Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya 17 ya Mwaka A wa Kanisa: Ufalme wa Mungu ni hazina iliyofichika, inahitaji sadaka na majitoleo makuu ili kuweza kuupata! Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya 17 ya Mwaka A wa Kanisa: Ufalme wa Mungu ni hazina iliyofichika, inahitaji sadaka na majitoleo makuu ili kuweza kuupata!  (AFP or licensors)

Tafakari Jumapili 17 Mwaka A: Ufalme wa Mungu Uko Kati Yenu!

Wazo kuu katika tafakari hii ni thamani ya kuwa katika ufalme wa Mungu hakuwezi kufananishwa na kitu kingine chochote. Kumbe, kufanya kila linalowezekana ili kuupata ufalme wa Mungu ni kwa maana zaidi katika maisha Tumwombe basi Mungu ayatie nuru macho ya mioyo yetu ili katika ulimwengu huu uliojaa vitu vingi vizuri, kila mara tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo. Ufalme!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 17 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Wazo kuu katika tafakari hii ni thamani, gharama na utamu wa kuwa katika ufalme wa Mungu hakuwezi kufananishwa na kitu kingine chochote. Kumbe, kuacha vyote na kufanya kila linalowezekana ili kuupata ufalme wa Mungu ni kwa maana zaidi katika maisha ya mwanadamu. Tumwombe basi Mungu ayatie nuru macho ya mioyo yetu ili katika ulimwengu huu uliojaa vitu vingi vizuri, kila mara tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo. Katika somo la kwanza la kitabu cha kwanza cha Wafalme, Mungu anamtokea Mfalme Sulemani alipohiji Gibeoni na kumwambia omba utakalo nikupe. Sulemani anaomba busara ili aweze kuliongoza vyema taifa lake akisema; Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?

Mwenyezi Mungu alikubali ombi lake, akamwongezea fahari, mali na maisha marefu kwani moyo uliomnyenyekevu hufungua milango ya Mungu. Mungu akamwambia, Kwa kuwa hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako tazama nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe. Chaguo la Sulemani ni kama mwangwi wa maneno ya Yesu yasemayo tafuteni kwanza ufalme wa Mungu mengine yote mtapewa kwa ziada. Je, Mungu akitokea nyakati hizi akakuambia omba lolote utaomba nini? Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake kwa Warumi anatuambia kuwa Mungu alitujua pia alituchagua tangu milele. Hivyo maisha yetu yamo katika umilele wa Mungu. Tumeshirikishwa uzima huu kwa njia ya Kristo. Katika Injili ilivyoandikwa na Mathayo tunaendela kutafakari sura ya 13 ambapo Matayo amekusanya mifano ya Yesu inayoelezea ufalme wa Mungu. Domenika hii Yesu anatumia mifano ya hazina na lulu kuelezea dhamani ya ufalme wa Mungu. Nao mfano wa wavu, kama ulivyo mfano wa magugu, wasema kuwa siyo watu wote wanaoingia katika Kanisa la Kristo wataokoka katika hukumu ya mwisho kama hawajiweki katika hali njema ya kiroho wataukosa ufalme wa Mungu.

Ufalme wa Mbinguni ni nini? Ufalme wa Mbinguni ni hali ya uwepo wa Mungu unaoleta furaha kwa wale walioko ndani yake. Ufalme huu unaanza kujengeka na kudhihirika hapa ulimwenguni, na baadaye kukamilika Mbinguni. Hapa ulimwenguni, mtu anakuwa katika ufalme wa Mungu pale anapoishi katika uwepo wa Mungu na kutimiza mapenzi ya Mungu. Kanisa ni chombo cha kuueneza ufalme wa Mungu na kuwaleta watu katika ufalme wa Mungu. Kwa maana hiyo, mtu anaweza akawa ndani ya Kanisa lakini yupo nje ya Ufalme wa Mungu kama haweki juhudi kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu. Tunasali katika sala ya Baba yetu tukisema; “Ufalme wako ufike utakalo lifanyike duniani kama mbinguni” (Mt 6:10). Kuingia katika umoja wa Kanisa unapaswa kuwa mwaliko wa awali wa kuingia katika ufalme wa Mungu. Tunaingizwa katika juya (nyavu). Kazi inayobaki ni kuhakikisha tunadumu katika kutenda mema mpaka mwisho wa maisha yetu ili wakianza kuchambua vilivyo katika juya ama neti basi tukutwe tukiwa tunafaa.

Hakuna kilicho kizuri kama kuwa ndani ya Ufalme wa Mungu. Lengo la maisha ya binadamu ni kuwa na furaha. Furaha ni hali ya kuridhika inayoletwa na tendo jema. Matendo mema ni matendo yanayoendana na mapenzi ya Mungu. Hivyo, kutimiza mapenzi ya Mungu kunaleta furaha na kiuhalisi ndiyo kuwa katika Ufalme wa Mbinguni. Hivyo, kuwa katika Ufalme wa Mbinguni kunaleta furaha. Hii furaha tunaanza kuionja tukiwa hapa duniani kwa kutenda matendo mema na pia furaha hii itakamilika katika Ufalme wa Mbinguni baada ya maisha ya hapa duniani. Kwa hiyo, lengo la maisha yetu linapaswa kuwa ni “kuuona uso wa Mungu na kuwa na furaha ya milele”. Mzaburi anasema; Ilikuwa hamu ya Moyo wangu kuuna uso wa Bwana. Mtume Paulo ansema; “Kama lengo la maisha yetu lipo katika vitu vya ulimwengu huu, basi sisi ni watu wakusikitikiwa sana” (1Kor 15:19). Ndiyo maana katika Injili Yesu analinganisha Ufalme wa Mungu na “kitu cha thamani kubwa”, “lulu iliyo njema au hazina kubwa sana.”

Ufalme wa Mungu unajitokeza katika maisha yetu ya kawaida. Historia inasema kuwa waisraeli walikuwa na kawaida ya kuficha vitu vya thamani ardhini katika mashamba yao wakati wa misukosuko ya kisiasa, maisha yalipokuwa hatarini. Pia iliwawia wevi na wanyang’anyi vigumu kugundua mali imelala wapi. Mwenye mali alipokufa bila kumuonesha mrithi, au alipokaa mbali muda mrefu, mali ilidumu ardhini. Kama mtu aliigundua mali iliyofichwa katika shamba la mwingine, hakuwa na haki ya kuitwaa mali ile kama yake. Njia ya kuipata mali hiyo ilikuwa kulinunua shamba au kulimiliki kwa mbinu na harakati zozote zile. Baada ya kufanya hivyo hazina zote chini ya ardhi zinakuwa zake. Katika mfano huu mkulima aliyeiona hazina aliificha zaidi ili ibaki salama hadi hapo atakapokamilisha mipango ya kumiliki shamba. Ni kawaida mtu anakuwa na furaha sana pale anapopata kitu cha thamani kubwa na anaona kuwa mengine yote aliyonayo si kitu. Kwa urahisi furaha na hiari, mtu huvitoa vitu vya zamani ili avipate vipya. Kwa furaha anauza yote aliyonayo na ananunua lile shamba lenye hazina. Vivyo hivyo enzi zile lulu zilikuwa na thamani sana, hata kuzidi dhahabu, ziliuzwa kwa bei kubwa sana. Wafanyabiashara walisafiri mbali kuzisaka lulu. Mfanyabiashara alikuwa tayari kuuza yote aliyonayo ilikupata lulu ya thamani.  

Kumbe anayetambua kuwa utawala wa Mungu ni kitu cha thamani kubwa, atafanya hivyo hivyo. Mtu anaamua kuyaacha ya zamani yaani mali, marafiki ili awe na uraia mwema katika utawala wa Mungu. Mifano hii inatuhakikishia kuwa ukristo ni lulu yenye thamani kubwa kuliko mengine yote. Lakini tunahitaji Hekima ya kujua mapenzi ya Mungu. Ndiyo maana Solomoni alipoambiwa na Mungu aombe lolote “aliomba Hekima ya kupambanua mema na mabaya”. Hili ndilo tunaloliihitaji maana ulimwengu huu umejaa vitu vingi vinavyong’aa. Tusipokuwa na hekima tunaweza kudhani tumegundua hazina au lulu kumbe ni dhambi na mauti. Hekima ya kutambua kuwa kutimiza mapenzi ya Mungu kunaleta furaha ya kweli kwanza hapa duniani na baadaye huko mbinguni. Kutimiza mapenzi ya Mungu si kazi rahisi kunahitaji gharama. Paulo anasema “Maana Ufalme wa Mungu si shauri la kula na kunywa tu, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu. Anayemtumikia Kristo namna hiyo humpendeza Mungu na kukubaliwa na watu” (Rum 14:17). Ndiyo maana Kristu anasema “Anayetaka kuwa mfuasi wangu lazima ajikane mwenyewe abebe msalaba wake na anifuate” (Mt 16:24). Tumuombe Mwenyezi Mungu atujalie roho ya hekima na busara ya kuweza kujua kuwa ufalme wake ni wa dhamani kuliko malimwengu yote.

23 July 2020, 13:33