Tafuta

Vatican News
Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, "ametia nia" ya kushiriki ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Makurunge, Jimbo Katoliki la Morogoro! Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, "ametia nia" ya kushiriki ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Makurunge, Jimbo Katoliki la Morogoro! 

Kardinali Pengo "Atia Nia" Ujenzi wa Kanisa la Makurunge!

Kwa moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, kwa mambo makuu aliyomtendea katika utume wake, Kardinali Polycarp Pengo, tarehe 15 Agosti 2020, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kigango cha Makurunge, Bagamoyo, Jimbo Katoliki la Morogoro. Mheshimiwa sana Padre Lazarus Vitalis Msimbe aliweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Makurunge.

Na Angela Kibwana, Bagamoyo na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho hapo tarehe 15 Agosti 2020, Baba Mtakatifu Francisko alisema kwamba, Bikira Maria ni nyota angavu inayowaongoza waamini kwenda mbinguni. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Bikira Maria, Mama wa Yesu, akiwa amekwisha tukuzwa mbinguni mwili na roho, ni sura ya mwanzo wa Kanisa ambalo litapata utimilifu wake katika ulimwengu ujao. Kadhalika anang’aa duniani kama alama ya hakika ya matumaini na ya faraja kwa taifa la Mungu lililo safarini, mpaka siku ya Bwana itakapokuja. Rej. LG. 68. Mwinjili Luka, anamweka Bikira Maria mbele ya macho ya waamini, akiwa anamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani “Magnificat” kwa kusema, “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana na roho yangu imemfurahia Mungu mwokozi wangu”.

Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema kwamba, Mwenyezi Mungu amemkuza mja wake, licha ya matatizo, fursa na changamoto mbali mbali ambazo aliweza kumkirimia katika maisha. Hii ni changamoto kwa waamini kutojikatia tamaa hata kidogo wanapokumbana na matatizo pamoja na changamoto za maisha. Mwenyezi Mungu apewe sifa na ukuu wake, kwa sababu Mungu ndiye chemchemi ya furaha ya kweli kutokana na uwepo wake wake wa daima. Mwenyezi Mungu yuko karibu na daima yuko tayari kuwashika mkono na kuwasaidia waja wake, kwa sababu udhaifu wa Mungu unajionesha kwa namna ya pekee, katika upendo wake wa dhati. Mwenyezi Mungu anawaangalia waja wake na anawapenda wadogo na wanyenyekevu wa moyo kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Mwenyezi Mungu alimtendea makuu Bikira Maria kwa kumjalia zawadi ya maisha, Neno wa Mungu aliyetungwa mimba tumboni mwake kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Ni katika muktadha wa moyo wa unyenyekevu na shukrani kwa Mwenyezi Mungu, kwa mambo makuu aliyomtendea katika maisha na utume wake, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania tarehe 15 Agosti 2020, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kigango cha Makurunge, Bagamoyo, Jimbo Katoliki la Morogoro. Mheshimiwa sana Padre Lazarus Vitalis Msimbe, Msimamizi wa Kitume, Jimbo Katoliki la Morogoro, aliweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Makurunge. Lengo la ujenzi wa Kanisa hili ni kuwasogezea karibu waamini huduma za maisha ya kiroho, ili kujenga Jumuiya ya waamini inayoinjilisha na kuinjilishwa. Jumuiya inayotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji! Waamini wengi walikuwa wanalazimika kwenda Bagamoyo mjini ili kushiriki Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kupata huduma za maisha ya kiroho.

Kanisa hili litasaidia sana kupunguza msongamano wa waamini kwenye Kanisa la Bagamoyo na hivyo kukuza imani na kuimarisha imani kwa kuwa na viongozi wa kiroho karibu. Kigango na baadaye Parokia, itasaidia kuimarisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam. Ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Makurunge, Bagamoyo utakapokamilika, hapa patakuwa ni mahali muafaka pa waamini kukutana, ili hatimaye, kuweza kuutafakari Uso wa huruma ya Mungu. Ni mahali muafaka pa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Kanisa hili litakuwa ni mahali pa kuadhimishia Mafumbo ya Kanisa na kurithisha imani, ili kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara kwa kutambua kwamba, familia, kimsingi ni Kanisa dogo la nyumbani. Ni mahali pa kumsifu Mwenyezi Mungu kwa moyo wa uchaji na ibada. Wazo la kushiriki ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Makurunge, Bagamoyo anasema Kardinali Polycarp Pengo ni kuonesha moyo wa shukrani kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa zawadi na rasilimali fedha walizomzawadia alipokuwa anang’atuka kutoka madarakani, kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Kwa kuguswa na mazingira na ushuhuda wa imani ya watu wa Mungu Parokia ya Moyo Safi wa Bikira Maria, Bagamoyo, Jimbo Katoliki la Morogoro, Mlango wa Imani Katoliki Afrika Mashariki, akaomba ridhaa kwa Padre Nicetas Stephen Kyara, Paroko wa Parokia hii, kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Makurunge. Kardinali Pengo katika mahubiri yake amesema kwamba, Bikira Maria ni mlango wa wokovu wa binadamu wote na kwa mantiki hii, Bagamoyo ni chemchemi ya imani na unaendelea kubaki kuwa ni Mlango wa Imani kwa Kanisa Katoliki Afrika  Mashariki. Hapa ni mahali ambapo Wamisionari wa kwanza walitua nanga ya: imani, matumaini na mapendo na huo ukawa ni mwanzo wa kuenea kwa Ukristo Afrika Mashariki. Mji wa Bagamoyo ni alama ya ukombozi, mahali ambapo mwanadamu amepata tena fursa ya kuinua moyo wake kwa imani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu baada ya kukombolewa kutoka utumwani, kashfa ambayo inaendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Makurunge ni heshima kubwa kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwakirimia watu wa Mungu Afrika Mashariki zawadi ya imani, inayopaswa kulindwa, kuendelezwa na kutolewa ushuhuda thabiti. Hii ni sehemu ya mchakato wa kuendeleza ukuu wa Mungu aliowafanyia waja wake kupitia Bagamoyo kama mlango wa imani. Eneo la Makurunge linapaswa kupewa hadhi yake kwa sababu hii ni njia panda ya kwenda kwenye Hifadhi ya Taifa ya Saadani ambayo ipo katikakati ya pembe tatu ya historia ya Bagamoyo, Pangani na Zanzibar. Ni matumaini ya watu wa Mungu eneo hili kwamba, Serikali itajenga barabara ya lami kuelekea Jiji la Tanga. Ni matumaini ya Kardinali Polycarp Pengo kwamba, watu wa Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam pamoja na wasamaria wema wataendelea kumuunga mkono, ili ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Makurunge uweze kukamilika na waamini kupata mahali bora zaidi pa kumtolea Mungu sala na ibada zao.

Ni matumaini ya Kardinali Pengo kwamba, Kigango hiki hatimaye, kitakuwa Parokia ambayo kimsingi ni kitovu cha uinjilishaji, wongofu wa kimisionari na mahali muafaka pa majadiliano ya kidini na kiekumene. Kwa upande wake, Mheshimiwa sana Padre Lazarus Vitalis Msimbe, Msimamizi wa Kitume, Jimbo Katoliki la Morogoro, amemshukuru na kumpongeza Kardinali Polycarp Pengo kwa “kutia nia ya kumjengea Mwenyezi Mungu” nyumba ya sala na ibada takatifu. Huu ni ushuhuda wa ukarimu wa watu wa Mungu Jimbo kuu la Dar Es Salaam ambao umemwilishwa katika moyo wa unyenyekevu na shukrani kutoka kwa Kardinali Polycarp Pengo. Hadi sasa jumla ya shilingi milioni 150 zimekwisha kutumika katika ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Makurunge. Itakumbukwa kwamba, Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu waliendeleza mji wa Bagamoyo na hatimaye, kuitwa “Mji wa Mariam” maana yake mji wa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Wamisionari hawa wakashuhudia nguvu ya Msalaba waliousimika kwenye Pwani ya Bagamoyo!

Kardinali Pengo anasema, Wamisionari hawa waliamini na kuthamini sana: nguvu, ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili! Bagamoyo ukawa Mlango wa Imani Afrika Mashariki. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 yaendelee kukoleza furaha ya Injili kwa familia ya Mungu nchini Tanzania! Fumbo la Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho linaonesha historia ya ubinadamu, matumaini ya watu wa Mungu na Kanisa katika ujumla wake. Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwili na roho, anaendelea kuliombea Kanisa ambalo bado liko safarini, ili liweze kupata neema ya uzima wa milele. Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake ya Kimama anaendelea kuwasindikiza watoto wa Kanisa ambao wako bondeni huku kwenye machozi, ili siku moja, waweze kufika mbinguni na kufurahia maisha na uzima wa milele. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni inakita mizizi yake katika imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni kielelezo cha ushindi wa nguvu ya upendo wa Mungu kwa waja wake.

Kardinali Pengo: Makurunge
27 August 2020, 13:24