Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho ni kielelezo cha imani, matumaini na faraja kwa watu wa Mungu wanaosafiri huku bondeni kwenye machozi. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho ni kielelezo cha imani, matumaini na faraja kwa watu wa Mungu wanaosafiri huku bondeni kwenye machozi. 

Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili Na Roho! Faraja!

Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni inakita mizizi yake katika imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Yesu kutoka kwa wafu. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni kielelezo cha ushindi wa nguvu ya upendo wa Mungu kwa waja wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio wa kumi na mbili katika Waraka wake wa kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki. Hii ilitokana na sababu kwamba tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya huku akihusianishwa na Adam mpya, mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Kumbe, kwa maneno mengine, Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa na hasa zaidi wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso uliofanyika kunako mwaka 431, ulipotamka kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos.” Bikira Maria ni Mama yake Kristo Yesu, ambaye ni Mwana wa Baba wa milele, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa linaungama kweli kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Kanisa linamwita kuwa ni Eva mpya kutokana na utii wake.

Bikira Maria ni kielelezo cha imani na ishara na utimilifu kamili wa Kanisa. Kumbe, kwa njia ya imani na utii wake thabiti, Bikira Maria akapewa upendeleo wa pekee kuweza kushiriki katika kazi ya ukombozo kama wanavyosema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kwa utii wake amekuwa Eva mpya, mama wa walio hai. Waamini wa Kanisa la Mashariki kwa miaka mingi walikuwa wanaiadhimisha Sherehe hii ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho  kama kielelezo cha kulala usingizi wa amani “Dormitio” na wataalam wengine wakaongeza kusema, “Somnum Mariae”. Mwili wa Bikira Maria uliokuwa umekingwa na dhambi ya asili, ukapalizwa mbinguni. Hiki ni kielelezo makini cha imani ya watu wa Mungu kama alivyokiri Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997. Kwa mwanga na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, akiwa ameungana na Maaskofu wenzake, Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 akatangaza rasmi kwamba, Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili ni sehemu ya Mafundisho tanzu ya Kanisa Katoliki. Bikira Maria tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anatukumbusha kwamba, maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria yanakwenda sanjari na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Bikira Maria, Mama wa Mungu kwa upendeleo na neema ya Mungu akabahatika kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na hivyo kushirikishwa kwa namna ya pekee kabisa katika Fumbo la Pasaka na utukufu wa Kristo Yesu. Hili ni Fumbo linaloonesha historia ya ubinadamu, matumaini ya watu wa Mungu na Kanisa katika ujumla wake. Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwili na roho, anaendelea kuliombea Kanisa ambalo bado liko safarini, ili liweze kupata neema ya uzima wa milele. Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake ya Kimama anaendelea kuwasindikiza watoto wa Kanisa ambao wako bondeni huku kwenye machozi, ili siku moja, waweze kufika mbinguni na kufurahia maisha na uzima wa milele. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni inakita mizizi yake katika imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni kielelezo cha ushindi wa nguvu ya upendo wa Mungu kwa waja wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni mwaliko kwa watoto wa Kanisa kulitafakari Fumbo hili la imani kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda kumwokoa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kristo Yesu aliyezaliwa, akateswa, akafa, akafufuka amepaa na mwili wake wa utukufu, hatima ya maisha ya waamini wote. Kumbe hapa duniani, watu wajibidiishe kumtumikia Mungu: kiroho na kimwili. Ikumbukwe kwamba, Kristo Yesu alipaa mbinguni kutokana na nguvu za Kimungu zilizokuwa zikitenda kazi ndani mwake. Bikira Maria amepalizwa mbinguni kwa mastahili ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu. Mama Kanisa anapenda kuchukua fursa hii, kuwaalika watoto wake wote waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia kuimarisha imani yao kwa nguvu ya upendo wa Mungu pamoja na kutambua kwamba, miili yao ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho
15 August 2020, 07:37