Vatican News
Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania imeandaa Mpango Mkakati kwa Mwaka 2020-2022. Imewachagua viongozi wapya kitaifa watakaokuwa chini ya Mama Evaline Malisa Ntenga. Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania imeandaa Mpango Mkakati kwa Mwaka 2020-2022. Imewachagua viongozi wapya kitaifa watakaokuwa chini ya Mama Evaline Malisa Ntenga.  (AFP or licensors)

Mpango Mkakati wa WAWATA Kwa Mwaka 2020-2022: Mama Ntenga!

Mpango mkakati wa utekelezaji wa maazimio kwa mwaka 2019-2022: Ni wanawake kujitakatifuza ili waweze kutakatifuza jamii kuanzia katika: Familia, Jumuiya ndogondogo za Kikristo na Jamii kwa ujumla kwa njia ya, kutoa elimu juu ya wito wa kuwa watakatifu, Mafungo ya maisha ya kiroho, tafakari mbalimbali, maisha ya sala na tafakari pamoja na hija za kiroho ndani na nje ya Tanzania!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women Of Tanzania Association) ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu. Jumuiya hii inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika”. Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Taswira ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ni kuona kila mwanamke mkatoliki wa Tanzania anaelewa nafasi yake na wajibu wake wa Kikristo kuanzia ngazi ya Familia, Jumuiya, Kanisa, jamii na Taifa kwa ujumla, pia wanawake wanakuwa na maendeleo fungamani ya kiuchumi ili kukidhi mahitaji msingi ya familia na hivyo kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na Jamii, na kufanya maisha ya hapa duniani kuwa taa na nuru katika Ulimwengu kama mawakili wa Yesu Kristo.

Malengo: WAWATA ilipoanzishwa kunako mwaka 1972, ilijiwekea malengo ili kupata mwelekeo utakaowafikisha mahali ambapo wanaweza kufanya tathmini ya Utume wao katika maisha na utume wa Kanisa na katika mchakato wa ukombozi mzima wa mwanamke mintarafu suala la maisha ya kiroho, mapambano dhidi ya ujinga, umaskini na maradhi. Malengo haya yalijikita zaidi katika mchakato wa kumjenga mwanamke katika imani thabiti ya Kikristo, ili aweze kuishi maisha matakatifu na hatimaye, ayatakatifuze malimwengu kwa ushuhuda wa maisha yake kama kielelezo cha imani tendaji. WAWATA pamoja na mambo mengine, inapania kumjengea mwanamke uwezo wa kujikomboa yeye na familia yake, ili aweze kuwakomboa watu wengine wenye shida, yatima na wasiojiweza. WAWATA inataka kumwendeleza mwanamke kielimu na kiujuzi ili aondokane na giza la kiroho, ujinga wa akili na aendeleze wengine sanjari nakKumwezesha mwanamke katika masuala ya kiuchumi ili kutegemeza familia, Kanisa na kuwategemeza wengine.

Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2020 imeadhimisha Mkutano mkuu wa 41 wa Uchaguzi uliofunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Desiderius M. Rwoma, Mwenyekiti wa Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Wajumbe katika mkutano huu wamepembuliwa kuhusu utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitatu iliyopita. Wamesomewa taarifa za mkutano wa WUCWO pamoja na taarifa za mradi wa mikopo (WASMEP). Mhasibu wa WAWATA Taifa, ametoa taarifa ya fedha kwa mwaka 2019-2020: makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2020-2021. Wajumbe wamepata nafasi ya kusikiliza taarifa za utekelezaji wa utume wa WAWATA majimboni, mafanikio, matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo, WAWATA inapojiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Wajumbe wamepokea na kuridhia vipaumbele vya mpango kazi kwa kipindi cha miaka 3 yaani kuanzia Mwaka 2020-2022. Hatimaye, wajumbe wakafanya uchaguzi na kuwapata “wanawake wa shoka” watakaoongoza WAWATA kuanzia mwaka 2020 hadi mwaka 2023.

WAWATA wamefungua mkutano mkuu wa 41 wa Uchaguzi hapo tarehe 29 Agosti 2020, wakati Mama Kanisa anaadhimisha kifodini cha Mtakatifu Yohane Mbatizaji. Huyu ni Nabii aliyetangaza na kusimamia ukweli, aliyekatwa kichwa na Mfalme Herode na wafuasi wake waliposikia wakaja na kuuchukua mwili wake kwenda kuuzika kwa heshima! Hivi ndivyo nyota angavu ya Yohane Mbatizaji, ilivyozimika baada ya kumshuhudia Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayeiondoa dhambi za ulimwengu. Yohane Mbatizaji ni kati ya watu maarufu wa Agano Jipya, anaishia kukatwa kichwa! Baba Mtakatifu Francisko anasema, kifodini ni huduma, utume na zawadi kubwa kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kifodini ni kielelezo cha ukatili wa binadamu dhidi ya watu waaminifu. Mfalme Herode alidhani kwamba, Yohane Mbatizaji alikuwa ni Nabii, alimwogopa, kwani alijua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu wa Mungu, akamlinda na kumsikiliza kwa furaha. “Alimsweka ndani” kwa vile Yohane Mbatizaji alimshutumu kwa uzinzi, lakini hakutumia fursa hii kutubu na kumwongokea Mungu. Hii ni kwa sababu alikuwa tayari amelewa madaraka kutokana na ufisadi, akasumbuliwa sana na dhamiri nyofu. Baba Mtakatifu anasema, Herodia aliyekuwa anamchukia Yohane Mbatizaji na matokeo yake akahakikisha kwamba, anamfutilia mbali kutoka katika uso wa dunia, kazi kubwa ya Shetani.

Herodia ni mwanamke ambaye hakufahamu maana halisi ya upendo na badala yake, akamezwa na chuki pamoja na uhasama dhidi ya Yohane Mbatizaji. Salome, binti Herodia aliahidiwa kupewa nusu ya Ufalme wa Herode! Watu hawa wote wanaonekana kwamba, walikuwa ni wateja wa Shetani, aliyehakikisha kwamba, shuhuda wa ukweli na utakatifu unazimwa kama “kibatari” na kutoweka katika sura ya nchi. Yohane Mbatizaji, akauwawa kikatili, peke yake mle gerezani kama ilivyo kwa wafidia dini na waungama imani wengi! Huu ni ushuhuda wa hali ya juu wa utakatifu unaofumbatwa katika maisha ya waamini. Ni maisha yanayomiminwa na sadaka inayotolewa, mwaliko na changamoto kwa waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu wahusika wanaozungumziwa kwenye Injili ya Marko mintarafu kifo chake, kama changamoto ya kumshuhudia Kristo si tu kwa maneno, bali kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu, kama alivyokuwa kwa Yohane Mbatizaji!

Ni katika muktadha huu, Askofu Desiderius M. Rwoma amewataka Wanawake Wakatoliki Tanzania kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ukweli na haki. Hizi ni tunu msingi zinazopaswa kuwaongoza katika maisha na utume wa Wanawake Wakatoliki Tanzania. Wanawake wajifunze kusamehe na kusahau, wawe ni vyombo vya haki, msamaha na upatanisho wa kweli na kwamba, hakuna sababu ya kuwekeana kinyongo na kutaka kulipizana kisasi. Hii ni changamoto inayoapaswa kufanyiwa kazi na wanawake wote, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Wanawake Wakatoliki wawe ni vyombo na mashuhuda wa mchakato wa uinjilishaji unaonafishwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Wanawake wawasaidie jirani zao kufahamu mafundisho tanzu ya Kanisa, Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na tunu bora za maisha ya ndoa na familia. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linawashukuru na kuwapongeza WAWATA kwa sadala na majitoleo yao katika, malezi na kuzitegemeza Seminari kwa hali na mali. Linawashukuru na kuwapongeza viongozi mbali mbali wa WAWATA waliojisadaka kutumikia na kuwajibika katika ngazi mbali mbali za uongozi pamoja na kuendelea kuwekeza katika malezi na majiundo makini kwa wasichana katika ngazi mbali mbali, ili kuwaandaa kwa leo na kesho yenye matumaini.

WAWATA: Mpango wa Muda Mrefu wa miaka minne (2019 hadi 2022) ulipitishwa na Mkutano Mkuu wa 39 wa WAWATA mara baada ya WAWATA  kuhudhuria Mkutano Mkuu wa  Wanawake Wakatoliki Ulimwenguni: (WUCWO) uliofanyika Dakar, nchini Senegal kunako mwezi Oktoba 2018. Hivyo basi miaka mitatu ijayo inapendekezwa kuwa uongozi mpya uendelee kutekeleza Mpango huo wa Muda Mrefu kwa kuzingatia, Tafakari ya nafasi ya WAWATA iliyofanyika katika adhimisho la Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara  pamoja na   Maazimio yaliyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., katika tafakari ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara na miaka 50 ya Halmashauri ya Walei kwa kuzingatia: DIRA: Wanawake Wakatoliki Wabebaji maji ya Uzima kwa Dunia yenye kiu ya Amani. DHIMA: Wanawake Wakatoliki Duniani tunaitwa kujitakatifuza ili kuutakatifuza ulimwengu katika Nyanja zote za maendeleo fungamani ya binadamu. “WUCWO” Women called to holiness to sanctify the world for a holistic   development.”

Mpango mkakati wa utekelezaji wa maazimio kwa mwaka 2019-2022: Ni wanawake kujitakatifuza ili waweze kutakatifuza jamii kuanzia katika: Familia, Jumuiya ndogondogo za Kikristo na Jamii kwa ujumla kwa njia ya, kutoa elimu juu ya wito wa kuwa watakatifu, Mafungo ya maisha ya kiroho, tafakari mbalimbali, maisha ya sala na tafakari pamoja na hija za kiroho ndani na nje ya Tanzania hasa kwenye maeneo matakatifu (Rej. Apostolic Exhortation Gaudete et exsultate: Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote (Rej. Encyclical Laudato si). WAWATA inatarajia kutenga siku moja katika mwaka ili kutoa elimu juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kusimama kidete kupiga rufuku matumizi ya taka za plastiki. Ni wajibu wa wanawake kupanda miti kuzunguka maeneo yao ili kuboresha mazingira. Ni wakati muafaka wa kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kuwa na mipango ya kusaidia familia zenye matatizo na mahitaji maalumu. Kuhakikisha kwamba watoto wanapata elimu ya awali na endelevu ya katekesi makini, Sakramenti za Kanisa na Neno la Mungu kwa wakati muafaka. Kuunda na kuboresha Jumuiya ndogo ndogo za watoto, ili wawe na viongozi wao, Ibada ya Misa zao na Kwaya za watoto kwenye Parokia na vigango vyao.

Watoto kuanzia darasa la kwanza wahimizwe kuingia Shirika la Utoto Mtakatifu ili kuwafunda wamisionari wa baadaye! Kuendeleza Mpango kazi wa Wasichana kama sehemu muhimu ya WAWATA. Kupiga vita ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya Wanawake na ulinzi wa mtoto katika hatua zote tangu kutungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika mtu. WAWATA wanahimizwa kuwa ni mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Maandalizi ya sherehe ya Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA (1972-2022): Septemba 2022 WAWATA Kama Jumuiya itatimiza Miaka 50 tangu kuidhinishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Ni tukio muhimu sana linalohitaji mandalizi ya kina mara tu uongozi mpya ukishashika hatamu. Kama moja ya shughuli za Jubilei hiyo Mkutano Mkuu wa 40 Uliamua kufanyike hija mbalimbali ikiwemo hija maalum ya nje ya Tanzania kama ile iliyoandaliwa mwaka 2019. Japo kuwa mandalizi ya hija yalianza ilibidi yasitishwe kutokana na janga la COVID-19.

Semina za Kanda Kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 Semina za Kanda zilizopangwa kufanyika kati ya Mwezi Juni na Julai 2020 ziliahirishwa. Hivyo inabidi zipangwe tarehe mpya ili kutekeleza mpango huu. Kuna umuhimu wa uongozi mpya wa kanda kushirikiana na uongozi uliopita ili kuendeleza jukumu hili. Katika Mkutano wa 40 ilikubaliwa kuwa semina za kanda zizingatie maagizo ya Taifa na WUCWO hususani Dira ya “Mwanamke Mkatoliki Mbebaji wa maji katika dunia yenye kiu ya Amani” Pamoja na Dhima na Mikakati elekezi iliyoaianishwa katika mpango wa muda mrefu. Uongozi wa WASMEP: Kutokana na mabadiliko yanayotarajiwa katika safu ya Uongozi wa WAWATA Taifa itabididi vile vile kufanya mabadiliko katika bodi ya Wadhamini ya WASMEP. WAWATA imewachagua: Mama Evaline Malisa Ntenga kutoka Jimbo kuu la Arusha kuwa Mwenyekiti Taifa, Mama Paschasia Rugumira, kutoka Jimbo Katoliki la Bukoba Makamu Mwenyekiti, Mama Stella Rwegasira kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam kuwa Katibu mkuu. Mama Faraja Mbena kutoka Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi, Katibu mkuu msaidizi. Na Mama Getrude Mtiga kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam amechaguliwa kuwa mhazini. WAWATA sasa ni wakati wa kuubeba vyema Msalaba wa huduma ya utumishi, hadi kieleweke!

WAWATA 2020
31 August 2020, 14:06