Tafuta

Vatican News
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa: Amana na Urithi kwa Watanzania tangu mwaka 1938- 2020. Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa: Amana na Urithi kwa Watanzania tangu mwaka 1938- 2020. 

Rais Mstaafu Ben Mkapa: Urithi na Amana Kwa Watanzania 1938-2020

Rais Mstaafu Mkapa alikuwa ni mtu mtulivu, mwenye uelewa mpana, uwajibikaji na utekelezaji wa majukumu yake kwa kiwango cha hali ya juu kabisa, kiasi cha kuaminiwa tangu awali na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania. Akakabidhiwa nyadhifa mbali mbali na hatimaye ya uongozi wake ni kuchaguliwa kuwaongoza watanzania katika Serikali ya Awamu ya Tatu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake ya Juma kuu kwa mwaka 2020 anasema, leo hii mwanadamu anataka kuona ufunuo wa Uso wa Mungu ambaye ni mwenye nguvu, mwenye mafanikio makubwa na anayetenda haki kadiri ya viwango vya binadamu na hata pengine, kadiri ya vionjo vya watu binafsi. Lakini, Injili inamwonesha Mwenyezi Mungu aliyejinyenyekesha na kuwa karibu pamoja na watu wake, kama jirani mwema na Fumbo la Pasaka, likawa ni kielelezo cha juu kabisa cha ufunuo wa huruma na upendo wake. Juu ya Msalaba, Yesu akaonesha kimya kikuu, akafungua mikono yake ili kuwakaribisha wote waliokimbilia huruma na upendo wake wa daima! Akaufunua utukufu wa Mungu, kwa kuonesha kwamba, kwa hakika alikuwa anapenda si kwa maneno, bali kwa vitendo. Kristo Yesu akaonesha ule upendo unaofumbatwa katika kimya kikuu, ili kuwakirimia waja wake maisha; hawalazimishi watu kumfuata, bali anawaachia uhuru unaowawajibisha! Hawatendei waja wake kama “watu wa kuja”, “wageni”, “wanyamahanga” au “vyasaka” bali rafiki na kujitwika udhaifu na dhambi za binadamu, ili kuweza kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Kwa maneno haya ya Baba Mtakatifu pengine kwa watanzania wanaoendelea kuomboleza kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu, Mzee William Benjamin Mkapa aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 81 katika usiku wa kuamkia tarehe 24 Julai 2020 akiwa Jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu ni maneno yenye tafakari nzito! Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika Fumbo la Pasaka, Mwenyezi Mungu ameganga na kuponya dhambi za binadamu; akamhurumia na hatimaye, kumkirimia maisha mapya. Kristo Yesu amegeuza hofu na mashaka ya binadamu kuwa ni chemchemi ya imani na matumaini. Pasaka ni ufunuo wa mapenzi mema ya Mungu kwa binadamu! Hii ni kwa sababu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni tukio la kihistoria na wala “si mambo ya kufikirika wala Hekaya za Abunuwasi”. Ndiyo maana baada ya ufufuko wa Kristo Yesu, waamini wanaambiwa “Msiogope”! Kristo Mfufuka ni msingi thabiti wa maisha ya wafuasi wake na kamwe hawawezi kuzama na kupotea kutoka katika uso wa dunia!

Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Kristo Yesu amekuwa karibu na kati ya watu wake, ameshinda dhambi na mauti. Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu unaowafikia na kuwaambata watu wote. Mwanadamu anaweza kubadili historia ya maisha yake kwa kumkaribia Mwenyezi Mungu na kupokea wokovu wake. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, anapenda kutoa salam za rambirambi kwa familia ya Mungu nchini Tanzania kwa kuondokewa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mzee William Benjamin Mkapa, Mkristo Mkatoliki aliyekuwa anaishi katika Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Upanga, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Ni kiongozi aliyeshiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Parokia yake ya Upanga. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi anawaalika watu wa Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam, kumkumbuka na kumwombea Marehemu Rais Mstaafu Benjamini William Mkapa, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na upendo aweze kumsamehe mapungufu yake ya kibinadamu katika utekelezaji wa majukumu, ili hatimaye, aweze kumstahilisha maisha na uzima wa milele.

Marehemu Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa amewaachia watanzania amana na urithi mzuri katika utendaji wake wenye kutukuka. Katika maisha yake, alikuwa ni mtu mtulivu, mwenye uelewa mpana, uwajibikaji na utekelezaji wa majukumu yake kwa kiwango cha hali ya juu kabisa, kiasi cha kuaminiwa tangu awali na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania. Akakabidhiwa nyadhifa mbali mbali na hatima ya uongozi wake ni kuchaguliwa kuwaongoza watanzania katika Serikali ya Awamu ya Tatu kuanzia tarehe 23 Novemba 1995 hadi tarehe 21 Desemba 2005 alipong’atuka kutoka madarakani. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi anasema, katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake kama Rais, amefanikiwa kuwaacha watanzania mahali pazuri zaidi pa kuishi. Alijitahidi kuishi kile alicho amini tangu akiwa kijana hadi mauti inamfika. Na kweli, amekuwa ni mfano bora wa kuigwa na familia ya Mungu nchini Tanzania.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa alikuwa ni kati ya wageni mashuhuri waliokuwa wamealikwa kwa ajili ya Sherehe ya Kumpongeza na Kumuaga, Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Nzigilwa alikuwa ni Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Saalam. Itakumbukwa kwamba, alipewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 23 Juni, 1995, kumbe, Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Jumamosi tarehe 25 Julai 2020 limetumia fursa hii, kwa ajili ya kumpongeza kwa Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, ameitupa mkono dunia, kabla ya kilele cha maadhimisho haya, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

ULALE PEMA BENJAMINI MKAPA

Ratiba elekezi ya mazishi ya Mzee Benjamin Mkapa inaonesha kwamba, atazikwa Jumatano tarehe 29 Julai 2020, majira ya saa 8 mchana kwenye Kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi, Mkoani Mtwara. Tukio hili linatanguliwa na shughuli ya kumuaga kitaifa, itakayofanyika, Jumanne tarehe 28 Julai 2020 kuanzia saa 6: 00 Mchana kwenye Uwanja wa Uhuru na itakapotimia saa 8: 00 mchana Mwili utasafirishwa kwenda Masasi kwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Nachingwea. Jumatatu tarehe 28 Julai 2020 watu wa Mungu watakuwa na fursa ya kutoa heshima zao za mwisho kwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa. Jumapili, tarehe 26 Julai 2020, Saa 4: 00 za Asubuhi, Ibada ya Misa Takatifu pamoja na watu wa Mungu kuanza kutoa heshima zao za mwisho.

Wakati huo huo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, kwa niaba ya watu wa Mungu nchini Kenya na Afrika Mashariki katika ujumla wake, anapenda kuungana na watanzania katika kuomboleza kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuhamasisha umoja na mshikamano wa kitaifa nchini Kenya, hasa baada ya machafuko wa kisiasa yaliyojitokeza baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya kunako mwaka 2008. Rais Mstaafu Mkapa akajipambanua kuwa rafiki mwema wa Kenya. Ni kiongozi ambaye alijituma sana ili kuhakikisha kwamba, wananchi wa Afrika Mashariki wanatekeleza ndoto yao ya kujipatia ustawi na maendeleo fungamani. Kwa muda wa siku tatu, kama kielelezo cha mshikamano na Tanzania, bendera ya Kenya itapeperushwa nusu mlingoni hadi Jumatano jioni, tarehe 29 Julai 2020, siku ambayo, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa atakuwa anapumzishwa kwenye usingizi wa amani Kijijini kwake Lupaso, Wilaya ya Masasi, Mkoani Mtwara.

Vyombo mbalimbali vya habari na mawasiliano ya jamii vinamtaja Mzee Benjamin William Mkapa kuwa kweli ni mwandishi wa habari mbobezi; mtetezi wa haki, amani, umoja, mshikamano wa kitaifa na demokrasia ya kweli. Alikuwa ni kiongozi mwadilifu, ambaye alipenda kuona kwamba, rasilimali fedha na utajiri wa Tanzania vinatumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi. Mzee Ben Mkapa, RIP.

Maombolezo Tanzania
25 July 2020, 14:35