Tafuta

Vatican News
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini Mwa Afrika Imbisa Limeonesha mshikamano wa dhati na Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe ambalo hivi karibuni limeshtumiwa sana na Serikali. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini Mwa Afrika Imbisa Limeonesha mshikamano wa dhati na Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe ambalo hivi karibuni limeshtumiwa sana na Serikali. 

Mshikamano wa IMBISA na Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati kabisa na Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe ambalo hivi karibuni, limerushiwa “makombora ya shutuma nzito” kutoka kwa Serikali ya Zimbabwe. Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe, ZCBP limeandika Waraka wa Kichungaji wa Mwezi Agosti 2020. Ukweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tarehe 19 Machi 2013 Baba Mtakatifu Francisko aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Ibada ambayo ilikuwa na uwakilishi mkubwa wa viongozi wa dini, madhehebu na wale wa Serikali bila kuwasahau wawakilishi wa maskini kutoka nchini Argentina. Baba Mtakatifu aliwataka waamini na viongozi wa Kimataifa kuwa ni walinzi makini wa jirani zao na watunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, madaraka ni kwa ajili ya huduma kwa maskini na wanyonge ndani ya jamii. Kama Papa anatamani kuwa ni daraja linalounganisha watu mbali mbali sanjari na kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na majadiliano. Ni katika muktadha huu, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati kabisa na Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe ambalo hivi karibuni, limerushiwa “makombora ya shutuma nzito” kutoka kwa Serikali ya Zimbabwe. Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe, ZCBP limeandika Waraka wa Kichungaji wa Mwezi Agosti 2020, unaofanya upembuzi yakinifu kuhusu fursa, matatizo na changamoto zinazoendelea kuwapekenya watu wa Mungu nchini Zimbabwe.

Maaskofu wanasema, mapambano bado kabisa yanaendelea kwa sababu maisha ya wananchi wa Zimbabwe ni muhimu sana na wala mchakato wa kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, kamwe hauna kikomo. Maaskofu wanasema, kila kizazi kinawajibika kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa sanjari na kuendelea kujikita katika mchakato wa kudumisha misingi ya amani. Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe katika Waraka wa Kichungaji wa tarehe 14 Agosti, 2020 linayaangalia matukio ya wakati huu, saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma, umuhimu wa kuenzi siku ya mashujaa na vikosi vya ulinzi na usalama. Maaskofu wanakazia umuhimu wa mchakato wa mageuzi makubwa kama sehemu ya mapambano dhidi ya umaskini na kwamba, kuna umuhimu wa kuunda jukwaa litakalojadili vipaumbele vya familia ya Mungu nchini Zimbabwe.

Serikali ya Zimbabwe kupitia kwa Waziri wa habari na huduma ya mawasiliano Bi Monica Mutsvangwa, Jumamosi, tarehe 15 Agosti 2020 ikatoa shutuma nzito dhidi ya Kanisa Katoliki nchini Zimbabwe, lakini kwa namna ya pekee kabisa dhidi ya Askofu mkuu Robert Christopher Ndlovu wa Jimbo kuu la Harare nchini Zimbabwe, ambaye ndiye Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe. Serikali ya Zimbabwe inamtaja Askofu mkuu Robert Christopher Ndlovu kuwa na mawazo mabaya kwa ajili ya Zimbabwe na kwamba, Kanisa Katoliki linataka kuigawa Zimbabwe vipande vipande na hatimaye, kuitumbukiza katika mauaji ya kimbari kama ilivyojitokeza nchini Rwanda kunako mwaka 1994. Serikali ya Zimbabwe inapinga na kulaani vikali Waraka wa Kichungaji uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe tarehe 14 Agosti 2020 katika mkesha wa maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA, linasikitishwa sana na jinsi ambavyo Serikali ya Zimbabwe ilivyoamua kushughulikia Waraka wa Kichungaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe, badala ya kujibu kero zilizobainishwa na kuanza kuzifanyia kazi, badala yake, Serikali ikaamua “kushusha makombora mazito mazito” dhidi ya Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe. Kwa bahati mbaya, Serikali ya Zimbabwe imenukuu baadhi ya maneno ya Baba Mtakatifu Francisko katika mapambano dhidi ya janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 na kusahau mambo msingi katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, tarehe 19 Machi 2013 mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alikazia: Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na ulinzi wa watu wote wa Mungu, hususan maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa upendo na unyenyekevu mkuu, kwa sababu maisha ya binadamu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kamwe wasiruhusu watu kumezwa na utamaduni wa kifo kutokana na kiburi, chuki na uhasama wa binadamu anayetaka daima kujimwambafai! Baba Mtakatifu Francisko alisema, maskini ni kati ya watu ambao wanapaswa kupewa upendeleo wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutangaza na kuwashuhudia Injili ya huruma na mapendo, kwa kuwahudumia kwa upendo, ili kweli nyota ya matumaini iweze kuwaangaza watu wa Mungu. Askofu Lucio Andrice Muandula wa Jimbo Katoliki Xai Xai, Msumbiji ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA anakaza kusema, Maaskofu Katoliki Zimbabwe, wameikumbusha Serikali dhamana na wajibu kwa raia wake, hususan maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Askofu Muandula anasema, jamii inayosimikwa katika tunu msingi za kiutu, inapaswa kuwashughulikia maskini na wanyonge zaidi katika jamii. Kwa Serikali ya Zimbabwe kutaka “kuwashikisha adabu na kuwanyamazisha” Maaskofu Katoliki Zimbabwe ni kuendelea kuwachanganya watu wa Mungu nchini Zimbabwe.

IMBISA inahitimisha ujumbe wake wa mshikamano wa dhati na Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe kwa kusema, kwamba, Kristo Yesu alikuja hapa ulimwenguni ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. Rej. Yn. 10: 10. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA, linasema, litaendelea kuunga mkono juhudi zinazotekelezwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe katika utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu nchini Zimbabwe, ili watu wa Mungu nchini humo, wawe na uzima, kisha wawe nao tele!

IMBISA: Zimbabwe
22 August 2020, 14:42