Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 15 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Nguvu ya Neno la Mungu katika maisha ya mwamini. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 15 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Nguvu ya Neno la Mungu katika maisha ya mwamini. 

Tafakari Jumapili ya 15 ya Mwaka A: Nguvu ya Neno la Mungu!

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 15 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa yanatufundisha na kutukumbusha juu ya nguvu ya Neno la Mungu kwa wale wanaolipokea na kuliishi na wajibu wa kila mwanadamu katika kulipokea, kulitunza na kuliishi Neno hili linalopandwa katika mioyo yetu ili litupatie matunda ya ukombozi wetu ni kama maji ya mvua yalowanishapo ardhi na mimea kuchipua.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 15 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya leo yanatufundisha na kutukumbusha juu ya nguvu ya Neno la Mungu kwa wale wanaolipokea na kuliishi na wajibu wa kila mwanadamu katika kulipokea, kulitunza na kuliishi Neno hili linalopandwa katika mioyo yetu ili litupatie matunda yake ya ukombozi wetu ni kama maji ya mvua yalowanishapo ardhi na mimea kuota. Lakini kama ilivyo kwa mbegu nzuri na iliyo bora ikipandwa katika udongo wenye rutuba inavyozaa mazao mengi na bora zaidi ndivyo lilivyo neno la Mungu lahitaji kupokelewa, kutunzwa na kuliishi ili kupata mafao yake. Waraka kwa Waebrania 4:12 unatuambia kuwa: Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu tena lina makali kuliko upanga uwao wote wenye makali kuwili, tena linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake, tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.

Katika somo la kwanza Nabii Isaiya ndiye anayelifananisha neno la Mungu na maji ya mvua yanavyoleta uhai kwa viumbe hai. Kama vile mvua inyeshapo haina budi kuilainisha ardhi, na kuichipusha, kustawisha na kuizalisha mimea ikampa mtu apandaye mbegu na mtu alaye chakula, ndivyo lilivyo neno litokalo katika kinywa cha Mungu kwa njia ya watumishi wake haliwezi kurudi bure bali lazima mapenzi ya Mungu ambayo kwayo hilo neno lilitoka lazima yatimizwe. Neno la Mungu linaonya, linakaripia, linafundisha, linarekebishwa na anaheri yule aonywaye na kuonyeka, akaripiwapo na kukaripika, afundishwapo na kufundishika, arekebishwapo na kurekebeshika, kwani ataishi kwa furaha maisha ya hapa duniani na kupata heri ya milele mbinguni. Ndivyo ilivyokuwa kwa waisraeli walipolipokea neno la Mungu, Mungu aliwakomboa kutoka utumwani Babeli na kuwarudisha katika nchi yao ya ahadi. Na kinyume chake ni kweli kwa wasiolipokea na kulikubali neno la Mungu adhabu ya milele ni yao nayo huanzia katika maisha ya hapa duniani.

Mtume Paulo katika Somo la Pili anatueleza kuwa mateso na mahangaiko ya wakati huu sio mahangaiko au mateso yaletayo kifo bali ni maandalizi ya mwanzo wa maisha mapya ya umilele. Paulo anatueleza kuwa kikomo cha mtu na ulimwengu mzima ni kimoja, kuuona utukufu wa Mungu. Tunajua kwamba ulimwengu umelaaniwa kwa ajili ya dhambi ya binadamu. Lakini kwa kadiri ile Mungu atakavyoitukuza miili yetu ndivyo atakavyofanya kwa ulimwengu mzima, viumbe vyote vitarudi na kuishi uhuru na utukufu wa watoto wa Mungu. Mtakatifu Yohane Christostom anasema kuwa katika mfano wa mpanzi Yesu anaeleza upendo na huruma ya Mungu inayojidhihirisha katika kazi na matendo yake katika kumkomboa mwanadamu kutoka mahangaiko na utumwa wa dhambi. Yesu anaposema mpanzi alitoka, ni kile kitendo cha Mungu muweza wa yote aliyeko mahali pote kujishusha, kuchukua hali yetu ya kibinadamu katika fumbo la umwilisho akawa mwanadamu na kuja kukaa kwa kuwa sisi hatukuwa na uwezo wa kumwendea yeye aliye mkatatifu kwa sababu ya dhambi zetu. Mungu kwa upendo wake, huruma yake na uvumilivu wake akashuka kuja kukaa nasi na kupanda ndani mwetu neno la uzima.

Uvumilivu wa Mungu katika kupanda Neno lake mioyoni mwetu bila ubaguzi, bila kuangalia mapungufu na dhambi zetu, akiheshimu uhuru wa kila mmoja wetu ni kama uvumilivu wa mkulima ambaye anapanda mbegu mahali popote shambani mwake bila kubagua maeneo akiwa na matumaini kuwa zitamea na kutoa mazao. Uvumilivu na matumaini ya mkulima vinajidhihirisha katika mfano wa mpanzi kama unavyosimuliwa na mwinjili Matayo ambapo licha ya kuwa kuna mambo ya kukatisha tamaa, ishara za majanga na matumaini madogo ya mkulima kupata mazao kwasababu; ndege wanavamia na kula mbegu kabla ya kuota, miamba inazuia mizizi ya mimea iliyoota kukua na hivyo jua linaikausha, miiba kuinaisonga mimea iliyoota na hivyo kushindwa kuzaa, mkulima huyu hakati tamaa, anavumilia na kuweka matumaini yake katika sehemu ndogo ya udongo mzuri ambapo mbegu zilimea na kuzaa mazao mazuri na mengi. Kama ilivyo kwa mbegu bora inavyotegemea udongo mzuri wenye rutuba ili imee, ikuu, ikomae na kutoa mazao mengi na mazuri, ndivyo ilivyo kwa neno la Mungu ili, liingie na kupenye mioyo yetu, likue, likomae na kuzaa matunda bora ndani ya maisha yetu linahitaji utayari wetu, imani yetu, upendo wetu, matumaini yetu na ujasiri wetu katika kulipokea, kulipa nafasi ndani mwetu na kuliacha litubadilishe.

Neno hili lapita uwezo wa ufahamu wetu, kumbe imani, matumaini, upendo, uvumilivu na usikivu vyahitajika ili liweze kuzaa matunda yake ndiyo maana Yesu anahitimisha mfano huu kwa kusema mwenye masikio na asikie. Katika ulimwengu mamboleo ambapo kuna sauti nyingi nzuri, tamu na za kupendeza masikioni na kutufanya tusikie lakini tusilielewe Neno la Mungu, vitu vingi vya kupenda mbele yetu na kuyafumba macho yetu yasiuone wema wema wa Mungu maana mioyo yetu imekuwa mizito tunahitaji kujifunza kwa bidii zaidi kulisoma, kulisikiliza na kulitafakari Neno la Mungu ili kwamba hawa ndege wasilile, hii miamba isilizuie kuzama mioni mwetu na jua hili likaikausha, ili hii miiba isilisonge na kulizuia lisizae matunda yake. Basi tumwombe Mungu atuonyeshe uso wake katika haki kama wimbo wa mwanzo unatuasa ili tuamkapo tushibishwe kwa sura yake, ambapo Mungu mwenyewe anatuonyesha mwanga wa ukweli wake kama tukiishika imani yetu na pale tunapodanganyika na yule mwovu kwa kulinyakua neno la Mungu ndani mwetu Roho Mtakatifu atusaidie kuturudisha katika njia ya haki, udhia au dhiki ikitokea kwa ajili ya Neno la Mungu tusichukizwe na kuliacha na shughuli za dunia hi ina udanganyifu wa mali usitusonge kiasi kwamba tukalisahau Neno la uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo.

09 July 2020, 13:48