Tafuta

Vatican News
Mama Olive Luena, ambaye ameitumikia WAWATA kwa Miaka 40 katika ngazi mbali mbali sasa anang'atuka kutoka madarakani kwa moyo wa shukrani kwa Mungu na Kanisa. Mama Olive Luena, ambaye ameitumikia WAWATA kwa Miaka 40 katika ngazi mbali mbali sasa anang'atuka kutoka madarakani kwa moyo wa shukrani kwa Mungu na Kanisa. 

Mama Luena: Miaka 40 ya Huduma kwa WAWATA! Hadi Machozi!

Katika kipindi cha Miaka 40 Mama Luena ameitumikia WAWATA kama: Katibu mkuu, kama Makamu Mwenyekiti na hatimaye Mwenyekiti WAWATA Taifa. Amewahi kuwa mjumbe wa WUCWO kwa muda wa miaka kumi na mwili na katika ngazi ya Kimataifa kuchaguliwa kuwa mojawapo wa Marais wa Kongamano la Dini mbali mbali “World Conference on Religion and Peace: 1995-2020."

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni mwaka 1977, Mama Olive Luena, akiwa msichana mbichi kabisa, alipochaguliwa kuongoza Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania katika ngazi ya Parokia, Jimbo na hatimaye kunako mwaka 1981 akachaguliwa kuongoza WAWATA Taifa. Hiki kilikuwa ni kipindi cha vuguvugu la WAWATA kutimiza miaka kumi tangu kuanzishwa kwake! Wengi, wakambeza na kumkejeli kwa kusema, kwamba, “WAWATA wamechagua Serengeti” wanataka kuizamisha ili ifutike kutoka uso wa maisha na utume wa Kanisa la Tanzania. Lakini kwa neema, baraka, imani thabiti, ushupavu na uthubutu, leo hii WAWATA inaendelea kupeta, bado miaka miwili tu, iadhimishe Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, matendo makuu ya Mungu, mwenye macho haambiwi, atazame mwenyewe! Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women Of Tanzania Association) ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu.

Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Taswira ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ni kuona kila mwanamke mkatoliki wa Tanzania anaelewa nafasi yake na wajibu wake wa Kikristo kuanzia ngazi ya Familia, Jumuiya, Kanisa, jamii na Taifa kwa ujumla, pia wanakuwa na maendeleo fungamani ya kiuchumi ili kukidhi mahitaji msingi ya familia na hivyo kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na Jamii, na kufanya maisha ya hapa duniani kuwa taa na nuru katika Ulimwengu kama mawakili wa Yesu Kristo. Mama Olive Luena, Mwenyekiti Mstaafu wa WAWATA Taifa, Jumapili tarehe 30 Agosti 2020 katika hotuba yake kwa wajumbe wa Mkutano mkuu wa 41 wa Uchaguzi mkuu uliofanyika kwenye Makao makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, Kurasini, imewashtua wanawake wengi, wakajikuta wakitokwa na machozi ya furaha na shukrani kwa Mama Luena kwa ushupavu aliouonesha wakati wote wa utumishi wake kama Mwenyekiti wa WAWATA Taifa, daima amekuwa ni kiongozi aliyetafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wanawake wote nchini Tanzania.

Katika hali ya unyenyekevu kabisa, Mama Luena amekiri kwamba, Mwenyezi Mungu huwateuwa waja wake na kuwapatia neema ya kutekeleza utume na majukumu anayowakabidhi. Yeye mwenyewe ni shuhuda na chombo cha huduma ya Mungu kwa WAWATA nchini Tanzania. Kumbe, viongozi wapya waliochaguliwa katika mkutano huu mkuu watambue kwamba, wanapaswa kutumikia na kuwajibika na Mwenyezi Mungu atawajalia neema na baraka za kuendeleza utume wake miongoni mwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Wanawake wasiogope,  na wala kutishwa na kejeli za “wajumbe na wapambe wao”, bali wawe na moyo mkuu, tayari kuitikia na kusema kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, “Mimi hapa nitume!”. Mama Luena ametamka wazi kwamba, sasa anang’atuka rasmi kutoka katika uongozi wa WAWATA, kwa furaha na bashasha, kwa moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu aliyemtendea mambo makuu katika maisha na utume wake.

Mama Luena analishukuru Kanisa Katoliki nchini Tanzania kwa fursa mbali mbali lilizomkirimia katika maisha na utume wake. Anaomba msamaha kwa mapungufu yake ya kibinadamu. Katika kipindi cha Miaka 40 Mama Luena ameitumikia WAWATA kama: Katibu mkuu kwa muda wa miaka 18 na kama Makamu Mwenyekiti na hatimaye Mwenyekiti WAWATA Taifa. Amewahi kuwa mjumbe wa WUCWO kwa muda wa miaka kumi na mwili na katika ngazi ya Kimataifa kuchaguliwa kuwa mojawapo wa Marais wa Kongamano la Dini mbali mbali “World Conference on Religion and Peace: 1995 hadi mwaka 2020”. Aliwahi kuteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa mjumbe wa Baraza la Kipapa la Waeli, ambalo kwa sasa ni Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni mwema wakati wote! Mama Luena amelishukuru Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kumwezesha kuwawakilisha wanawake na hatimaye kujenga majadiliano ya kidini na kiekumene na wanawake watanzania.

Mama Luena, hakuwa nyuma “kama kiatu cha raba” familia ya Mungu nchini Tanzania kwa kutambua mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, akateuliwa kuwa ni mjumbe wa Bunge la Katiba. Huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu kama ilivyokuwa kwa yule Mwanamke Msamaria aliyekutana na Kristo Yesu pale Kisimani, akapyaisha maisha yake na kuwa mtu mpya kabisa! Yaani inapendeza kusikia wanawake wa shoka kama Mama Olive Luena akisimulia matendo makuu ya Mungu katika maisha na utume wake! Nasi wapambe tunachombeza kwa kusema, Big Up Mama Olive Luena, makali yako tumeyaona! Hadi raha! Achana na wapambe!

Mama Luena
30 August 2020, 14:10