Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu Kanda ya Tanzania, tarehe 8 Agosti 2020 wamefanya kumbukizi la Miaka mitano tangu walipozundua kanda ya Tanzania. Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu Kanda ya Tanzania, tarehe 8 Agosti 2020 wamefanya kumbukizi la Miaka mitano tangu walipozundua kanda ya Tanzania. 

Wosia wa Askofu Isuja Kwa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Tanzania

Katika kumbukizi la Miaka mitano tangu kuanzishwa kwa Kanda ya Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Hayati Askofu Mathias J. Isuja wa Jimbo Kuu la Dodoma katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Miaka 50 ya Uwepo wake nchini Tanzania aliwapatia wosi maalum! Leo wanakumbushwa tena wosia huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Akiongozwa na tafakari ya kina juu ya: Huruma na Upendo wa Mungu ambao umefunuliwa kwa mwanadamu kwa njia ya Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu, Mtakatifu Gaspari Del Bufalo tarehe 15 Agosti, 1815 alianzisha Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S. Mtakatifu Gaspari alipenda kujua lugha elfu ili kuwafikishia watu wote ulimwenguni, Habari Njema ya Wokovu kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda wote. Damu Azizi ya Yesu ndiyo msingi na chemchemi ya maisha ya kiroho, kijumuiya na kitume ya Wamisionari hawa. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Miaka 50 ya Uwepo wake nchini Tanzania, tarehe 8 Agosti 2015, Shirika likazindua Kanda ya Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania.

Mwaka 2020, Kanda ya Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu inafanya kumbukizi la miaka mitano tangu kuanzishwa kwake. Padre Vedasto Ngowi, C.PP.S., Mkuu wa Kanda Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi nchini Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, leo hii Shirika lina wamisionari 87 wanaojisadaka katika maisha na utume wa Shirika na Kanisa ndani na nje ya Tanzania. Seminari kuu ya Mtakatifu Gaspari Morogoro ina jumla ya Majandokasisi 49. Mafrateri waliohitimu malezi mwaka wa kwanza ni 10 na sasa wako tayari kuanza masomo ya falsafa. Waliohitimu malezi ya mwaka pili ni 5, nao wako tayari kuanza masomo ya taalimungu. Hii ndiyo rasilimali watu inayopaswa kuendelezwa kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania, daima kwa kusoma alama za nyakati na kuendelea kuwa waaminifu kwa karama ya Shirika ambayo kimsingi ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa.

Kwa muda wa zaidi ya miaka 50 ya uwepo na utume wao nchini Tanzania, Wamissionari wa C.PP.S., wamekuwa kweli ni mashuhuda wa upatanisho unaobubujika kutoka katika tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo Yesu, dhamana wanayoitekeleza kwa njia maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa na huduma makini kwa familia ya Mungu nchini Tanzania hususan katika sekta elimu, afya, mawasiliano, maji na huduma kwa maskini na ustawi wa jamii. Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S. wakisukumwa na kauli mbiu ya: Elimisha, Tibu na Fariji walianza rasmi kutoa huduma za afya Itigi, Manyoni, Singida nchini Tanzania 15 Septemba 1987. Lengo kuu likiwa ni kutoa huduma kwa maskini na wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Nia hii njema ilizidi kukuwa na baada ya miaka miwili huduma ilipanuka na hivyo kufunguliwa rasmi kwa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, na Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Tanzania awamu ya Pili hapo tarehe 15 Mei 1989.

Kunako mwaka 2000 uongozi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu uliamua kupanua wodi ya watoto iliyokuwa na vitanda 45 na kufikisha vitanda 150. Hii ilitokana na ukweli kwamba, kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Juni ya kila mwaka kutokana na ugonjwa wa malaria na upungufu wa damu, Hospitali ya Mtakatifu Gaspar hupokea watoto wagonjwa wengi sana. Hivyo hitaji hili lilipelekea kujenga wodi hii mpya ambayo ilifunguliwa rasmi tarehe 23 Novemba 2003 na Hayati Benjamini William Mkapa, Rais wa Serikali ya Awamu ya tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa zaidi ya Miaka 30 ya uwepo wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, imeendelea kupanuka na kukua katika shughuli na huduma zake na Mwezi Novemba Mwaka 2010 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kuipandisha hadhi na kuwa Hospitali ya Rufaa ngazi ya mkoa.

Hospitali ina jumla ya vitanda 320. Katika wodi kuu nne ambazo ni:-Wodi ya magonjwa mchanganyiko (Medical ward), Wodi ya Upasuaji (Surgical ward), Wodi ya Uzazi na Magonjwa ya Kike (Obstetrics & Gynaecology), Wodi ya watoto chini ya miaka 12 (Paediatrics ward) na Wodi maalum na ya magonjwa ya mlipuko ((Privates & Isolation). Kwa hivi sasa Hospitali ina jumla ya watumishi 297 kati yao 50 tu ndio wanalipwa ruzuku na Serikali. Hospitali inao madaktari bingwa 5. Ili kuboresha zaidi huduma ya tiba kwa wagonjwa, kwa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, ikaanzisha Chuo cha Uuguzi cha Mtakatifu Gaspar, kwa kuongozwa na kauli mbiu mbiu “Tufanye mengi, vizuri na kwa haraka”.

Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar ni sehemu muhimu sana ya jibu la kilio cha Damu nchini Tanzania. Ongezeko kubwa la vifaa tiba vya hospitali limekuza hospitali kwa kiasi kikubwa tofauti na mwanzo. Katika miaka 30 majengo mengi yameongezwa, na kubadili mwonekano. Hospitali hii ni mojawapo ya kazi kubwa sana za wamisionari wa Damu Azizi na inaperusha bendera yao. Kwa sababu ya utendaji wa hospitali hii kwa miaka mingi utu na matumaini yameonekana katika vijiji mbalimbali vya jirani. Vijiji hivi pia vimenufaika na huduma za umeme na upatikanaji wa maji safi na salama. Huduma zingine za kijamii na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pia zimeanzishwa kwa sababu ya uwepo wa hospitali hii. Huu ni mfano wa kweli katika kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini miongoni mwa watanzania! Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo yaliyopewa kipaumbele tangu kuanzishwa kwa Hospitali hii.

Kipindi cha Miaka mitano iliyopita ni muda muafaka wa kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni katika muktadha huu, Radio Vatican inapenda kuwakumbusha Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania yale mambo msingi yaliyosemwa na Hayati Askofu Mathias Josefu Isuja, “Mnyakaya na Babu” wa Jimbo Kuu la Dodoma katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Miaka 50 ya Uwepo wake nchini Tanzania. Aliwapongeza kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma Parokiani na kwa hakika idadi ya Parokia na waamini wanaowahudumia imeongezeka maradufu. Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa Shirika kuwa na idadi kubwa ya miito, wakati ambapo kuna baadhi ya Majimbo wana “ukame wa miito”. Idadi ya wamisionari wazalendo imeongezeka maradufu na hivyo kuchangia kwa kasi kubwa zaidi mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Hayati Askofu Mathias Josefu Isuja aliwashukuru na kuwapongeza Wamisionari kutoka Italia, walijizatiti kuandika historia ya Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania. Aliwataka wamisionari wazalendo, kuiga ari, moyo, sadaka na majitoleo ya waasisi wa Shirika nchini Tanzania. Waendelee kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na mapendo kwa ari, moyo mkuu; kwa bidi, juhudi na maarifa. Kama Shirika, wameachiwa urithi, amana na utajiri mkubwa wa: karama ya Shirika inayofumbatwa katika tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu, rasilimali watu, vitu na miundombinu inayopaswa kutumiwa kikamilifu kwa ajili ya mchakato wa uinjilishaji wa watu wa Mungu kwa uaminifu na weledi, daima wakiwa tayari kusoma alama za nyakati na kujibu kilio cha damu! Majadiliano katika ukweli na uwazi, yawasaidie kuendeleza au kubadili mwelekeo wa utume wao kwa kuzingatia tunu msingi za maisha ya Kikristo! Lengo ni kuhakikisha kwamba, ndoto ya Mtakatifu Gaspari inaendelea kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania.

Hayati Askofu Isuja

 

10 August 2020, 14:22