Tafuta

Askofu Emmanuel Adetoyese Badejo wa jimbo la Oyo, Nigeria, katika tafakari kuhusu janga baada ya virusi vya corona. Askofu Emmanuel Adetoyese Badejo wa jimbo la Oyo, Nigeria, katika tafakari kuhusu janga baada ya virusi vya corona.  

Nigeria#coronavirus:Baada ya janga jukumu jipya ulimwenguni linahitajika!

Ulimwengu umepoteza ubinadamu wake pia ni ulimwengu uliougua na ambao unahitaji dharura ya kuponyeshwa kiroho.Ndivyo anaandika Askofu Emmanuel Adetoyese Badejo,wa jimbo la Oyo,Nigeria,katika tafakari yake ndefu kuhusu janga baada ya virusi vya corona.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Askofu Emmanuel Adetoyese Badejo, wa jimbo la Oyo, Nigeria, katika tafakari yake ndefu kuhusu janga baada ya virusi vya corona anasema jukumu jipya la ulimwengu linahitajika kulinda haki za wote na kuwapa mahitaji yao. Katika tafakari hiyo iliyo chapishwa katika tovuti ya Shirikisho la mabaraza ya Maaskofu Kanda ya Afrika Magharibi (Recowa-Cerao), anasema “Ulimwengu unakabiliwa na wakati mgumu sana. Sizungumzii tu mahitaji ya vifaa na muundo,  lakini pia siasa, uchumi na wasiwasi wa kijamii na kiroho. Sekta zote ziko kwenye shida ya kupata pumzi” amesema Askofu Badejo.

Hatari za covid-19 hazijatatuliwa

Kwa upande mmoja, janga la Covid-19 bado ni hatari na halijatatuliwa, lakini kwa upande mwingine, ubaguzi wa rangi, ugaidi, mizozo ya kikabila, ujambazi wa kutumia silaha, unyanyasaji wa watoto wadogo, ubakaji na dhuluma vimeongezeka katika nchi nyingi. “Na ingawa juhudi kubwa zinafanywa kushughulikia shida hizi mambo mengi bado yanapaswa kufanywa ili kurejesha haki za kijamii. Ulimwengu umepoteza ubinadamu wake pia ni ulimwengu uliougua na ambao unahitaji dharura ya kuponyeshwa kiroho”, anaandika Askofu huyo wa Nigeria.

Lazima kurudi katika mambo muhimu

Kwa maana hii Askofu anasisitiza kwamba inahitajika kurudi katika mambo yaliyo muhimu hasa kwa familia moja ya wanadamu yenye mshikamano ambayo undugu bado ni muhimu sana. Suluhisho zinazowezekana katika kutatua shida za ulimwengu ni lazima, ambapo zijumuishe kuamsha tena hisia za kiroho na kuzaliwa upya kwa maadili, vinginevyo zitabaki hivyo hivyo katika majaribu ya wakati. Onyo kwa upande Askofu Badejo ni kwamba, thamani ya kiroho na maadili ambayo Muumba aliumba ulimwengu, lazima iwe msingi wa utaratibu mpya wa ulimwengu ambao unalinda haki halali za wote na kutazama hasa  wote wahitaji zaidi.

Uwajibikaji kwa ajili ya uinjilishaji na wokovu

Kwa kutoa ushuhuda wake binafsi, amebainisha kwamba katika jimbo lake la Oyo, amezindua mpango mpya wa kichungaji, alioupatia jina la “Uwajibikaji kwa ajili ya uinjilishaji na wokovu”, huo ni pamoja na mzunguko wa katekesi iliyojikita katika  Amri Kumi za Mungu  na huduma ya huruma wa kimwili na kiroho katika mwanga daima wa mafundisho jamii ya Kanisa. Kila parokia, kila harakati, kila chama na vikundi na waamini binafsi wamealikwa  kutoa mchango wao ili kufanikisha azma nzuri  ya kujenga ulimwengu ulio bora, ulimwengu mpya ambapo kila mtu anaweza kufurahi usawa  wa hadhi na umakini kwa kila hali.

01 July 2020, 16:56