Maaskofu wa Colombia wanasitikitishwa na mauaji ya kinyama wa vijana nchini mwao Maaskofu wa Colombia wanasitikitishwa na mauaji ya kinyama wa vijana nchini mwao 

Colombia:Ask.Mkuu wa Bogotà: Tunaweza kuvaa barakoa lakini hatuwezi kukaa kimya mbele ya vurugu

Askofu Mkuu wa Bogota nchini Colomba anasema wanaweza kuvaa barakoa lakini hawawezi kukaa kimya mbele ya vurugu zinazoendelea kuongezeka katika nchi yao hivyo anatoa ushauri kwamba wasiruhusu uhusiano wao wa kijamii uondoke,sio kuruhusu ukue woga wa pande zote unaowalazimisha wajione kama maadui.Anasema hayo kutokana na vitisho vya mauaji yaliyotokea hivi karibuni nchini mwao.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Hatuwezi kukaa kimya mbele ya vikundi ambavyo vinawanyanyasa watu, watu wa asilia, Waafrika wa Colombia, wanaume na wanawake. Hatuwezi kukaa kimya mbele ya vitisho na mauaji ya wale waliorejeshwa na kujumuishwa kwenye mchakato wa amani. Hatuwezi kukaa kimya wakati vikosi vya wafu vinatafuta kuharibu tumaini la Wakolombia kwa damu na moto. Amesema hayo Askofu mkuu Luis José Rueda Aparicio wa  jimbo kuu katoliki la Bogotà, katika taarifa iliyochapishwa tarehe 18 Agosti 2020 kwenye Tovuti ya Baraza la Maaskofu kufuatia na mauaji yaliyofanywa siku za hivi karibuni dhidi ya vijana wa Cali na Samaniego (Nariño).

Zimwi linalokua na kuharibu nchi

Kwa mujibu wa Askofu Mkuu wa Bogota amesema “Tunaweza kuvaa barakoa lakini hatuwezi kukaa kimya mbele ya vuruguzinazoendelea na ambazo zinaoneshwa  dhidi ya watu wetu, kama zimwi anayeharibu na ambaye anakua katika nchi yetu”. “Vitendo hivi vya vikundi haramu vilivyo na silaha, ambavyo vinazuia uhuru wa jumuiya za vijijini na mijini, Askofu mkuu amethibitisha vinazalisha  tabia ya utamaduni wa kifo na hofu na inaonyesha kuwa vita bado vinaendelea na mapigano katika maeneo tofauti ya nchi kama vile  huko Chocó , katika uwanda wa Cauca, Nariño, Putumayo na katika eneo lote la Amazonia, Arauca na katika tambarare, huko Catatumbo, Magdalena  ya Kati, Kusini ya  Cauca antioqueño, Córdoba na Urabá.

Wito wa askofu Mkuu wa Bogota wa amani

Askofu mkuu wa Bogota kwa maana hiyo ametoa wito wake wa amani kwamba “Katikati ya janga hili tunatoa wito wa kusitisha mapigano, tunatoa wito wa kupambania umoja dhidi ya biashara ya dawa za kulevya, tunatoa wito wa maridhiano ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiikolojia.” Na hatimaye anawaalika viongozi wote wa nchi kufanya kazi kwa pamoja na kutekeleza mazungumzo ya dhati, ya uwajibikaji na ya kidugu. Kadhalika Askofu mkuu anaomba kwamba “tusiruhusu uhusiano wetu wa kijamii uondoke, sio kuruhusu ukue woga wa pande zote unaotulazimisha tujione kama maadui, tusijifungie kwenye ubishi wa milelele  wakati maskini zaidi katika mikoa yetu na katika vitongoji vya miji yetu wameachwa bila kujali, hadi kifo, kama vile habari inayokuja na kupita tu. Tunahitaji makubaliano ya raia kwa ajili ya amani, maisha na maridhiano”.

Maaskofu wanaonesha masikitiko na ukaribu wa familia za waathiriwa

Hata hivyo maaskofu katoliki nchini Colombia katika taarifa yao  kufuatia na matukio hayo wanasema:“Sisi, maaskofu Katoliki wa Colombia, tunaelezea masikitiko yetu makubwa na wasiwasi wetu kufuatia mauaji ya vijana 5 huko Cali na vijana 8 huko Samaniego (Nariño), waliouawa kikatili mnamo tarehe 11 na 15 Agosti”. Kwa maana hiyo maaskofu wa Colombia, katika taarifa iliyotolewa kwenye ukurasa wao kwenye Tovuti ya Baraza la Maaskofu wanaonesha  ukaribu wao na mshikamano kwa familia za waathiriwa na kwa wenyeji wa miji ambayo uhalifu huu ulifanyika. Katika taarifa yao inabainisha kuwa “matukio haya yanaongezwa na vitisho vinavyolenga watu fulani na jamuiya, mauaji ya viongozi wa kijamii na wapiganaji wa zamani wa FARC-EP, na mapigano ya silaha kwa  sababu ya udhibiti wa njia za usafirishaji wa dawa za kulevya, ambazo zimethibitishwa hivi karibuni katika idara nyingine za nchi, kama vile Norte de Santander, Chocó na Cauca”.

Serikali  inatakiwa kuhakikisha usalama wa raia

Mbele ya kukabiliwa na hali hii kubwa, mateso, shida, ukosefu wa fursa na ukiukwaji wa haki msingi za watu,  maaskofu wameomba serikali kuzingatia zaidi juhudi zake za kuhakikisha usalama na kutoa msaada kwa jamuiya zilizoathiriwa sana na wimbi hili la vurugu na kuendelea kusonga mbele kwenye njia ya utekelezaji wa Hati za Makubaliano ya Amani. Wameshauri vikundi haramu vilivyo na silaha kukomesha vitendo vyao vya vurugu na mapigano, katika hali ambayo tayari ni mbaya kutokana na janga la virusi vya corona na kutoa wito kwa  watu wa Colombia, ili waungane kwa ujasiri kujitoa kutetea uhai, kuwa na  maridhiano, kwa amani na kwa ajili ya mpango wa pamoja  na kuwaalika jumuiya nzima Katoliki kuongeza sala kwa kina.

19 August 2020, 14:42