasoma ili kuelewa zaidi juu ya imani yetu.

Kujua ni msingi wa mahusiano jinsi tunavyofahamu mtu au kitu ndivyo tutakavyohusiana nacho. Iwapo tunajua kuwa kitu fulani ni kibaya tutakiepa. Ukikielewa vizuri kitu basi utahusiana nacho vizuri; usipokielewa vizuri mahusiano yako na kitu hicho hayatakuwa ya kweli. Ndiyo maana wanaotaka kuoana wanajitahidi kujuana kwanza. Kumbe tunavyomjua Yesu ndivyo tunavyohusiana naye. Ni muhimu sana kujua Yesu ni nani ndipo utajua namna ya kuhusiana naye. Wayahudi hawakumuelewa Yesu ni nani. Mwanzoni walimuona kama mfalme na mkombozi wao kutoka na maadui zao, baadae wakamwona kama mwanaharakati na mwana mapinduzi na mpinzani wa kisiasa mwisho wakamwona kama mhalifu na wakaamua kumuua kwa kumtundika Msalabani. Kumbe, hata katika maisha ya kawaida ukijua kuwa Yesu ni Mungu anaweza yote, utamkabidhi maisha na mahangaiko yako. Ukijua kuwa Yesu ni Mungu anajua yote hutamdanganya. Ukijua kuwa Yesu ni Mungu na Mungu ni upendo na anatupenda, utamwamini na kumtegemea katika shida zako zote. Ukijua kuwa Yesu ameukomboa ulimwengu kwa msalaba, hutakimbia mateso katika maisha yako. Ukijua kuwa Yesu ni Mungu na kwa Mungu siku moja ni kama miaka elfu na miaka elfu ni kama siku moja hutakata tamaa hata ikionekana kuwa sala zako hazijibiwi haraka maana unaelewa kuwa Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake (2Pet 3:9).

Lakini ukidhani kuwa utawala wa Kristo ni wa hapa duniani utamwomba ukae mkono wa kulia au wa kushoto katika utawala wake kama wana wa Zebedayo ili upate sifa na utajiri hapa duniani bila kushughulikia maisha ya kiroho. Ukidhani kuwa Yesu ni ATM utamwomba na kutaka akutimizie hapo hapo kama ATM. Hutakuwa mvumilivu. Usipojua kuwa Kristo alisema anayetaka kunifuata lazima abebe msalaba wake, utakimbia mateso katika maisha. Usipojua Kristo anaongea namna gani utasikiliza sauti nyingine zinazokuita na utapoteza maisha yako na kujuta baadaye kama Mtakatifu Augustino nimechelewa mno kukujua wewe ee Bwana. Funguo zinaashiria mamlaka na majukumu aliyopewa Mtume Petro kama kiongozi wa Kanisa. Lakini pia sisi kama Wakristo kwa ubatizo, tukiwa chini ya Baba Mtakatifu, tunashiriki katika hizo funguo yaani katika jukumu la kuwafunguliwa watu ufalme wa mbinguni yaani kuwapatia habari njema, kuwafundisha maisha ya kumfuasa Yesu kwa mifano mema ya maisha yetu. Ili tuweze kuwafundisha watu vizuri Yesu ni nani, lazima sisi wenyewe tumjue.

Hatuwezi kumfundisha Kristo kwa watu ikiwa kama sisi hatumjui. Tutambue kuwa tukizishikilia funguo tulizokabidhiwa bila kuwafungulia wengine waingie tutalinganishwa na Mafarisayo aliowalaumu Kristo akisema. Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnawafungia watu mlango wa wa ufalme wa mbinguni. Ninyi wenyewe hamuingii ndani, wala hamuwaruhusu wanaotaka kuingia waingie” (Mt 23:13-14). Tutambue pia kumjua Kristo sio rahisi. Mtume Paulo ametwambia katika somo la pili anasema; Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani! Maana ni nani aliyeijua nia ya Bwana? Kumbe, ili kumjua vyema Kristo lazima tuwe na imani ya kupokea ufunuo wa Mungu unaotolewa kupitia Maandiko Matakatifu, mafundisho ya Mababa wa imani, sala na tafakari binafsi. Lakini pia utambuzi binafsi ni wa muhimu katika imani. Ifike wakati usimjue Yesu kwa jinsi tu unavyosikia au unavyofundishwa au unavyosoma katika vitabu bali kwa jinsi ya maisha yako. Ndiyo maana tunasoma katika injili ya Yohane; Pilato akaingia tena ndani ya ikulu, akamwita Yesu na kumuuliza: Ati wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi? Yesu akamjibu: Je, hayo ni maneno yako mwenyewe, au wengine wamekuambia habari hiyo juu yangu? (Yn 18:34). Hata Yesu hakuridhika na majibu ya Mitume kuhusu jinsi watu wanavyosema; alitaka kujua wao binafsi ambao ameishi nao; wameona aliyoyatenda wametambua yeye ni nani?

Utambue kuwa mkristo sio kujua kuhusu Kristo bali kumjua Kristo. Kumtambua Kristo hakutegemei kwenda darasani. Unaweza ukapata madigrii ya taalimungu lakini ukawa hujamtambua Kristo. Unaweza kufahamu mengi kuhusu Kristo lakini usimfahamu Kristo. Yesu amemwambia Mtume Petro Mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye Mbinguni. Hii inahitaji unyenyekevu. Ndivyo, tulivyoimba katika Shangilio. Kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili ukawafunulia watoto wachanga. Katika wimbo wa katikati tumeimba Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu. Naye amjua mwenye kujivuna. Kristo anawafunulia wanyenyekevu siri za mbingu ili waweze kutambua nguvu za Mungu katika maisha yao na hivyo kuwa imara hata katika mateso. Hivyo, tunaalikwa kuwa watu wa tafakari juu ya matendo ya Mungu katika maisha yetu. Tuwe watu wa sala na kumkabidhi Mungu njia zetu ili ajifunue yeye ni nani na atuongoze katika kila jambo. Kila mara ujiulize Yesu ni nani kwangu?

21 August 2020, 07:31