Tarehe 23 Agosti 2020 Askofu mkuu Beatus Kinyaiya amezindua Kanisa la Parokia ya Chamwino IKulu. Rais JPM akaendesha harambeee ya kichangia Msikiti kwa ajili ya waamini wa dini ya Kiislama: Majadiliano. Tarehe 23 Agosti 2020 Askofu mkuu Beatus Kinyaiya amezindua Kanisa la Parokia ya Chamwino IKulu. Rais JPM akaendesha harambeee ya kichangia Msikiti kwa ajili ya waamini wa dini ya Kiislama: Majadiliano. 

Askofu mkuu Kinyaiya Abariki Kanisa; Rais JPM na Ujenzi wa Msikiti

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya tarehe 23 Agosti 2020 amebariki Kanisa la Parokia, Nyumba ya Mapadre na Pango la Bikira Maria, Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Chamwino. Ikulu, Jimbo kuu la Dodoma. Rais John Pombe Magufuli kwa ridhaa ya Askofu mkuu akaendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa Msikiti na kufanikiwa kupta shilingi milioni 48 na mifuko 48 ya saruji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” unapania kupyaisha ari na mwamko wa wito na utume wa kimisionari katika maisha na utume wa Kanisa na umuhimu wa Parokia kama kitovu cha uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Parokia, ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha imani tendaji. Parokia ni mahali ambapo, utamaduni wa watu kukutana unapaswa kujengwa na kudumishwa, ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene; mshikamano pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa ajili ya watu wote. Jumuiya ya Kiparokia inapaswa kuwa ni wasanii wa utamaduni wa ujirani mwema, kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa kwa namna ya pekee, katika Injili ya huduma.

Pamoja na ukweli huu, Mama Kanisa anatambua kwamba, kuna uhaba mkubwa wa miito ya Kipadre katika baadhi ya maeneo, kiasi kwamba, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache katika shamba la Bwana. Kumbe, kuna haja ya kuwa na mwelekeo na utambuzi mpya wa “dhana ya Parokia”. Parokia inapaswa kuwa ni Jumuiya ya waamini inayoinjilisha na kuinjilishwa. Hii ni Jumuiya inayotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji! Parokia ni mahali muafaka pa waamini kukutana, ili hatimaye, kuweza kuutafakari Uso wa huruma ya Mungu katika kina na mapana yake. Ni mahali muafaka pa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Parokia ni mahali pa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kurithisha imani, ili kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara kwa kutambua kwamba, familia, kimsingi ni Kanisa dogo la nyumbani.

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania, tarehe 23 Agosti 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kuzindua Kanisa la Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Chamwino, Jimbo Kuu la Dodoma. Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania akiwa Kanisani hapo tarehe 7 Juni 2020, aliendesha harambee ya kuchangia upanuzi wa Kanisa la Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Chamwino ili kuweza kukidhi ongezeko la idadi ya waamini katika Parokia hii, baada ya Jiji la Dodoma kupanuka kwa kasi kubwa. Rais Magufuli alifanikisha kuchangisha kiasi cha shilingi milioni 17, 229, 000 na mifuko 76 ya saruji na kutaka upanuzi wa Kanisa hili kuanza mara moja bila kuchelewa! Tarehe 23 Agosti 2020 Kanisa la Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Chamwino, Nyumba ya Mapadre pamoja na Pango la Bikira Maria yakazinduliwa Askofu mkuu Beatus Kinyaiya, matendo makuu ya Mungu.

Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Kinyaiya amekazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa na kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu. Waamini wajibidiishe kumfahamu Kristo Yesu kwa njia ya Maandiko Matakatifu, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na huduma kwa maskini. Amewaalika waamini wa Chamwino kulitumia Kanisa kama nyumba ya: Sala, Ibada na mahali pa kuadhimishia Mafumbo Mtakatifu ya Kanisa. Ili waamini waweze kujichotea neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa, hawana budi kujiandaa kikamili na kushiriki vyema katika maadhimisho ya Mafumbo hayo. Tume ya Taifa ya Uchaguzi, NEC, hivi karibuni ilitangaza kwamba, kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani zitaanza rasmi tarehe 26 Agosti hadi tarehe 27 Oktoba 2020, huku tarehe ya uchaguzi ikianguakia siku ya jumatano ambayo ni tarehe 28 Oktoba 2020. Askofu mkuu Kinyaiya amewataka watanzania wenye sifa za kupiga kura kujitokeza kwa wingi ili kutekeleza wajibu wao kikatiba.

Amewataka watanzania kuwachagua wachamungu na watu wenye hofu ya Mungu. Wawe ni watu wanaojizatiti zaidi kutafuta mafao mapana ya kitaifa; watu wenye ari na moyo wa kutaka kukuza na kudumisha tunu msingi za kitanzania ambazo ni: amani, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa licha ya tofauti zao mbali mbali. Watanzania wawachague viongozi wanaojiamini na wala si watu wanaotegemea imani za kishirikina; viongozi wasiopenda kupokea wala kutoa rushwa, bali watu wanaotafuta ridhaa ya kuongoza nchi kwa njia za halali. Wakati wa kampeni wawasikilize na kupima sera, ili hatimaye, wafanye uamuzi wa busara wakati wa kupiga kura! Askofu mkuu Kinyaiya katika sala maalum ya kumwombea Rais Magufuli, amewaombea pia wale wote wanaowania nafasi za uongozi katika ngazi mbali mbali nchini Tanzania, ili wapate ulinzi kutoka juu mbinguni, wawe salama salimini katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020. Mchakato mzima uanze na kupata hitimisho lake kwa baraka za Mwenyezi Mungu. Wote wawe na afya njema ya kiroho na kimwili, tayari kuwatumikia watanzania bila ya kujibakiza, daima wakitetea utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi.

Kati ya mambo yaliyovuta hisia za watu wengi kutoka ndani na nje ya Tanzania ni kitendo cha unyenyekevu, kilichooneshwa na Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, kuomba ruhusa kwa Askofu mkuu Kinyaiya ili aweze kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti kwa ajili ya waamini wa dini ya Kiislam, eneo la Chamwino Ikulu, Dodoma, ambao kwa sasa haukidhi ongezeko la idadi ya waamini wa dini ya Kiislam katika eneo hili. Katika kampeni hii, Rais Magufuli amefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 48, mifuko 48 ya saruji na lori 5 za mchanga kutoka kwa familia ya Mungu Parokia ya Chamwino, Jimbo kuu la Dodoma. Rais Magufuli ametumia fursa hii pia kukagua eneo la ujenzi wa Msikiti huu mpya. Lengo ni kuliwezesha eneo la Chamwino Ikulu kuzungukwa na wachamungu. Kumbe, kampeni kwa ajili ya kuchangia Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo eneo hili, itaendelea.

Kwa upande wake, Padre Charles Kitima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katokiki Tanzania, TEC, amempongeza Rais Magufuli kwa uchaji wa Mungu, upendo kwa watanzania na kwamba, amefanya mambo makubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi. Ni kati ya viongozi wa Bara la Afrika waliojipambanua kupambana na rushwa bila makunyanzi na matokeo yake yanaonekana. Leo hii, Rais Magufuli ni mfano bora wa kuigwa katika mapambano dhidi ya rushwa ndani na nje ya Bara la Afrika. Ikumbukwe kwamba, uinjilishaji mpya unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza.

Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu Injili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia ni mambo yanayowaunganisha wote bila ubaguzi hata kidogo. Damu ya Wakristo, itaendelea kuwa ni mbegu ya Ukristo na mchakato wa umoja wa Wakristo. Wakristo wote wanateseka na kudhulumiwa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kumbe, uekumene wa damu una nguvu sana kama kielelezo cha ushuhuda wa imani yenye mvuto na mashiko! Takwimu zinaonesha kwamba, hata katika ulimwengu mamboleo, bado kuna Wakristo wanaoendelea kuteseka kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni katika muktadha huu, Mashuhuda wa uekumene wa damu, wanawataka Wakristo kubaki wakiwa wameungana, ili mbegu hii iweze kuzaa matunda ya umoja, upendo na mshikamano wa dhati.

Leo hii kuna wafiadini wengi zaidi duniani, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo. Mashuhuda wa uekumene wa damu kutoka katika Makanisa mbali mbali kwa sasa wanaunganishwa na kifungo cha upendo huko mbinguni. Mbegu waliyopandikiza duniani, itazaa matunda kwa wakati wake. Lengo kuu ni ushuhuda wenye mvuto kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Mama Kanisa anaendeleza juhudi za uinjilishaji unaofumbatwa pia katika mchakato wa majadiliano ya kidini. Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Chamwino Dodoma
24 August 2020, 13:34