Mama Kanisa tarehe 15 Agosti ya Kila Mwaka anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, kielelezo cha utukufu wa mwili wa mwanadamu. Mama Kanisa tarehe 15 Agosti ya Kila Mwaka anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, kielelezo cha utukufu wa mwili wa mwanadamu. 

Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho: Utukufu!

Baba Mtakatifu Pio XII akitoa tamko la kupalizwa mbinguni mwili na roho Bikira Maria alisema: “Kwa sababu hii baada ya kumtolea Mungu sala na maombi ya kudumu, na baada ya kuomba mwanga wa Roho wa kweli, tunatanga kuwa: Ni ufunuo wa imani kwamba Mama safi wa Mungu, Maria Bikira daima, baada ya maisha yake hapa duniani alipalizwa mwili na roho katika utukufu wa mbinguni”

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Katika mwaka wa Kiliturujia Mama kanisa ameweka siku kumi za kumheshimu Bikira Maria katika adhimisho la Misa Takatifu ambapo siku 4 ni za kumbukumbu, siku 3 ni sikukuu na 3 sherehe. Kumbukumbu: tarehe 22 Agosti Bikira Maria Malkia na Mama yetu, 15 Septemba, mama yetu wa mateso, 7 Oktoba mama yetu wa Rozari na 21 Novemba kutolewa Bikira Maria mwenye heri. Sikukuu: 25 Machi, kupashwa habari Bikira Maria kama atakuwa Mama wa Mungu, 31 Mei kumtembelea Elizabeth, 8 Septemba kuzaliwa Bikira Maria, Sherehe: 1 Januari, Bikira Maria Mama wa Mungu, 15 Agosti Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, 8 Desemba Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili. Kumbe kila tarehe 15 Agosti ya kila mwaka Kanisa linaadhimisha sherehe ya kupalizwa mbinguni Bikira Maria Mama wa Mungu. Kupalizwa mbinguni kwa Bikira Maria ni utimilifu wa neema alizojaliwa kwa kukingiwa dhambi ya asili. Kukingiwa kwake dhambi ya asili ni kwa sababu katika mwili wa Bikira Maria ndipo Yesu alipata umwilisho. Hivyo basi kupalizwa mbinguni Bikira Maria, ni moja ya mafundisho makuu ya imani ya Kanisa Katoliki. Licha ya kuwa maandiko matakatifu hayasemi moja kwa moja kuhusu kupalizwa mbinguni Bikira Maria mwili na Roho. Kanisa kwa njia ya mapokeo ambayo ni chanzo kimojawapo cha ufunuo wa kimungu limepokea na kufundisha habari ya kupalizwa Mbinguni Bikira Maria kuwa ni ufunuo wa kweli.

Kanisa limefikia hatua hiyo baada ya tafakari na majadiliano ya kina na kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu. Sherehe hii ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni ilitambuliwa na kanisa rasmi na kuanza kuadhimishwa mwaka 1950 baada ya kutangazwa na Papa Pius XII katika Barua ya kipapa inayoitwa Munificentissimus Deus yaani “Mungu Mkarimu”, tarehe 1 Novemba 1950 katika sherehe ya watakatifu wote. Baba Mtakatifu Pio XII akitoa tamko la kupalizwa mbinguni mwili na roho Bikira Maria, Mama wa Mungu asiye na doa la dhambi alisema: “Kwa sababu hii baada ya kumtolea Mungu sala na maombi ya kudumu, na baada ya kuomba mwanga wa Roho wa kweli, tunaarifu, tunaadhimisha, tunaeleza wazi kabisa na kutangaza kuwa: ni ufunuo wa imani kwamba Mama safi wa Mungu, Maria Bikira daima, baada ya maisha yake hapa duniani alipalizwa mwili na roho katika utukufu wa mbinguni”.  Kabla ya kutangazwa siku hiyo rasmi, tangu karne ya 5, kulikuwepo tayari na vikundi vya watu, na sehemu mbalimbali hasa Roma makao makuu ya Kanisa wakiamini kuhusu kupalizwa mbinguni Bikira Maria, na kwamba mwili wake haukuoza kaburini.

Hivyo makanisa mengi yalijengwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa Bikira Maria mpalizwa mbinguni, miji na sehemu mbalimbali za kuabudia ziliwekwa chini ya ulinzi wa Bikira Maria mpalizwa mbinguni. Baada ya hali hiyo kuonekana miongoni mwa wakristo wengi, Papa Pio XII mwaka 1946, aliitisha mkutano wa Maaskofu na kuwaomba wafanye uchunguzi kuhusu swala hilo. Baada ya uchunguzi huo, maaskofu walitoa taarifa na kusema kwamba, inafaa kutamkwa rasmi kuhusu kupalizwa mbinguni Mama Bikira Maria. Kumbe, hata kama Biblia haisemi, waziwazi kuhusu kifo cha Bikira Maria wala kupalizwa kwake mbinguni, Kanisa haliachi kutoamini kuhusu kupalizwa kwake mbinguni kwani muunganiko wa Yesu Kristo Mkombozi wetu na Bikira Maria katika mpango mzima wa ukombozi wa mwanadamu hapa duniani ni sababu tosha ya kuamini. Kunako 8 Desemba 1854 Papa Pio IX alitangaza rasmi, Bikira Maria ni mkingiwa dhambi ya asili toka siku ile ya kutungwa kwake mimba tumboni mwa mama yake kama matayarisho ya kuwa mama wa Mungu, alizaliwa akiwa na uzima wa neema ya utakaso na katika maisha yake Bikira Maria hakutenda dhambi wala hakuwa na doa lolote la dhambi hivyo mwili wake haukupaswa kuoza. Bikira Maria alibaki Bikira daima kabla na baada ya kumzaa mkombozi kwani alichukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Mtaguso wa Efeso mwaka 431 ulitamka wazi kuwa Bikira Maria ni Mama wa Kristo kwa Kigiriki “Christokos” kwani mwili wake ulichukua mimba ya mkombozi wetu Yesu Kristo, na ni Mama wa Mungu Kigiriki “Theotokos”, maana fumbo la umwilisho yaani Mungu kujifanya Mtu ulifanyika mwilini wake. Kumbe Bikira Maria ameshiriki kikamilifu kazi ya ukombozi wetu na mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Lakini bado pia maandiko matakatifu hayako kimya juu ya Bikira Maria. “Ishara kubwa ikaonekana mbinguni, ambapo mwanamke aliyevikwa jua, pia na mwezi chini ya miguu yake, na taji la nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake” (Ufu 12:1). Katika somo la kwanza kutoka kitabu cha ufunuo, mwanamke anayeongelewa ni mfano wa Birika Maria tabernakulo ya kwanza na ni mfano wa Kanisa, joka ni mfano wa shetani na mtoto wa mwanamke ndiye Masiya Yesu Kristo. Vita kati ya joka na mwanamke ni mapambano kati ya nguvu za giza na Kanisa. Liturujia humlinganisha Mama Maria na Kanisa kwa sababu ya kufaulu kumshinda shetani kwa nguvu ya Kristo.

Mtume Paulo katika Somo la pili anatueleza kwamba, Yesu Kristo amemshinda shetani na ubaya wake yaani, dhambi na mauti. Ushindi huu umedhihirishwa katika ufufuko wa Yesu Kristo, na pia utadhirishwa zaidi nyakati za mwisho miili yetu itakapofufuliwa. Tunda lingine la ushindi wa Kristo ni kupalizwa Bikira Maria mbinguni. Injili yaeleza ndiyo ya Bikira Maria isiyo na mtikisiko wala manung’uniko kwa wito wa Mungu licha ya hatari na magumu ambayo angeyapata naye anaitaka na kusema; Mimi ni mtumumishi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema Lk 1: 38). Jibu lake la kukubali umwilisho wa Mungu ndani mwake lilifumbatwa katika utii wake wa kimapendo na utayari wake wa kushirikiana na Mungu katika kutekeleza mpango wa ukombozi wa mwanadamu. Kwa maana hiyo, Bikira Maria, alikubali mwito huo wa kuwa mama wa Mungu, na ukweli huo ulijidhihirisha wazi katika fumbo la umwilisho Neno akatwaa mwili akakaa kwetu (Jn 1: 14). Kumbe kutokana na ndiyo yake, imani yake, utii na utayari wake, Bikira Maria amekuwa sababu ya ukombozi wake yeye mwenyewe na ukombozi wa mwanadamu kwa ujumla. Hivyo Bikira Maria alistahili tuzo la utukufu mbinguni.

Bikira Maria alitii mara moja bila kukawia, nasi tunapaswa kuwa na utii tunapopata ujumbe toka kwa Mungu kupitia neno lake, mapokeo na kwa viongozi wake. Kwa ubatizo wetu, tumekuwa watoto wapenzi wa Mungu. Kwa maana hiyo, tumebarikiwa na Mungu, hivyo nasi tunastahili tuzo la utukufu mbinguni kama Mama Bikira Maria kama tutaishi ahadi zetu za ubatizo. Bikira Maria katika maisha yake hapa duniani; amepata mateso mengi sana. Alikubali kubeba ujauzito bila kujali aibu na adhabu ya kifo ambayo angeipata kwa kutupigwa mawe kutokana na kukosa uaminifu mbele ya macho ya binadamu kama ilivyokuwa desturi ya wayahudi, alivumilia yote hadi chini ya msalaba alipomwona mwanaye anakata roho. Bikira Maria alipokea ujumbe wa Mungu na akakubali kuchukua mimba ili auzalie ulimwengu Mkombozi. Maria alijitoa kwa Mungu kuwa mali yake mwili na roho. “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema.” Je, kwa nini asipalizwe mbinguni mwili na roho?

Moyo wake wa unyenyekevu, moyo wake wa kujitoa mwili na roho katika utumishi kwa Mungu unadhihirishwa wazi kabisa na tendo lake la kuondoka toka nyumbani kwake na kwenda kwa haraka mpaka mji wa Yuda katika nchi ya milimani. Anakwenda kwa jamaa yake Elizabeti baada ya kudokezwa na malaika kuwa Elizabeti ni mjamzito wa miezi sita. Anafika huko na kukaa naye kwa muda wa miezi mitatu, ili kumsaidia jamaa yake Elizabeti katika kipindi kigumu cha kumzaa mtangulizi wa Yesu yaani Yohane mbatizaji katika uzee wake. Ahadi ya kuwa mama wa Mungu kwa kumzaa Kristo haikumfanya ajisikie kuwa yeye ni mtu wa kutumikiwa bali kwa unyenyekevu anajifanya kuwa mtumishi. Katika mazingira hayo ya kujiona mtumishi anapokea neno la ‘heri’ kutoka kwa jamaa yake Elizabeti. Maria anaambiwa ana heri kwa sababu amesaadiki, maana Bwana atayatimiza yale yote aliyomwambia. Kupalizwa mbinguni kwa Bikira Maria ni ishara ya matumaini na kitulizo kwa kanisa. Tukio hili la kupalizwa linathibitisha kuwa baada ya maisha ya hapa duniani tutaendelea kuishi maisha ya heri mbinguni, kama tukiwa wafuasi waaminifu wa Kristo.

Kumbe kifo sio mwisho wa maisha, bali ni mwanzo wa maisha mengine ambayo hayana mwisho maisha ya utakatifu baada ya ufufuko wa miili, ambapo roho zetu zitarudi tena katika miili ya utakatifu katika heri ya milele mbinguni. Tusisahau kuwa kuna adhabu ya milele motoni, kwa wale ambao hawaishi kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kumbe hatuna budi kuthamini mwili ambao ni hekalu la Roho Mtakatifu. Bikira Maria ni mwombezi wetu mbinguni, ni Mama mwenye huruma na yupo tayari kutusaidia na kutuombea mastahili tunayohitaji toka kwa mwanae, tusali bila kuchoka katika siku zote za maisha tupitishie maombi yetu kwa Mama Maria ili ayafikishe kwa mwana wake wa pekee. Tuepuke nafasi zinazotupelekea katika vishawishi vya dhambi na pale tunapotenda dhambi tusichelewe kwenda kwenye kitubio ili kumpa Yesu nafasi ndani ya mioyo yetu, nasi tuweze kukaa ndani yake. Usafi wa moyo na unyenyekevu ni vitu vya msingi katika maisha ya kiroho. Mama Maria yu tayari daima kutuombea msamaha kwa mwanae pale tunapokuwa tayari kutubu dhambi zetu tulizozitenda.

Maria awe kwetu ni mfano wa kumfuasa Kristo kwa ukaribu tukitegemea kwamba hata sisi siku moja tutashiriki utukufu wa Yesu kama Maria anavyoshiriki hata sasa. Sherehe ya kupalizwa Bikira Maria mbinguni inatukumbusha kuwa mmoja wa familia yetu, mama yetu amefikia taji ya utukufu wa mbinguni. Mungu alikuwa na mpango na Maria tangu mwanzo wa ulimwengu, wakati wa maisha yake hapa duniani, Mungu alihakikisha kuwa Maria hakosi chochote kitakachomsaidia kuwa mwaminifu kwake. Maria alikuwa mwaminifu kwa Mungu siku zote. Kumbe tunaalikwa kujikabidhi kwa mpango wa Mungu wa ukombozi wetu, kukua kila wakati tukitambua udhaifu wetu na hitaji la Mungu katika maisha yetu, kuweka matumaini yetu yote katika huruma na upendo wa Mungu, kujibu upendo wa Mungu kwetu kwa kuwahudumia jirani. Maria anatualika kufanya yote kwa unyenyekevu na udogo lakini kwa uaminifu. Tukiungana na Kristo hapa duniani, tutaungana naye pia mbinguni na kule tutashiriki utukufu wa mama yetu milele. Siku moja nasi pia tutafurahia kupalizwa kwetu mbinguni.

 

14 August 2020, 14:14