Maandamano makali nchini Mali kuomba Keita ajiuzulu urais Maandamano makali nchini Mali kuomba Keita ajiuzulu urais 

Mali:Viongozi wa dini nchini Mali watoa wito kuwataka watu kuwa watulivu!

Rais wa vyama vya kitume na utume wa kimisionari wa uinjilishaji wa kiprotestanti,amewaomba wakristo kuombea amani ya nchi ya Mali na zaidi kusali kwa kuziombea familia ambazo zimekumbwa katika mivutano ya kisiasa na kijamii.

Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican

Viongozi wa dini na Serikali nchini Mali wamekaa chini na kujadili mstakabali wa nchi yao. Mkutano huo ulijumuisha viongozi wa dini akiwemo Kardinali Jean Zerbo, Askofu Mkuu wa jimbo kuu Bamako, Rais wa Baraza la Ushauri la Waislam Bwana Cherif Ousmane Madani Haidara na Nouhou Ag Infa Yattara, Rais wa Jumuiya za kitume na za umisionari wa uinjlishaji wa kiprotestanti. Viongozi hawa wameutaka umma kutumia mitandao inayopatikana nchini Mali na mitandao mingine ya kijamii ili kutatua migogoro na machafuko yanayoendelea nchini humo. Hata hivyo kwa mujibu wa Kardinali Zerbo amekiri kuwepo kwa machafuko hayo na kwamba nchi ya Mali haistahili matendo ya uvunjifu wa amani yaliyofanywa kipindi kilichopita katika miji ya nchi hiyo.

Wamempinga rais Ibrahim Boubacar Keita, ambaye anaonesha kutokuwa na uwezo wa kutatua changamoto kubwa zinazoikumba nchi ya Mali zikiwemo kukosa usalama kwa raia wake, rushwa, kufungwa kwa mashule na Taasisi ya Afya huko Bamako na kusababisha kufanyika kwa maandamano yaliyoongozwa na kikundi cha M5 (RFP), yaani kikundi cha Muungano wa Vikosi vya Kizalendo, na kusababisha takribani watu 11 kufariki na  makumi kutiwa mbaroni. Viongozi hawa wa dini wameomba ushirikiano kutoka kwa washiriki wa kisiasa, wa kidini na jamii nzima. Jamii imechoshwa na migogoro ya kiuchumi na mashambulio ya kijihadi yanayoendeleza machafuko ya nchi humo, wanasema. Pamoja na haya wamekemea pia hatua zilizochukuliwa na Rais za kuzuia harakati za kidemokrasia na kumwomba afunge mikutano ya Bunge ili kupisha harakati za kuunda serikali ya mpito.

Upinzani unahitaji ushirikiano wa Rais, lakini mara nyingi vyama vya Serikali vimekuwa vikiwachukulia viongozi wa upinzani kama vinara wa maandamano na ya waandamanaji na kuwatia nguvuni. Ikumbukwe kuwa, Jumamosi jioni, tarehe 11 Julai 2020, Rais wa Baraza la Ushauri la Kiislam, aliwaomba umati wa watu kuwa na utulivu na kusitisha maandamano yanayoshiria machafuko ya nchi. Aidha, ameomba kutatutua changamoto zinazowakabili kwa njia ya majadiliano. Viongozi wa kislam wameiomba Serikali kutimiza wajibu wake wa kutua huduma stahiki kwa wananchi wake na kuawachia waandamanaji wa makundi ya M5 RFP waliokamatwa na kufungwa.

Hata hivyo zaidi ya wapinzani 20 walikamatwa toka Ijumaa wakiwemo viongozi wa maandamano ya kutaka kujiuzulu kwa Rais Keita. Kiongozi wa maandamano nchini Mali, ambaye pia ni kiongozi wa kidini, Imam mwenye ushawishi mkubwa Mahmoud Dicko, alitoa wito wa kuwepo utulivu Jumapili. Tarehe 12 Julai 2020. Hali ya wasiwasi iliendelea kushuhudiwa katika mitaa ya mji huo hapo, wakati mamia ya watu walipokusanyika kuhudhuria mazishi ya waandamanaji waliouawa. Maandamano hayo katika miji kadhaa ya nchi, yalisababisha kuundwa kwa vuguvugu la M5, linalowajumuisha viongozi wa kidini, wa kisiasa na wale wa asasi za kiraia, liloanzisha maandamano tangu mwanzoni mwa mwezi Juni.

Katika juhudi za kumaliza maandamano nchini mwake, Rais Keita alitangaza kuunda serikali ya mseto na kuivunja mahakama ya kikatiba, ambayo uamuzi wake wa kubatilisha matokeo ya awali ya uchaguzi wa bunge mapema mwaka huu, ulikuwa kiini cha maandamano hayo. Licha ya tangazo hilo la Rais Keita, viongozi wa waandamanaji wanaendelea kumtaka ajiuzulu. Rais Ibrahim Boubacar Keita mwenye umri wa miaka 75, ameiongoza Mali tangu mwaka 2013, baada kushinda katika uchaguzi wa kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa pili mwaka 2018.

15 July 2020, 15:39