Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 16 ya Mwaka A wa Kanisa: Huruma ya Mungu imefumbatwa katika imani na matumaini katika toba na wongofu wa ndani. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 16 ya Mwaka A wa Kanisa: Huruma ya Mungu imefumbatwa katika imani na matumaini katika toba na wongofu wa ndani. 

Tafakari Jumapili 16 ya Mwaka A: Uvumilivu, Imani na Matumaini!

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya 16 inaendelea kutufundisha ukuu wa Huruma ya Mwenyezi Mungu ambaye hana haraka katika kutuadhibu tunapomkosea. Anatuacha tuendelee kuishi pamoja na walio wema mpaka wakati wa hukumu ya mwisho. Uvumilivu huu wa Mungu unatupata nafasi kuifaidi huruma yake kwa kufanya toba kwa wakati ili hukumu ya mwisho isitutie hatiani.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 16 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Kwa anguko na Adamu na Eva mahusiano kati ya Mungu na mwandamu yanaelezwa katika uhusiano wa huruma na upendo Mungu kwa mwanadamu. Huruma hii inaelezwa kwa namna mbalimbali ili mwanadamu aweze kuilewa na kuipokea. Masomo ya domenika ya 15A yalieleza uhusiano wa huruma na uvumilivu wa Mungu kwa kuhusianisha Neno lake na maji ya mvua na Neno lake na mbegu alizopenda mpanzi tena kwa uvumilivu. Masomo ya Dominika hii yanaendelea kutufundisha ukuu wa Huruma ya Mungu ambaye hana haraka katika kutuadhibu tunapomkosea. Anatuacha tuendelee kuishi pamoja na walio wema mpaka wakati wa hukumu ya mwisho. Uvumilivu huu wa Mungu unatupata nafasi kuifaidi huruma yake kwa kufanya toba kwa wakati ili hukumu ya mwisho isitutie hatiani.

Somo la kwanza kutoka kitabu cha Hekima ya Sulemani linatueleza kuwa Mungu anaweza kuadhibu mabaya na kulipa mema; angependa kutuangamiza kwa uovu wetu lakini kwa hekima na huruma yake anatupatia nafasi ya kutubu kama anavyosema Sulemani; “Walakini, desturi yako unauzuia hata uwezo wako, na kuhukumu kwa upole, na kututawala kwa uvumilivu mwingi. Yaani uwezo unao, wakati wote utakapo kuutumia…lakini endapo watu wametenda dhambi unawajalia toba.” Hulka hii ya Mungu ilimfanya mzaburi atafakari na kuimba wimbo wa mwanzo domenika hii unaosema; Tazama, Mungu ndiye anayenisaidia; Bwana ndiye anayenitegemeza nafsi yangu. Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhambihu; ee Bwana, nitalishukuru jina lako maana ni Jema (Zab. 54:4,6) na katika wimbo wa katika tunaimba na kusema; kwa maana wewe, u mwema, umekuwa tayari kusamehe (Zab. 86:5).

Katika Injili huruma ya Mungu imefumbatwa katika uvumilivu wake na imani aliyonayo kwa mwanadamu ya kubadilika na kumrudia yeye akitumia sera ya viache vyote vikuwe pamoja hata wakati wa mavuno. Tunasali vyema katika sala ya imani kuwa Mungu hadanganyiki wala hadanganyi na mafundisho ya Kanisa yatueleza kuwa Mungu ajua yote hata mawazo yetu. Kumbe mwovu yeyote kunawiri si kwa sababu Mungu haoni uovu wake bali ni huruma yake na uvumilivu wake Mungu ndivyo vinayompa mdahmbi nafasi ya kutubu na kubadilika. Basi tutumie vizuri huruma na uvumilivu huu tusingoje hata siku ya mwisho siku ya hukumu. Tusidhani na kujiaminisha kuwa tunapoendelea kufanikiwa licha ya matendo yetu maovu kwamba Mungu haoni au hana nguvu ya kutuadhibu lakini ni kinyume chake anaona yote na uwezo anao ila anatupatia nafasi ya kutubu na kubadilisha mwenendo wetu. Tutumie vizuri Sakramenti ya kitubio anakopitishia Mungu huruma yake kwetu wadhambi.

Injili inatukumbusha tujikinge dhidi ya wapanda magugu. Shamba linaweza kulinganisha na nafsi ya mtu binafsi. Kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kila alichokiumba Mungu na tazama ni chema sana. Kwa uumbaji Mungu anakuwa amepanda ndani mwetu imani na mwenendo mwema wa maisha. Lakini katika kukua kwetu tubadilika na kujifunza tabia tofautitofauti kutoka kwa watu waovu. Yoshua bin Sira anasema “marafiki wabaya huharibu hata watu wema.” Katika hali hii ndani mwa mtu adui shetani aliyefanya kazi kupitia kwa marafiki waovu amepanda magugu ndani mwa mtu na hivyo mtu huanza kuwa na tabia zisizokuwa mzuri. Kumbe kila mmoja ana wajibu wa kujilinda na yule mwovu asije kupanda ndani mwake uovu wake. Wazazi nao wana wajibu wa kuwalinda na kuwaelekeza vyema watoto wao ili asiwepo yeyote wa kupanda magugu katika mwenendo wa maisha yao. Mtoto asipokuwa na msingi nzuri toka nyumbani, ni rahisi kwa yule mwovu kumfundisha tabia mbaya na za ajabu kabisa ambazo zitamuangamiza.

Jambo lingine tunalofundishwa katika Injili hii ni kutowahukumu wengine kwani ni vigumu kutambua nani mwema na ni nani mbaya kwa macho na maono yetu. Hivyo, tusiwahukumu watu na kuwawekea alama kwamba huyu ni mwema na huyu ni mbaya kwa kuangalia tu mwonekano wa nje. Mtu anaweza kuwa anaonekana mwema kwa macho au maneno lakini ni mwovu ndani mwake. Mwingine anaweza kuwa anaonekana kwa watu kuwa ni mwovu; lakini ni mwema ndani mwake; tatizo tu ni kwamba watu hawakumuelewa. Tuache hukumu kwa Mungu anayejua mioyo ya watu. Paulo anatuonya akisema Basi msihukumu kabla ya wakati wake; acheni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayafichua mambo ya giza yalofichika, na kuonesha wazi nia za mioyo ya watu (1Kor 4 :5). Hii haimaanishi kuwa watu wakikosea tuwaache tu na tusiwaadhibu au kuwakosoa. Kinachokatwaza hapa ni kukata tamaa kwamba mtu hawezi kubadilika. Muache atabadilika. Hata kumkemea au kumuadhibu aliyekosa inaonesha kuwa bado tuna matumaini katika mtu huyo kuwa anaweza kubadilika. Pasingekuwa na matumaini pasingekuwa na haja ya kumuadhibu.

Injili inatufundisha pia kutowabagua watu wasio na uwezo. Wale watumishi walitaka kung’oa magugu ili ngano ikue vizuri. Katika maisha yetu kuna mwelekeo wa kuwanyanyasa au kuwatenga wasiojiweza na walemavu ili walio wazima waishi vizuri. Huu ndio mwanzo wa utamaduni wa kifo unaolenga kukatisha maisha maisha ya wanyonge kama walemavu, vikongwe, wagonjwa mahututi na hata ambao bado hawajauona mwanga wa jua wasio na hatia wala uwezo wa kujitetea wanakatishwa maisha kwa kuuwawa tumboni mwa mama zao. Viacheni vyote vikuwe hata wakati wa mavuno. Malaki anashuhudia ukweli huu akisema Hapo ndipo mtakapotambua tena tofauti iliyopo kati ya waadilifu na waovu; naam, kati ya mtu anayemtumikia Mungu na asiyemtumikia (Mal 3 :18). Kristo anasisitiza pia akisema atawaweka kondoo upande wake wa kulia na mbuzi upande wake wa kushoto (Mt 25 : 33). Watu wabaya wakijidai katika kufanikiwa kwao watambue kuwa hukumu ipo. Kumbe tusishangae kwa nini Mungu hawaondoi haraka watu waovu na kuwaulia mbali. Anaviacha vyote vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno, aje kutenganisha ngano na magugu.

Injili inatufundisha pia kutokung’ang’ania yale yanatufanya tuukose ufalme wa Mungu na kutualika kuyacha. Kwa asili sisi ni binadamu, lakini tusione kuwa kule kuwa mwanadamu ni kitu cha kushikamana nacho kwa nguvu bali tuachilie hayo yote tujichukulie hali ya kimungu na tuonekane kama watoto wa Mungu. Itamfaa nini mtu kuupata ulimwengu mzima na kuipoteza nafsi yake” (Mk. 8 :36). Maisha ya mwanadamu tangu anapotungwa mimba ni safari ya kuacha. Tunaanza kwa mbegu za kike na kiume kuacha sehemu zao zinakozaliwa na kuamua kuungana, baada ya hapo kilichoundwa kwa muunganiko wa mbegu kinaamua kuacha tumbo la mama kichanga kinazaliwa. Tunaacha uchanga na kuingia utotoni, tunaacha utoto tunaingia ujana, tunaacha ujana, tunaingia utu uzima, tunaacha utu uzima, tunaingia uzeeni. Tunaendelea kuacha taratibu kadiri umri unavyoongezeka mpaka hatua ya mwisho tunapokufa na kuiacha dunia na mambo yake yote. Kumbe kufa ndiyo hatua ya mwisho ya kuacha ambapo hata roho inauacha mwili ndiyo maana Kristo aliamua kufa Msalabani kutufundisha kuacha yote kwa ajili ya Mungu.

Mtume Paulo anasema “Naam, tunalo tumaini na ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana 2Kor. 5: 8. Tusipojifunza kuacha taratibu kwa hiari, tutalazimika kuacha tutakapo kufa. Kifo kikitufikia tutaacha yote. Huwezi kufanikiwa katika lolote kama hauna moyo wa kuacha. Huwezi kuwa na uaminifu katika ndoa au wito wowote au jambo lolote kama hauna moyo wakuacha na kusema inatosha. Huwezi kuwa na kiasi katika jambo lolote kama hauna moyo wa kuacha. Katika maisha ya kawaida, huwezi kuwahi sehemu yoyote kama huna moyo wa kuacha kile unachofanya. Huwezi kutunza maagano kama huna moyo wa kuacha. Huwezi kusema inatosha kama huna moyo wakuacha. Tukishafanikiwa kutambua kuwa tuko dhaifu, basi tukubali kuacha. Kama ni hasira ukubali kuacha, kama ni ubaguzi ukubali kuacha, kama ni wivu ukubali kuacha, kama ni urafiki mbaya ukubali kuacha, kama ni uongo na kusengenya wengine ukubali kuacha, kama ni kumdharau mme wako au mke wako, ukubali kuacha, kama ni nyumba ndogo au kidumu, ukubali kuacha, kama ni ulevi ukubali kuacha.

Kama anavyotuambia Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wa Warumi kuwa sisi binadamu ni dhaifu, hali kadhalika sala zetu. Lakini kwa sababu Roho wa Mungu yu ndani mwetu sala zetu zinapata mastahili na kusikilizwa na Mungu. Maana Roho hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo ; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu. Basi tumuombe Mungu kupitia huyo Roho atujalie kuwavumilia watu wabaya huku tukiwaombea na kuwaonyesha mfano mzuri wa maisha ili nao waachane na uovu wabadilike na kumrudia Mungu. Pia Mungu atujalie tutumie vyema uvumilivu wake wa kutuacha tuendelee kuishi hata kama tunatenda mabaya kwani si kwamba haoni bali anatupatia muda wa kutubu. Atujalie tuwe na moyo wa toba na kubadilika ili hukumu ya mwisho itukute tukiwa ngano bora na hivyo, tukusanywe katika ufalme wa mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.

17 July 2020, 10:28