Uharibifu mkubwa wa majengo ya bandarini kutokana na mlipuko huko Beirut nchini Lebanon. Uharibifu mkubwa wa majengo ya bandarini kutokana na mlipuko huko Beirut nchini Lebanon. 

Lebanon:Baraza la Makanisa ya Mashariki watoa wito wa mshikamano!

Baraza la Makanisa ya Mashariki(Mecc)wanatoa wito kwa Makanisa yote ulimwenguni,Jumuiya ya Kimataifa na watu wenye mapenzi mema kuingilia kati kwa njia ya mshikamano ili kuisadia nchi ya Lebanon baada ya mlipuko mkubwa sana ambao umeharibu jiji la Beirut.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Baada ya wiki mbili tangu mlipuko wa kutisha uliotokea tarehe 4 Agosti 2020 na kuharibu jiji la Beirut nchini Lebanoni na zaidi kusababaisha vifo vya watu karibia 134, na maelfu kujeruhiwa, Baraza la Makanisa ya Mashariki (Mecc) limetoa wito kwa Makanisa yote  ulimwenguni, jumuiya ya Kimataifa na watu wote wenye mapenzi mema kujikita kutoa mshikamano wa dhati. Katika nchi hiyo hadi sasa imepiga magoti na Makanisa mahalia hayana majengo yao, hawana uwezo wa kujikwamua peke yao katika mahitaji yote ya wakati huu na kwa ajili ya ujenzi mpya, wanathibitisha.

Majengo mengi yakiwemo Makanisa, hospitali na shule vimeharibika

Mamia ya majengo likiwemo la silos ambalo lilikuwa linahifadhi karibia asilimia 85 za ngano ya Nchi na makanisa yamepata madhara makubwa au kuharibika kabisa, kwa mujibu wa taarifa  iliyotolewa tarehe 16 Agosti 2020. Katika hayo yanaongezea uharibifu mkubwa wa Hospitali tatu za kikristo ambazo zinawapokea wagonjwa wa aina zote wawe wakristo au waislam. Baraza la Makanisa ya Mashariki (Mecc ) aidha limebanisisha  kuwa shule nyingi katoliki katika mitaa ya Gemmayzeh, Mar Mikhael na Achrafieh zimeharibiwa sana kwa wiki hizi chache zilizobaki kabla ya kuanza mwaka mpya wa masomo mwezi Septemba. Mtaa wa Kikristo jijini Beirut umewaharibiwa kabisa na karibu makanisa 10 yameharibiwa sana. Katika hayo yote, linaongezea dharurua ya janga la Covid-19 ambalo linaendelea kwa kasi kubwa kuweka majaribu magumu sana ya mfumo mzima  wa kiafya nchini humo.

Kanisa limekuwa likitoa msaada wa dharura katika historia ya majanga

Katika taarifa wanabainisha kuwa, wakati wa migogoro mingine nchini Lebanon ambayo imekabiliana nayo katika historia, Makanisa ya Kikristo yamekuwa bega kwa bega daima kuwa mstari wa mbele kubeba jukumu la kusaidia watu, lakini leo hii, kwa mujibu wa Mecc, hawana uwezo wa kutoa huduma hiyo  kwa sababu ya majengo yao ya kiafya na kielimu yameharibika na kwa maana hiyo ukarabati utakuwa wa lazima unaohitaji mamia ya milioni ya  dola za kimarekani. Hadi sasa watu wa kujitolea kutoka sehemu mbali mbali na makundi ya vyama vya kiraia wanaendelea kutoa msaada wao mkubwa, katika magofu yaliyojaa kwenye barabara, makanisa na hospitali. Hata hivyo Monasteri na shule nyingine  ambazo hazikupata uharibifu zimefunguliwa ili kuwakaribisha watu ambao wamebaki bila makazi na wanaendelea kutoa msaada wa kugawa chakula na mahitaji yaliyo muhimu tu.

Wito wa Mecc ili kupunguza uzito unaolelewa Makanisa

Kwa upande wake, Mecc tayari imechukua hatua ya kusaidia familia zilizo katika mazingira hatarishi kwa kusambaza vifaa vya usafi, vifaa vingine binafsi, seti za nguo, mashuka na vifaa vingine vya nyumbani, chakula, madawa, vifaa vya kinga ya Covid-19, mifuko na troli  kwa ajili ya watu wanaojitolea kusafisha makanisa, hospitali na barabara za mitaa. Katika  msaada huo pia ni pamoja na utoaji wa madawa kwa watu wengi walio na magonjwa sugu au saratani. Katika hatua itakayofuata, Baraza hili pia litashiriki katika ukarabati wa nyumba zilizoharibiwa, shule na zahanati. Kwa hayo yote hayawezi kufanywa bila kuwa na msaada wa kimataifa. Kwa maana hiyo, ndipo wito wa Baraza la Makanisa ya Mashariki (Mecc) unatolewa ili kuweza kupunguza uzito inaoelemewa nyuma ya  mabega ya Makanisa na kuikomboa mioyo ya raia walio hatarini na familia zilizoathiriwa na janga hili ambalo halijawahi kutokea na kuondokana  na jiwe la mateso, hofu kubwa na kukata tamaa.

19 August 2020, 12:49